Habari rafiki yangu
ambaye umekuwa msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri. Karibu makala hii
ambapo nakuletea uchambuzi wa kitabu cha 3 kati ya vitabu 30 ambavyo
nimejiwekea lengo kuvisoma katika kipindi cha mwaka huu 2020.
Born to Win ~ Dream Big
Mwalimu Augustine Mathias
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
onclick='window.open(
Kama bado hujajiunga
na kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya kupata neno la
tafakari kila siku pamoja na kujumuika na watu wenye mtazamo sawa, tafadhali
fanya hivyo KWA KUBONYEZA HAPA na kujiunga
na kundi letu. Nafasi ni chache hivyo fanya maamuzi ya kujiunga sasa.
Kitabu ninachokushirikisha
kupitia makala hii ni “The Principles and Power of Vision”
kutoka kwa mwandishi Dr. Myles Munroe ambaye ni mwandishi na mhamasishaji mkuu
wa maswala ya Uongozi, Kiroho na Mtalaamu mwelekezi kwenye masuala ya biashara
na Serikali. Amefanikiwa kuandika vitabu mbalimbali ikiwepo kitabu cha Keys to
Leadership na vingine vingi.
Katika kitabu hiki mwandishi
anatushirikisha nguvu iliyopo katika kuishi maisha yenye misingi na kanuni
ambazo zinaongozwa na maono binafsi kutokana na ukweli kwamba maono ni chanzo
cha tumaini katika maisha. Moja ya zawadi kubwa ambayo mwanadamu amepewa ni
uwezo wa kuona. Kazi ya macho ni kuwezesha kuangalia vitu wakati maono ni kazi
ya moyo. Kwa tafsiri hii macho yanayoangalia ni mengi wakati macho yenye uwezo
wa kuona (maono) ni machache sana.
Vitu vyote vvya muhimu
au ambavyo vimewezesha kuboresha maendeleo katika historia ya mwanadamu chanzo
chake ni maono kutoka kwa watu wachache. Watu wenye maono waliwezesha na
wanaendelea kugundua, kubuni na kuboresha maisha ya mwanadamu kijamii,
kiuchumi, kiutamaduni, kiroho na kisiasa.
Maono yana nafasi ya
kukumboa kutoka kwenye vikwazo ambavyo unaviona kwa macho na kukupeleka kwenye
nafasi ya kile ambacho moyo wako unakuambia kuwa ndipo hapa ndipo maisha yako
yanatakiwa yafikie. Maono hayo yanayokuwezesha kuona vitu ambavyo hujawahi
kuona kwa macho yako na kuvitafsiri katika uhalisia wa maisha yako.
Maono pia yana nafasi ya kuwezesha uvumilivu
katika nyakati za kukata tamaa na maumivu katika maisha. Ni kupitia maono
katika kipindi hicho mhusika anakuwa na tumaini jema na uvumilivu katika
maisha.
Kwa ufupi chochote unachokiona kurahisisha
maisha katika Ulimwengu wa sasa ni matokea ya maono ya watu waliohusika katika
uvumbuzi/ugunduzi na ubunifu. Fikira kuhusu ugunduzi mbalimbali kwenye
miundombinu ya usafiri, fikiria kuhusu ugunduzi katika sekta ya viwanda,
kilimo, afya, umeme, mawasiliano na vitu vyote vilivyorahisisha maendeleo
katika historia ya mwanadamu.
Pale ambapo hakuna maono watu wataangamia kama
ambavyo imeandikwa katika vitabu vya maandiko matakatifu. Tasfiri yake ni
kwamba kama watu hawana tumaini jema katika maisha ya baadae matokeo yake ni
maisha ambayo watu wanashindwa kujidhibiti wenyewe na hivyo wanageukia kwenye
matendo yasiyo na nidhamu.
Dunia sasa inakosa ina watu wengi ambao hawana
maono ikilinganishwa na watu wenye maono. Tamaa binafsi au taifa (nchi)
zinazidi kuongezeka kuliko uhalisia wa kile ambacho kinaubiriwa na watu au
mataifa hayo. Ndio maana matendo ya mauaji yanazidi kuongezeka, vita vinazidi
kutawala na kupoteza maisha ya watu wasio na hatia.
Hofu, kukosa tumaini la maisha, kukosa uhakika
wa maisha, usalama mdogo, mihemko ya kijamii au kisiasa, migogoro ya kidini au
kisiasa, magonjwa na kasi ya uharibifu wa mazingira vinazidi kutawala maisha ya
sasa. Hii ni dalili kuwa Dunia ina watu wachache wenye maono ikilinganishwa na
idadi ya watu wasio na maono.
Mwandishi wa kitabu kupitia kitabu hiki
anakusudia kuisaidia jamii kuishi maisha yenye maono. Wapo ambao wanaishi
maisha yasiyo na maono, wapo ambao wana maono lakini hawajui wafanye nini ili
kuyaishi maono hayo na wapo ambao waliwahi kuwa na maono lakini wakapoteza
maono hayo kutokana na changamoto za kimaisha. Basi kama upo kati ya makundi
hayo, kitabu hiki ni muhimu kwako. Katika kitabu hiki utafunuliwa namna ambavyo
umezaliwa kwa sababu maalum na umezaliwa ili kuleta tofauti katika kuibadilisha
Dunia kuwa mahala pazuri pa kuishi.
Karibu ushirikiane nami kujifunza machache
kati ya mengi ambayo tunashirikishwa katika kitabu hiki:
UTANGULIZI
1. Mwenyezi
Mungu ameumba mwanadamu na ndani yake akampa thamani ya kipekee ambayo ndio
inamtofautisha na wanadamu wengine. Hata hivyo, watu wengi wanajiangalia kwa
jinsi walivyo katika mwonekano wa juu na kujithaminisha katika kundi la watu
wasiyo na thamani katika Dunia hii. Mwandishi anatushirikisha kuwa, wengi kwa
mtazamo wa juu wanajiona wana thamani ya udongo mfinyanzi wakati ndani mwao kuna
thamani ya Dhahabu ambayo haijatumika. Mungu hakuumba mtu wa wastani bali
aliumba mtu mwenye mamlaka na thamani ya hali ya juu. Bila kujali wewe ni nani,
una rangi gani, nchi yako au historia ya maisha yako; unatakiwa kutambua kuwa
umeumbwa kwa kusudi maalum na kusudi hilo unatakiwa kuliishi kwa faida ya ya
jamii inayokuzunguka na viumbe wengine hapa Duniani.
2. Je
Maono ni nini? Maono ni ule uwezo wa kuwa na macho ambayo
yanaona vitu vilivyo mbali ya upeo wa wako. Macho yako yanaona nini? Katika
mantiki ya maono macho yako pamoja na kuona vitu vinavyoonekana yanatakiwa kuwa
na sifa ya ziada ya kuona vitu visivyoonekana na ambavyo havijaumbika. Kupitia
uwezo huo unaweza kuumba vitu vipya kutokana na picha unayoijenga kupitia maono
uliyonayo. Maono ni uwezo wa kuona matukio ya maisha yajayo na kufanikisha
maisha hayo au maono ni uwezo wa kujenga picha ya jinsi gani maisha yako
unataka yawe na kuhakikisha kila mara unafanya kwa ajili ya kukamilisha picha
hiyo katika uhalisia wake.
3. Je
maono yako ni yapi? Baada ya kutambua kuwa umeumbwa kwa ajili ya
kusudi maalumu hapa Duniani na umeumbwa kwa ajili ya kuleta tofauti ya kipekee
hapa Duniani; wajibu wako sasa ni kutambua maono ya maisha yako ni yapi. Baada
ya kugundua upo Duniani humu kwa ajili ya kufanikisha nini kinachofuata na
kuhakikisha unakuwa na ustahimilivu/uvumilivu. Unapogundua kusudi la maisha
yako na unaweza kuliona katika picha (maono) hakika hakuna wa kukusimamisha. Na
kadri unavyokuwa mvumilivu wa kuishi kulingana na maono yako ndivyo kuna nafasi
kubwa kutoka kwenye maisha ya sasa hadi kwenye maisha uliyonayo katika picha ya
maono yako.
SEHEMU
YA KWANZA: KWA NINI MAONO?
4. Maono ni ufunguo wa kukamilisha kusudi la
maisha. Kutokana na kukosa maono, watu wengi wanaishi bila kufahamu thamani
ya maisha yao. Ukiuliza swali rahisi la “kwa nini unashi?” ni wachache sana
ambao wataweza kukumbia thamani iliyopo kutokana na uwepo wao hapa Duniani.
Wengi wanaishi ili mradi tu kwa sababu wapo hai kwa maana hawa msukumo wa kuona
thamani iliyopo katika maisha yao. Ukitaka kugundua ukweli huu, angalia idadi
ya watu ambao hawapendi kazi wanazofanya. Wanaenda kazini au kwenye biashara
ili mradi tu wapate ridhiki ya kukidhi mahitaji yao lakini kazi wanazofanya
hazitoki kwenye kiini cha moyo wao. Ndio maana tafiti zinaonesha kuwa siku
Ijumaa watu wengi wanakuwa na furaha ikilinganishwa na siku ya Jumatatu. Hii ni
kwa Ijumaa watu wanakuwa na shauku ya kuanza siku za mapumziko za mwisho wa
wiki.
5. Umezaliwa
kwa ajili ya kufahamika kwa kazi maalum. Unapoishi kwa kuongozwa na
dira ya maono inakuwa rahisi kwako kujitofautisha na watu wengine. Mwandishi
anatushirikisha kuwa umezaliwa kuleta tofauti katika Dunia hii ambayo hakuna
mwingine anayeweza kuleta tofauti hiyo zaidi ya wewe. Wewe ni wa kipekee na
ndio maana Dunia nzima hakuna mwenye alama za vidole zinazofanana na zako.
Swali muhimu la kujiuliza ni kwamba hadi sasa bila kujali umri ulionao umefanya
nini kuelekea kwenye kusudi la maisha yako? Watu wengi wanazikwa na zawadi za
kipekee ambazo Mwenyezi Mungu amewajaliwa toka siku walipoumbwa. Je na wewe upo
tayari kuwa mmoja wao? Wapo wengi ambao hawaridhiki na hali au nafasi
walizonazo kwa sasa lakini hawachukui hatua madhubuti za kuwasogeza kutoka sehemu
walipo kuelekea kwenye ndoto zao na mwisho wake wanandelea kuwa na nafasi hizo
hizo hadi mwisho wa maisha yao. Je na wewe upo tayari kuwa mmoja wao?
6. Unapogundua
maono yako katika maisha yanakuwezesha kupata nguvu na dhamira ya kuishi maisha
yenye faida kwa jamii na viumbe wengine. Mwandishi
anatushirikisha kuwa katika jamii Kuna makundi ya aina tatu za watu: kundi la kwanza linahusisha watu ambao
hawatambui kuwa kuna mabadiliko katika mazingira wanayoishi; kundi la pili linahusisha watu
wanaoshangaa baada ya kuona mabadiliko yametokea; na kundi la tatu linahusisha watu ambao wanasababisha mabadiliko
yatokee. Watu wengi wanatamani mafanikio mazuri au kilele bora cha maisha yao
lakini hawana dhamira ya kweli katika kujibidisha kupata mafanikio hayo. Ni kutokana
na ukweli huu, Dunia ina watu wachache ambao wanajibidisha kuleta mabadiliko
katika jamii ikilinganishwa na wale wanaotamani maisha ya mafanikio bila
kuchukua hatua zozote. Maono ni msingi wa msukumo kwa mhusika kutekeleza ndoto
zake kwa vitendo.
7.
Maono yanamwezesha mhusika kutambua kalama na vipaji alivyonavyo. Kila
mwanadamu ameumbwa kufahamika kwa ajili ya kalama na vipaji alivyopewa toka
enzi za uumbwaji wake. Kupitia kalama na vipaji hivyo mhusika anafanikisha
kuishi maono yake na hivyo kutimiza kusudi la maisha yake hapa Duniani. Pointi
muhimu ya kukumbuka hapa ni kwamba kalama na vipaji ndiyo ufunguo wa kila
mwanadamu kufanikisha maisha yake. Si elimu wa nini ambacho kitakufanya
ufanikiwe kimaisha kwani ingekuwa hivyo kila mwenye elimu ya uzamivu (Phd)
angekuwa na maisha yenye uhuru wa kifedha na furaha. Kumbe pamoja na kuwa na
elimu unatakiwa kutumia kalama na vipaji ulivyopewa kwa ajili ya kufanikiwa
kimaisha. Na kwa mtazamo kufanikiwa kimaisha si lazima uwe na elimu bali ni kwa
jinsi utatambua na kutumia kalama na vipaji ambavyo umepewa na Mwenyezi Mungu.
8. Hatua
ya kwanza katika kugundua kwa nini unaishi ni kufahamu kuwa umepewa maono toka
siku uliyoumbwa. Maono hayo yanatokana na kusudi la maisha
yako ambalo chimbuko lake ni kutoka kwa Muumba wako. Na kusudi lipo kwa muda
maalumu, kwa maana ulizaliwa katika muda na majira sahihi kwa ajili ya ukamilisho
wa kusudi la maisha yako. Na muda au majira hayo ndiyo siku za kuishi kwako
hapa Duniani. Kila kilichoumbwa na mwenyezi Mungu hapa Duniani kimeumbwa kwa
ajili ya ukamilifu wa kazi maalumu. Mfano, angalia wanyama, mimea, wadudu au
vitu visivyo na uhai. Kila kitu kipo kwa ajili ya ukamilifu wa kazi
iliyokusudiwa na Muumba na ndivyo ilivyo katika maisha ya kila mwanadamu. Kila mwanadamu
ameumbwa kwa ajili ya ukamilifu wa kazi maalumu na ya kipekee hapa Duniani. Wajibu
wako ni kutambua kusudi la maisha yako ni lipi na kuanza kuliishi ukiwa na
maono makubwa mbele ya safari yako. Kumbe, kama haujatambua kusudi la maisha
yako ni vigumu kuishi maisha yenye maono.
9. Kila
mmoja ameumbwa kwa ajili ya kutimiza jukumu maalum kama sehemu ya kuishi kusudi
la maisha yake. Jukumu hilo ndilo linayapa thamani maisha ya
kila mwanadamu kwani anayetambuwa wajibu anatakiwa kujibu kuwa “nimezaliwa kwa
ajili ya….”. Hiki ni kilio cha sauti ambayo inatakiwa kila mara isikike ndani
mwako kama sehemu ya kukumbusha kuwa bila kujali umri wako au historia yako,
upo Duniani humu kwa ajili ya kukamilisha jukumu maalumu. Na jukumu hilo lina
uzima wa milele ndani mwake sawa na Muumba wako alivyo na uzima huo wa milele
na wa kwanza na wa mwisho (Alpha na Omega). Kumbuka umeumbwa kwa mfano na sura
yake hivyo maisha yako ni kwa ajili ya ukamilisho wa kusudi maalumu. Tafsiri yake
ni kwamba Mungu alipokuumba kwa ajili ya kusudi maalumu moja kwa moja alishakuwezesha
kupata matokeo aliyokusudia uyapate endapo tu utajitambua wajibu wako hapa Duniani.
10. Je
matamanio ya ndani mwako kuhusu maisha kwa ujumla yako wapi?. Watu
wengi wanasoma vitabu kuhusiana na kusudi la maisha au maono lakini wanabaki
kujiuliza ni lipi kusudi la maisha yangu? Mwandishi anatushirikisha kuwa kusudi
la maisha yako lipo ndani mwako. Je umekuwa kufanikisha nini katika maisha
yako? Umekuwa na mawazo na fikra zipi ambazo zinakurudia kila mara katika akili
yako. Je umekuwa na mipango ipi ya mara kwa mara ambayo umekuwa ukihairisha
kila mara? Hayo si mawazo, fikra wala mipango yako bali ndilo jukumu kubwa
ambalo Mwenyezi Mungu kila mara anakukumbusha kuwa amekuumba kwa ajili ya
kukamilisha kusudi maalumu kwa faida ya viumbe vyote hapa Duniani.
11. Unapotambua
kwa nini umeumbwa moja kwa moja unakuwa umetambua
kusudi la maisha yako. Unapofanikiwa
kuliona kusudi la maisha yako kwa picha katika akili yako ukiongozwa na Imani, moja
kwa moja unakuwa umetambua maono ya
maisha yako. Hata hivyo ili kuendelea kuishi kusudi la maisha yako
unatakiwa kujiweka karibu na Muumba wako katika maisha yako ya kila siku. Ni kupitia
ushirika wako na Muumba utaendelea kugundua mipango aliyoiweka ndani mwako
tangu enzi ulipoumbwa.
12.
Hatua ya inayofuata baada ya kutambua maono yako ni kufahamu vikwazo ambavyo
vinaweza kukukwamisha husiishi maono ya maisha yako. Mwandishi
anatushirikisha kuwa watu wengi waanakabiliwa na changamoto tatu ambazo ni: a) Kutotambua
asili ya maono yao – Je maono yako ni ya aina gani?; b) Kushindwa kutambua
gharama iliyopo katika kuishi maono ya maisha yao; na c) Kushindwa kuambua
kanuni za maisha yenye maono.
A.
KUTOTAMBUA
ASILI YA MAONO YAO
13. Maono
ni maalumu kwa ajili kufanikisha jambo flani katika maisha yako. Watu
wengi wanashindwa kuishi maisha yenye maono kwa kuwa hawana lengo kuu la nini
wanataka kufanikisha katika maisha yao. Unaweza kufanya kazi kwa bidii lakini
kama hauna lengo mahsusi juu ya nini unataka katika maisha yako ni sawa na kazi
bure. Maono ni lazima yawe maalumu na ndani ya muda maalum tofauti na hapo si
maono bali ni matakwa au mahitaji tu. Kumbe, maono yanatakiwa kuwa sentensi
fupi yenye msisitizo maalumu na mipaka ya wazi (muda wa utekelezaji). Kumbuka kuwa
lengo la maono ni kukutofautisha na watu wengine wote sawa na ilivyo kwenye
alama za vidole vyako. Hivyo, ni lazima liwekwe wazi na liwe na upekee kwani
hili ndilo linakutofautisha na watu wengine wanaokuzunguka.
14. Watu
wengi wanashindwa kuwa na maono yenye umaalumu wa kipekee kwa vile wanashindwa
kutofautisha maono na matamanio ya kifikra. Matamanio hayo ya
kifikra yanajirudia mara kwa mara katika maisha yao na hakuna mpango maalumu
kwa ajili ya kukamilisha fikra hizo. Mfano, badala ya kusema natamani nipungue
uzito kaa chini na ainisha mbinu za namna ya kupunguza uzito na anza
kuzitekeleza mara moja. Badala ya kusema natamani kuwa na uhuru wa kifedha, kaa
chini ainisha njia unazotakiwa kuzitumia kufikia uhuru wa kifedha unaotamani
katika maisha yako.
15. Sababu nyingine inayopelekea watu washindwe
kuishi maono yao ni kukosa maamuzi. Kukosa maamuzi ya kuchukua hatua kwa
muda mrefu ni chanzo kikubwa cha kuua maono kwa watu wengi. Ni watu wachache
sana wenye orodha ya vitu wanavyotaka kukamilisha katika kipindi cha maisha
yao. Kukosekana kwa orodha hiyo inapelekea watu kugusa gusa kwenye kila eneo na
mwisho wake maisha yao hayana dira maalumu. Hali hii inapelekea kila mara
kuchelewa kuchukua maamuzi au kuairisha mambo na matokea yake ni kuishia kwenye
maisha ya kawaida kuliko mafanikio halisi waliyoandikiwa.
16. Sababu
nyingine ambazo zinapelekea watu washindwe kuishi maono ya maisha yao ni pamoja
na:-
ü Kutanguliza udhuru kila mara – Wakati
mwingine mtu anafahamu anatakiwa afanye nini kwa ajili kufikia matamanio katika
maisha yake lakini kila anapotaka kuchukua hatua anajisemea rohoni kwa sasa
siwezi hadi hapo mambo yangu yatakapokaa sawa. Ukweli ni kwamba hakuna hata
simu moja ambapo mambo yake yatakaa sawa.
ü Tabia ya kutafuta mlinganyo katika maisha
– Wengi
wanashindwa kuchukua hatua zinazolenga kuishi maono yao kwa vile wanahisi kwa
kufanya hivyo watasababisha upande mwingine wa maisha yao kuyumba. Mfano, mtu
anahisi kuwa kwa kuishi maono ya maisha yake atapoteza muda wa kufanya mambo
mengine aliyozoea katika maisha ya kila siku.
ü Kukosa vipaumbele – Mara nyingine
watu wanajaribu kuchukua hatua japo wanajikuta wakifanya mambo mengi kwa wakati
mmoja. Hali hii inapelekea hakuna hata moja ambalo linazalisha matunda
ipasavyo.
ü Kuwajibika katika vipaji vingi – Kuna
watu wamejariwa kuwa na vipaji vingi, changamoto iliyopo kwa watu wa aina hii
ni kushindwa kuchagua kipaji kimoja ambacho ndicho kinabeba kusudi la maisha
yao. Fikiria watu maarufu kama Christiano Ronaldo, Kobe Bryant, Mother Thelesa,
Serena Williums na wengine wengi, kama watu hawa wasingechagua kutumia kipaji
kimoja kati ya vingi walivyonavyo hakika wasingeweza kupata mafanikio ambayo
walifanikisha.
B.
KUSHINDWA
KUTAMBUA GHARAMA ILIYOPO KATIKA KUISHI MAONO YAO
17. Hiki
ni kikwazo cha pili kwa watu kutokuishi maisha yenye maono. Watu wengi
wanahitaji kufanikisha mambo mengi katika maisha lakini wanashindwa kutambua ni
gharama ipi wanatakiwa kutoa kwa ajili ya kupata kile wanachotamani. Ukweli ni
kwamba mafanikio yanatokana na uwekezaji wa kila aina kulingana na aina ya
mafanikio unayotaka. Unatakiwa kutoka kwenye ukanda wa faraja (comfort zone)
ambao umekuzunguka na kuachana na maisha ya unafiki. Kundi hili linahusisha
vikwazo vifuatavyo:-
ü Kuhisi kuwa hawana bahati – Mtu
anapojenga Imani kuwa maisha yake yanatawaliwa na bahati mbaya moja kwa moja
anashindwa kuchukua hatua zinazolenga kuishi kusudi la maisha yake kwa anaamini
kuwa hawezifanikisha lolote katika maisha yake.
ü Kulalamikia nguvu zilizopo nje ya uwezo
wao
– Watu wengi wanaamini katika maisha wameshindwa kufanikiwa watu wanaowazunguka
wana nia mbaya na mafanikio yao. Wengine wanahisi mazingira sio rafiki kwao
kufanikiwa. Hapa ndipo unakuta mtu analalamikia Serikali, Wazazi, Mwenza wake
au Jamii inayomzunguka.
C.
KUSHINDWA
KUTAMBUA KANUNI ZA KUISHI MAISHA YENYE MAONO
18. Hiki
ni kikwazo cha tatu kwa watu kuishi maisha yenye maono. Watu wenye mafanikio
makubwa hawajapata mafanikio hayo kwa bahati tu bali mafanikio yao yametokana
na kutumia kanuni ambazo zipo na zilishajaribiwa na kutumiwa na watu wengine
kwa muda mrefu. Sehemu ya pili ya uchambuzi wa kitabu hiki itagusa kanuni 12
ambazo unatakiwa kuziishi ili uwe na maisha yenye maono.
SEHEMU YA PILI: KANUNI 12 ZA
KUISHI MAISHA YENYE MAONO
Kabla ya kuanza sehemu hii mwandishi
anatushirikisha sehemu ya maandiko matakatifu kutoka kitabu cha Yoshua sehemu
ile ambapo Yoshua alikuwa anapokea jukumu la Musa baada ya kifo cha Musa. Na
nukuu sehemu ya maandiko hayo “hakuna mtu atakayekushinda
siku zote za maisha yako. Nitakuwa pamoja nawe kama nilivyokuwa pamoja na Musa.
Daima nitakuwa nawe wala sitakuacha kamwe. Uwe imara na hodari kwa kuwa wewe
utawaongoza watu hawa kuirithi nchi ambayo niliwaahidi wazee wao kuwa nitawapa.
Ila tu, uwe imara na hodari; uwe mwangalifu na kuzingatia sheria yote
aliyokuamuru mtumishi wangu Musa. Fuata kila sehemu ya sheria hiyo nawe
utafanikiwa popote uendapo. Hakikisha kuwa hutakisahau kamwe kitabu hiki cha
sheria bali kila siku utajifunza kitabu hiki cha sheria, mchana na usiku, ili
upate kutekeleza yote yaliyoandikwa humu, nawe utafanikiwa na kustawi popote
uendapo” (Joshua 1: 5 – 8).
Mwandishi anatushirikisha kuwa kwa maneno
mengine Mungu alikuwa akimwambi Joshua, “utafanikiwa endapo utajifunza na
kufuata kanuni zangu”. Mungu alimhakikishia mafanikio endapo atafuata na
kuheshimu kanuni ambazo Musa mwenyewe aliziheshimu. Hivyo, Mungu alimwamuru
Joshua kujifunza kutoka kwenye maisha ya Musa na siyo kuigiza maisha ya Musa. Ndivyo
ilivyo katika kuishi maisha yenye maono, unaweza kujifunza kanuni kutoka watu
wenye mafanikio hila hautakiwi kuigiza maisha yao.
Karibu ujifunze kanuni 12 za kuishi maisha
yenye maono ambazo ambazo zinakusudia kulinda, kuhifadhi na kukuhakikisha ndoto
zako zinatimizwa katika kipindi cha maisha yako.
19.
Kanuni #1: Mara zote ongozwa na maono yaliyo wazi. Kukamilisha
maono yako unatakiwa kuongozwa na kusudi la maisha ambalo lipo wazi. Watu wote
waliofanikiwa kimaishan; kwa kutaja tu baadhi Abrahamu, Musa, Daniel na wengine
wote tunaowafahamu katika historia ya maisha mwanadamu kama vile J.K. Nyerere,
Nelson Mandera, Kwame Nkrumah, Albert Einsten na wengineo kwa pamoja kila mmoja
wao aliongozwa na kusudi maalumu ambalo lilimfanya atimize maono yake. Mwongozo
wa maono ni ufunguo wa mafanikio kwa yeyote anataka kuishi maisha yenye thamani
katika Dunia hii. Unahitaji kufahamu kwa nini ulizawaliwa (kusudi la maisha) na
kuwa na uwezo kujiona katika picha kubwa ya kuishi mapana ya kusudi la maisha
yako (maono). Maswali muhimu ambayo kila mtu anatakiwa kujiuliza ni:
ü Je ni
mambo yapi unataka kukamilisha katika maisha yako?
ü Je
kazi unayofanya kwa sasa inakusaidia katika kukamilisha kusudi la maisha yako?
ü Je
maisha unayoishi leo hii yanaacha alama yoyote katika Dunia hii baada ya ukomo
wa maisha yako?
ü Je
una picha kubwa ya mafanikio unayotaka kufanikisha kutokana na kuishi kusudi la
maisha yako?
ü Je upo
kubadilika na kuachana na ukanda wa faraja (comfort zone) na kuelekea kwenye
mabadiliko halisi yatakayowezesha kuishi kusudi la maisha yako?
ü Je upo
tayari kuchukua hatua zinazolenga kubadilisha matamanio kuwa uhalisia kwani
umeishi muda mrefe katika matamanio hayo bila kuchukua hatua?
Haya ni machache ambayo nimejifunza kutoka
katika sehemu hizi nilizokushirikisha katika kitabu hiki. Hakika kuna mengi
ambayo mwandishi anatushirikisha kwa ajili ya kuboresha maisha yetu hapa
Duniani. Tukutane Jumapili ijayo ya tarehe 8 Machi, 2020 kwa ajili ya kumalizia
kanuni 11 zilizobakia. Jiunge na mtandao wa Fikra za Kitajiri kwa KUBONYEZA HAPA.
Endelea
kusambaza makala hizi kwa kadri uwezavyo ili ndugu, jamaa na marafiki wanufaike
kwa kujifunza maarifa mbalimbali kutoka kwa waandishi wa vitabu. Kumbuka
umepata makala hii bila malipo yoyote hivyo hakikisha na wewe unaisambaza bure.
(Unaposambaza makala hizi hakikisha haukopi na kupest badala yake share link). Nakutakia
mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu isiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Mwalimu Augustine Mathias
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua pepe: fikrazatajiri@gmail.com