Habari ya leo rafiki na
msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri. Ni matumaini yangu kuwa unaendelea
vizuri katika mapambano ya kuboresha maisha yako kwa kuhakikisha kila siku
unakuwa bora zaidi kupitia ushindi mdogo mdogo. Leo hii ninakuletea uchambuzi
maalumu wa kitabu cha The Rules of Money ambacho
kimeandikwa na mwandishi mahiri Richard Templar.
Kupitia kitabu hiki
mwandishi anatushirikisha kanuni 107 za pesa ambazo kupitia uchambuzi huu
nitakushirikisha kanuni zote ili uanze kuzitumia kwa ajili ya kutengeneza pesa zaidi
na zaidi katika mchezo huu wa fedha. Kwa ujumla katika kitabu hiki
tunafundishwa kuwa pesa hawezi kununua furaha au mapenzi yako bali pesa inaweza
kununua kila aina ya vitu na hivyo kukuwezesha kumiliki kila aina vitu unavyohitaji.
Lakini katika yote ni muhimu kukumbuka kuwa furaha ya kweli juu ya matumizi ya
pesa yako inatengenezwa na wewe mwenyewe kutoka ndani mwako.
Kanuni hizi zimegawanyika
katika makundi saba na kila kundi lina kanuni zinazokuhusu wewe na pesa yako.
Karibu tujifunze wote kwa haya machache niliyojifunza kwenye kitabu hiki;
SEHEMU
YA KWANZA: FIKRI KITAJIRI (THINKING WEALTHY)
1. Kanuni ya Kwanza: Kila mtu anaweza kuwa na fedha anazozitaka,
ni suala la yeye kujiweka sawa kwenye kanuni za kutengeneza fedha. Kuwa na
pesa ni haki ya kila mmoja bila kujali rangi, kabila, umri, historia ya wazazi
wake au utaifa wake. Kila siku inafungua mlango kwako kwa ajili ya kutumia
fursa zilizopo ili kuweza kutengeneza pesa unazotaka na hivyo ni muhimu kwako kujifunza
mbinu wanazotumia matajiri kutengeneza pesa zaidi na mbinu hizo zipo wazi kwa
kila mmoja. Kitu pekee kinachoweza kukukwamisha ni wewe mwenyewe na mtazamo
wako juu ya upatikanaji wa fedha. Kanuni hii ndio kanuni kuu ya kutengeneza
pesa na kanuni nyingine zinahusu wewe kujijengea misingi ya ya kuendelea
kutengeneza pesa zaidi na ziadi.
2. Kanuni ya Pili: Kuwa na maana yako ya neno “utajiri”. Katika
kanuni hii mwandishi anatushirikisha kuwa utajiri unaanza na wewe kufafanunua
nini maana ya utajiri kwa mtazamo wako. Nini hasa unataka kupata ili ukishapata
vitu hivyo ndo uone kuwa umekuwa tajiri. Hivyo kabla haujaanza safari ya utajiri
anza kwa kuadaa orodha ya yale yote unayoyataka katika maisha yako ya utajiri. Hapa
haupaswi kujifunga kwa kutengeneza picha finyu bali unatakiwa kuwa na fikra
pana ambazo pengine zinakufanya uziogope kwa sasa.
3. Kanuni ya Tatu: Tengeneza lengo lako. Baada
ya kuwa na maana yako ya utajiri ambayo ni sawa na kilele cha safari yako hivyo
unapaswa kutengeneza lengo kubwa ambalo litakuwa ni njia ya kuelekea kwenye
kilele hicho. Hapa unapaswa kuweka muda
ambao unategemea kufikia kilele cha utajiri wako, eleza njia zipi zitatumika
kufikia utajiri huo, ainisha changamoto ambazo ambazo unahisi zinaweza
kukukwamisha na hatimaye kuwa na mpango wa kupambana na changamoto hizo. Lengo
linatakiwa liwe linatekelezeka, lenye uhalisia na linatoka ndani mwako.
4. Kanuni ya Nne: Lifanye lengo lako kuwa
siri. Unapoanza safari ya kuishi lengo kubwa ulilojiwekea ina
maana kuwa unaanza maisha mapya ambayo yatakufanya uwe mtu wa tofauti
ikilinganishwa na maisha yako ya zamani. Hivyo katika maisha haya mapya wapo
wengi ambao hawatafurahia jinsi unavyobadilika kutokana na chuki zao au wivu
kwa vile unaelekea kwenye maisha ya tofauti na wao. Kwa hali kama hii unatakiwa
malengo uliyojiwekea yawe siri yako ili husikatishwe tamaa na maneno ya jamii
inayokuzunguka.
5. Kanuni ya Tano: Watu wengi ni wavivu wa
kufikia utajiri wao. Hakuna njia nyingine ya kuwa tajiri zaidi ya
kufanya kazi kwa bidii. Ni lazima uwe tayari kufanya kazi kwa nguvu zako zote
kuhakikisha unafanikisha malengo uliyojiwekea. Hakikisha unaamka asubuhi na
kuanza kutekeleza majukumu yako ya kila siku na hata pale unapoenda kulala
fanya hivyo ukiwa katika picha kubwa ya lengo kubwa la maisha yako.
Husitegemee kuwa tajiri kwa fedha za
kurithi, fedha za bahati na sibu au fedha za kuokota. Watu wengi wanataka
utajiri lakini hawapo tayari kujibidisha ili wafikie utajiri huo, hawapo tayari
kujifunza, hawapo tayari kufanya kazi, hawapo tayari kutoa sadaka kwa ajili ya
kuupata utajiri na mbaya zaidi wengi wana fikra hasi kuwa ili uwe tajiri ni lazima
uende kwa wachawi au utajiri ni kwa ajili ya wateule wachache. Utajiri wa kweli
hauko hivyo bali ni lazima uandaliwe kwa kutumia misingi na mifumo ambayo
inakuhusisha wewe kama mhusika mkuu wa safari hii. Hii nikutokana na ukweli
kwamba matajiri wote wana sifa kubwa ya kufanya kazi za ziada kiasi kwamba kazi
wanazofanya kwa siku ni zaidi ya zile tunazofanya kwa mwezi mzima.
6. Kanuni ya Sita: Jifanyie tathmini
ambayo ni ya kweli. Ili uwe tajiri ni lazima ujifanyie upekuzi
kwanza. Katika upekuzi huu unatakiwa kufahamu ni tabia zipi ambazo
zimekufikisha hapo ulipo na hatimaye weka mikakati ya kukabiliana na tabia
ambazo zinakukwamisha. Kaa chini na fikiria ni tabia zipi ambazo ukianza
kuzifanya zitapelekea utajiri wako uongezeke na anza mara moja kuzifanyia kazi. Kuwa mkweli kwenye matumizi ya pesa
yako, muda, marafiki na manunuzi yako. Kisha
jenga tabia ya kutenga kiasi cha fedha kwenye kila shilingi inayoingia mkononi
mwako kwa ajili ya uwekezaji wa muda mfupi na muda mrefu.
7. Kanuni ya Saba: Fahamu imani/kauli zako
kuhusu pesa na vyanzo vya kauli hizo. Katika jamii tunazoishi
kuna kila kauli juu ya fedha na utajiri kwa ujumla. Wapo wanaoamini kuwa pesa
ni chanzo cha maovu yote, utajiri ni kwa wateule tu, matajiri ni watu wabaya,
warafi, wachoyo, wachawi kwa maana ya kwamba hauwezi kuwa na fedha na kwa
wakati huo huo ukawa msafi wa roho, ni afadhari kuwa maskini na kauli
nyinginezo. Je wewe imani/kauli zako juu ya fedha na utajiri ni zipi? Pata
muda wa kutafakari na hatimaye jipe imani/kauli mpya ambazo zitakupeleka kwenye
mtazamo mpya juu ya pesa na utajiri.
8. Kanuni ya Nane: Fahamu kuwa Utajiri ni
Mchakato na sio zawadi. Katika kutafuta utajiri ni lazima
ujitoe kufanya kazi kwa bidii ili fedha zifuatie kama zawadi kwa bidii na
ubunifu katika utendaji kazi wako. Kadri unavyofanyakazi kwa bidii na ubunifu
ndivyo utavyopata pesa zaidi.
9. Kanuni ya Tisa: Andaa sababu
zinazokusukuma kuwa tajiri. Hakikisha unaandaa sababu
za kwa nini unataka kuwa tajiri. Eleza nini utafanyia pesa zako pindi ukiwa na
pesa za ndoto yako, chagua ni starehe zipo utakuwanazo pindi ukiwa tajiri,
sehemu zipi utapenda kutembelea, vitega uchumi vipi utapenda kuwa navyo n.k.
Hapa unatakiwa kuandaa sababu ambazo zitakufanya uridhike na kufurahia utajiri
wako badala ya kuja kuangamizwa na utajiri wako. Pia andaa orodha ya vitu
ambavyo hautakuwa tayari kufanya kupitia utajiri wako ili kesho na keshokutwa
uongozwe na hiyo kuepuka matumizi mabaya ya fedha zako.
10. Kanuni
ya Kumi: Fahamu kuwa Pesa zinatengeneza Pesa. Tumia
pesa zako kuhakikisha zinatengeneza pesa nyingine zaidi na zaidi. Ndio maana
matajiri wanaendelea kuwa matajiri wakati masikini nao wanaendelea kuwa
masikini. Hivyo kwa kutumia kanuni
hii unatakiwa kutumia pesa kidogo ulizonazo sasa kwa ajili ya kuzalisha pesa
zaidi na zaidi kwani hiyo ndo njia pekee ya kuwa tajiri. Hakikisha unatenga
kiasi cha pesa katika pato lako kwa ajili ya kuwekeza ili kiasi hicho ndo
kitumike kama mbegu ya kuzalisha pesa nyingine. Kama ilivyo kwa mkulima au
mfugaji hawezi kula mbegu au mifugo yake yote na akategemea kuzalisha zaidi
shambani au mifugo kuongezeka ndivyo ilivyo kwenye fedha. Uamzi upo mikononi
mwako kati ya kuchagua kuwa masikini au kuwa kati ya matajiri.
11. Kanuni
ya Kumi na Moja: Kokotoa faida kabla ya kuwekeza fedha zako. Utajiri
ni hesabu hivyo unatakiwa kabla ya kuwekeza kwenye kitega uchumi chochote kile
ni lazima ufanye hesabu za kufahamu faida yako itakuwa kiasi gani hadi pale
utakapofanikiwa kurejesha kiasi ulichowekeza. Changanua faida na hasara kwenye
kila aina ya uwekezaji unaotaka kufanya. Unapochanganua faida za mradi flani
unatakiwa kukumbuka suala la kodi na gharama nyingine ambazo zitawezesha mradi
wako uendelee kukuingizia faida.
12. Kanuni
ya Kumi na Mbili: Kama utachukulia pesa kama suluhisho la matatizo utaiona kama
chanzo cha matatizo. Katika safari yako ya utajiri ni lazima
ukumbuke kuwa pesa hazitaweza kumaliza matatizo yako yote ya kimahusiano, afya,
kijamii, usalama, kiroho na furaha. Hivyo ni muhimu kufahamu fika matatizo yote
hayo wewe ndo muhusika mkuu wa kuyatatua na wala sio fedha zako. Fedha haziwezi
kukupa furaha ya kudumu, amani, upendo, kupunguza uzito wa mwili wako na
mengine mengi na badala yake vitu hivi vinaanzia ndani mwako.
13. Kanuni
ya Kumi na Tatu: Unaweza Kutengeneza Pesa za Kutosha, Unaweza Kuipenda Kazi
Yako na Unaweza Kupata Usingizi Vizuri. Kwenye jamii kumekuwepo na
upotoshaji kuwa ili kuwa tajiri ni lazima kwanza uuze roho yako au uwatoe
sadaka ndugu zako (maarufu kama ufreemason), uwe mchoyo, banifu, kukosa
usingizi na kukosa muda wa kuwajali watu wengine; lakini ukweli ni kwamba utajiri
wa kweli ni kinyume kabisa na mitazamo
hiyo. Hii ni kutokana na ukweli ambao tumeuona kwenye kanuni ya kwanza kuwa
fedha zipo nyingi na za kutosha kwa ajili ya yeyote yule ambaye anajua mbinu
halali za kuzitafuta na mbinu hizo zipo wazi kwa kila mmoja. Hivyo wewe ndo
mwamuzi wa maisha yako ya utajiri lakini muhimu ni kufahamu kuwa unaweza kuwa
tajiri na ukaendelea kupenda kazi yako na kupata usingizi vizuri tu.
14. Kanuni
ya Kumi na Nne: Husitengeneze Pesa kwa Kuwa Mtu Mbaya. Hakikisha
unatafuta utajiri kwa njia ambazo ni halali kwani pesa za namna hii ndo zitakupa
amani kutoka rohoni mwako tofauti na fedha za wizi, udanganyifu, rushwa, uchawi
au kwa kuvunja sheria kwa namna yoyote ile. Mwandishi anatufundisha kuwa ni
muhimu zoezi la kutengeneza fedha ulichukulie kama sehemu ya mchezo ambao uwa
unaupenda sana na hivyo uendelee kutengeneza fedha kwa kadri upendavyo kupitia
mchezo wa fedha. Hii ni kutokana na ukweli kwamba tunahitaji utajiri kwa ajili
ya kuendelea kuyaboresha maisha yetu hivyo hatupo tayari kuona utajiri wetu
unakuwa chanzo cha kutuweka mbali na wapendwa wetu, kazi zetu, nyumba zetu, hobi
zetu na mengine mengi.
15. Kanuni
ya Kumi na Tano: Fahamu Uhusiano Kati ya Pesa na Furaha. Ni
muhimu kufahamu kuwa pesa haiwezi kununua furaha. Wote ni mashahidi kuwa pesa
kidogo zinaweza kukufanya uwe na maisha ya uzuni hasa pale mahitaji ya pesa yanapozidi
kiasi ulichonacho. Hata hivyo wapo matajiri wengi ambao wanaishi maisha ya
uzuni pamoja na kwamba wana pesa nyingi. Muhimu ni kufahamu kuwa unaweza kuwa
masikini/tajiri na ukawa na furaha au ukakosa maisha ya furaha. Hivyo, jambo la
muhimu unatakiwa ufahamu kuwa furaha inaanzia ndani mwako pasipo kujali kipato
ulichonacho. Hii ni kutokana na ukweli kwamba sio pesa au vitu unavyomiliki
vitakufanya uwe na furaha bali furaha unaitengeneza mwenyewe.
16. Kanuni
ya Kumi na Sita: Fahamu Tofauti kati ya Bei na Thamani. Sio
lazima bei ya kitu iendane na thamani ya kitu hicho. Mfano, ni kawaida sana
kukuta chupa moja ya soda katika duka la kawaida inauzwa kwa shilingi 1,000/
lakini soda hiyohiyo ikauzwa kwa shilingi 5,000/ katika hotel kubwa. Kinachotofautisha
bei ni mazingira ambayo soda hiyo inatolewa kwa mteja. Somo la kujifunza ni
kwamba watu wapo tayari kulipia ongezeko la thamani ya huduma yako kuliko
thamani halisi ya huduma husika. Kama unataka kuwa tajiri ni lazima ufahamu
somo hili na kulitumia kwa ajili ya kuzalisha faida zaidi kwa ajili ya kuongeza
utajiri wako.
17. Kanuni
ya Kumi na Saba: Fahamu Jinsi Matajiri Wanavyofikri. Kama
unataka kuwa tajiri ni lazima uwe tayari kujifunza maisha ya matajiri jinsi wanavyofikria,
wanvyofanyakazi, wanavyovaa, wanavyotumia pesa zao na maisha yao kwa ujumla. Hii
ni kutokana na ukweli kwamba kama unaenda vitani kwa ajili ya ushindi ni lazima
utumie muda mwingi kumsoma mpinzani wako ili utakapokuwa kwenye uwanja wa vita
hasikusumbue. Ndivyo ilivyo kwenye kutengeneza utajiri ni lazima uwe tayari
kufahamu zaidi juu pesa, upate muda wa kuongea na matajiri, kusoma historia zao
na kuhakikisha unakuwa na kiu ya kufahamu mbinu wanazotumia kukuza utajiri wao.
18. Kanuni
ya Kumi na Nane: Husiwe na Wivu na Mafanikio ya Wengine. Wote
tunaweka juhudi kila mmoja kwa muda wake na kila mmoja mipango yake hivyo
hakuna sababu ya kuwa na wivu kwa mafanikio ya wengine kwani jinsi walivyo ni
matokeo ya jitihada na ubunifu katika kazi zao. Jambo la muhimu unaloweza kufanya
ni kujifunza kutoka kwao ili kufahamu namna ambavyo wamefanikisha ndoto za
maisha yao. Hivyo kila unapopata nafasi ya kukutana na mtu mwenye mafanikio
hakikisha unajifunza kitu kipya kutoka kwake. Fanya yale wanayoyafanya matajiri
na hatimaye na wewe utakuwa kama wao.
19. Kanuni
ya Kumi na Tisa: Kazi Ngumu ni Kujidhibiti Mwenyewe Kuliko Unavyopaswa Kudhibiti
Pesa Yako. Kazi kubwa iliyopo mbele yako ni wewe
kubadilika na kufanya yale yanayofanywa na matajiri. Kwa maana nyingine
kubadilisha tabia zako ili ziendane na tabia za matajiri. Hapa unapaswa
kujiuliza maswali kama haya; Je nipotayari kuanza safari ya utajiri? Je nipo
tayari kubadilika? Je nina nia ya kweli ya kuwa tajiri? Je nipo tayari
kuvumilia pasipo kukata tamaa? Je nipo tayari kujitoa sadaka? Je nina nguvu za
kutosha?. Majibu ya maswali haya ni mwanga tosha kuonesha kama upo tayari
kuanza safari ya utajiri. Ukifanikiwa katika hatua hii ndipo utagundua kuwa ni
vigumu kujidhibiti kuliko ambavyo utadhibiti pesa yako.
Mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri, haya ni machache kati ya mengi ambayo nimejifunza kwenye sehemu hii ya kwanza ya kitabu hiki cha The Rules of Money, naamini kama utayafanyia kazi yataboresha maisha yako. Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi (Unaposambaza makala hizi hakikisha haukopi na kupest badala yake share link ili hatimiliki za mwandishi wa makala ziheshimiwe). Nakutakia mapambano mema.
Uchambuzi wa kina wa kanuni zote (107) umeandaliwa kwa mfumo wa pdf na unapatikana kwa gharama ya Shilingi za Kitanzania (TSHS) elfu tano tu (5,000/=). Uchambuzi wa kanuni zote una jumla ya kurasa 39 na ni kitabu ambacho unaweza kusoma kwenye simu yako ya mkononi kama ni simu janja (smart phone) au kwenye kompyuta mpakato (pc).
Kupata uchambuzi wa kanuni zote tuma pesa yako kwa njia ya M-pesa au Airtel Money kupitia namba zifuatazo:-
M – Pesa tumia namba: 0763 745 451 (Majina ni Augustine Mathias)
Airtel Money tumia namba: 0786 881 155 (Majina ni Augustine Mathias)
Baada kutuma pesa hiyo nitumie ujumbe kwenye namba ya airtel (0786 881 155) ukiwa na barua pepe yako ili nikutumie uchambuzi wa kanuni hizi moja kwa moja kwenye mtandao wako.
Karibu kwenye mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI ili upate elimu isiyokuwa na mwisho.
Born to Win~Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: 0786881155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua pepe: fikrazatajiri@gmail.com
Ukurasa wa facebook: Fikra za Kitajiri: Fikri na Kutenda Kitajiri: Elimika na Tajirika