UCHAMBUZI WA KITABU The Rules of Life: A Personal Code for Living a Better, Happier and More Successful Kind of Life (Kanuni za Maisha: Mwongozo kwa kila Mtu Kuishi Maisha Bora, yenye furaha na kila aina ya mafanikio)

Habari ya leo rafiki na msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri. Ni matumaini yangu kuwa unaendeleza mapambano ya kuwa bora zaidi katika kila sekta ya maisha yako kupitia ushindi mdogo mdogo unaoupata kila siku. Leo hii ninakuletea uchambuzi maalumu wa kitabu cha The Rules of Life ambacho kimeandikwa na mwandishi mahiri na tajiri Richard Templar. Pia, unaweza kujifunza mengi kuhusiana na kanuni za pesa kutoka kwenye kitabu chake cha Rules of Money.

Soma: Kanuni za Pesa: Jinsi ya Kuzitengeneza na Jinsi ya Kuendelea Kutengeneza Pesa Zaidi

Kupitia kitabu hiki mwandishi anatushirikisha kanuni 106 za maisha ambazo kupitia uchambuzi huu nitakushirikisha kanuni 30 za mwanzo ikiwa ni mwanzo wa kukuletea uchambuzi wa kitabu hiki. 

Mwandishi anatushirikisha kuwa watu wote wanaangukia kwenye makundi mawili ya maisha; kundi la kwanza ni watu ambao wamefanikiwa kimaisha katika kila sekta kwa maana ya afya, kiroho, kijamii na kiuchumi. Watu hawa wanaishi maisha yenye furaha siku zote za maisha yao. Kundi la pili linajumuisha watu ambao wanaangaika kila mara kwa ajili ya kufanikiwa kimaisha na watu katika kundi hili wanaishi maisha yasiyo na furaha na mara nyingi wanateseka katika maisha yao ya kila siku.

Mwandishi anatumia kitabu hiki kutushirikisha kanuni mbalimbali ambazao kila mmoja wetu anaweza kuzitumia kwa ajili ya kuwa kati ya kundi la watu wenye mafanikio kwenye kila sekta ya maisha. 
Kupitia kitabu hiki tunafundishwa kanuni za maisha ambazo zinajumuisha kanuni binafsi ambazo zinatoa mwongozo wa kuishi maisha binafsi; kanuni za mahusiano zinatoa mwongozo wa maisha ya mahusiano na wenza wako; kanuni za maisha ya familia na urafiki ambazo zinatoa mwongozo wa kuishi maisha ya familia na urafiki kwa watu wa karibu na mwisho ni kanuni za mwongozo wa kuishi kwenye jamii inayotuzunguka.

Mwandishi anatukumbusha kuwa kanuni hizi sio kanuni mpya katika maisha yetu bali ni kanuni ambazo zipo katika maisha yetu ya kila siku japo namna ambavyo kila mmoja wetu anaziishi ndicho kipimo cha kututofautisha kimafanikio. 
Hivyo, kitabu hiki sio ufunuo wa kanuni mpya bali ni ukumbusho wa namna wa kuishi kanuni hizi katika maisha yetu ya kila siku. Hivyo, kanuni hizi ni rahisi, za kawaida na zinaweza kutumika kila sehemu. Karibu tujifunze wote machache niliyojifunza kwenye kitabu hiki;

SEHEMU YA KWANZA: KANUNI KWA AJILI YA NAFSI YAKO (Rules for You)
Katika sehemu hii mwandishi anatushirikisha kanuni mbalimbali kwa ajili ya mafanikio binafsi. Sehemu hii inajumuisha kanuni ambazo zitatusukuma kuamka asubuhi na mapema kwa ajili kufikia viwango tulivyojiwekea. Hii ni pamoja na kuwa na mtazamo chanya katika mazingira yanayotuzunguka sambamba na kupunguza msongo wa mawazo katika maisha yetu ya kila siku.

1. Kanuni ya Kwanza: Yafanye yawe siri yako. Kadri utakavyotumia sheria hizi, utajikuta katika mafanikio makubwa kwenye kila sekta ya maisha yako na kwa asili mwanadamu anavyofanikiwa zaidi ndivyo anatamani watu wengi wafahamu hatua alizofikia katika maisha yake. Sheria hii inatukumbusha umuhimu wa kuhakikisha tunatunza siri za mafanikio yetu kwa kadri tunavyoweza. Mwandishi anatushirikisha kuwa katika kanuni hii tunapaswa kuacha mafanikio yetu yazungumze yenyewe hivyo sisi hatupaswi kuyahubiri wala kushawishi watu kwa namna yoyote ile kuishi kanuni hizi. Kwa kifupi kanuni hii inatukumbusha kufanya vitu kimya kimya kwa kadri tunavyoweza.

2. Kanuni ya Pili: Kuzeeka ni lazima lakini si lazima kuwa na mwenye busara kadri umri unavyoongezeka. Tumezoea kusikia msemo wa “uzee ni busara”, katika kanuni hii mwandishi anatushirikisha kuwa si kweli kuwa uzee ni busara kwa wapo wazee ambao bado wanafanya makosa mengi katika maisha yao. Kanuni hii inatukumbusha kuwa bila kujali uzoefu wetu ni muhimu kuhakikisha tunajifunza kila mara kwa kadri tunavyoongezeka umri. Muhimu ni kuhakikisha kila mara tunajifunza kutokana na makosa tuliyoyafanya siku za nyuma na makosa hayo yasijirudie katika maisha yetu ya sasa. Hata hivyo, kadri tunavyojifunza kutokana na makosa ndivyo tunatakiwa kutambua kuwa sio watu wote wana busara. Kwa kanuni hii, wajibu wetu ni kujifunza kusamehe na kuwa na roho ya uvumilivu dhidi ya tabia mbaya za watu wanaotuzunguka.

3. Kanuni ya Tatu: Kubali kuwa kilichofanyika kimefanyika bila kujali kimenyika vipi. Mwandishi anatushirikisha kuwa watu wengi wanafanya makosa kwa kupenda au bila kufahamu kuwa wanafanya makosa hayo. Kanuni hii inalenga kutukumbusha kuwa hatutakiwi kuwa watumwa wa makosa tunayofanya siku nenda rudi. Hatupaswi kuishi dimbwi la hisia za kujutia makosa au kuwa na hasira kutokana na makosa tuliyofanya. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kadri unavyoishi maisha ya majuto na manunguniko ndivyo unatengeneza sumu ambayo inakuathiri ndani kwa ndani na hatimaye ni afya kudhoofika. Hii ni pamoja na kuhakikisha tunaondoa imani kandamizi na matukio ya kihistoria katika familia au makuzi yetu kwenye maisha ya sasa.

4. Kanuni ya Nne: Jikubali Mwenyewe. Bila kujali kasoro ulizonazo kutokana na historia au makosa yako ya nyuma sasa unatakiwa kujikubali kuwa wewe ni wewe na hakuna mwingine hivyo unatakiwa kujipenda kwa namna ya kipekee. Kumbuka kuwa hatuna uwezo wa kubadilisha yaliyotokea huko nyuma. Kanuni hii inatukumbusha kuwa baada ya kujikubali tunatakiwa kuainisha mapungufu tuliyonayo ili yawe msingi wa kubadilisha maisha yetu. Muhimu hapa ni kukumbuka kuwa tupo jinsi tulivyo kutokana na matukio yaliyotokea katika maisha yetu. Katika kanuni hii mwandishi anatufundisha kuwa hatutakiwi kuwa watu wa kutafuta mabaya ndani yetu na kuyabebea bango badala yake tunatakiwa kutambua kuwa mabaya yameshatokea na wajibu wetu ni kurudi kwenye mstari.

5. Kanuni ya Tano: Fahamu kipi chenye tija na kipi hakina tija. Kanuni hii inatukumbusha kuwa na uchaguzi sahihi katika maisha yetu. Yapo mengi ambayo tungependa kufanya au kujihusisha nayo katika maisha ya kila siku lakini kutokana na muda au uwezo kifedha tunajikuta hatuna uwezo wa kuyakamilisha. Hivyo, Kanuni hii inatutaka kujikita kwenye yale yenye tija na kuachana na mambo yasiyo na umuhimu katika maisha yetu kwa wakati husika. Kwa ujumla tunapaswa kujikita kwenye yale ambayo yanakamilisha matamanio ya mafanikio ya maisha yetu hasa kuwa na maisha yenye furaha. Fikiria zaidi ni yapi yenye tija katika maisha yako nay ape kipaumbele katika za maisha yako.

6. Kanuni ya Sita: Yatoe maisha yako kwa ajili ya ukamilisho wa kitu chenye thamani. Huwezi kujua yapi yenye tija au ambayo hayana tija kama hauna ramani ya maisha yako. Je maisha yetu tunayotoa kwa ajili ya ukamilisho wa nini katika ulimwengu? Tumeumbwa kwa ajili ya kukamilisha kitu hapa duniani na hicho ndicho kinayapa thamani maisha yetu. Wajibu wetu ni kutambua lipi ni kusudi la maisha yetu hapa duniani. Kanuni hii inatukumbusha umuhimu wa kuthamini maisha yetu na watu wanaotuzunguka hii ni kutokana ukweli kwamba ukamilisho wa kusudi la maisha yetu unatuzunguka kwenye yale tunayofanya kila siku. Kanuni inatukumbusha kutimiza wajibu wetu kwa ukamilisho kwa maana ya ubora wa hali ya juu.

7. Kanuni ya Saba: Kuwa na fikra huru. Haupaswi kuwa na fikra zilizofungwa kwenye baadhi imani au mitazamo katika maisha. Kufungwa kwenye imani au mitazamo mbalimbali ni mwanzo wa kushindwa kufikia viwango vya mafanikio unavyohitaji katika kila sekta ya maisha yako. Kanuni hii inatupa uwanja mpana wa kufikia malengo tunayojiwekea katika kila sekta ya maisha yetu. Hapa ndipo maisha tunatakiwa kuyaona kama mfululizo wa safari yenye kila aina ya uzoefu na matukio ya kuvutia na kila hatua ya safari hiyo inafungua nafasi kwetu kwa ajili ya kuburudika, kujifunza, kuvumbua vitu au sehemu mpya na kuongeza marafiki na uzoefu mpya. Kumbuka kuwa sio kila HAPANA ni HAPANA au kila NDIYO ni NDIYO, hivyo unahitaji kuwa na muda wako wa kutafuta zaidi ya kile unachoambiwa.

8. Kanuni ya Nane: Kuwa na hobi ya kujua jinsi dunia inavyokwenda nje ya maeneo uliyozoea. Kanuni hii inatukumbusha umuhimu wa kujifunza uzoefu mbalimbali kutoka sehemu tofauti za ulimwengu kwa kutumia mbinu mbalimbali za kujifunza kama vile kuangalia, kusoma, kutembea, kusikiliza, kuonja na kuongea. Mara zote lenga kujifunza mbinu mpya katika maisha hasa kwa kujaribu vitu vipya katika maisha. Hapa tunakumbushwa umuhimu wa kuwa na taarifa muhimu kuhusu yanayoendelea katika ulimwengu wa sasa kwenye fani za muziki, michezo, sayansi, filamu, kilimo, mawasiliano na biashara. Achana na mawazo au kauli kama vile “Sijawahi kufanya…., sitaki….” na kauli nyinginezo ambazo zinakuzuia kujaribu uzoefu mpya katika maisha yako.

9. Kanuni ya Tisa: Mara zote jitahidi kuwa upande wa Malaika na sio upande wa Ibilisi. Kila siku ya maisha yetu tunakabiliwa na maamuzi mengi ambayo mara nyingi yanaangukia kwenye pande mbili ambazo ni upande chanya au hasi. Kila uamuzi tunaofanya katika maisha yetu yanaathiri jamii inayotuzunguka, familia au dunia kwa ujumla wake na athari hizo zinaweza kuwa chanya au hasi. Katika kanuni hii mwandishi anatutaka kuhakikisha tunajitahidi kufanya maamuzi ya upande wa Malaika kwa maana ya kufanya maamuzi yenye athari chanya. Katika kanuni hii tunakabiliwa na changamoto ya kuhakikisha tunalinganisha mizania kati mema tunayotaka sisi dhidi ya jamii inayotuzunguka.

10. Kanuni ya Kumi: Samaki aliyekufa ndiye anaogelea kufuata mawimbi. Ukweli ni kwamba maisha ni magumu na tunatakiwa kumshukuru Mungu kwa ugumu huo maana kama maisha yangekuwa na marahisi kusingekuwa na haja ya kuthubutu au kuwa ubunifu wa kila aina. Kutambua hilo ni muhimu kuhakikisha tunapambana nyakati ngumu tunazokutana nazo katika maisha yetu ya kila siku. Ujumbe wa kanuni hii ni kwamba tunatakiwa kuhakikisha tunapambana na mawimbi yanayotukabili katika maisha yetu ya kila siku badala kukubali kuyumbishwa au kupelekwa na mawimbi hayo. Kumbuka kadri tunavyopamba ndivyo tunaimarika zaidi kwa mapambano yaliyopo mbele yetu.

11. Kanuni ya Kumi na Moja: Kuwa wa mwisho kutoa sauti yako. Kanuni hii inatukumbusha umuhimu wa kusikiliza kwanza kabla ya kuanza kutoa maamuzi. Kumbuka kuwa kadri unavyosikiliza kutoka kwa wengine ndivyo unakuwa na uelewa mpana kwenye mada unayotakiwa kutolea maamuzi. Pia, kanuni hii inatufundisha umuhimu wa kuachana na mabishano au ugomvi wa kila aina. Ni kanuni ngumu kuitekeleza hasa kama upo kwenye nyakati ambazo unaona kuwa umeonewa. Unafanikiwa kuepuka mabishano au ugomvi wowote jamii inayokuzunguka itakuona kuwa mtu mpole na mara zote watu wapole huwa wanaaminiwa na kutegemewa na jamii inayowazunguka.

12. Kanuni ya Kumi na Mbili: Kuwa na utamaduni wa kujishauri mwenyewe. Ndani ya nafsi zetu kuna chemichemi ya busara na hekima ambazo tunatakiwa kuzitumia kwa kusikiliza sauti yetu ya ndani. Sauti hii ndio inatuongoza kuchagua mema dhidi ya mabaya pale ambapo tunajifunza kuisikiliza na kuifuata. Pia, sauti hii mara nyingi inatuongoza katika kuomba msamaha na kusahihisha makosa tunayotenda katika maisha yetu ya kila siku. Mwandishi anatushirikisha kuwa muhimu tunatakiwa kujifunza kusikiliza sauti ya ndani ili sauti hiyo iwe mshauri mkuu wa kuchagua kufanya maamuzi yaliyo bora zaidi. Habari njema ni kwamba kadri unavyozoea kuisikiliza sauti ya ndani ndivyo sauti hiyo inakuwa mshauri mkuu ambaye unaongozana nae kila mahali unapokuwa.

13. Kanuni ya Kumi na Tatu: Hakuna hofu, hakuna mshangao, hakuna kusita na hakuna shaka. Moja, haupaswi kuwa na hofu juu ya kitu chochote katika maisha yetu ya kila siku. Ni kawaida mwanadamu kuwa na hofu ya vitu au matukio mbalimbali na hofu hii inatufanya tushindwe kufikia viwango vya mafanikio tunayoyataka. Kanuni hii inatukumbusha kuwa kwa namna yoyote ile tunatakiwa kushinda hofu ambazo zimekuwa zinatukabili kwenye maisha yetu ya kila siku.

Mbili, maisha yamejaa kila aina mashangazo, hata hivyo matukio mengi yanayoonekana kuwa ya kushangaza saikolojia inaonesha kuwa kabla ya hayajatokea yanaandaliwa na sisi bila kujua. Kanuni hii inatutaka kuwa makini katika matendo au fikra zetu ili muda wote tuwe macho kwa ajili ya kuepuka matukio ya mshangao kwenye maisha ya kila siku.


Tatu, watu wengi wanapoteza fursa nyingi kutokana na tabia ya kusita kuchukua maamuzi kwa muda muafaka. Kanuni inatukumbusha umuhimu wa kuhakikisha mara zote tupo macho kwa ajili ya fursa zinazojitokeza mbele yetu. Hatupaswi kusubiria msaada kutoka kwa watu wengine ili watufumbue macho kutambua fursa zilizopo maana kwa kufanya hivyo fursa nazo zitakuwa zimechukuliwa na wale ambao wapo makini muda wote.

Nne, baada ya kujiridhisha kwenye maamuzi unayotaka kuchukua haupaswi kuwa na shaka kiasi ambacho utajikuta unayarudia mara kwa mara. Epuka kuwa na wasiwasi dhidi ya maamuzi ambayo tayari umefanyia kazi. Jiamini na mara moja anza mara moja kutekeleza mpango ambao umeufanyia maamuzi ukiwa na uhakika kuwa utafanikiwa kwa kiwango kikubwa.

14. Kanuni ya Kumi na Nne: Natamani ningefanikisha hilo – na nitafakisha. Majuto ni sehemu ya maisha yetu hasa kutokana ukweli kwamba tunaweza kujutia fursa ambazo tulishindwa kuzitumia katika maisha yetu na fursa hizo pengine tunaona kuna watu walizichangamkia na zimewatoa kimaisha. Pia, tunaweza kujutia matokeo ya maamuzi ambayo tulichukua katika maisha yetu lakini pengine hayakuzaa matunda kama tulivyokusudia. Mwandishi katika kanuni hii kwanza anatukumbusha kuwa hatupaswi kuwa watu wa kukaa muda wote tunajutia kuwa kwa nini tukio fursa flani haikutokea kwenye maisha yetu. Pointi muhimu ya kujifunza ni kwamba katika jamii kuna watu ambao muda wote wanajiona kuwa hawana bahati na ndio maana wapo jinsi walivyo wakilinganisha na watu waliofanikiwa zaidi yao. Hatupaswi kwenye kundi la watu wa namna hii kutokana na ukweli kwamba hata kama tunajutia basi tuhakikishe majuto hayo yanakuwa sehemu ya kujifunza kuboresha maamuzi yetu. Hivyo baada ya kujuta kwa kauli ya “natamani…..” hakikisha kauli hiyo inafuatiwa na kauli ya “sasa nita…..”.

15. Kanuni ya Kumi na Tano: Wakati mwingine ni sahihi kukata tamaa. Mwandishi anatushirikisha kuwa mara nyingi tunajikuta tupo njia ambayo sahihi japo wakati tunaingia tulidhania kuwa ni njia sahihi na salama. Kanuni hii inatukumbusha umuhimu wa kufanya tathimini ya mara kwa mara dhidi ya maamuzi ambayo tunayatekeleza na pale ambapo tunajikuta kuwa tunaenda kinyume na matarajio hatuna budi kukata tamaa kwa ajili ya tafuta njia nyingine ambayo ni sahihi zaidi. Muhimu hapa tunakiwa kutofautisha kukata tama ambako kumeelezwa katika kanuni hii dhidi ya kukata tamaa ambako kumesababishwa na uzembe, uvivu, changamoto au kushindwa kuwajibika ipasavyo. Katika hali kama hiyo, kanuni inatukumbusha kuwa tunapaswa kung’ang’ana mpaka tufikie malengo tuliyojiwekea.

16. Kanuni ya Kumi na Sita: Hesabu moja mpaka kumi kabla ya kujibu au kuitikia kwa vitendo kama huna uhakika. Mwandishi anatushirikisha kuwa katika maisha ya kila siku mara nyingi tunajikuta kwenye hali ambayo tunatakiwa kutoa majibu ndani ya muda mfupi, kabla ya kujibu ni vyema kujipa muda wa kutafakari ili majibu tunayotoa yawe na uhalisia. Hii ni njia ambayo itakuongezea heshima kuliko kutoa majibu ambayo yatakufanya uonekane wa hovyo. Njia nzuri ya kukabiliana na hali kama hiyo ni kuhesabu moja mpaka kumi kimya kimya wakati ukijipa nafasi ya kutafakari.

17. Kanuni ya Kumi na Saba: Badilisha kinachowezekana achana na yasiyowezekana. Katika maisha ukweli ni kwamba tuna muda mfupi wa kukamilisha yale yote tunayokusudia kukamilisha katika maisha yetu. Kulingana na ukweli huu kuna kila sababu ya kuhakikisha tunatoa kipaumbele kwenye matukio ambayo ni ya muhimu na kuacha kupoteza muda kwenye matukio ambayo hayana tija. Hakikisha unafanyia kazi ambayo una uwezo wa kuyabadilisha na achana na yale ambayo ni vigumu kuyabadilisha. Kanuni hii itakusaidia kukamilisha mambo mengi katika maisha kuliko kugusa na kila sehemu na kuacha bila kukamilisha.

18. Kanuni ya Kumi na Nane: Lenga kuwa bora zaidi katika kila unachokifanya – Na sio kufanya kwa mazoea. Mwandishi anatushirikisha kuwa kanuni hii inatutaka kuhakikisha kila tunachofanya tutimize wajibu wetu kwa ubora au weledi wa hali ya juu ili kuhakikisha matendo yetu yanakuwa chachu ya kubadilisha ulimwengu kuwa mahala pazuri pa kuishi. Kama ni mfanyakazi hakikisha unatimiza majukumu yako kiasi ambacho hakuna mtu ataweza kufikia viwango vyako, kama ni mzazi hakikisha unakuwa mzazi na mlezi bora kuliko wote waliowahi kuwepo, kama ni mwanasiasa hakikisha unakuwa mwanasiasa bora kuliko wote kwa kugusa maisha ya wananchi na kama ni mwalimu hakikisha unakuwa mwalimu bora kuliko wote. Hakika kununi hii inatukumbusha kupenda kazi zetu, kutokana na hilo tunapaswa kutimiza majukumu kwa kuongozwa na mapenzi ya kazi na sio kwa ajili ya malipo. Hapa tunapaswa kujiwekea viwango vya juu katika utendaji kazi wetu na kuhakikisha viwango hivyo vinaboreshwa mara kwa mara.

19. Kanuni ya Kumi na Tisa: Husitegemee kuwa mkamilifu. Sisi ni binadamu na hivyo hatutegemei kuwa wakamilifu katika kila jambo tunalofanya. Kutokana na ukweli huu mwandishi anatushirikisha kuwa pale tunapokosea au kushindwa kufikia matarajio tusikate tamaa maana kuna somo kubwa ambalo unajifunza kutokana na makosa au kutofikia matarajio. Pia, mwandishi anatukumbusha kuwa kutokana na kutokuwa wakamilifu hatupaswi kuwakatisha tamaa wengine kwani mara zote tunahitaji kuwa na kiu ya kujifunza kutoka kwa wanaotuzunguka. Kumbuka kuwa wewe ulivyo ni zao la mafanikio na makosa mbalimbali ambayo yametokea katika historia ya Mkoa wako.

20. Kanunu ya Ishirini: Mara zote husiogope kuwa na ndoto. Katika kanuni hii mwandishi anatushirikisha kuwa kati ya vitu ambavyo haupaswi kujiwekea ukomo ni kwenye ndoto kutokana na ukweli kwamba sio lazima ndoto ziwe na uhalisia. Kumbe kanuni hii inatutaka kuwa na ndoto tena ndoto kubwa kwa ajili ya maono ya maisha yetu tena ndoto ambazo zinatufanya tuziogope kila tunapozifikiria. Kumbuka kuwa watu wengi wanashindwa kuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa wamekuwa na ndoto finyu. Kwa maana nyingine kadri unavyokuwa na ndoto finyu ndivyo unavyopata matokeo finyu.

21. Kanuni ya Ishirini na Moja: Kama unahitaji kuruka nje ya daraja kabla ya kufanya hivyo hakikisha unajua urefu wa maji. Kanuni hii inatukumbusha umuhimu wa kuchukua tahadhari katika maamuzi yetu kwenye maisha ya kila siku. Katika maisha ni mara nyingi tunajikuta katika nyakati za kujiuliza hivi ni kwa nini nimefanya au kuhusika kwenye tukio la hovyo kama hili. Mwandishi anatushirikisha kuwa ili kuepukana na nyakati kama hizo katika maisha ya kila siku ni lazima kuhakikisha kabla ya kufanya maamuzi yoyote tunakuwa na uchambuzi wa athari za matokeo ya maamuzi hayo.

22. Kanuni ya Ishirini na Mbili: Husikubali kuendeshwa na historia ya maisha yako. Ya nyuma yamepita ni kwa nini ukubali kuwa mtumwa wa matukio ya nyuma. Kumbuka kuwa hauwezi kubadili lolote kati ya matukio ya historia ya maisha yako lakini una uwezo mkubwa wa kubadilisha matukio ya maisha yako ya sasa kwa ajili ya maisha ya baadae. Kumbe kipaumbele kikubwa katika maisha yetu si katika namna tulivyoishi siku zilizopita bali ni kwa namna gani tunatakiwa kuishi katika maisha ya sasa. Kumbuka pia kuwa maamuzi ya sasa kwenye maisha yako ya kila siku yana nafasi kubwa ya kubadilisha maisha yako yajayo katika upande chanya au hasi. Hivyo, husikubali kuja kujutia maamuzi unayofanya sasa katika siku zijazo na vivyo hivyo husiendelee kujutia matukio au matendo uliyofanya siku zilizopita na badala yake kuwa na mikakati ya kuachana na yote unayoona hayakuwa sahihi katika historia ya maisha yako. Ishi hapa, ishi sasa na ishi kulingana na nyakati za wakati husika.

23. Kanuni ya Ishirini na Tatu: Husiishi katika wakati ujao. Mwandishi anatushirikisha kuwa watu wengi wanaishi kwa kutegemea kuwa nyakati zijazo ndizo zitakuwa na zenye neema kubwa katika maisha. Kumbe hapa ndipo wengi tunakosea kutokana na ukweli kwamba hakuna mwenye uhakika wa maisha yake siku zijazo. Pia, hapa tunahitaji kukumbuka kuwa hakuna siku ambayo mwanadamu ataridhika na hali iliyopo hasa katika mahitaji ya kila siku. Kumbe, kama ni furaha hakikisha kila sekunde ya maisha yako inakupa furaha ya ndoto zako, vivyo hivyo kwa kila tamanio la maisha yako. Penda kana kwamba kesho hautakuwa na muda wa kupenda tena; furahia maisha kana kwamba kesho hautakuwepo; fanya kazi kana kwamba hakuna siku nyingine ya kufanya kazi kama sasa; wekeza kana kwamba hauna muda wa kuwekeza tena; patanisha na kufariji kana kwamba kesho hautaweza kufanya hivyo; na kadhalika na kadhalika. Katika yote ni muhimu kujivunia kuwa na nguvu za kukuwezesha kuendelea kupumua au kuwa hai katika kila sekunde ya maisha yetu na hivyo kuishi maisha kwa ukamilifu wake wa sasa na bila kujali upo sehemu ipi, una nini au unaumwa.

24. Kanuni ya Ishirini na Nne: Endelea na maisha ukiepuka kelele za yaliyopita. Mwandishi anatushirikisha kuwa kamwe kasi ya maisha haiwezi kupungua kadri umri wako unavyoongezeka na badala yake kasi itaendelea kuongezeka zaidi. Kasi hii ya maisha inaendelea kusababisha presha na msongo wa mawazo kwa watu wengi kadri umri wao unavyoongezeka. Ili kuepukana na presha/msongo wa mawazo, mwandishi anatushirikisha kuwa baada ya kuwa na ndoto kubwa za maisha sasa tunatakiwa kuwa na mpango mkakati wa kutimiza ndoto hizo. Mpango mkakati huu sasa tofauti na ndoto wenyewe unatakiwa kuwa na uhalisia na muda maalumu wa kufikia malengo ndani ya mkakati husika. Hivyo, katika maisha hakikisha una mpango mkakati wa ukuaji kwenye kila sekta ya maisha ambao unautekelezwa kila siku ya maisha yako. Ili ufanikiwa kuwa na mpango mkakati bora wa maisha ni lazima kwa utambue ni nini unahitaji kukamilisha katika siku za maisha yako.

25. Kanuni ya Ishirini na Tano: Ishi kwa kufuata misingi ya maisha yako – husiwe mtu wa kuyumba yumba. Mwandishi anatushirikisha kuwa katika maisha unahitaji kuwa na misingi au kanuni unazozifuata na kanuni hizo unapaswa kuziishi siku zote za maisha yako. Epuka kuwa maji ya moto, vuguvugu na baridi katika nyakati tofauti za maisha yako wakati wewe ni yule yule. Epuka kuwa mnafiki dhidi ya nafsi yako na badala chora mstari ambao mara zote jitahidi kuufuata siku zote za maisha yako. Hata hivyo, unatakiwa kuhakikisha misingi unayoifuata inafahamika kwa watu wako wa karibu ili iwe rahisi kwao kuishi na wewe katika maisha yako ya kila siku.
  
26. Kanuni ya Ishirini na Sita: Vaa kana kwamba kila siku ni muhimu kwako. Siku muhimu kwako ni leo kwani leo ndio siku ambayo una uhakika nayo na wala sio kesho. Mwandishi anatushirikisha kuwa kutokana na ukweli kuwa leo ndio siku muhimu katika maisha yetu hivyo hatuna budi kuiheshimu kila siku tunayobahatika kuiona. Na hatuwezi kufanya hivyo kama hatujitambua sisi ni nani na tupo kwa ajili ya kukamilisha yapi katika maisha yetu. Kila siku amka asubuhi andaa nguo safi, piga mswaki, nyoa ndevu, weka vizuri nywele zako n.k kwa ajili ya mwonekano bora, mvuto bora au kujihisi vyema katika shughuli zako za siku husika. Hakika kama utafanikiwa kufanya hivi kila siku utapata maajabu ambayo yatapelekea uweze kujiamini, kuheshimika na kuaminiwa pia na jamii inayokuzunguka.

27. Kanuni ya Ishirini na Saba: Kuwa na mfumo wa imani. Mwandishi anatushirikisha kuwa imani ina nguvu ya kumuongoza mtu yeyote katika siku za neema au siku za kilio. Kumbe, hapa tunakumbushwa kuwa wenye imani thabiti wanaweza kustawi katika nyakati zote ziwe za neema au kilio kuliko wale ambao hawana imani katika maisha yao. Hapa tunahitaji kufahamu kuwa imani ni kuwa na matarajio juu ya mambo yanayosadikika katika ulimwengu huu, kuhusu kuumbika kwa ulimwengu, viumbe vilivyomo na hata maisha ya baadae baada ya maisha ya hapa duniani. Hivyo, katika maisha hakikisha una mfumo wa imani na hakikisha imani hiyo inakuongoza katika kila sekta ya maisha yako na imani hiyo iwe siri yako kwani si lazima watu wote waamini katika kile unachoamini.

28. Kanuni ya Ishirini na Nane: Tenga nafasi kidogo kwa ajili yako katika ratiba yako ya kila siku. Mwandishi anatushirikisha kuwa kanuni hii ni ngumu kwa watu wengi kwa kuzingatia kuwa ratiba za walio wengi zimejazwa maangaiko kwa ajili ya watu wao karibu au majukumu yao ya kila siku. Kumbe wanashindwa kutenga muda kidogo kila siku kwa ajili ya kupumzisha kila kitu, kuwa na nguvu mpya na hata kuwa kujihuisha upya. Tenga dakika 20 hadi 30 kwa ajili yako pekee, ndiyo, kwa ajili yako pekee kwani muda huo ndio wa kujifanyia sevisi kwenye kila sekta ya maisha yako. Tumia muda huu kwa ajili mapumziko tu bila kufanya chochote zaidi ya kuvuta pumzi na kufurahia uhai ulionao. Unaweza kuchagua sehemu bora ya kujipumzisha kama vile kwenye bustani au sehemu yoyote ile ambayo haina mwingiliano au makelele ya watu.

29. Kanuni ya Ishirini na Tisa: Kuwa na mpango. Mpango unakupa ramani, dira, njia, lengo, shabaha, mkakati na mwongozo wa maisha yako. Mpango huu unakuelekeza ni wapi unatakiwa kufika na lini unatakiwa kufikia hapo. Kumbuka kuwa kama una tamanio lolote la maisha yako pasipo kuwa na mpango tamanio hilo litaendelea kuwa ni ndoto tu. Ukishakuwa na mpango njia za kufikia mpango huo ndizo sasa unatakiwa kuzifanyia kazi. Tekeleza njia hizo katika maisha yako ya kila siku na hatimaye hakikisha unafanya mapitio ya mpango wako ili kujua kama unakupeleka unakokusudia kufika.

30. Kanuni ya Thelathini: Kuwa mcheshi/mchangamfu. Katika kanuni hii mwandishi anatushirikisha kuwa maisha ni magumu kulingana na majukumu ya kila siku tunayopambana nayo. Hata hivyo, ugumu wa maisha sio tiketi ya kushinda siku nzima umenuna badala yake kila dakika unahitaji kuwa mcheshi na mwenye tabasamu kwa wanaokuzunguka. Furahia kila dakika inayopita katika maisha yako pasipo kujali hali ya maisha unayopitia na njia bora ya kufanya hivyo ni kujenga utamaduni wa kujinenea kauli nzuri na pengine kujicheka mwenyewe dhidi ya matendo unayoona hayajaenda sawa. Kwa kufanya hivyo unapata msukumo wa kujirekebisha kabla hata wanaokuzunguka hawajaona makosa yako. Pia, njia nyingine ya kuwa mchangamfu muda wote ni mara zote kutafuta hali chanya katika kila tukio badala ya hali hasi.

Hizo ni kanuni 30 kati ya 106 ambazo mwandishi Richard Templar anatushirikisha katika kitabu hiki. Endelea kutembelea mtandao huu kwa ajili ya uchambuzi wa kanuni zote.

NB:
Uchambuzi wa kina wa kanuni zote (107) za kitabu cha Rules of Money (Kanuni za Pesa) umeandaliwa kwa mfumo wa pdf na unapatikana kwa gharama ya Shilingi za Kitanzania (TSHS) elfu tano tu (5,000/=). Uchambuzi wa kanuni zote una jumla ya kurasa 39 na ni kitabu ambacho unaweza kusoma kwenye simu yako ya mkononi kama ni simu janja (smart phone) au kwenye kompyuta mpakato (pc).



Kupata uchambuzi wa kanuni zote tuma pesa yako kwa njia ya M-pesa au Airtel Money kupitia namba zifuatazo:-


M – Pesa tumia namba: 0763 745 451 (Majina ni Augustine Mathias)
Airtel Money tumia namba: 0786 881 155 (Majina ni Augustine Mathias)

Baada kutuma pesa hiyo nitumie ujumbe kwenye namba ya airtel (0786 881 155) ukiwa na barua pepe yako ili nikutumie uchambuzi wa kanuni hizi moja kwa moja kwenye mtandao wako.

Karibu kwenye mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI ili upate elimu isiyokuwa na mwisho.

Born to Win~Dream Big 

Augustine Mathias Bilondwa

Namba ya Simu:      0786881155
Mwanzilishi wa Mtandao wa 
fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua pepe:  fikrazatajiri@gmail.com

onclick='window.open(