NENO LA LEO (MACHI 29, 2020): *[JIBU] JE NAWEZA KUWA TAJIRI KWA KUAJIRIWA?*

👉🏾Habari ya asubuhi rafiki yangu na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni siku nyingine tena ambayo tumezawadiwa uhai kwa ajili ya kuendeleza bidii za kuishi ndoto za maisha yetu. Hakika siku zinakimbia kama bado haujaanza kutekeleza kwa vitendo malengo uliyojiwekea katika kipindi cha mwaka huu 2020 ni wakati wa kuamka usingizini maana robo ya kwanza ya mwaka inaelekea ukingoni.

JIUNGE NA KUNDI LA WHATSAPP LA FIKRA ZA KITAJIRI KWA  KUBONYEZA HAPA NA KUJIUNGA BURE. Jiunge sasa nafasi ni chache.

✍🏾Karibu katika neno la tafakari ya leo ambapo nitajibu swali la mwenzetu ambaye aliuzia juu ya kwanini watu wengi wenye mafanikio kifedha hawapendi kuajiriwa. Kwanza nitoe pongezi kwa muuliza swali lakini pia kwa wale waliochangia mada ndani ya kundi. Naungana na mjadala uliokuwepo kuhusiana na mada hiyo japo sikuwa na wa kushiriki nanyi.
✍🏾 Ukweli ni kwamba kuna imani nyingi katika jamii tunayoishi kuhusiana na utajiri na wafanyakazi. Wapo watu wengi katika jamii ambao wanapowatazama wafanyakazi wanaona kuwa tayari wamefanikiwa kimaisha. Ni kutokana imani hizo watu wengi wanaamini wafanyakazi wana hela nyingi hasa kwa vile kila mwisho wa mwezi wana uhakika wa kupata mshahara.
✍🏾Hali hii inatokana na maisha ambayo wafanyakazi wengi wanaishi katika jamii inayozunguka. Ukweli ni kwamba wafanyakazi walio wengi wanaishi maisha ya kuigiza. Wengi kwa nje wanaonekana matajiri lakini ndani ya mioyo yao kuna msongamano wa mambo mengi. Wapo ambao ni watumiaji wakubwa kwenye kumbi za starehe, wapo ambao wanabadilisha magari tena yenye thamani kutokana na mikopo, wapo ambao wanapanga kwenye nyumba za kifahari na wapo ambao wamefanikiwa kujenga nyumba nzuri za kuishi na hata za kupangisha kutokana na mikopo au matumizi ya pesa za Serikali kinyume na taratibu. Hata hivyo, wapo baadhi ya wafanyakazi ambao wanaendesha maisha yao kwa kufuata misingi ya kanuni za pesa.
✍🏾Niweke wazi kuwa binafsi ni Mwajiriwa wa Serikali katika ngazi nzuri ya kiutawala (Afisa Misitu wa Mkoa). Kutokana na ajira hii nimejifunza mengi ambayo hakika ni kipindi muhimu katika maisha yangu. Nilianza kazi mwishoni mwa mwaka 2013 na nategemea kustaafu mwishoni mwa mwaka 2025 nikiwa na umri wa miaka 40. Hapa nalenga kukuonesha kuwa hata kama umeajiriwa unatakiwa ufanye kazi hiyo ukiwa na malengo binafsi.

*Zifuatazo ni faida za ajira kuelekea kwenye Uhuru wa kifedha*
✍🏾Ajira ni sehemu ambapo unaweza kukusanya mtaji wa kuanzisha uwekezaji mbalimbali. Unapofanya kazi hautakiwi kutegemea mshahara kuwa utakuwezesha kumaliza mahitaji yako ya kipesa. Wafanyakazi wengi ambao wanakidhi mahitaji yao ya kipesa bila kuwa na msongo wa mawazo ni wale ambao nje ya muda wao wa kazi wana miradi kadhaa ya kujiongezea kipato.
✍🏾Mfanyakazi ajira yake ni dhamana kwenye taasisi za fedha. Ukweli ni kwamba masharti ya kukopa kwenye taasisi za fedha kama hauna dhamana in mengi na yanaambatana na riba kubwa. Hila kwa mwajiriwa ni tofauti maana Mwajiri wake anabeba dhamana hivyo kuwa rahisi kupata mikopo yenye riba nafuu. Mfano kwa watumishi wa Serikali kuu kuna mikopo yenye riba ya asilimia 4℅. Hata hivyo wengi wanakopa bila kufuata kanuni za pesa na kujikuta mikopo hiyo inawaingiza kwenye shimo kubwa.
✍🏾Ajira ni sehemu ambapo unaweza kupata taarifa za fursa nyingi hasa zinazojitokeza kwenye taasisi unayofanyia kazi. Mfano, mwajiriwa wa Serikali ni rahisi kufahamu fursa zilizopo Serikalini kabla ya watu wengine nje ya mfumo. Ukiwa na macho pamoja na uwezo kifedha utafaidika na fursa hizo.

*Changamoto ya ajira katika kuelekea kwenye Uhuru wa kifedha*
✍🏾Ajira ni utumwa kutokana na ukweli kwamba ili upate mshahara ni lazima uuze muda, maarifa, uhuru na nguvu zako kwa mwajiri wako. Hapa ndipo changamoto inakoanzia unaweza kuwa unalipwa mshahara mkubwa lakini hauna muda wa kufanya shughuli zako za kukuza kipato chako. Mfano, wafanyakazi wengi wa mashirika yasiyo ya kiserikali wanapata mishaharamishahara mikubwa lakini hawana muda wa kufanya shughuli za ziada za kyjiongezea kipato. Matokeo yake ni kwamba mfanyakazi wa Serikali ambaye ana muda wa kutosha na anautumia vizuri anaweza kutengeneza kipato sawa na huyo aliyeajiriwa kwenye mashirika au sekta binafsi.
✍🏾Mshahara hauwezi kukufanya uwe tajiri. Wanaokokotoa kiwango cha mshahara huwa wanazingatia kiwango ambacho kitakidhi mahitaji ya kawaida ili mtumishi aweze kuendelea kuitimikia kazi yake. Kama mshahara ungetosheleza mahitaji yote na kubakiwa na ziada wengi wenye akili wangeacha kazi na kufanya shughuli zao. Pia wapo ambao wangeshindwa kufanya kazi kwa kuendekeza starehe kutokana na wingi wa pesa wanazopata.
✍🏾Ajira ni sehemu ambapo unatekeleza mipango ya mtu au taasisi na siyo mipango binafsi. Hapa ajira inaweza kuwa chanzo cha kujichelewesha kwenye mipango binafsi kwa kuwa mipango yako inaingiliwa na majukumu yako ya kazi.

*Je niache kazi na kujiajiri?* Ndiyo ili uwe na uhuru wa kushugulika na majukumu yako huna budi kuacha kazi na kujiajiri mwenyewe. Hila kabla ya kufanya hivyo hakikisha umeweka vitega uchumi ambavyo vinakuingizia kipato sawa/zaidi ya mshahara unaopata. Huwa kuna usemi maarufu kuwa husichome meli unayosafiria kabla kuwa na mbadala ambao utakuvusha salama. Hivyo kabla ya kuacha kazi weka mazingira ya kukuvusha salama katika kipindi ambacho utakuwa hauna kazi. Hii ni pamoja na kuweka mpango kazi ambao unaufanyia kazi kila siku kabla ya kuacha kazi.
✍🏾Mwisho, neno la tafakari ya leo limetukumbusha kuwa ajira inaweza kuwa sehemu ya kufikia utajiri wa ndoto yako au ikawa sehemu ya kuishi mshahara kwa mshahara. Wajibu wako ni kuhakikisha upata maarifa sahihi juu ya matumizi ya pesa unayopata kutokana na mshahara wako. *Naendelea kukumbusha kupata nakala yako ya uchambuzi wa kitabu cha Rules of Money ambacho utapata kanuni 107 kuhusu pesa.*
👐🏾Nakutakia kila la kheri kwenye siku hii ya leo. Kumbuka husikose kutoa mrejesho wa kile ambacho unajifunza kutokana na uwepo wako kwenye kundi hili.

*BON TO WIN ~ DREAM BIG*
🗣🗣 *Mwalimu Augustine Mathias*
Mawasiliano: 0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua pepe: fikrazakitajiri@gmail.com
Tovuti: fikrazakitajiri.blogspot.com
Kujiunga Kundi la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI, bofya link hii:https://chat.whatsapp.com/JACBxr9kX7K0qt58cQTrrw
onclick='window.open(