Ni matumaini yangu kuwa unaendelea
kupambana kwa ajili ya ukamilisho wa maisha yako. Leo hii nakuletea uchambuzi
wa kitabu cha mpendwa wetu Marehemu Dr. Reginald Mengi cha I Can, I Must, I Will. Kitabu hiki
nilikinunua kwa TSHS 35,000/= mnamo mwezi Machi, 2019 kwenye duka moja la
Vitabu Mkoani Morogoro. Niliomba sana kupunguziwa bei lakini bahati mbaya
muuzaji kwanza hakuwa na lugha nzuri kwa wateja hivyo ilinibidi tu ninunue kwa
kuwa nilishazunguka kwenye duka jingine na kuambiwa kuwa walikuwa wameishiwa.
Ninachohitaji
kukushirikisha hapa wala si bei niliyonunulia wala tabia ya muuzaji wa duka
bali ni ile nia ya dhati niliyokuwa ya kupata kitabu hiki ambacho niliamini
kitaniwezesha kujifunza mengi kutoka kwa mwanamafanikio nguli wa Kitanzania
aliyeanzia chini kabisa na kufanikiwa kuwa miongoni mwa matajiri ndani ya ardhi
ya Tanzania na hata Africa kwa ujumla. Bahati mbaya nilipomaliza kusoma kitabu
hiki mnamo mwezi Aprili, 2019 nikiwa najiandaa kuwashirikisha wengine
nilichojifunza ndani ya kitabu hiki nikawa nimepata ajali ya pikipiki ambayo
imenifanya niuguze mguu kwa kipindi cha mwezi hadi sasa bila kufanya chochote.
Mungu ni mwema naendelea vizuri kiasi ambacho hata leo nina nguvu za kuendelea
kushirikisha mengi ninayojifunza kwenye vitabu mbalimbali.
Nikiwa nimelazwa
hospitali baada ya ajali ndipo nikapata habari za kifo cha ghafla cha Dr.
Reginald Abraham Mengi, hakika sikuamini taarifa hizo maana ni kama vile
nilikuwa naangaza maisha yake yote kupitia kitabu hiki. Kila nilivyokuwa
naangaza maisha yake nilimuona Mzee Mengi akiwa anaelekea kwenye mafanikio
makubwa zaidi aliyokuwa nayo wakati anaandika kitabu kutokana na misimamo ya
hali ya juu niliyojifunza juu yake. Hakika Dr. Mengi umeondoka muda ambao sisi
kama vijana tulikuwa bado tuna mengi ya kujifunza kutoka kwako.
Hata hivyo, pamoja na
kwamba umeondoka tukiwa bado tunahitaji mengi kutoka kwako kama lilivyo jina
lako, hakika tunashukuru kwa zawadi ya urithi wa vizazi na vizazi uliyotuachia
kwa ajili ya kuboresha sekta mbalimbali za maisha yetu.
Baada ya kukushirikisha
hayo machache kuhusiana na masikitiko ya juu ya kifo cha Mpendwa wetu Dr.
Reginald Abraham Mengi, karibu nikushirikishe machache niliyojifunza kwenye
urithi aliotuachia mimi na wewe. Kwa ujumla kupitia kitabu hiki Dr. Mengi
ametushirikisha maisha yake kuanzia akiwa mtoto, akiwa mwanafunzi, wakati
anaanzisha biashara yake ya kwanza, namna alivyopanua biashara zake, wajibu
aliokuwa nao kwa jamii, misimamo yake kwenye mfumo wa Serikali kwa awamu zote
tano, wajibu wake kwenye uhifadhi wa mazingira na matarajio yake kwenye kukuza
biashara kwa siku za baadae. Karibu tujifunze machache kati ya mengi yaliyopo
kwenye kitabu hiki:-
A. KUHUSU VIKWAZO VYA KUANZISHA BIASHARA
1.
Hakuna wakati ulio sahihi
zaidi kwako kuanzisha biashara.
Kupitia kitabu hiki
mwandishi anatushirikisha kuwa kinachoamua ni wakati uanzishe biashara ni
dhamira ya kweli kutoka ndani ambayo kila mara inakupa msukumo wa kuchukua
hatua dhidi ya fursa iliyopo mikononi mwako. Naamini wengi wetu tumeshindwa
kuchukua hatua za kuanzisha biashara kwa vile kila wakati tunaona kuwa wakati
sahihi wa kuanzisha biashara bado haujafika aidha kutokana na hali ya kimfumo,
mtaji, historia au mazingira. Kumbe tunachofundishwa kupitia kitabu hiki ni
kuwa mara zote tunahitaji: kuongozwa na dhamira ya kweli ambayo kila mara
inatupa msukumo; kuwa na roho ya kuthubutu; kuwa wabunifu na kutokuogopa hatari
(risk) zinazoweza kujitokeza katika biashara husika.
2.
Kamwe historia haina
nafasi ya kuamua mafanikio ya mtu.
Kupitia kitabu hiki
Mwandishi anatushirikisha kuwa pamoja na kwamba familia ya mzee wake ilikuwa familia
masikini kiasi ambacho alikuwa akienda shuleni peku, lakini historia hiyo ya
maisha haikuwa kikwazo kwake yeye au kaka yake aitwaye Elitira Mengi kufikia
mafanikio waliyofikia. Kupitia kitabu hiki anatushirikisha namna ambavyo kaka
huyo alianzia biashara ya chini kabisa ikiwa ni pamoja na kuuza mayai mpaka
akafikia hatua tajiri Mkubwa Mkoani Kilimanjaro mwenye asili ya Tanzania na
hata kujenga nyumba ya ghorofa katika kipindi cha utawala wa Rais JK Nyerere.
Hapa tunahitaji kujifunza kuwa mlango wa mafanikio upo wazi kila mmoja wetu
bila kujali historia ya maisha yake. Muhimu ni kutambua nini unataka katika
maisha yako na kuangalia fursa zilizopo ili fursa hizo zibadilishwe kutoka
kwenye changamoto na kuwa biashara.
3.
Mfumo wa Serikali si
kigezo cha kushindwa kufikia mafanikio.
Hapa mwandishi
anatushirikisha namna ambavyo baada ya kurudi kutoka Scotland ambako alisomea
uhasibu na kufanya kazi alikutana na Tanzania mpya ambayo kipindi hicho Sera ya
Ujamaa ilikuwa ndo misingi ya utawala wa Mwalimu JK Nyerere. Sekta nyingi za
uzalishaji mali zilikuwa chini ya Serikali na baadhi ya Wafanyabiashara wenye
asili ya India pamoja na wazawa akiwemo kaka yake Elitira walinyanganywa mali
zao na mali hizo kuwa mali za Serikali. Hata hivyo, hali hii haikuwa kigezo kwa
Dr. Mengi kutulia na kuacha kutafuta fursa. Ni katika kipindi hiki mwishoni mwa
utawala wa Mwalimu JK Nyerere, Dr. Mengi alianzisha kiwanda chake cha kwanza
cha kalamu chini ya Kampuni ya Tanzania Kalamu Company Limited. Somo kubwa
hapa, tujiulize ni mara ngapi tunalalamikia mifumo iliyopo kama kikwazo cha
kupata mafanikio zaidi.
4. Mafanikio kwenye taaluma yako yasiwe kikwazo cha kutokuchukua
hatua za kiabiashara.
Mwandishi anatushirikisha
kuwa baada ya kurejea kutoka Scotland aliendelea kufanya kazi na Taasisi
isiyokuwa ya Serikali iliyojulikana kwa jina la Cooper and Lybrand (C&L) jambo
lilomfanya aonekane kuwa sio mzalendo kwa nchi yake ikizingatiwa kuwa kipindi
hicho nchi ilikuwa kwenye Sera ya Ujamaa. Hata hivyo, Dr. Mengi hakuvunjika
moyo aliendelea kutimiza majukumu yake kiasi ambacho hata wakuu walianza
kutambua mchango wake. Katika kipindi hicho cha kilele cha mafanikio katika
kazi yake alianza kupata teuzi za kitaifa kama vile kuteuliwa na Mwalimu
Nyerere kama Mwenyekiti wa Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi (NBAA). Hata hivyo,
pamoja na mafanikio hayo Dr. Mengi aliona bado ana ombwe kubwa ndani yake nalo
ni kuhakikisha anatumia kwa kadri awezavyo: vipaji alivyonavyo, uwezo, akili na
nguvu ili kufikia mafanikio makubwa zaidi. Somo kubwa hapa ni kwamba hatupaswi
kuridhika na mafanikio ya muda mfupi badala yake kila hatua tunahitaji kuwa na
mpango wa kusonga hatua ya zaida.
5.
Mtaji si kigezo cha
kushindwa kuanzisha biashara
Wengi tumeshindwa kuanzisha
biashara kwa kisingizio kuwa hatuna mtaji, kupitia kitabu hiki Dr. Mengi
anatupa somo kuwa mtaji wa kwanza ambao upo kwa kila mmoja ni uaminifu. Hapa
tunaona Dr. Mengi alivyoanzisha biashara yake ya kwanza kwa kukopeshwa
malighafi za kutengenezea Kalamu kwa makubaliano ya kulipa deni hilo ndani ya
siku 30. Ili kulinda mtaji wa uaminifu pale alipopata changamoto hasa katika
usafirishaji wa mzigo ambao hakumfikia kwa muda aanzishe utengenezaji wa kalamu
na kuuza na hatimaye arejeshe pesa ilimbidi atafute njia mbadala ya kupata
fedha ili afanikiwe kurejesha ndani ya muda wa makubaliano jambo ambalo
alilifanikisha kwa asilimia zote. Wewe na mimi kuna somo kubwa la kujifunza
kwenye hili kutokana na ukweli kwamba kwa sasa fursa za upatikanaji wa mikopo
ni nyingi ukilinganisha na enzi zake.
6.
Husikubali mtazamo wa
watu wanaokuzunguka uwe kikwazo kwako.
Mwandishi anatushirikisha
kuwa pamoja na kwamba Uongozi wa Rais ya awamu wa pili uliruhusu raia kufanya
biashara au kumiliki uchumi wa nchi bado athari za Uchumi wa Kijamaa
ziliendelea kuathiri mitazamo ya wengi sambamba na sekta ya uchumi kwa ujumla.
Hali hii ilitokana na mitazamo ya baadhi ya Viongozi ambao walikuwa bado
wanaamini kwenye Ujamaa ikizingatiwa kuwa bado Mwalimu Nyerere alikuwa ana
nguvu ndani ya Chama cha Mapinduzi kama mwenyekiti wa chama. Hali hii
iliendelea kumuathiri Dr. Mengi hata kipindi ambacho alikuwa amefungua kiwanda
cha Bonite Bottlers jijini Moshi kwa
ajili ya uzalishaji wa vinjwaji baridi vya soda za Coca Cola. Na katika kipindi hicho Mwalimu Nyerere alisimama wazi
kupinga uanzishwaji wa viwanda vinavyotegemea malighafi kutoka nje ya nchi
akisema kwa mawazo yake havikuwa na msaada katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
Hata hivyo, yote hayo hayakumvunja moyo Dr. Mengi bali aliendelea kupiga kazi
kwa tahadhari na uangalifu mkubwa.
7.
Husiogope upinzani wa
kibiashara.
Mwandishi anatushirikisha
kuwa wakati anaanzisha kiwanda cha Bonite
Bottlers kwa ajili ya uzalishaji wa soda jamii ya Coca Cola alitegemea kukutana na changamoto kwenye soko kwa
kuzingatia kuwa kulikuwa na kampuni pinzani ya Fahari Bottlers ikizalisha vinjwaji vya soda jamii ya Pepsi na kwa
asilimia kubwa ilikuwa imeteka soko la Tanzania la vinjwaji baridi. Hata hivyo,
hii haikuwa sababu ya yeye kutokuanzisha kiwanda cha Bonite Bottlers kwa vile
tayari alishaona kuwa fursa ya vinjwaji baridi ipo hasa katika mikoa ya
kaskazini mwa Tanzania. Tunahitaji kujiuliza ni mara ngapi tumepoteza fursa za
kibiashara kwa kigezo cha uwepo wa washindani wakubwa wa kibiashara kwenye
fursa husika.
B.
KUHUSU FURSA, USIMAMIZI
NA UKUAJI WA BIASHARA
8.
Kila changamoto katika
jamii ni fursa ya kibiashara.
Katika katabu hiki
Mwandishi anatushirikisha jinsi alivyoanzisha biashara mbalimbali kwa kuangalia
changamoto zilizokuwepo katika jamii katika vvipindi vya nyakati tofauti.
Biashara yake ya kwanza ilianzishwa kutokana na uhaba mkubwa wa kalamu nyakati
hizo; Bonite Bottlers kwa ajili ya
kutengeneza soda za Coca cola na maji
ya kunywa ya Kilimanjaro vivyo hivyo ilianzishwa kutokana na uhaba mkubwa wa bidhaa
hizo katika ukanda wa Kaskazini mwa Tanzania. Pia, IPP Group kwa ajili ya
huduma za Magazeti, Runinga (ITV) na Redio pia ilianzishwa katika kipindi
ambacho kulikuwa na uhitaji mkubwa wa huduma hizo hasa kutokana na uhaba wa
vyombo vya habari vinavyomilikiwa na sekta binafsi. Kwa ujumla Dr. Mengi katika
kitabu hiki anatushirikisha kuwa katika kipindi cha miaka ya 1983 hadi 1992
alikuwa ameanzisha makampuni mbalimbali kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa
nyingi zilizokuwa zinapatikana kwa shida kama vile sabuni, dawa ya meno,
cement, ‘toilet paper’, mafuta, chaki na bidhaa nyinginezo. Somo kubwa kwetu
hapa ni kujiuliza je jamii tunayoishi kwa sasa hakuna changamoto ambazo
zinaweza kugeuzwa kuwa fursa za biashara?
9.
Kadri biashara inavyokua
unahitaji kuboresha mazingira ya biashara.
Mwandishi anatushirikisha
kuwa alianzisha utengenezaji wa Kalamu ndani ya eneo la nyumba aliyokuwa
akiishi. Hata hivyo, kadri biashara ilivyopanuka ilitakiwa kutafuta eneo ambalo
lingefaa kuendena na kasi ya ukuaji wa biashara. Hata hivyo, haikuwa rahisi
kupata eneo la kupanga kutokana na gharama kubwa za kodi hasa katika maeneo ya
viwanda vidogo vidogo kipindi hicho katika eneo la Barabara ya Pugu (sasa
barabara ya Nyerere). Hata hivyo, changamoto hii hakumfanya akate tama badala
yake ilimbidi kutafuta mbinu mbadala ambayo ilimuwezesha kupata eneo la kukodi
kwa gharama nafuu. Somo kubwa ni kwamba kila changamoto ya kibiashara ina
suluhisho pale mmiliki wa biashara akiwa amedhamiria kuitatua.
10.
Biashara inahitaji
usimamizi wa karibu.
Mwandishi anatushirikisha
changamoto iliyokumba nyakati ambazo alihitaji kusimamia biashara zake kwa
ukaribu zaidi na wakati huo huo akitakiwa kuendelea kufanya kazi na kampuni ya
Cooper and Lybrand (C&L) kama kiongozi kwa tawi la Tanzania. Japo yalikuwa
maamuzi magumu kwake kuachana kufanya kazi na kampuni ambayo aliisimia kwa
kipindi kirefu lakini yalibakia kuwa maamuzi sahihi kwa ajili ya kupata muda wa
kutosha wa kusimamia biashara zake. Na hapa ndipo aliamua kuafuata njia ambayo
ni wachache wanaoifuata – njia ya kujiajiri mwenyewe badala ya kuajiriwa. Somo
kubwa hapa ni kwamba chochote tunachofanya kwa lengo la kujiongezea kipato
uwepo/usimamizi wetu wa karibu ni wa maana sana kwa ajili ya uendelevu na
ukuaji wa mradi husika.
Dr. Reginald Abraham Mengi
alifanikiwa kufikia mafanikio makubwa na sasa hatunaye katika ulimwengu huu,
lakini muhimu ni kutambua hakika Dr. Mengi ataendelea kuishi kupitia
urithi huu wa kitabu cha I Can, I must, I
will. Kizazi cha sasa na vizazi vijavyo kuna mengi ya kujifunza kutoka kwa
bilionea huyu mwenye asili ya kitanzania na aliyefanikisha utajiri wake ndani
ya ardhi ya Tanzania.
Kupata uchambuzi wote wa kitabu hiki changia
TSHS. 5,000/= kama sehemu ya kusapoti jitihada zangu za kuendelea kukupatia
maarifa mbalimbali kupitia uchambuzi wa vitabu vya mafanikio kwenye kila sekta
ya maisha yetu. Tuma mchango wako kupitia namba ya simu +255 763 745451 au +255
786 881155 kisha nitumie ujumbe wa sms kuomba kutumiwa uchambuzi wote wa
kitabu.
Pia unaweza kupata uchambuzi wa Kitabu cha
Rules of Life (Kanuni za Maisha) kwa kulipia TSHS. 5,000/=. Ndani ya uchambuzi wa kitabu hiki utapata kanuni (106) ambazo zimechambuliwa
kwa lugha rahisi na kuandaliwa kwa mfumo wa pdf. Uchambuzi huu una jumla ya
kurasa 40 na ni kitabu ambacho unaweza kusoma kwenye simu yako ya mkononi
(smart phone) au kwenye kompyuta mpakato (pc).
Tuma pesa kwa njia ya
M-pesa au Airtel Money kupitia namba zifuatazo:-
M – Pesa tumia namba: +255
763 745 451 (Majina ni Augustine Mathias)
Airtel Money tumia namba:
+255 786 881 151 451 (Majina ni Augustine Mathias)
Xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Pia unaweza kupata
uchambuzi wa Kitabu cha “The Rules of
Money” ambacho pia kimeandikwa na Mwandishi Richard Templar.
Uchambuzi wa kina wa Kitabu cha The Rules of Money (Kanuni 107) umeandaliwa
kwa mfumo wa pdf na unapatikana kwa gharama ya Shilingi za Kitanzania (TSHS)
elfu tano tu (5,000/=). Uchambuzi wa kanuni zote una jumla ya kurasa 39.
Kupata uchambuzi wa kanuni zote tuma pesa yako kwa njia ya M-pesa
au Airtel Money kupitia namba zifuatazo:-
M – Pesa tumia namba: 0763 745 451 (Majina ni Augustine Mathias)
Airtel Money tumia namba: 0786 881 151 451 (Majina ni Augustine
Mathias)
Karibu
kwenye mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI
ili upate elimu isiyokuwa na mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Augustine Mathias Bilondwa
Namba ya Simu: 0786881155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua pepe: fikrazatajiri@gmail.com