NENO LA LEO (MACHI 19, 2020): [MUHIMU] KADRI MILANGO YA DUNIA INAVYOZIDI KUNSINYAA NDIVYO WENYE MACHO WATAFAIDIKA.

👉🏾Habari ya asubuhi rafiki yangu na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni matumaini yangu kuwa umeamka salama na upo tayari kuendeleza bidii ya kufikia mafanikio ya malengo muhimu katika maisha yako. Ni jambo la heri kuona kuwa tumebahatika kupata zawadi hii ya uhai katika siku ya leo hivyo ni vyema tuitumie kwa faida.

JIUNGE NA KUNDI LA WHATSAPP LA FIKRA ZA KITAJIRI KWA  KUBONYEZA HAPA NA KUJIUNGA BURE. Jiunge sasa nafasi ni chache.

✍🏾Karibu katika neno la tafakari ya leo ambapo nitakushirikisha umuhimu wa kuwa na macho yanayoona fursa katika kipindi hiki ambacho milango ya Dunia inazidi kusinyaa. Wote tumeshuhudia katika kipindi cha miezi kadhaa toka kugundulika kwa kirusi cha CORONA (Covid – 19) nchi nyingi zinazidi kuwa visiwa. Mashirika ya ndege na vyombo vingine vya usafirishaji vimefunga kwa muda safari zake ambazo awali zilikuwa zikielekea sehemu ambazo kwa sasa zinakabiliwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya CORONA.

✍🏾Pia, zipo nchi au maeneo mengine ambayo watu wamedhuiwa kutoka nje ya maeneo wanakoishi kwa hofu ya kuepuka kusambaza ugonjwa au kupata maambukizi. Kwa kifupi ni kwamba Dunia inapitia katika kipindi cha taharuki ambayo inaambatana na hofu kubwa pamoja na tishio la ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja au taifa kwa ujumla.

✍🏾Ni katika kipindi hiki maamuzi na matendo yako ndiyo yataamua ni kiwango gani utaathirika na ugonjwa wa CORONA. Maamuzi hayo yatakuwa na athari kwenye biashara yako kama tayari unamiliki biashara, kwa wanyakazi wako kama tayari unao, wateja wako na hata jamii nzima inayokuzunguka.

✍🏾Ni katika kipindi hiki watu wenye macho ya kuona fursa ambazo zinaambatana na kusinyaa kwa milango ya Dunia watainuka na kutengeneza utajiri mkubwa sana. Mfano, mara nyingi tumekuwa tukilalamikia uwepo wa bidhaa za China katika soko jinsi unavyoathiri bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi. Bila kujali mtaji wako hapa kuna fursa nyingi ambazo unaweza kuchangamkia kwa ajili ya kufaidika na kufungwa kwa safari za China kwa wafanya biashara wengi.

✍🏾Ni katika kipindi hiki hautakiwi kuwa na hofu wala papala ambazo zitapelekea kuanza kupoteza mtaji wako au akiba uliyojiwekea. Kwa kifupi ni kwamba tunaelekea katika kipindi ambacho wengi wataanza kuuza sehemu ya biashara au rasilimali wanazomiliki. Hapa ndipo utaona umuhimu wa kuwa na fedha ya akiba maana fedha hiyo endapo utakuwa na maamuzi sahihi itakuwezesha kumiliki biashara au rasilimali ambazo hukuwahi kufikiria kuzimiliki kwa kiwango cha pesa utakayonunulia.

✍🏾Ni kipindi ambacho uchumi unasinyaa na wasiwasi unasambaa kwa kasi kuliko hata jinsi CORONA yenyewe inavyosambaa. Ukiruhusu kuwa sehemu ya wale ambao wanahofia ugonjwa kwa kujituliza bila kuwa na ubunifu katika kazi zao hakika umekwisha. Ubunifu ndiyo silaha pekee ambayo itakuvusha kutoka kwenye hatari hii ya anguko la kiuchumi. Huu sio muda wa kukaa kwenye TV kama vile CNN, BBC, TBC, ITV, Sky New na channel nyinginezo kwa lengo la kuangalia hatari iliyopo mbele yako. Kadri unavyozidi kuujaza moyo wako hofu ndivyo unazidi kupunguza uwezo wa macho yako kuona fursa zilizojificha ndani ya ugonjwa wa CORONA.

✍🏾Ni kipindi ambacho unatakiwa kuwa mchoyo kwa ajili ya kulinda mtaji au akiba yako ili itumike kwa faida. Kama ambavyo tajiri Warren Buffet anavyosema “unatakiwa kuwa na hofu katika kipindi ambacho kila mmoja anakuwa na uchoyo wa kujimilikisha mali na katika kipindi ambacho kila mmoja ana hofu ndipo wewe unatakiwa kuwa uchoyo unaolenga kukuza biashara yako”. Tafsiri yake ni kwamba nyakati ambazo kila mmoja anakimbilia kuuza wewe ndo unatakiwa kununua na nyakati ambazo kila mmoja ananunua wewe unatakiwa kutulia.

✍🏾Ni kipindi ambacho hautakiwi kuruhusu lawama zitawale akili yako. Hiki si kipindi cha kutafuta mchawi ni nani bali unatakiwa kuhakikisha upo tayari kubeba msalaba wako katika kila hali ambayo utakutana nayo katika kipindi hiki.

✍🏾Ni kipindi ambacho unatakiwa kubadilisha mfumo mzima wa utendaji kazi au uendeshaji wa biashara yako. Hiki siyo kipindi cha kuendelea kulazimisha kufanya kazi au biashara kwa kutumia mbinu ambazo unaona hazileti matokeo kama ilivyozoeleka.

✍🏾Mwisho, neno la tafakari ya leo limeendelea kutukumbusha kuwa zipo fursa nyingi katika kipindi hiki ambacho milango ya Dunia inazidi kusinyaa. Wajibu wetu ni kuruhusu macho yetu yaone fursa hizo na kuzichangamkia kwa ajili ya kukuza uchumi wetu katika kipindi hiki ambacho uchumi unaelekea kusinyaa.

👐🏾Nakutakia kila la kheri kwenye siku hii ya leo. Kumbuka husikose kutoa mrejesho wa kile ambacho unajifunza kutokana na uwepo wako kwenye kundi hili.

 BORN TO WIN ~ DREAM BIG 

🗣🗣 Mwalimu Augustine Mathias 
Mawasiliano: 0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua pepe: fikrazakitajiri@gmail.com
Tovuti: fikrazakitajiri.blogspot.com
onclick='window.open(