NENO LA LEO (MACHI 7, 2020): JE MACHO YAKO YANAONA NINI?

👉🏾Habari ya asubuhi rafiki yangu na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni matumaini yangu kuwa umeamka salama na upo tayari kuendeleza moto wa kupiga hatua zinazolenga kukufikisha kwenye kilele cha mafanikio ya malengo uliyojiwekea kwenye kila sekta ya maisha yako.

JIUNGE NA KUNDI LA WHATSAPP LA FIKRA ZA KITAJIRI KWA  KUBONYEZA HAPA NA KUJIUNGA BUREJiunge sasa nafasi ni chache.

✍🏾Karibu katika neno la tafakari ya leo ambapo nalenga kukufundisha siri kubwa ya kuona fursa katika mazingira yanayokuzunguka. Siri hii si nyingine bali ni kuyafundisha macho kuona upande chanya badala ya hasi katika kila fursa inayojitokeza mbele yako. kabla kuangalia upande hasi unatakiwa kuanza na upande chanya kwenye kila fursa inayojitokeza.

✍🏾Kabla ya kuendelea na ufafanuzi wa neno la tafakari ya leo hebu tujifunze kitu kutoka kwenye maongezi haya: Juzi nilibahatika kuwa sehemu moja na Mtumishi mmoja wa shirika la Wanyamapori (TANAPA) ambaye kwa haraka haraka anaweza kuwa na zaidi ya miaka 50. Tukiwa kwenye gari na watumishi wenzake akaanzisha maongoezi ambayo yalihusiana na thamani iliyopo kwenye uwekezaji wa ardhi.

✍🏾Hii ni sehemu ya kwanza ya maongezi: “mwaka 1993 nikiwa ndo naanza kazi niliitiwa kununua kiwanja ambacho kilikuwa barabara kuu pale Himo Mkoani Kilimanjaro, kiwanja kile kilikuwa kikubwa na kipo eneo zuri la biashara hila kwangu mimi cha kwanza nilichokiona katika kiwanja kile ni uwepo wa mawe kwenye kila eneo la kiwanja. Nakamwabia yule kijana aliyetaka kuniuzia hapa unataka watoto wangu waje kujikwaa na kutoa kucha kila siku kutokana na mawe haya au unataka kuniibia? Ukweli kile kiwanja niliachana nacho japo kilikuwa kinauzwa kwa Tshs. 30,000/= kwa kipindi kile. Hilo ndo lilikuwa kosa langu, baada ya miaka 10 kiwanja kile kilikuja kuuzwa kwa milioni thelathini (Tshs. 30M) na hadi sasa kuna kituo cha mafuta kimejengwa pale”.

✍🏾Sehemu ya pili ya maongezi yake: “2001 nikiwa Kahama nikamfuata kijana mmoja wa ardhi anionyeshe kiwanja cha kununua. Kijana yule akanieleza kuna kiwanja kizuri sana hebu ona ramani yake kabla hatujaenda kukiona. Kweli niliona kipo eneo zuri kwenye ramani na ndipo tukaenda kukiona. Baada ya kufika kwenye eneo la kiwanja ilikuwa kidogo nimchape kijana yule kibao maana kiwanja alichopamba awali kilikuwa na mashimo ya mengi maana uchimbaji wa mchanga ulikuwa unaendelea ndani ya eneo lile. Yule kijana akaendelea kunisihi ninunue kiwanja kile kwa kuwa kipo barabara kuu ya Kahama kuelekea Burundi. Nilikataa kununua kiwanja kile na hilo lilikuwa kosa langu la pili. Baada ya miaka 5 nilipita tena katika eneo lile na sikuweza kuliona eneo lenye mashimo bali nilichokiona ni Hoteli kubwa ya kifahari. Baada ya pale nilijifunza kutokana na makosa yangu na ndipo nikaanza kuwekeza kwenye ardhi bila kujali ina kasoro gani”.

✍🏾Kupitia maongezi haya tunachojifunza ni kuwa mhusika alichoweza kuona katika viwanja vyote ni vikwazo au upande hasi kwenye fursa hizo. Katika kiwanja cha kwanza aliona mawe kama kikwazo akasahau kuwa mawe hayo angeweza kuyaona katika upande wa fursa na yakatumika kwa ajili ya kuongeza thamani ya kiwanja. Mfano, angeweza kutumia mawe hayo wakati wa ujenzi wa msingi au kuponda kokoto kwa ajili ya kazi za ujenzi. Katika kiwanja cha Kahama yeye aliona mashimo kama kikwazo katika kiwanja husika akasahau kuwa mashimo yale yalikuwa ni ya muda tu maana angeweza kutumia gharama ndogo kuziba mashimo hayo kwa kujaza kifusi cha udongo.

Somo jingine la kujifunza kutokana na maongezi hayo ni kuwa kadri unavyotanguliza kuona upande hasi ndivyo unapoteza nafasi ya kuona upande chanya kwenye fursa husika. Unapotanguliza upande hasi unajikuta umejifunga ndani ya boksi kiasi ambacho hautaweza kuona upande chanya wa fursa husika. Kumbe hapa ambacho ungetakiwa kufanya baada kuona kuwa pamoja na kwamba fursa inaonekana kuwa na thamani kubwa kwa baadae hila kwa wakati huo ina changamoto kadhaa. Tumia changamoto hizo zilizopo kumponda muuzaji ili akupunguzie bei katika biashara husika.

✍🏾Mwisho, neno la tafakari ya leo limetufunulia umuhimu wa kutazama upande chanya katika kila fursa tunayokutana nayo badala ya kutanguliza upande hasi. Unapotanguliza upande hasi moja kwa moja unaifunga akili yako kuona upande chanya kwenye fursa iliyopo mbele yako. Macho yako yanaona nini? Kuanzia sasa hakikisha macho yako yanaona upande chanya kwenye kila fursa inayojitokeza.

Nakutakia kila la kheri kwenye siku hii ya leo. Kumbuka husikose kutoa mrejesho wa kile ambacho unajifunza kutokana na uwepo wako kwenye kundi hili.

BORN TO WIN ~ DREAM BIG

🗣🗣 Mwalimu Augustine Mathias
Mawasiliano: 0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua pepe: fikrazakitajiri@gmail.com
Tovuti: fikrazakitajiri.blogspot.com

onclick='window.open(