👉🏾Habari ya asubuhi rafiki yangu na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Namshukuru Mungu kwa asubuhi hii ya leo kwa kuwa amenizawadia siku muhimu. Ni siku ambayo najiona kuwa nina deni la kulipa kutokana na uhai wangu hapa Duniani. Pia, namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kuendelea kukufikishia kazi hii pamoja na wewe kuendelea kujifunza kitu hata kama ni kidogo lakini naamini upo moto wa mabadiliko ndani ya moyo wako.
JIUNGE NA KUNDI LA WHATSAPP LA FIKRA ZA KITAJIRI KWA KUBONYEZA HAPA NA KUJIUNGA BURE. Jiunge sasa nafasi ni chache.
✍🏾Karibu katika neno la tafakari ya leo ambapo nitakushirikisha namna ambavyo unaweza kubadilisha mchezo unaoupenda kutoka kwenye kujifurahisha na kuwa fursa kwako kutengeneza pesa. Kwa wapenzi wa mpira wote tunafahamu kuwa leo ni siku ya mechi kubwa ya watani wa jadi wa Kariakoo. Naamini pia humu ndani wengi ni wapenzi wa mpira kama sio kwa Tanzania basi kwa ligi kuu za Ulaya. Ni jambo jema maana baada ya kuweka bidii katika kazi kwa majukumu ya wiki nzima sio mbaya kutumia masaa kadhaa kuiburudisha nafsi yako.
✍🏾Pamoja na kwamba wengi ni wapenzi wa mpira au mchezo wowote lakini ukweli ni kwamba ni wachache sana wanaotengeneza pesa kutokana na michezo hiyo. Wengi wanapoteza pesa nyingi kwa kufuatilia michezo hiyo kuliko wanavyotengeneza pesa. Vijana wengi siku hizi wanaendelea kumtajirisha Mhindi kupitia mchezo wa “Betting” wakitegemea kuwa ipo siku watakuwa matajiri kupitia nguvu ya “jero” au “buku”. Ukweli ni kwamba wanaoliwa fedha ni wengi kuliko wanaopata na ndio maana Mhindi anaendelea kuwa tajiri na wale wazee wa nguvu ya “jero/buku” wanaendelea kuwa masikini. Kupitia neno la tafakari ya leo nakushauri uanze kutengeneza pesa kupitia mchezo unaoupenda kwa kutumia mbinu zifuatazo:-
✍🏾 Moja, Tengeneza pesa kupitia vifaa au picha za michezo. Kwenye matukio ya mechi kubwa watu wapo tayari kununua picha, jezi, skafu, vikombe au kofia zinazoendana na ujumbe wa Timu wanayoshabikia. Wajibu wako ni kuwa mbunifu kwa kuandaa vifaa hivyo kulingana na ukubwa wa mechi husika. Na kadri mechi inavyokuwa kubwa ndivyo mihemko ya watu inavyoongezeka na kadri mihemko inavyoongezeka ndivyo watu wananunua. Kumbuka siri iliyopo katika kuuza ni kutambua kuwa watu wananunua kulingana na hisia.
✍🏾 Mbili, Anzisha kibanda cha kuonesha mpira. Hii ni njia nyingine ambayo unaweza kutengeneza pesa nyingi kwa kutoza shilingi mia tano kwenye kila mtu anayekuja kuangalia mechi kwako. Hapa utatengeneza pesa kupitia hiyo tozo ya mlangoni pamoja na kuuza vinjwaji, mishikaki, chips au vitafunwa kama biscuit. Kuanzisha biashara hii sio lazima uwe na mtaji mkubwa kwani unatakiwa kuwa na TV yenye gharama ikiwa kubwa si zaidi laki sita (kadri TV inavyokuwa kubwa ndivyo utapata watazamaji wengi) pamoja na Vingamuzi vya Azam TV na DSTV au unaweza kutumia Cable kama sehemu uliyopo kuna huduma hiyo. Kupitia biashara hii utafaidika mara mbili kwani utaweza kuangalia mpira bila hasara wakati ukitengeneza pesa.
✍🏾 Tatu, Anzisha blog ya taarifa za michezo. Ukweli ni kwamba unapoandika makala yoyote kuhusu michezo itasomwa na watu wengi zaidi kuliko makala nyinginezo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba michezo inafuatiliwa na watu wa rika zote. Kupitia blog za michezo kama una wafuatiliaji wengi (idadi kubwa ya watembeleaji wa blog yako) utatengeneza pesa za matangazo na hivyo kunufaika na mchezo unaoupenda. Hii ni fursa ambayo ipo hai katika karne hii 21 kutokana na mapinduzi ya teknolojia ya mawasiliano ambapo kila mtu kwa sasa anaweza kupata huduma ya mtandao wa intaneti.
✍🏾 Nne, Anzisha ligi ya mchezo unaoupenda. Kupitia ligi unaweza kutengeneza pesa kupitia pesa za kiingilio na matangazo. Tumeona namna ambavyo ligi ya mechi za mchangani ambavyo imekuwa ikiongezeka umaarufu kwa Mkoa wa Dar es Saalam na kuweza kukusanya watazamaji wengi. Kadri watazamaji wanavyokuwa wengi ndivyo waandaaji wanatengeneza pesa. Ukiwa na ubunifu unaweza kutengeneza pesa kupitia ligi za aina hii katika eneo lako.
✍🏾 Tano, Anzisha duka la vifaa vya michezo. Katika pointi ya kwanza tumeona namna unavyoweza kuuza vifaa vya michezo kulingana na ukubwa wa mechi. Bado unaweza kuanzisha Duka linalouza vifaa orijino vya michezo ambapo utakuwa na fursa ya kuuza vifaa vya Timu mbalimbali ambazo zina wapenzi wengi. Muhimu ni kuhakikisha Duka unalianzisha kwenye eneo la kimkakati ambapo utapata wateja wengi. Pia, unatakiwa kutumia mbinu za kujitangaza kwa kutumia mitandao ya kijamii ambapo utapata fursa ya kuuza kwa wateja ambao wapo mbali na eneo la Duka lako.
✍🏾Mwisho, kupitia neno la tafakari ya leo nimekushirikisha fursa zilizopo za kutengeneza pesa kupitia mchezo unaoupenda. Fursa hizi zote hazihitaji mtaji mkubwa ili uanze kutengeneza pesa na hivyo kufuatilia michezo husika kwa faida. Kama una mtaji wa kutosha pia unaweza kutengeneza pesa kwa kuanzisha Academy ya mchezo uupendao, Klabu za michezo, TV/Radio inayojikita kwenye taarifa za michezo, Kituo cha Mafunzo ya Michezo au Gazeti la Michezo. Hizo ni fursa ambazo zipo wazi kwa ajili yako kutengeneza pesa kupitia michezo, wajibu wako ni kuchagua fursa kulingana na uwezo wa mtaji wako.
👐🏾Nakutakia kila la kheri kwenye siku hii ya leo. Kumbuka husikose kutoa mrejesho wa kile ambacho unajifunza kutokana na uwepo wako kwenye kundi hili.
BORN TO WIN ~ DREAM BIG
🗣🗣 Mwalimu Augustine Mathias
Mawasiliano: 0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua pepe: fikrazakitajiri@gmail.com
Tovuti: fikrazakitajiri.blogspot.com
Kujiunga Kundi la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI, bofya link hii: https://chat.whatsapp.com/JACBxr9kX7K0qt58cQTrrw