NENO LA LEO (MACHI 20, 2020): [CHUKUA HATUA] HOFU NI ADUI NAMBA MOJA KATIKA SAFARI YAKO YA MAFANIKIO

👉🏾Habari ya asubuhi rafiki yangu na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Namshukuru Mungu kwa kunipa zawadi mpya katika maisha yangu ambayo nina deni la kuhakikisha naitumia vyema katika kuliishi kusudi la maisha yangu. Ni asubuhi ambayo naamini umeamka salama na upo tayari kuendeleza bidii ya kufikia mafanikio katika malengo uliyojiwekea.

JIUNGE NA KUNDI LA WHATSAPP LA FIKRA ZA KITAJIRI KWA  KUBONYEZA HAPA NA KUJIUNGA BURE. Jiunge sasa nafasi ni chache.

✍🏾Karibu katika neno la tafakari ya leo ambapo nakusudia kukushirikisha hatua muhimu za kukabiliana na hofu ya aina yoyote katika maisha yako. Mwanadamu ni kiumbe ambacho kinatawaliwa na hisia katika maisha yake. Hisia hizo mara nyingi zinaweza kuwa na athari chanya au hasi katika maisha ya muhusika. Ni kutokana na athari hizo wanafalsafa wanasisitiza kuwa binadamu yeyote anayehitaji kutawala maisha yake anatakiwa kufahamu namna ya kukabiliana na hisia zenye athari hasi katika maisha.

✍🏾Ubongo wa mwanadamu unaitikia vichocheo vya aina mbalimbali vinayapelekea hisia tofauti katika mwili. Sayansi ya ubongo inaonesha kuwa vichocheo vya hisia vinajengwa katika sehemu ya ubongo inayoitwa na “Amygdala”. Amygdala nayo inapeleka vichocheo vya hisia kwenye sehemu ya ubongo inayoitwa “Hypothalamus” ambayo kazi yake ni kutawala mwitikio wa vichocheo vyote vinavyohusiana na hisia katika mwili wa mwanadamu. Hypothalamus inafanya kazi yake kwa kuzalisha homoni ambazo zinasaidia mwili wa kuchukua hatua stahiki kuhusiana na aina na hisia.

✍🏾Mwili wa mwanadamu katika maisha ya kila siku unazungukwa na vichocheo vya hisia mbalimbali ambazo ni pamoja na: wasiwasi, upendo, hasira, hofu, furaha, huzuni, mshangao, chuki au matarajio. Katika neno la tafakari ya leo tutajifunza namna ya kukabiliana na hofu kwa kuwa ina athari nyingi katika safari yako ya mafanikio.

✍🏾Mwanadamu anakabiliwa na hofu nyingi lakini kati ya hizo namba moja ni hofu ya kutokuwa na uhakika wa maisha ya baadae. Katika maisha hayo ya baadae hofu kubwa ya mwanadamu ipo kwenye swali kubwa la ni namna gani siku za mwisho za maisha yake jinsi zitakavyokuwa. Kwa tafsiri ya haraka haraka ni kwamba mwanadamu ana hofu juu hatari za maisha ambazo zitapelekea kifo chake.

✍🏾Tunafahamu kuwa sababu kubwa zinazopelekea kifo ni magonjwa, ajali au majanga ya kidunia. Katika kipindi hiki hofu kubwa inayotishia maisha ya mwanadamu ni ugonjwa wa CORONA (Covid 19). Katika neno la tafakari ya jana niliandika kuwa hofu hii inasambaa katika Ulimwengu kuliko hata namna ugonjwa wenyewe unavyosambaa. Hivyo, neno la leo ni mwendelezo wa kukuondoa katika hofu inayoambatana na ugonjwa huu katika maisha yako.

✍🏾 Je nawezaje kuepukana na hofu ya aina yoyote katika maisha yangu? Zipo nyingi za kukabiliana na hofu ambazo zimeandikwa na wanafalsafa na wanasaikolojia. Katika makala hii nitakushirikisha mbinu tano zifuatazo:

✍🏾 Moja, husijifungie ndani na tatizo lako. Tatizo lolote ambalo linapelekea uwe na hofu katika maisha yako ya kila siku unatakiwa kutambua kuwa siyo wewe wa kwanza kupatwa na tatizo hilo. Kadri unavyojifungia ndani na tatizo lako ndivyo tatizo husika litaongezeka, kumbe, unachotakiwa kufanya katika kila tatizo linalokukabili ni kutafuta msaada wa ushauri na mawazo kutoka kwenye jamii inayokuzunguka. Ushauri huu unaweza kuupata kwa njia ya kujisomea, uzoefu wa watu ambao wameshapitia kwenye tatizo kama lako au wataalamu katika sekta ya tatizo linalokufanya uwe na hofu.

✍🏾 Mbili, kuwa mkweli dhidi ya hali inayopelekea hofu. Kadri unavyotafuta ushauri na mawazo kutoka kwa jamii inayokuzunguka ni lazima kwanza utambue kuwa ushauri au mawazo hayo hayatakuwa na msaada kama bado haujatambua chanzo halisi cha hofu yako. Tafsiri yake ni kwamba unatakiwa kupata elimu ya kutosha kuhusiana na hali inayopelekea hofu kwenye maisha yako.

✍🏾 Tatu, kubaliana na hali au mambo ambayo yapo nje wa uwezo wako. Wapo watu wengi katika jamii ambao wanapoteza muda mwingi kuhofia matukio au hali ambazo zipo nje ya uwezo wao wa kuzizuia au kuzitawala. Kanuni ni kwamba katika kila hali au tukio unatakiwa utimize wajibu wako kwa kutumia uwezo ulioko ndani yako na zaidi ya hapo uache asili ichukue nafasi yake. Mfano, haina tija kuishi katika hofu ya ugonjwa bali wajibu wako ni kuchukua tahadhari stahiki zinazokukinga na ugonjwa husika.

✍🏾 Nne, chukua tahadhari binafsi wewe na watu wako wa karibu. Tunafahamu kwa katika kila tukio ni lazima pawepo kisababishi chenye nguvu sawa na mwitikio utakaotokea. Tafsiri yake ni kwamba katika kila chanzo cha hofu uliyonayo unahitaji kujiuliza ni tahadhari zipi ambazo unaweza kuzichukua wewe binafsi kwa ajili ya kujilinda dhidi ya hofu hiyo.

✍🏾 Tano, jikite kwenye fikra chanya. Kupitia sheria ya asili ya kupanda na kuvuna, tunafahamu kuwa tunavuna kulingana na kile tunachopanda. Kadri unavyojikita kwenye hisia hasi katika hofu iliyopo mbele yako ndivyo kuna nafasi kubwa ya kupata matokeo hasi hayo unayoyawaza. Kumbe katika kila hofu inayokukabili unatakiwa kutazama upande chanya ambao umejificha ndani ya hofu husika.

✍🏾Mwisho, neno la tafakari ya leo limetufunulia jinsi ambavyo hofu ina athari chanya katika maisha yetu ya kila siku. Zaidi tumeona kuwa mwanadamu hofu yake kubwa ipo kwenye uoga wa baadae kwa kuwa hakuna mwenye uhakika katika siku za maisha yake ya baadae. Hata hivyo, siku za maisha hayo ya baadae zinaandaliwa na matukio ya maisha ya sasa. Katika maisha ya sasa unaweza kuepukana na hofu kwa kutumia njia tano ambazo zimeainishwa katika makala hii.

👐🏾Nakutakia kila la kheri kwenye siku hii ya leo. Kumbuka husikose kutoa mrejesho wa kile ambacho unajifunza kutokana na uwepo wako kwenye kundi hili.

 BORN TO WIN ~ DREAM BIG 

🗣🗣 Mwalimu Augustine Mathias 
Mawasiliano: 0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua pepe: fikrazakitajiri@gmail.com
Tovuti: fikrazakitajiri.blogspot.com
onclick='window.open(