NENO LA LEO (MACHI 17, 2020): TENGENEZA TIMU IMARA NA TIMAMU KWA AJILI YA USHINDI UNAOTAMANI.

👉🏾Habari ya asubuhi rafiki yangu na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ninamshukuru Mungu kwa ajili ya zawadi hii ya leo ambayo ni muhimu kwangu katika kuendeleza moto wa mafanikio. Pia, namshukuru Mungu kwa ajili yako ambaye unaendelea kujifunza kitu kutokana na uwepo wako katika kundi hili.

Zaidi ya yote furaha yangu ni kubwa pale ninapoona kuwa umebedilika kifikra na hadi sasa umeanza kuchukua hatua muhimu zinazolenga kufanikisha malengo ya maisha yako.

JIUNGE NA KUNDI LA WHATSAPP LA FIKRA ZA KITAJIRI KWA  KUBONYEZA HAPA NA KUJIUNGA BURE. Jiunge sasa nafasi ni chache.

✍🏾Karibu katika neno la tafakari ya leo ambapo ni mwendelezo wa umuhimu wa kutambua kuwa utachelewa sana kufanikiwa kama unafanya mchezo wa mafanikio peke yako. Mafanikio katika chochote unachofanya au unachokusudia kufanya kwa ajili ya kufikia matamanio ya ndoto yako ni lazima utambue kuwa kuna watu wema na waaminifu ambao wapo tayari kushirikiana na wewe.

✍🏾Katika mradi wowote ambao umedhamiria kuutekeleza unatakiwa kutambua kuwa tayari wapo watu wema ambao wanasubiria kukushika mkono na kukuvusha. Wapo watu wema ambao wanakusudia mshirikiane katika kukamilisha manunuzi ya bidhaa za biashara unayofanya. Wapo watu wema ambao wanahitaji uwashike mkono ili nao wakusaidie katika kutimiza majukumu yako. Wapo watu wema ambao wanahitaji kupata wema wako ili wawe mabalozi wa kukusimamia miradi yako.

✍🏾Swali la kujiuliza ni kwamba kama kila kona kuna watu wema mbona watu huwa wanakwama kufikia mafanikio wanayotamani. Watu wanakwama kufikia mafanikio ya ndoto za maisha yao kutokana na sababu kuu mbili zifuatazo:-

✍🏾 Moja, watu wengi hawana Imani chanya dhidi ya watu wanaowazunguka. Kila wanapoona sura za watu kinachotafsiriwa kutoka katika sura hizo ni upande hasi. Mfano, watu wanaogopa kuibiwa, kudhurumiwa, kutapeliwa au migogoro kutoka kwa watu ambao wangekuwa wa msaada kwao. Kanuni ni kwamba, hauwezi kujua ubaya au uzuri wa mtu kabla ya kufanya nae kazi.

 ✍🏾 Mbili, watu hawana utamaduni wa kuwainua wale wanaofanya nao kazi. Mawazo na akili ya watu wengi imejikita kwenye maendeleo binafsi na kusahau kuwa wale wanaofanya nao kazi wana haki ya kupata mahitaji yao muhimu. Mfano, katika jamii tunayoishi kuna watu wengi ambao wanalalamika kudhulumiwa na mabosi wao kutokana na kutolipwa ujira wa kazi walizofanya. Wapo watu wanafanya kazi mwezi mzima lakini mwisho wa mwezi wanaashia kuambulia nusu ya malipo au kutokulipwa kabisa.

✍🏾Mwisho, neno la tafakari ya leo linatukumbusha kuwa baada ya kutengeneza timu imara ndani ya familia kuna kila sababu ya kuongeza watu wengine ndani ya timu kwa ajili ya kukuza mtandao wako. Wajibu wako kama Kapteni wa Timu ni kutambua umuhimu wa kila mmoja ndani ya timu na kuhakikisha kila mmoja anapata stahiki yake. Kumbuka, Timu imara inajengwa kwa kuthamini na kulinda maslahi ya kila mmoja ndani ya timu kulingana na wajibu na uhusika wake.

👐🏾Nakutakia kila la kheri kwenye siku hii ya leo. Kumbuka husikose kutoa mrejesho wa kile ambacho unajifunza kutokana na uwepo wako kwenye kundi hili.

BORN TO WIN ~ DREAM BIG 

🗣🗣 Mwalimu Augustine Mathias 
Mawasiliano: 0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua pepe: fikrazakitajiri@gmail.com
Tovuti: fikrazakitajiri.blogspot.com
onclick='window.open(