Habari ya leo rafiki na msomaji
wa mtandao wa fikra za kitajiri. Ni matumaini yangu kuwa unaendelea vizuri na
mapambano kwa ajili ya kuyaboresha maisha yako. Kama ambavyo nimekuahidi
kukuletea uchambuzi wa kitabu kimoja kila mwisho wa wiki (ijumaa), leo hii
ninakuletea uchambuzi wa kitabu cha Be Obsessed or Be Average ambacho
kimeandikwa na mwandishi Grant Cardone.
Nikuombe uendelee kutumia
maarifa unayoyapata kupitia uchambuzi wa vitabu hivi kwa ajili ya kuyaboresha
maisha yako ili kwa pamoja tunafanikiwe kusonga mbele na hatimaye tuishi kusudi
la maisha yetu. Ili kupata makala za uchambuzi wa vitabu moja kwa moja kwenye
barua pepe yako BONYEZA HAPA na kujaza fomu
kisha bonyeza jiunge (subscribe) na utakuwa tayari umejiunga kwenye mfumo wa makala
za mtandao wa fikra za kitajiri.
Grant Cardone ni mwandishi,
mhamasishaji, mzungumzaji na mkurugenzi aliyefanikiwa zaidi katika anga za
kitaifa na kimataifa. Amekuwa mwandishi bora wa vitabu hadi kufanikiwa vitabu
vyake vitano kuchaguliwa kwenye orodha ya New York Times kama mwandishi na
muuzaji bora wa vitabu. Katika
kitabu hiki mwandishi anatuhamasisha kuamua kati ya kuwa walevi wa matamanio ya
mafanikio ya maisha yetu au kuamua kuwa mtu wa kawaida. Mwandishi anatufundisha
kuwa bila ya kuwa walevi wa matamanio ya mafanikio ya ndoto za maisha yetu
kamwe hatuwezi kufikia anga za watu waliofanikiwa zaidi. Karibu tujifunze wote mambo
muhimu 25 niliyojifunza kwenye kitabu hiki:-
1. Mwandishi anatufundisha kuachana na
tabia ya kuridhika na jinsi tulivyo na badala yake tunakiwa tuwe na kiu ya kuwa
bora zaidi. Hapa mwandishi anatufundisha namna amabavyo watu wengi wameshindwa
kufikia mafanikio makubwa sana kutokana na tabia ya kuridhika na jinsi walivyo.
Ili kufikia anga za watu walifanikiwa zaidi kamwe husikubali kuridhika na jinsi
ulivyo bali kila siku hakikisha unakuwa na shauku ya kuwa bora zaidi na zaidi.
Ili
kufanikiwa katika zoezi la kuwa bora zaidi, Mwandishi anatufundisha kuachana na
tabia ya kulinganisha mafanikio yetu na watu wengine na badala yake tunatakiwa kuwa na viwango binafsi vinavyotusukuma kuendeleza ubora katika kile tunachofanya.
2. Unaweza kuwa mlevi wa mambo mabaya au
mazuri katika kuamua hatma ya maisha yako ya baadae. Ulevi wa mambo mabaya
umekuwa ni adui namba moja kwa watu wanaotaka kufikia mafanikio makubwa sana
katika maisha yao. Hapa mwandishi anatushirikisha namna alivyokuwa mlevi wa
madawa ya kulevya na uvutaji wa bangi hadi kufikia hatua ya kukataliwa na kila
mmoja kwenye jamii akiwemo mama yake mzazi hata kufikia hatua ambayo naye
alianza kujikataa mwenyewe.
Hata
hivyo baada ya kupata nuru mpya katika maisha yake mwandishi anatushirikisha
namna ambavyo kila mtu alivyo na uwezo wa kuubadilisha ulevi wa mambo mabaya
hadi ulevi wa matamanio ya mafanikio makubwa ya ndoto za maisha yake. Hii ni
kutokana na ukweli ambao yeye mwenyewe amepitia kwenye maisha ya hovyo hadi
hatua ya kutushirikisha mafundisho kama haya na hapa ndipo anatushirikisha kuwa
kila aina maisha unayoyataka uamzi ni lazima uanzie ndani mwako.
3. Kadri mtu anavyobadilisha maisha ya
ulevi wa mambo mabaya na kuwa na ulevi wa kusudi la maisha yake ndivyo macho
yake ya ndani yanavyoanza kuona fursa nyingi ambazo awali hakuwahi kuziona au
kuhisi kama zinawezekana. Hapa mwandishi anatushirikisha namna ambavyo
alifanikiwa kuwa muuzaji bora kwenye kampuni aliyokuwa akifanyia kazi na
hatimaye fursa nyingi kuanza kumiminika zaidi na zaidi. Katika maisha kama haya
ndipo akaanza kuona upendo wa watu wake wa karibu ambao awali walishamtelekeza
kutokana na tabia yake ya kubwia unga.
Somo muhimu la
kujifunza hapa ni kwamba kadri utakavyopendwa na watu wengi ndivyo na njia za
mafanikio zitafunguka zaidi kutokana na ukweli kwamba mafanikio yanapatikana
kutokana na yale tunayoyafanya kila siku. Na yale tunayoyafanya kwa njia moja
au nyingine ni lazima yawaguse watu hivyo kadri watu wanavyokupenda zaidi
ndivyo na huduma zako zinavyopendwa zaidi. Kama unataka kupata mafanikio
makubwa sana ni lazima uhakikishe matendo yako ni yale yanayowavuta watu wengi
kwa kadri iwezekanavyo.
4. Kuwa na ulevi wa matamanio ya mafanikio
ya maisha yetu ni zawadi ambayo kila mmoja amepewa. Tunapoanza kutumia zawadi
hii ndipo tunafanya maamuzi ya kuondokana na maisha ya kuwa watu wa kawaida na kuanza kuishi
maisha tunayoyastahili kwani hayo ndo maisha ambayo tuliumbwa ili tuyaishi. Na kadri
tunavyoishi maisha haya ndivyo tunajitenga na wale ambao wanaishi maisha ya
ulevi wa mambo mabaya na kujikuta katika ulimwengu wa watu wenye ulevi wa matamanio
ya maisha ya mafanikio tu.
5. Mwandishi anatufundisha kuwa ili kuwa
na mafanikio ni lazima tuwe na kiu ya mafanikio katika kila kona ya maisha yetu.
Tusiihie kupata mafanikio kwenye sekta moja na kuridhika bali mafanikio
yanahitaji kupambana kwa ajili ya kuongeza ubora katika kila hatua tuliyonayo.
Kwa uasili dunia haina mipaka kwa watu wake wanaojua kutumia vyema zawadi wanazopewa
na dunia hii. Hivyo katika safari ya mafanikio ni lazima uwe tayari kuonekana kuwa
mbinafsi kutokana na roho ya kuhitaji kuongezeka kila siku. Kama wewe ni
milionea fikiria zaidi jinsi ya kuwa bilionea na zaidi na zaidi. Kwa maana hii
mafanikio yanapimwa na uwezo wako wa hali ya juu kabisa katika kutumia vipaji
ulivyonavyo. Mfano, kama wewe ni mchezaji wa mpira unatakiwa kufikiria kucheza
mpira kuliko mchezaji yeyote aliyewahi kuwepo kwenye ulimwengu wa soka.
6. Uwezo wako wa hali ya juu katika
kuendea mafanikio ya maisha yako unaongezeka mara dufu pale unapogundua thamani
halisi ya maisha yako. Hata hivyo wengi tumeshindwa kufikia uwezo wetu wa juu
kabisa kutokana na tabia ya kuridhika na hatua tunazozipiga. Kama unataka kuwa
miongoni mwa watu wenye mafanikio makubwa zaidi lazima kila mafanikio
unayoyapata ujiulize ni kipi cha ziada unaweza kufanya ili kuongeza thamani
pale ulipofikia. Kila hatua jione kuwa bado haujafanikiwa kutumia uwezo halisi ulionao
kwani ni wazi kuwa yale tunayoyafanikisha ni asilimia 20 tu ya uwezo halisi
tulionao. Hivyo, hakikisha kuwa unatafuta jitihada za kutumia asilimia 80
inayobakia kwa kadri uwezavyo.
7. Epuka ugonjwa wa kuwa wa kawaida au
wastani. Wengi wetu katika tabaka la watu wenye mafanikio ya wastani wamejikita kwenye upeo wa kuwa na yale ya muhimu tu kwa ajili ya kuwawezesha kuishi badala kujikita kwenye upeo wa kuwa
na mafanikio ya hali ya juu katika kila wanalogusa. Hii ni kutokana na ukweli
kwamba watu katika tabaka hili wanashindwa kufikia viwango vya mafanikio kutokana na
fikra walizonazo juu yao ambazo zimepelekea muda wote wajione kuwa viwango vya
mafanikio yao vimefikia ukomo.
Sababu
kubwa ambayo imepelekea watu wengi kuwa wa kawaida au wastani ni mazingira na
makuzi waliyoyapata kutoka kwenye jamii inayowazunguka. Mfano, watu wengi toka
enzi za utoto wamefundishwa kutokuwa na tabia ya kutaka zaidi kwa vile
anayefanya hivyo anaonekana mchoyo, mrafi, mbinafsi, wa ajabu, banifu, wakizamani
na kadharika. Kama unataka kufikia viwango vya mafanikio ya hali ya juu ni
lazima uwe tayari kupenya kwenye mitazamo ya namna hii na kuhakikisha
unazungukwa na watu ambao mnaendana kifikra na mtazamo kwenye mafanikio ya
maisha.
8. Haijalishi watu wana mapenzi kiasi gani
juu yako lakini kati yao hakuna hata mmoja mwenye ndoto za maisha yako kwani ni
wewe pekee unayejua ndoto za maisha yako. Ili kufikia anga za juu katika ndoto zako ni lazima uwe tayari kuepuka hofu ya kwamba watu wako wa karibu
watakuona vipi kwa vile unaenda kinyume na mazoea yao. Maisha yako ni msalaba
ambao ni wewe pekee unatakiwa kuubeba na kuufikisha salama.
9. Ukitaka
kufanikisha jambo lolote ni lazima kwanza utambue sababu zinazokusuma kufanya
hivyo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kadri unavyosukumwa na sababu nzito
ndivyo unavyopigana kuhakikisha kuwa unafanikiwa katika yale unayoyafanya. Hivyo unapoziendea ndoto zako hakikisha kwanza unaorodhesha sababu kuu za
kwa nini unataka kufanikisha ndoto hizo.
10. Ondoa shaka katika yale ambayo
umezamilia kuyatekeleza. Hii ni kutokana na ukweli kuwa hofu imekuwa ni kiini
cha ugaidi kwenye mfumo wa akili za watu na hivyo kupelekea kudumaza watu walio
wengi katika dunia hii. Kama unataka kufikia viwango vya mafanikio makubwa ya
ndoto zako ni lazima kwanza upambane na kuishinda hofu yako ili uanze
kuthubutu. Kila mtu ana hofu japo tunatofautiana jinsi tunavyopambana na hofu
hizi, husikubali kukukili kuwa umeumbwa na hofu bali jifunze kutoka kwa
wanafamanikio wengine jinsi ambavyo walivyofanikiwa kushinda hofu zao.
11. Tunafanikisha yale tunayoyapa
vipaumbele katika maisha yetu ya kila siku. Na kadri tunavyoyapa kipaumbele kwa
kiasi kikubwa ndivyo tunavyofanikiwa zaidi. Mwandishi anatufundisha kuwa jinsi
tunavyozidi kufanikiwa ndivyo tunapata hamasa ya kuendelea kupambana zaidi kwa
ajili ya mafanikio makubwa sana.
12. Epuka mfumo wa kuweka malengo kila
wakati na badala yake hakikisha unaweka mfumo wa malengo mapana ya kila sekta
ya maisha yako ili kila unapopumua na kufikiri fanya hivyo ukiwa kwenye picha kubwa ya malengo yako. Hakikisha kila unapolala unavyofanya hivyo kwa kuyawaza malengo hayo,
pia hakikisha kila siku unayaandika malengo haya na kuyasoma mara tatu kwa siku
mpaka pale yatakapokuwa sehemu ya maisha yako ya kila siku. Baada ya kufanya hivyo
utaona kila kona ya mazingira yako ipo kwa ajili ya kukuwezesha kufikia malengo
yako.
13. Ili uendelee kuwa katika misingi ya
matamanio ya mafanikio ya maisha yako ni lazima uwe tayari kujifunza vitu
vipya. Jifunze jinsi ya kuwa bora zaidi kwa yale unayoyafanya. Jifunze jinsi ya
kukabiliana na changamoto mpya, jifunze jinsi wengine walivyofanikiwa kwenye
yale yanayoonekana kikwazo kwako na hatimaye tumia maarifa hayo kufikia ndoto
za maisha yako.
Hakikisha unapata elimu sahihi juu ya fedha, uchumi, biashara
na jinsi kuwapata wafanyakazi wenye uchu wa mafanikio ili hatimaye kwa pamoja
wewe na wafanyakazi wako muongee lugha moja. Jifunze jinsi ya kuilinda fedha
yako kwa kuepuka matumizi ya hovyo yaliyozoeleka kwenye jamii inayokuzunguka.
14. Wafanye watu wako wa karibu watambue
kuwa sasa unaishi maisha ya ndoto zako. Hii ni pamoja na kuhakikisha kuwa
wanafamilia, marafiki, wafanyakazi wenzio, ndugu au mwajiri wako wanatambua
msimamo wako juu ya maisha yako mapya. Wafanye watambue kuwa huna muda wa
kulalamika, huna muda wa kuishi maisha ya hofu, maisha ya majungu na kwa kufanya
hivyo hakikisha kila mmoja anatambua kusudi na dhamira ya maisha yako mapya ili
pasiwepo mtu wa kukwamisha.
15. Epuka sana kuwa na likizo kwa ajili ya
kupata muda wa kupumuzika pasipo kujishughulisha na kazi yoyote. Mwandishi
anatumia msemo kuwa kama unataka kukutana na mwovu (shetani) ruhusu muda wa wazi
katika ratiba yako. Hivyo, badala ya kutumia muda wa likizo kwa ajili ya kulala
na kufanya mambo ambayo sio muhimu, tumia muda wa likizo yako kwa kuhuisha upya
matamanio ya mafanikio ya ndoto kubwa ya maisha yako. Hakikisha unapata muda wa
kujiuliza ni wapi unaweza kuboresha zaidi, jitathimini wapi umekosea na wapi
umefanya kwa ufanisi zaidi.
16. Ulevi wa matamanio ya mafanikio ya
ndoto za maisha yako sio tu kujikita kwenye sehemu moja ya maisha yako bali
inahusisha mafanikio katika kila sekta ya maisha yako. Hii inajumuisha
mafanikio ya kiroho, kiuchumi, familia, afya, kijamii, maarifa/elimu na fedha.
Hivyo watu wenye matamanio ya mafanikio ya maisha yao hawachagui sekta moja
bali kila sekta ya maisha yao wanaipa kipaumbele kwa ajili ya mafanikio ya viwango vya juu na
wanatafuta kila njia ya kufanikiwa katika sekta hizo.
17. Kadri unavyozidi kufanikiwa ndivyo watu
wanaokubeza wanavyo ongozeka. Hii ni kutokana na ukweli kwamba pale
unapotangaza dhamira ya matamanio ya mafanikio ya maisha yako ndivyo kila hatua
unayopiga wapo wengi wanaosubiria kuona kama ulikuwa na dhamira ya kweli hama
ulikuwa unajaribu. Kuwa tayari kupambana kwa ajili ya kutimiza dhamira yako
pasipokujali yale yanayozungumzwa kwenye jamii inayokuzunguka. Hapa unatakiwa
kukumbuka kuwa sio kila neno unaloambiwa na wanaokuzunguka kuwa lina nia mbaya
juu yako lakini tatizo ni kwamba baadhi ya maneno yanaweza kukutoa kwenye
msimamo wako.
Mfano, angalia sentensi kama hizi “kuwa
makini”, “angalia hatua zako”, “haraka haraka haina baraka”, kwanini hujitese
hivyo?, kwanini hauridhiki? na nyinginezo. Sentensi zote hizo zina nia nzuri
juu yako lakini shida ni kwamba wewe ndo unajua hatua zako na hao wanaokupa
tahadhari hizo wengi wao hawajawai kujaribu yale uliyodhamiria kufanya. Njia
nzuri ya kuwanyamazisha ni kuhakikisha unawajibu kwa ushindi katika kila eneo
unalogusa.
18. Ili ufanikiwe kuwatala wengine na
mazingira yanayokuzunguka ni lazima uwe tayari kujitawala mwenyewe. Hapa
unatakiwa uwe na uwezo wa kudhibiti hisia zako katika kila sehemu ya maisha
yako ili kila unaloamua kufanya au kutofanya liwe ndani ya misingi
uliyojiwekea. Mwandishi anatufundisha kuwa kufikia viwango vya mafanikio
makubwa inabidi uwe tayari kudhibiti na kutawala fikra zako juu ya uwezo wako,
juu ya fedha, matumizi ya muda, matumizi ya fedha zako, jamii inayokuzunguka,
kazi/fani yako na hatimaye uwe tayari kutawala utambulisho wa biashara yako
kwenye jamii.
19. Tumia mitandao ya kijamii kwa ajili ya
kutangaza yale unayoyafanya. Mwandishi anatushirikisha kuwa baada ya
kuanzishwa kwa mitandao ya kijamii kuna makundi matatu yalitokea ambayo ni (a)
waliolalamika juu ya uwepo wa mitandao hii (b) Mashabiki wa mitandao hii
(watumiwaji kufikisha ujumbe) na (c) waliotumia mitandao hii kujitangaza na
kuuza bidhaa zao.
Katika
ulimwengu huu wa mapinduzi ya teknolojia ya habari kama unataka kufanikiwa kwa
kiwango cha hali ya juu hakuna namna nyingine zaidi ya kuwa kwenye kundi la
tatu ili kuhakikisha unatumia nguvu zako zote kutangaza biashara zako kupitia
mitandao hii kutokana na unafuu wake kwenye gharama za matangazo. Epuka kabisa
kuwa mtumiwaji wa mitandao kwa maana ya kundi la pili kwani kufanya hivyo sio
unapoteza muda wako bali unaharibu hata mfumo wako wa fikra.
20. Njia mojawapo ya kukufanya uendelee kuwa
kwenye viwango vya mafanikio ni kuwa mtu wa hatari katika kila eneo la maisha
yako. Inabidi uwe mtu hatari kwa wapinzani wako, mtu hatari kwa wateja wako kwa
kuwapatia kile wanachotaka, kuwa hatari kwa mwajiri/waajiriwa wako kwa
kuhakikisha unatimiza wajibu wako na kuwa mtu hatari kwa watu wako wa karibu
ili waendelee kuheshimu muda wako na misingi uliyojiwekea katika maisha yako ya
kila siku. Ili uendelee kuwa mtu hatari unahitaji kufanya yafuatayo;
- Hama kijiji/mji uliokulia na kwenda kuanzisha makazi yako mapya sehemu nyingine kwa ajili ya kupata changamoto na mitazamo mipya. Kuhama kutafanya husiwe kwenye mazingira ya kuridhika ambayo ni hatari kwa wewe kuendelea kutafuta mafanikio zaidi;
- Muda wote tafuta uhusiano na watu wapya. Hakikisha muda wote unatafuta watu wapya hasa waliofanikiwa zaidi, wahamasishaji au watu maarufu kwa ajili ya kupata changamoto na elimu mpya;
- Mafanikio hayaji kwa kutafuta umaarufu bali endelea kuishi misingi ya maisha yako na kamwe husifanye biashara kwa kutaka uonekane mwema kwa wale unaofanya nao biashara. Kama kuna nafasi ya kuomba punguzo fanya hivyo na muda wote husionekane kuwa muhitaji sana wa bidhaa/huduma husika;
- Kuwa tayari kuwekeza katika mazingira hatarishi (risk), husiogope kuwekeza kwa vile unaogopa risk;
- Jifunze kutumia teknolojia mpya kwa ajili ya kuboresha yale unayoyafanya;
- Kuwa tayari kufanya mashambulizi ya fursa mpya kwa muda wote;
- Husikubali kuridhika na kipindi ambacho mambo yatakuwa hayaendi vizuri bali pambana utoke kwenye hali hiyo; na
- Jifunze kutumia hofu kwa kuibadilisha na kupata ubunifu wa vitu vitakavyoinua maisha yako. Hofu ni kipimo cha jinsi ambavyo utafanikiwa kufanya vitu na sio kuacha kufanya vitu;
21. Jifunze kuwa muuzaji (sales person) kwa
kadri uwezavyo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba mauzo ndo mafuta ya kuendesha
kila aina ya biashara/kampuni/taasisi. Biashara au kampuni bila mauzo ni mfu. Ili
kuboresha mauzo yako ni lazima kuhakikisha;
- Unatoa bidhaa/huduma inayokidhi mahitaji ya walengwa (wateja) na hapa unapaswa ujiweke kwenye nafasi ya wateja na kujipima kama ndo mteja je ungeendelea kununua bidhaa/huduma hiyo?;
- Tangaza bei ya bidhaa/huduma yako kwa kila mteja pale unapopata nafasi ya kufanya hivyo na hakikisha unamshawishi mteja kufanya biashara na wewe;
- Muda wote fikiria kufikia kiwango cha juu cha mauzo ya bidhaaa/huduma yako na hakikisha kila mfanyakazi wako umempa lengo lake la mauzo na pale anapofanikiwa kufikia lengo mpongeze;
- Namba hazidanganyi bali watu ndo wanadanganya hivyo hakikisha kila muda unayatathimini mafanikio ya mauzo yako kwa namba na si vinginevyo. Kupitia namba unaweza kukadiria mauzo, pato na kukua kwa biashara yako katika siku za mbeleni;
- Hakikisha kila siku una kikao cha mauzo na wafanyakazi wako na kitika vikao hivi lengo liwe kuhakikisha kila mmoja ndani ya timu ana hamasa ya kuongeza mauzo zaidi; na
- Hakikisha kila siku unapiga simu kwa ajili ya kuwashawishi wateja kununua bidhaa/huduma zako.
22. Toa ahadi zaidi kwa wateja juu ya bidhaa/huduma zako na wasilisha bidhaa/huduma kwa idadi/viwango vya juu. Na katika yote haya epuka sana kutoa mihadi za uongo kwa wateja bali ahidi kile ambacho kitamridhisha mteja. Pia hakikisha kila unapomtangazia mteja biashara yako fanya hivyo kwa kujiamini ukiwa na ujasiri wa hali ya juu ili mteja ajenge imani katika kile unachotaka kumuuzia.
Badilisha mbinu za kushawishi wateja
kulingana na aina ya wateja pamoja na upungufu wa wapinzani wako katika soko. Hakikisha
unatumia nafasi zinazoachwa wazi na wapinzani wako katika soko kwa ajili ya
kuvuta wateja wengi zaidi kwako. Hata hivyo, mara zote unatakiwa kuhakikisha mteja
wako anakuwa mshindi katika kila hali kama ambavyo tumezoea msemo wa mteja ni
mfalme. Hapa ndipo unatakiwa kufahamu kuwa wateja hawanunui kwa bei
unayowatajia bali wananunua kutokana na thamani ya bidhaa/huduma unayowapa. Hivyo
hakikisha unamfanya mteja atambue thamani ya bidhaa/huduma yako kwake kwa haraka
zaidi iwezekanavyo.
23. Hakikisha unatengeneza timu ya
wafanyakazi wenye uchu wa kufanyakazi. Hii ni sawa na Rais wa Marekani Donald
Trump alivyoliweka sawa katika kitabu chake cha “How to Get Rich – Jinsi ya Kuwa Tajiri” kuwa anafanya kazi na wale
walio bora na kama wewe hauna ubora hauna nafasi katika kampuni zake. Vivyo hivyo
mwandishi Grant Cardone anasisitiza juu ya umuhimu wa kuwa na timu ya wanyakazi
wenye dhamira ya kufanya kazi kwa mafanikio ya kampuni/biashara na ya kwao pia. Pia,
anatushirikisha umuhimu wa kuhakikisha tunajenga timu imara ya wafanyakazi
unaowaamini ili kuepuka biashara kuendeshwa na mtu mmoja (mmiliki) kama ilivyozoeleka
katika biashara nyingi.
Kutengeneza timu ya wafanyakazi bora ni
njia ya pekee ya kukuza biashara yako kutokana na ukweli kuwa biashara ni watu
na kila mtu ana kipaji tofauti na cha mwenzake. Hata hivyo ili kufanikiwa zaidi
ni lazima kuhakikisha kila mmoja kwenye timu anajua majukumu yake na ana shauku
ya kufanya hivyo pasipo kulazimishwa au kuogopa uwepo wa bosi wake. Na hapa
ndipo unatakiwa kujenga utamaduni wa biashara yako ili kila mmoja kwenye timu
ajue utamaduni huu pasipo kujali ni mgeni au ni mkongwe kwenye timu yako.
24. Husiwe mwepesi wa kukimbia kutokana na
kutopata majibu ya haraka, pambana ukiwa mvumilivu mpaka matokeo tarajiwa
yapatikane. Kawaida tunapopanga tunachukulia kuwa kila kitu kitaenda sawa katika
kufanikisha mipango yetu lakini mara nyingi mazingira hayapo hivyo. Katika uhalisia
ni lazima utakutana na changamoto na hivyo utakuwa kwenye milima na mabonde,
unachotakiwa ni kuendelea kuamini katika wazo lako pasipo kukata tamaa. Na daima
husitafute visingizio kwa ajili ya kuachana na wazo lako kwani kukimbia ni
dalili ya kushindwa.
25. Hakikisha unakaa katika shauku ya
kufanikiwa zaidi kwa kadri uwezavyo kwa kutumia kila aina ya rasilimali
ulizonazo. Tumia mafanikio yako uliyonayo kwa wakati huo kwa ajili ya kuongeza
changamoto zitakazokusukuma kutafuta zaidi na zaidi. Hatimaye tengeneza urafiki
na watu waliofanikiwa zaidi yako ili kupitia wao upate changamoto za kuboresha
zaidi mafanikio yako.
Soma: Januari, 2017 Umetuachaje?
Haya ni machache kati ya
mengi niliyojifunza kutoka kwenye kitabu ambacho nashauri kila mmoja mwenye
utamaduni wa kusoma vitabu akisome. Rafiki naamini kuwa kama utayafanyia kazi
yatakupa mabadiliko makubwa ya maisha yako. Niendelee kukuomba usambaze jumbe
hizi kwa kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye
tufanikiwe kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi. Nakutakia mapambano mema.
Ili kupata makala za namna
hii acha taarifa zako kwa kujaza fomu hapo chini.
Karibuni kwenye fikra
tajiri ili upate elimu hisiyokuwa na mwisho.
Born to Win~Dream Big