Habari rafiki yangu
ambaye umekuwa msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri. Karibu katika mwendelezo wa kukamilisha uchambuzi wa kitabu cha 3 kati ya vitabu 30 ambavyo
nimejiwekea lengo kuvisoma katika kipindi cha mwaka huu 2020.
Kama bado hujajiunga
na kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya kupata neno la
tafakari kila siku pamoja na kujumuika na watu wenye mtazamo sawa, tafadhali
fanya hivyo KWA KUBONYEZA HAPA na kujiunga
na kundi letu. Nafasi ni chache hivyo fanya maamuzi ya kujiunga sasa.
Kitabu ninachokushirikisha
kupitia makala hii ni “The Principles and Power of Vision”
kutoka kwa mwandishi Dr. Myles Munroe ambaye ni mwandishi na mhamasishaji mkuu
wa maswala ya Uongozi, Kiroho na Mtalaamu mwelekezi kwenye masuala ya biashara
na Serikali. Amefanikiwa kuandika vitabu mbalimbali ikiwepo kitabu cha Keys to
Leadership na vingine vingi.
Kama hukusoma uchambuzi wa awali unaweza kusoma makala hiyo kwa kubofya hapa chini:-
Soma: Mambo Niliyojifunza kwenye kitabu cha The Principles and Power of Vision: Kanuni na nguvu ya Maono.
Karibu ujifunze kanuni 12 za kuishi maisha
yenye maono ambazo ambazo zinakusudia kulinda, kuhifadhi na kukuhakikisha ndoto
zako zinatimizwa katika kipindi cha maisha yako.
19.
Kanuni #1: Mara zote ongozwa na maono yaliyo wazi. Kukamilisha
maono yako unatakiwa kuongozwa na kusudi la maisha ambalo lipo wazi. Watu wote
waliofanikiwa kimaishan; kwa kutaja tu baadhi Abrahamu, Musa, Daniel na wengine
wote tunaowafahamu katika historia ya maisha mwanadamu kama vile J.K. Nyerere,
Nelson Mandera, Kwame Nkrumah, Albert Einsten na wengineo kwa pamoja kila mmoja
wao aliongozwa na kusudi maalumu ambalo lilimfanya atimize maono yake. Mwongozo
wa maono ni ufunguo wa mafanikio kwa yeyote anataka kuishi maisha yenye thamani
katika Dunia hii. Unahitaji kufahamu kwa nini ulizawaliwa (kusudi la maisha) na
kuwa na uwezo kujiona katika picha kubwa ya kuishi mapana ya kusudi la maisha
yako (maono). Maswali muhimu ambayo kila mtu anatakiwa kujiuliza ni:
ü Je ni
mambo yapi unataka kukamilisha katika maisha yako?
ü Je
kazi unayofanya kwa sasa inakusaidia katika kukamilisha kusudi la maisha yako?
ü Je
maisha unayoishi leo hii yanaacha alama yoyote katika Dunia hii baada ya ukomo
wa maisha yako?
ü Je
una picha kubwa ya mafanikio unayotaka kufanikisha kutokana na kuishi kusudi la
maisha yako?
ü Je
upo kubadilika na kuachana na ukanda wa faraja (comfort zone) na kuelekea
kwenye mabadiliko halisi yatakayowezesha kuishi kusudi la maisha yako?
ü Je
upo tayari kuchukua hatua zinazolenga kubadilisha matamanio kuwa uhalisia kwani
umeishi muda mrefe katika matamanio hayo bila kuchukua hatua?
20. Kanuni
#2: Tambua uwezo ulionao katika kufanikisha kuishi maono yako. Unapogundua
ndoto ya maisha yako pia utagundua uwezo uliyopo ndani mwako kwa ajili ya
kutimiza ndoto hiyo. Kumbuka kuwa uwezo huo unategemea jukumu ambalo Muumba
anakusudia ulitimize kupitia maisha yako. Na kulingana na jukumu hilo amekupa
uwezo ambao unatakiwa kuutumia kukamilisha jukumu husika. Uwezo huu umejificha
ndani mwako na haujatumika kutokana na kuishi maisha ya kujitathimini chini ya
kiwango. Hapa ndipo unatakiwa kufahamu
kuwa Muumba wetu hajatuumba na kutuacha wapweke bali nguvu yake imo ndani mwetu
kwa ajili ya kutuongoza. Kupitia yeye tunaweza kukamilisha jambo lolote ambalo
linaonekana kuwa gumu katika maisha yetu. Kupitia uumbaji wako Mungu amekupa
kila uwezo unaotakiwa kwa ajili ya kukamilisha jukumu analokutaka ulikamilishe
katika kipindi cha uhai wako.
21.
Kanuni #3: Tengeneza Mpango wa Kufanikisha Maono yako. Ili
ufanikiwe unahitaji kuwa na mpango ambao unakuongoza katika safari ya kuishi
maono uliyonayo. Mwenyezi Mungu amekupa maono hila wajibu wako ni kuhakikisha
unaandaa mpango kwenye karatasi kwa ajili ya kuutumia mpango huo kutimiza maono
uliyopewa. Mwenyezi Mungu nae ataongoza hatua zako katika kutekeleza mpango
wako na hatimaye kufanikisha matamanio ya maisha yako. Katika kuandaa mpango wa
kutimiza maono yako ni lazima uanze kwa kujiuliza maswali haya: a) Mimi ni
nani? Swali hili linalenga kukumbusha kwa nini umeumbwa kwa maana umeumbwa kwa
ajili ya kukamilisha kazi gani hapa Duniani – kumbuka kuwa wewe ni wa kipekee
na upo tofauti mtu yeyote yule Duniani; b) Je nataka kuelekea wapi? Swali hili
linalenga kukumbusha maisha kuwa mpango unaouandaa unatakiwa kukamilisha kusudi
la maisha yako na si vinginevyo; c) Je kwa sasa nina uwezo gani au namiliki
nini? Majibu ya swali hili yanalenga kukumbusha kuwa safari ya kuishi maono ya
maisha yako inaanzia kwenye uwezo au vitu unavyomiliki kwa wakati huo; na d)
Ufanye mpango wako kuwa siri maana watu watakukatisha tamaa.
22. Kanuni #4: Kuwa na Hamasa juu ya Maono yako.
Hamasa ndio itakuongoza kugundua thamani halisi ya maisha yako. Hamasa ndio
inawaongoza watu kugundua kitu cha muhimu na thamani katika maisha kuliko
maisha yao yenyewe. Kumbuka kuwa maandiko matakatifu yanasema wale wenye kutaka
kuokoa maisha yao wenyewe watayapoteza (Mathew 16:25). Tafsiri yake ni kwamba
uzima wa kweli upo kwenye maisha yako kwa ajili ya wengine. Unatakiwa kuikana
nafsi yako kwa ajili ya kusudi maalumu la maisha yako. Je una njaa/kiu kiasi gani
kwa ajili ya kutimiza maono yako? Kiwango cha kiu/njaa uliyonayo ndicho
kinaonesha hamasa yako kuishi maisha ya maono. Kiwango hicho ndicho
kinakusukuma kutoridhika na hali ya maisha yako na hivyo kuongeza jitihada za
kuyafanya maisha yako yawe na thamani zaidi. Hamasa ya kweli ndio itakuongoza
kupita kwenye vikwazo vya mabonde na milima, baridi na moto, vita na Amani na
kuendelea na maisha ya kusudi la maisha yako (2Wakorintho 11: 22-28). Hamasa ndiyo
itakuongoza kunyanyuka mara baada ya kuanguka na kuendelea na safari ya kusudi
la maisha yako. Kumbuka kuwa wengi wanashindwa kutimiza kusudi la maisha yao
kwa kuwa wanakata tamaa pale wanapoanguka.
23.
Kanuni #5: Jenga Imani dhidi ya maono yako. Kuona ni kazi ya macho
wakati maono ni kazi ya roho. Unaweza kuwa na macho ya kuona lakini ukakosa
maono kwa kuwa hiyo ndiyo zawadi kubwa ambayo Mungu amempa mwanadamu. Uwezo wa
kuona vitu visivyoonekana au uwezo wa kuumba vitu ambavyo havijaumbika ndiyo
zawadi ya kipekee ambayo inamfa Mwanadamu afanane na Muumba wake kwa sura na
mfano wake (Mwanzo 1:26). Maono yanamwezesha mtu kuona vitu kwa jinsi
vinavyotakiwa kuwa (ambavyo havijaumbika) wakati macho yasiyo na maono yanaona
vitu jinsi vilivyo (vilivyoumbwa tayari). Tafsiri yake ni kwamba hatupaswi
kuruhusu yale ambayo macho yetu yanaona kuamua kile ambacho roho yetu inaamini.
Kwa maneno mengine ni kwamba tunatakiwa kutembea katika Imani kuliko kutembea
kwa upeo wa macho yetu. Ukiwa na Imani ni rahisi kuona vitu unavyotarajiwa kuwa
navyo na kuviishi katika maisha ya sasa. Imani inakuwezesha kuona vikwazo kama
sehemu ya fursa za kukufikisha kwenye maisha ya maono yako. Na ni kupitia Imani
unakuwa na tumaini la maisha na kuishi maisha yasiyo na chembe ya uoga wala
hofu.
24. Kanuni #6: Fahamu mchakato wa Maono. Mwenyezi
Mungu ana mpango na makusudi kwa kila maisha ya mwanadamu na mpango huo
unajidhihirisha taratibu katika maisha ya mhusika. Hata hivyo, pamoja na kwamba
Mungu ana makusudi na maisha ya kila mwanadamu ni mara chache sana kukufunulia
kuhusu kusudi hilo bali anakuongoza hatua kwa hatua katika kulitambua na
kuliishi katika maisha ya kila siku. Mungu amefanya hivyo ili kila mwanadamu
ajifunze na kujenga tabia kadri anavyopiga hatua kuelekea kwenye kusudi la
maisha yake. Kama kila mtu angepewa mafanikio anayotaka bila kutumia jitihada
zozote maisha yasingekuwa na thamani. Wengi tunaona mafanikio tunayotamani
katika maisha yetu katika picha kubwa hila tunatamani tupate mafanikio hayo
kesho yake. Mpango wa Mungu haupo hivyo unahitaji kuona kilele cha mafanikio
katika maisha yako na kuweka mikakati ya kuishi kila siku kwa ajili ya kufikia
kilele hicho. Ni lazima kutambua kuwa hadi maono yako yakamilike ni lazima
upitie kwenye mateso, milima, mabonde, kukataliwa, kujituma, kujikataa mwenyewe,
na kutoa sadaka halali ya kila aina. Kwa kifupi ni lazima utambue kuwa
ukamilisho wa maono ya maisha yako unaambatana na kulipa gharama. Kipindi hicho
cha mpito ni kwa ajili ya kukuandaa na kukujenga kiakili, kifikra, kitabia na
kihekima.
25. Kanuni
#7: Jenga vipaumbele vya maono ya maisha yako. Maisha
yako jinsi yalivyo ni majumuisho na matokeo ya maamuzi na machaguzi unayofanya
kila siku ya maisha yako. Ili ufanikiwe kuishi maono ya maisha yako ni lazima
uwe na vipaumbele ambavyo vinakusogeza kwenye kilele cha maono ya maisha yako. Vipaumbele
hivyo ndivyo vinatakiwa kuwa msingi kwako katika kufanya maamuzi ya kuchagua
yapi unaweza kufanya au kutofanya katika maisha yako ya kila siku. Maisha yamejaa
mbadala unapochagua kuacha tukio moja unakuwa umeamua kuchagua mbadala wake. Hapa
ndipo unatakiwa kujua thamani ya kutumia maneno NDIYO na HAPANA katika maisha
yako ya kila siku. Kadri unavyosema NDIYO kwenye tukio moja unakuwa umesema
HAPANA kwenye mbadala wake. Unatakiwa kufahamu kuwa unaweza kufanya au
kushiriki kwenye jambo au tukio lolote lakini sio kila tukio hilo ni muhimu
katika maisha yako. Kumbe, ufanikiwe kuishi kusudi la maisha yako unatakia
kujikita kwenye vitu au matukio ambayo yanachangia kwenye ukamilifu wa malengo
ya maisha yako. Mwisho, ulifanikiwa kufika unakokusudia unatakiwa kuwa na alama
zinazokuongoza katika maisha ya kila siku. Fanya yote unayofanya lakini
ukifahamu hitimisho au kiashiria cha mafanikio ni kipi kwa kila lengo
unalotekeleza katika maisha.
26. Kanuni
#8: Tambua mchango wa watu wanaokuzunguka. Hakuna namna nyingine
ya kufikia kusudi la maisha yako bila uwepo wa mchango wa jamii inayokuzunguka.
Katika jamii unatakiwa kufahamu makundi ya aina mbili; kundi la kwanza ni la
watu ambao wapo tayari kukusaidia au kukuwezesha kutimiza kusudi la maisha yako
na kundi la pili ni watu ambao watakukwamisha kutimiza kusudi la maisha yako. Wapo
watu ambao Mwenyezi Mungu amekuandalia tayari kwa ajili kukushika mkono katika
safari yako ya kutimiza kusudi la maisha yako. Wajibu wako ni kuwatambua watu
hao na kujua namna ya kuishi nao katika maisha yako ya kila siku. Unatakiwa kuifahamu
na kuitumia Sheria ya Asili ya Mjumuiko – Sheria hii inasema wewe ni zao la
wale ambao unatumia muda mwingi kukaa nao kwa muda mrefu. Tafsiri yake ni
kwamba wale unaokaa nao kwa muda mrefu wana mchango chanya au hasi katika
kufikia kusudi la maisha yako. Kama unahitaji kufanikiwa zaidi kwenye maono ya
maisha yako, unatakiwa kutumia sheria hii kuondoa watu ambao hawana msaada
katika kuliishi kusudi la maisha yako na kutumia muda mwingi kutengeneza
marafiki ambao mnaendana kifikra, kimawazo na kitabia.
27.
Kanuni #9: Tambua uwezo ulionao katika kuishi maono yako. Mungu
amekuumba na kukupa zawadi ya maono na zawadi hiyo inaambatana na uwezo wenye
vipawa/vipaji ndani yake. Watu wengi wanakuwa waoga kufikia ndoto kubwa iliyopo
ndani mwao kwa vile kila wanapoifikiria wanajitathimini kwa wakati husika na
kujiona hawana uwezo wa kuiweka ndoto hiyo katika uhalisia wake. Wajibu wako ni
kutambua nini unataka katika maisha yako na kuhakikisha unaandaa kwa maandishi mpango
utakaokuwezesha kutimiza hitaji hilo la maisha yako. Pengine yawezekana ndoto
yako ni kubwa kiasi ambacho unaogopa, pengine unajiona kwa sasa hauna
rasilimali na uwezo wa kukuwezesha kuiweka ndoto yako katika uhalisia wake. Kubwa
ambalo unatakiwa kutambua ni kuwa kama upo katika njia sahihi kulingana na
kusudi la Muumba wako hakika ndoto hiyo itabadilishwa kuwa halisi. Pia,
unatakiwa kutambua kuwa uwezo wa kutimiza ndoto zako tayari upo mikononi mwako,
safari inaanzia kwenye kile unachomilika kwa sasa. Kitu cha thamani ambacho
Mwenyezi Mungu ametupa ni ardhi hadi pale utakapomiliki ardhi na vyote
vilivyopo ndani yake ndipo unaianza safari ya maono ya maisha yako.
28. Kanuni
#10: Kuwa Imara katika safari ya kufanikisha maono yako. Kila
maono ni lazima yajaribiwe ili kupima ukweli na uimara wake. Unatakiwa kutambua
kuwa safari ya kuelekea kwenye kilele cha mafanikio ya maono yako kutakuwepo na
dhiki, msongo wa mawazo, kukatishwa tamaa, nyakati za machukizo, kupingwa au
kukataliwa na mengine mengi. Uimara wako katika nyakati hizo ndio
utakaokuwezesha kusonga mbele na hatimaye kusherekea mafanikio ya maono yako. Msimamo
wako wa kuishi kulingana na kanuni au vipaumbele vya maisha yako ndio
utakuwezesha kupita salama katika nyakati ngumu za maisha yako. Ni lazima
katika kila hatua unayopiga uwe tayari kukabiliana pamoja na kutatua changamoto
zinazokuyumbisha ushindwe kupiga hatua. Ni lazima utambue kuwa changamoto na
nyakati ngumu unazopita kwa ujumla wake zinakuandaa kwa mtu yule ambaye unamuona
katika picha kubwa ya maono yako.
29. Kanuni
#11: Kuwa mvumilivu kusubiria ukamilisho wa maono yako. Ukamilimisho
wa maono yako unategemea na kiwango cha uvumilivu hadi pale ambapo utavuna
matunda. Ni watu wachache sana ambao wanaweza kuvumilia hadi mwisho kwani walio
wengi huwa wanahitaji mafanikio ya haraka haraka na matokeo yake wanakata
tamaa. Wengi huwa wanaishia njiani kutokana na kushindwa kuvumilia hadi mwisho.
Ni katika uvumilivu huu unatakiwa kutambua kuwa maisha unayopitia kwa sasa hata
kama hayana uhalisia na matamanio ya maono yako ni kwa ajili ya kukuandaa
kuelekea kwenye mafanikio ya maono yako. Uvumilivu huleta Amani katika nyakati
za wasiwasi na uvumilivu pia ni ufunguo wa kushinda shida katima maisha. Kwa tafsiri
ya haraka kupitia kanuni hii unatakiwa kuzishinda hisia zako katika kila hali
kwa ajili ya kufanikiwa kushinda vishawishi au vikwazo ambavyo vinalenga
kukutoa kwenye malengo uliyojiwekea kuelekea kwenye kusudi la maisha yako.
30. Kanuni
#12: Kaa katika Muunganiko na chanzo halisi cha maono yako. Kama ambavyo
tumeona kuwa maono ni zawadi pekee ambayo Muumba amempa mwanadamu, kanuni hii
inatukumbusha umuhimu wa kuwa na muunganiko na muumba wetu ambaye ni chanzo
halisi cha maono yetu. Ni kupitia sara Mwanadamu anaunganika na Muumba wake.
Kupitia sara Mwanadamu anaendelea anafunuliwa na Muumba wake kuhusu kusudi la
maisha yake. Pia, kupitia muunganiko wa sara Mwenyezi Mungu anampa hamasa ya
kuendelea kupiga hatua zaidi kutimiza kusudi la maisha yake.
SEHEMU
YA TATU: NGUVU YA MAONO
31. Kila
mwanadamu amezaliwa kwa ajili ya kufanya kitu cha kipekee katika kipindi cha
maisha yake. Umeumbwa kwa ajili ya kufanya kitu ambacho kitaacha rutuba kwa
vizazi vyako ili viote na kuchipua kupitia rutuba yako. Maisha yetu
yanagawanyika katika misimu mine: Msimu
wa kwanza ni kipindi cha kuzaliwa na
utegemezi – katika msimu huu tunategemea zaidi usaidizi kutoka nje wa uwezo
wetu. Mfano, utegemezi kutoka kwa wazazi au walezi kupata mahitaji yetu muhimu
ya maisha. Msimu wa pili ni kipindi cha kujitegemea
– katima msimu huu mhusika anakuwa tayari anaweza kujitegemea kukidhi mahitaji
yake yote ya maisha. Huu ni msimu ambao unatakiwa kutambua umezaliwa kwa ajili
ya kufanya nini (kusudi la maisha yako). Msimu
wa tatu ni kipindi cha kutegemewa
– katika kipindi hiki unatakiwa kuwa tayari umefanikisha ndoto za maisha kiasi
ambacho unaweza kuwa msaada wengine kufanikisha ndoto zao. Na hapa ndipo
unaweza kupitisha maono yako kwenda kizazi kingine. Msimu wa nne ni kipindi cha kifo
ambapo katika kipindi maisha ya mhusika anatakiwa kuacha alama ambayo ni rutuba
muhimu kwa vizazi vingine kuishi maisha bora ya kusudi la maisha yao. Katika kipindi
hiki kizazi kinachobakia kinatakiwa kujivunia siku za maisha yako. Kwa tafsiri
hii ni kwamba maono yanatuwezesha kuishi maisha yenye thamani katika Dunia hii.
32. Unapogundua
na kuishi maono ya maisha yako ni njia ya kujitambua wewe ni nani. Unapojitambua
wewe ni nani kwa maana umezaliwa kwa ajili ya kufanikisha nini katika maisha
yako ni hatua ya kuishi maisha yenye dira. Dira hiyo unatakiwa kuiandika kwenye
maandiko ili kila uiboreshe kulingana na mwongozo wa Muumba wako. Dira hiyo
inatakiwa kuvunjwa katika malengo madogo madogo ambayo kila mara unajibidisha
kuyakamilisha katika maisha yako. Unapoandika malengo ya maisha yako unatakiwa kuzingatia
hatua hizi:-
ü Hatua ya kwanza: Ondoa vikwazo vyote – Kaa sehemu
ambapo hakuna usumbufu wowote na orodhesha malengo yako kwenye kila sekta ya
maisha yako. Fanya zoezi hili kila mara kwa ajili ya kuainisha malengo na
kuyafanyia tathimini.
ü Hatua ya pili: Itambue nafsi yako halisi –
Bila
kutambua kuwa umeumbwa kwa ajili ya kukamilisha nini Duniani humu maisha yako
yatakuwa yenye msukosuko. Unatakiwa kujibu maswali haya kuhusu nafsi yako. Je
mimi ni nani? Mimi ni nani kulingana na mtazamo wa Muumba wangu? Natoka wapi na
nahitaji kwenda wapi? Kwa nini nipo hapa nilipo?
ü Hatua ya tatu: Tafuta maono yako ya ukweli
– Hapa
ndipo unahitaji kutambua maono yako halisi. Unapotambua maono yako halisi
utaanza kuona vitu ambavyo hukuwahi kuviona. Katika hatua hii unatakiwa kuruhusu
fikra huru na kuweza kujibu maswali haya: Je nahitaji kukamilisha nini katika
maisha yangu? Je ni vitu gani nahamasika kufanya? Ni vitu vipi ambavyo
napendelea kufanya zaidi hata kama silipwi kutokana na kazi hiyo? Ni vitu vipi
ambavyo napendelea kufanya kiasi ambacho naweza kusahau kula au kulala? Je
ungependa kuwa mzazi wa aina gani? Je ungetamani siku ya mazishi yako wosia
wako uwe wa aina gani? Je ni alama ipi ambayo ungependa kuiacha katika jamii
inayokuzunguka?
ü Hatua ya nne: Gundua motisha yako ya
kweli – Maono kutoka Mungu kamwe haya uchoyo kwa wengine. Mara zote
yanalenga ya kuvuta wengine na kuwawezesha kuishi maisha yenye thamani. Maono ya
kweli yanalenga kuibadilisha Dunia kuwa mahala pa zuri pa kuishi. Hapa unatakiwa
kujibu maswali haya: Je maono yangu yanasaidia vipi wengine? Je nina motisha
ipi kwa ajili ya maono yangu? Je ni kwa nini nataka kutekeleza yale
ninayohitaji kukamilisha? Je naweza kukamilisha maono yangu na kuendelea kuwa
mwadilifu?
ü Hatua ya tano: Ainisha kanuni za maisha
yako – Kanuni ni falsafa
za kuongoza maisha yako. Kwa maneno ni mengine ni misingi unayojiwekea kwa
jinsi gani unataka maisha yako yawe. Orodhesha kanuni hizo katika kila sekta ya
maisha yako. Mfano, sitamwabudu miungu zaidi ya Mungu aliye hai, nitawekeza
asilimia …. kama sehemu ya kukuza pato langu.
ü Hatua ya sita: Chagua malengo ya maisha yako – Malengo
ni hatua muhimu kuelekea kwenye ukamilifu wa maono yako. Malengo ni alama za
wazi kukuonesha kuwa unaelekea kwenye ukamilifu wa maono ya maisha yako.
Ainisha malengo kwenye kila sekta ya maisha yako na kuyaandika.
ü Hatua ya saba: Ainisha rasilimali
ulizonazo – Katika hatua hii unatakiwa kuainisha
rasilimali ulizonazo na zile unazotakiwa kuwa nazo kwa ajili ya kukamilisha
maono yako. Ainisha uwezo ulionao, ainisha madhaifu yako, ainisha rasilimali
unazohitaji n.k.
ü Hatua ya nane: Jikite kwenye kuishi maono
yako – Hakikisha kila siku unatekeleza shughuli ambazo
zinachangia kwenye ukamilifu wa maono yako. Pia, yakabidhi maisha yako kwa
Muumba ili akuongoze kwenye kila hatua ya maisha yako.
Hakika kuna mengi ya kujifunza kutoka katika
kitabu hiki kwa yeyote ambaye anahitaji kuishi maisha yenye thamani kwake na
jamii inayomzunguka. Mwandishi ametushirikisha mengi katika kitabu hiki na haya
niliyokushirikisha ni sehemu tu kati ya mengi yaliyopo katika kitabu hiki. Jiunge
na mtandao wa Fikra za Kitajiri kwa KUBONYEZA HAPA.
Endelea
kusambaza makala hizi kwa kadri uwezavyo ili ndugu, jamaa na marafiki wanufaike
kwa kujifunza maarifa mbalimbali kutoka kwa waandishi wa vitabu. Kumbuka
umepata makala hii bila malipo yoyote hivyo hakikisha na wewe unaisambaza bure.
(Unaposambaza makala hizi hakikisha haukopi na kupest badala yake share link). Nakutakia
mapambano mema.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu isiyokuwa na
mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Mwalimu Augustine Mathias
Namba ya Simu: +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua pepe: fikrazatajiri@gmail.com