Mambo 25 Niliyojifunza Kwenye Kitabu cha Keys to Leadership (Misingi ya Uongozi)

Habari ya leo rafiki na msomaji wa mtandao wa fikra za kitajiri. Nimatumaini yangu kuwa upo vizuri na unaendelea kupambana kwa ajili ya kuyaboresha maisha yako. Leo ninakuletea uchambuzi wa kitabu cha Keys to Leadership na pia nipende kukufahamisha kuwa kwa mwaka huu nimejipanga kila mwisho wa wiki (ijumaa) kukuletea uchambuzi wa kitabu kimoja ili kupitia vitabu hivi tuweze kuyaboresha maisha yetu. 

Kitabu hiki kimeandikwa na Dr. Myles Munroe ambaye ni mwandishi na mhamasishaji mkuu wa maswala ya uongozi, kiroho na mtalaamu mwelekezi kwenye masuala ya biashara na serikali. Katika kitabu hiki mwandishi amejikita katika misingi muhimu ya uongozi ambayo inajumuisha uongozi binafsi na jamii inayokuzunguka. Karibu nikushirikishe mambo muhimu 25 niliyojifunza kutoka kwenye kitabu hiki.

1. Kila mtu ameumbwa kuongoza na kila mmoja amepewa jukumu la kukamilisha hapa duniani na jukumu hilo ndilo linaloamua sehemu ya uongozi kwa kila mmoja wetu. Na hili kutimiza jukumu hili ni lazima kila mtu aanze kwa kutengeneza fikra za kuwa kiongozi imara katika eneo husika.


 2. Uongozi bora unajengwa na misingi ya kuwa na roho ya shauku, ubunifu, nidhamu, fikra chanya, kujiamini, amani, kujali muda na huruma. Kama mtu anataka kuwa kiongozi bora lazima kwanza aanze na kujifunza misingi hii muhimu ili iwe mwongozo katika safari anayoiendea. Na mtu anapoanza kuishi misingi hii anaanza kubadilika kutoka kuwa mfuasi na kuwa kiongozi.

3. Viongozi wa kweli hawatafuti madaraka bali wanaongozwa na shauku ya kuwatumikia wafuasi wao kupitia vyeo walivyonavyo. Kama unataka kuwa kiongozi jenga nidhamu ya kufanya vitu kwa manufaa ya jamii nzima na sio kutafuta manufaa binafsi tu.

4. Ujinga mkubwa binadamu alionao ni juu ya kujijua yeye mwenyewe. Kwa maana mwonekano wa binadamu ni matokeo ya jinsi anavyojifikiria yeye mwenyewe na imani anazoamini juu ya uwezo wake. Yale unayoyaamini ndiyo yanayokufanya uonekane jinsi ulivyo. Kama unataka kuwa kiongozi bora jifunze kufikiria kuwa unaweza kuwa kiongozi wa aina hiyo na si vinginevyo na kumbuka kuwa hakuna mwanadamu anayeweza kuishi nje ya mipaka ya imani yake. Hii ni kutokana na ukweli kwamba fikra zinazaa imani, imani inaleta mtazamo na mtazamo unaleta tabia na tabia ndio inatoa mwonekano wa matendo yako.

5. Fedha zinaweza kukupa utajiri na mamlaka yanaweza kukupa nguvu lakini vyote hivi haviwezi kukufanya uwe kiongozi bora bali sifa za uongozi bora zinaanzia kwenye tabia yako na tabia hii ni matokeo ya yale unayoyafikiria na kuyaamini katika maisha yako ya kila siku.

6. Uongozi ni fadhila unayopata kutokana na uaminifu wa wafuasi wako walionao juu yako. Ili wafuasi wako waendelee kukuamini ni lazima uwe tayari kujua misingi inayopelekea uaminiwe na wafuasi wako ili uendelee kujiimarisha katika misingi hiyo.

7. Tabia zako zina nguvu sana katika kuamua uwe mtu wa aina gani kuliko kitu chochote kile hapa dunia. Kutokana na ukweli huu tabia ulizonazo ndizo zinaamua ubora wako katika kila sehemu ya maisha yako. Na tabia hizi ni chimbuko la mtazamo wako juu ya maisha yako na hivyo wewe ni chimbuko la mtazamo wako na mtazamo wako ni wewe. Hivyo, kama hauwezi kudhibiti mtazamo wako kamwe hauwezi kujidhibiti wewe mwenyewe na hivyo hauwezi kudhibiti tabia zako.


8. Mtazamo au tabia ni sifa kuu ya kutofautisha kati ya mtu aliyefanikiwa na yule aliyeshindwa. Kutokana na ukweli huu fursa nyingi zimepotea au kusubirishwa kutokana na mtazamo au tabia za watu kuliko sababu yoyote ile. Hivyo kama unataka kuziona fursa zaidi na zaidi katika eneo unaloongoza huna budi kutathmini upya mtazamo au tabia zako katika maisha yako ya kila siku. Kadri utakavyobadilisha mtazamo/tabia zako ndivyo utakavyoona fursa nyingi zilizokuwa zinakusubiria.

9. Kila mmoja wetu kwa asili ni kiongozi hata kama muhusika hajitambui. Uongozi huu wa asili tulionao hauna uhusiano wowote na utaifa, rangi, kipato, umri, jinsi au elimu wala kitu chochote kile bali kwa asili kila mmoja wetu ameumbwa na kupewa mamlaka ya kutawala mazingira yanayomzunguka. Kuwa katika nafasi ya ufuasi hakukuondolei uongozi wako wa asili bali uongozi umerithishwa kwa asili na hivyo ni wajibu wako kutafuta sehemu inayokusubiria kwa ajili ya kutumia kwa vitendo urithi huu wa asili.

10. Uongozi wa kweli unatokana na mtazamo sahihi uliojengeka kwenye misingi ya kuwahamasisha na kuwapa motisha wengine. Hii ni ukamilisho wa ugunduzi wa makusudi ya nafsi yako (the purpose of your life). Hivyo, uwezo wako wa kuongoza unatokana na picha iliyojengeka akilini mwako. Kwa ukweli huu mawazo/fikra zako ndizo zinazo amua uwezo wako.

11. Kama unataka kuwa kiongozi bora lazima ujifunze kwanza jinsi ya kubadili mtazamo wako kwa sababu mtazamo una nafasi kubwa ya kuamua jinsi tunavyoishi kwenye mazingira yanayotuzunguka. Ni lazima ujifunze jinsi ya kufikiri, kuzungumza, mavazi, vitendo, kutembea, majibu, kuamua, kazi na kuishi kama kiongozi.

12.  Wengi wetu leo hii tumeshindwa kuwa viongozi kutokana na kutokujiamini sisi wenyewe. Hatujiamini kwa yale tunayoyafanya na pengine tunafikiria tutaonekanaje kwenye jamii. Hii ni kutokana na ukweli kwamba viongozi wa kweli wanagundua na kufahamu makusudi ya nafsi yao na hivyo ni rahisi kwao kushawishi mazingira yanayowazunguka kuliko wanavyoweza kushawishiwa na mazigira hayo. Vilevile viongozi wa kweli wanalenga kutatua changamoto wanazokutana nazo na hivyo wanatakiwa kuwa wabunifu katika yale wanayoyafanya.

13. Kila mmoja wetu ana wajibu wa kugundua makusudi ya nafsi yake na kuhakikisha anarekebisha mtizamo wa maisha kulingana na madhumuni ya nafsi yake. Mara nyingi tumeshindwa kuishi makusudi ya maisha yetu kutokana na kukatishwa tamaa au kuwa na hofu kwa pale tunapopaswa kuthubutu.

14. Kiongozi imara ni yule mwenye uwezo wa kushawishi wengine kupitia shauku na hamasa ambayo imejengwa kwenye msingi wa huruma. Kama unataka kuwa kiongozi imara ni lazima uwe tayari kuwahamasisha wengine ili kupitia matendo yako nao waweze kuchukua hatua kuyaboresha maisha yao.

15. Uongozi wa kweli haupimwi kwa yale unayoyafanya bali unapimwa kwa mtazamo au tabia zako. Kwa maana hii kiongozi wa kweli anaweza kujifunza kutoka kwa viongozi wengine lakina hapaswi kuwa wao bali anatakiwa atumie vipaji alivyonavyo katika kutimiza jukumu la maisha yake alilopewa kama zawadi ya uwepo wake hapa duniani.

16. Viongozi hawasubiri mambo yatokee bali wao wanakuwa ni sehemu ya kuandaa mambo yao ya baadaye (leaders create their own future). Kwa maana hii viongozi hawasubiri watu wengine wawafanyie yale wanayoyataka bali wao wanakuwa mstari wa mbele katika kutekeleza yale wanayoyahitaji katika maisha yao ya baadae.

17. Viongozi wa kweli hawana kazi bali wana jukumu la maisha yao yote hivyo viongozi wa kweli hawana kustaafu wala kuwa likizo katika kipindi cha maisha yao yote.

18. Kama utaweza kuwa na hisia za hatima ya maisha yako kwa yale yaliyopita na yale yanayokuja na ukapata picha kubwa ya maisha yako hadi inakuogopesha mwenyewe basi tambua kuwa njia yako ya kuwa kiongozi bora inaanzia hapo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba shauku ya uongozi inaanzia kwa kuunganisha picha ya maisha yako yaliyopita na yale yajao.

19. Binadamu tunao uwezo wa kufanya mambo mengi lakini si yote tunayoyafanya yana mchango katika kutimiza kusudi la maisha yetu. Kiongozi bora ni yule anayefanya yale yanayomsaidia kutimiza kusudi la maisha yake. Viongozi wa kweli lazima waweze kutofautisha jema na baya au fursa ya kweli na ya ovyo na hivyo wapo tayari kuweka vipaumbele kwenye majukumu yao ya kila siku.

20. Viongozi wa kweli wana malengo yanayotokana na mtazamo wao na malengo haya ndiyo yanayowatofautisha viongozi kutoka kwa wafuasi wao. Hivyo kiongozi bora anajua jinsi yakuweka malengo sahihi na kuhakikisha malengo haya yanakuwa kinga dhidi ya ushawishi wa kufanya yale ambayo hayapo kwenye mpango wa malengo ya maisha yake ya kila siku. Kama kiongozi bora unatakiwa kila siku unaweka bidii ya kufikia malengo yako kwa kuwa malengo yako ndio maisha yako na husipofanya hivyo watu wengine watatawala maisha yako.

21. Malengo yanatusaidia kuwa na viashiria vya hatua zetu na hivyo kuepuka kuahirisha yale tuyoliyopanga kutekeleza. Viongozi wa kweli wanatumia orodha ya malengo yao kama mwongozo wa matendo yao na hivyo wanakuwa na nidhamu ya hali ya juu pale wanapotekeleza majukumu yao.

22. Viongozi wa kweli wanapenda kufanya kazi kwa kushirikiana na wenzao kwa vile shauku yao kubwa ni kuona kila mmoja akifanikiwa. Hivyo viongozi bora wanatambua ukweli kuwa mtu hawezi kufanikiwa kwa kufanya kazi peke yake. Pia, katika kutimiza hili viongozi bora wanathamini michango ya wenzao kutokana na ukweli kwamba kila mmoja wetu ameumbwa na kupewa kipaji tofauti na cha mwenzake.

23. Ubunifu ni hazina pekee walionayo viongozi bora. Viongozi bora wana imani katika uzoefu lakini hawatumii kigezo cha uzoefu kama nyenzo pekee ya utendaji kazi bali wanajifunza kila siku kwa ajili ya kujiongezea maarifa pamoja na ubunifu katika kutekeleza majukumu yao.


24. Viongozi wa kweli kamwe hawafungwi na tamaduni za jamii inayowazunguka. Hii ni kutokana na athari za tamaduni kudumaza shauku ya uongozi. Kama unataka kuwa kiongozi bora hakikisha kila ukikutana na fursa, changamoto au tatizo jifunze kufikiria katika njia ya hali tofauti na ulivyoizoesha akili yako ili uepuke kufanya vitu kwa mazoea bali fanya vitu kwa ubora wa hali ya juu.

25. Viongozi wa kweli wanatambua kuwa nidhamu binafsi ni msingi namba moja katika mitazamo na matendo yao na hii ni kutokana na ukweli kwamba nidhamu ni inathibitisha viwango vya hali ya juu kwa kiongozi husika. Hivyo ili kuwa na viwango vya hali ya juu ni lazima uwe tayari kuzuia hisia na mihemko yako kwa kila maamuzi unayoyafanya.

Haya ndiyo niliyojifunza katika kitabu hiki. Ni matumaini yangu kuwa ukiyafanyia kazi yatabadilisha maisha yako kwa ujumla. Niendelee kukuomba usambaze jumbe hizi kwa kadri uwezavyo ili yale unayojifunza yawafikie wengi na hatimaye tufanikiwe kuibadilisha dunia hii kuwa mahali pazuri pa kuishi. Nakutakia mapambano mema.

Ili kupata makala za namna hii acha taarifa zako kwa kujaza fomu hapo chini.

Karibuni kwenye fikra tajiri ili upate elimu hisiyokuwa na mwisho.
Born to Win~Dream Big
A.M. Bilondwa
0786881155
fikratajiri@gmail.com





Subscribe to our mailing list

* indicates required

onclick='window.open(