NENO LEO (FEBRUARI 2, 2020): JINSI UNAVYOWEZA KUKAMILISHA LENGO KWA URAHISI

👉🏾Hongera rafiki na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI kwa kubahatika kuiona asubuhi hii ya leo ambayo ni siku muhimu katika kukoleza moto wa mabadiliko. Wapo wengi walitamani kuiona siku hii lakini hawakufanikiwa hivyo ni jambo la kushukuru na kuhakikisha unaitumia vyema kwa ajili ya kufikia kusudi la maisha yako au kifupi mafanikio ya ndoto yako.

✍🏾Karibu katika neno la tafakari ya leo ambalo linaendelea kutukumbusha umuhimu wa kuwa na malengo katika kila sekta ya maisha yetu na jinsi gani tunaweza kutimiza malengo hayo kwa urahisi.

✍🏾Kwa maneno rahisi, lengo linaweza kuelezewa kama ramani ambayo mhusika naiandaa kwa ajili ya kumuongoza kutoka pointi A kuelekea pointi B katika kipindi cha muda maalum. Katika ramani hiyo mhusika anaweka wazi mbinu, njia na viwango ambavyo vitatumika kama vipimo au viasharia vya kuonesha kuwa amefikia pointi B kama alivyokusudia. Kutokana na tafsiri hii rahisi kuna mambo mengi ya kujifunza.

👉🏿Moja, kabla kuweka lengo katika maisha uanatakiwa ujue uko wapi kwa sasa au nyakati hizo unazoandaa lengo.

👉🏿Mbili lazima uwe na dhamira au msukumo wa ndani wa kwa nini unataka kutoka sehemu ulipo kwa sasa kuelekea sehemu ya matamanio. Msukumo huu unatakiwa kuwa nguvu za kutosha ili ukuvushe njiani bila kukata tamaa.

👉🏿Tatu, ni lazima ufahamu unataka nini au unataka kufikia mafanikio yapi katika maisha yako. Au kifupi ni lazima ufahamu kusudi la lengo hilo nini katika kubadilisha maisha yako ya wakati huo.

👉🏿Nne, ni lazima uandae njia au mikakati ambayo itatumika kufikia mwisho wa lengo.

👉🏿Tano, ni lazima uwe mbinu za kujitathimini ili kuona kama upo njia inayoelekea kwenye kusudio la lengo au umeliacha lengo hilo.

👉🏿Sita, ni lazima uwe na mbinu za kujipima au kitaalamu tunasema viashiria ambavyo vitatumika kuonesha kuwa kweli umefikia sehemu uliyokusudia.

👉🏿Saba, ni lazima liwe na muda maalum wa utekelezaji wake. Mfano, linaweza kuwa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja au miaka 10 na kuendelea.

✍🏾Baada kuweka lengo kubwa sasa linatakiwa kuvunjwa vunjwa katika malengo madogo ambayo yanatakiwa kukamilishwa ndani ya muda mfupi. Kwa maana nyingine ni kwamba maneno madogo yanasaidia kuelekea kwenye ukamilisho wa lengo kuu. Malengo hayo kutoka kwenye lengo kuu ambalo ni la muda mrefu sasa unapata malengo ya siku, mwezi, mwaka n.k.

✍🏾Hapa ndipo watu wengi huwa wanakosea maana baada ya kuwa na lengo kubwa hawaweki malengo madogo ambayo yatawabana katika kila siku ya maisha yao kwa ajili ya ukamilisho wa lengo kuu. Kumbe, baada ya kuweka lengo kuu unatakiwa kujiuliza ili nikamilishe lengo hili natakiwa kufanya nini kila siku, wiki au mwezi kwa ajili ya kufikia ninakokusudia.

✍🏾Mfano, kama nimelenga mwaka huu kukusanya mtaji wa milioni tano. Cha kwanza nitajiuliza ili nifikie lengo natapaswa kila mwezi nijilipe kwanza kiasi gani cha pesa. Baada ya kupata kiwango ninachotakiwa kujilipa kwa mwezi natakiwa nijiulize ili kiwango hicho kitimie natakiwa kila siku nitenge shilingi au nipunguze matumizi yapi ambayo siyo lazima kwenye orodha ya matumizi yangu ya siku.

✍🏾Mwisho, naendelea kukumbusha kuwa mabadiliko ya aina yoyote unayotaka kuyapata katika maisha yako ni lazima utambue kuwa yaanzia ndani mwako. Ni lazima uwe tayari kubadilika kifikra, kimtazamo na tabia. Bila kufanya hivyo hata uweke malengo kiasi gani kamwe hautofika.

👐🏾Nakutakia kila la kheri katika siku hii leo.
🗣🗣 Mwalimu Augustine Mathias

KUPATA MAFUNDISHO HAYA KILA SIKU PAMOJA NA KUJUMUIKA FAMILIA YA FIKRA ZA KITAJIRI BONYEZA HAPA

onclick='window.open(