👉🏾Habari ya asubuhi mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni mategemeo yangu kuwa umeamka salama na upo tayari kuendeleza jitihada za kuboresha maisha yako ili kufikia maisha ya ndoto zako.
KUMBUKA UNAWEZA KUPATA MAFUNDISHO HAYA KILA SIKU PAMOJA NA KUJUMUIKA FAMILIA YA FIKRA ZA KITAJIRI KWA BONYEZA HAPA NA KUJIUNGA
✍🏾Karibu katika neno la tafakari ya leo ambalo linaendelea kusisitiza juu ya umuhimu wa kuwa na malengo ambayo yanapimika na kutekelezwa katika maisha yako ya kila siku.
✍🏾Mafanikio kwenye kila sekta ya maisha yako ni lazima yaanze na ndoto, baada ya kuwa ndoto unatakiwa kutengeneza lengo ambalo linatafsri ndoto hiyo na lengo hilo linatakiwa kuwekewa mikakati midogo midogo inayolenga kukamilisha lengo husika.
✍🏾Ndoto ni ile picha kubwa unayokuwa nayo kwenye sekta ya maisha ambayo unahitaji kuiboresha au kufanikiwa zaidi. Na ili uwe na mafanikio makubwa unatakiwa kuwa na ndoto tena kubwa ambazo zinakuogopesha kila unapoziwaza. Kila mara unatakiwa kuishi katika ndoto hiyo mchana na usiku hadi pale ambapo utaitafsiri kwa kuitengenezea lengo.
✍🏾Baada ya kuandaa lengo ambalo lina sifa zote tulizojifunza katika neno la tafakari ya jana unatakiwa kuweka mikakati ya kulitimiza lengo husika. Mikakati hiyo ni lazima ianze na mabadiliko ya fikra, mtazamo na tabia. Ili ufikie lengo jipya unatakiwa kujenga tabia mpya ambazo zinaendana na malengo yako.
✍🏾Hapa ndipo watu wengi huwa wanashindwa kukamilisha malengo yao kwa vile ni vigumu sana kubadilika kifikra, kimawazo na kitabia kwa vile mabadiliko hayo yanaambatana na mabadiliko ya mfumo mzima wa maisha.
✍🏾Malengo yote katika maisha ili yakamilishwe ni lazima yaambatane na kutoa sadaka. Sadaka inayozungumzwa hapa ni rasilimali ya muda, rasilimali, nguvu (kwa maana ni lazima ufanye kazi kwa jitihada) na kuachana na matukio au vitu unavyopenda zaidi hasa vile ambavyo vinakukwamisha kufikia lengo husika.
✍🏾Wakati mwingine unatakiwa kutoa sadaka ya kuachana na marafiki uliowazoea kama unaona wanaenda kinyume na mtazamo wako mpya. Kumbuka kuwa, sadaka zote utakazotoa zinatakiwa kukubalika kisheria katika jamii unayoishi na si vinginevyo.
✍🏾Mfano, kama umelenga kuboresha afya yako kwa kupunguza kitambi na baada ya kufuatilia ukaambiwa kuwa moja ya sababu inayopelekea uwe na kitambi ni unywaji wa bia na kula sana vyakula vya wanga. Moja kwa moja sadaka ya unayotakiwa kuitoa ni kuachana na bia na vyakula vya wanga. Unapoachana na bia moja kwa moja kuna marafiki utawapoteza.
✍🏾Mwisho, kupitia tafakari ya leo unatakiwa kutambua kuwa ili ufikie lengo ni lazima ujikane na kukubali kubadilisha mfumo mzima wa maisha. Watu wengi wanahitaji mabadiliko lakini ni wagumu kubadilisha mfumo wa maisha yao. Hali hii inapelekea watu kufifisha ndoto walizonazo kwa kuwa kila mara wanaweka malengo ambayo hayatekelezeki kiasi ambacho malengo hayo yanageuka kuwa ndoto tena.
👐🏾Nakutakia kila heri katika siku ya hii ya leo.
🗣🗣 Mwalimu Augustine Mathias