👉🏾Hongera rafiki yangu na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI kwa asubuhi ya leo ambayo ni siku muhimu kwako kuendelea moto wa mafanikio kwenye malengo uliyojiwekea katika kila sekta ya maisha yako.
✍🏾Karibu katika neno la tafakari ya leo ambalo linatufunulia juu ya umuhimu wa kukamilisha majukumu yetu kwa viwango vya hali ya juu. Neno hili linatukumbusha kuwa katika maisha kuna *kujaribu kufanya* na *kufanya*.
✍🏾Tofauti iliyopo kati ya kujaribu kufanya na kufanya ni kwamba anayejaribu hana uhakika na anachokifanya ikilinganishwa na anayefanya. Kwa tafsiri ya haraka ni kwamba huyu anayejaribu kufanya hana lengo linalomuongoza. Hata kama ana lengo, lengo hilo bado hajaliwekea mikakati ya kulikamilisha. Ukiwa hauna lengo unakuwa unajaribu jaribu kila kitu na inapotokea ukakutana na changamoto unasimama hapo hapo na kujisemea hili halitekelezeki.
✍🏾Kwa upande mwingine huyu anayefanya moja kwa moja anakua anajua nini anafanya. Ana uhakika na njia anazotumia kwa kuwa tayari amejiridhisha kuwa njia hizo ndizo sahihi katika kuelekea kwenye ukamilifu wa lengo kuu lake.
✍🏾Kwa bahati mbaya Jamii imejaa idadi kubwa ya watu ambao hawana uhakika na njia wanazosafiria kwa maana watu wanaojaribu kufanya ikilinganishwa na watu ambao wanafanya. Hali hii imepelekea kuwa na asilimia 20 ya watu wenye mafanikio ikilinganishwa na asilimia 80 ya watu ambao kila kukicha wanaangaika bila mafanikio kwa kuwa njia wanazotumia ni za kubahatisha.
✍🏾Ili ufanikiwe katika kila lengo lako ni lazima ujikite kwenye kufanya kazi kwa viwango vya hali ya juu. Unahitaji kuongozwa na weledi na ubunifu ili kwa pamoja viwe silaha ya kukutofautisha na wale wanaojaribu. Unatakiwa kutambua kuwa hakuna njia ya haraka kufikia lengo lako bali njia zote zinakutaka utumie bidii na maarifa na uvumilivu juu.
✍🏾Kitika kufikia lengo kuu huna budi kutambua kuwa changamoto na kushindwa ni sehemu ya somo ambalo linakulenga ukomae na hatimaye ujifunze kutokana na makosa hayo. Husirudie makosa yale yale au kukata tamaa kwa kuwa njia ambayo umeitumia haijakufikisha sehemu uliyokusudia. Kaa chini tafakari njia mbadala baada ya kujua ulikosea wapi katika njia ya awali.
✍🏾Mwisho, namalizia kwa kukumbusha kuwa katika kila unachofanya epuka neno 'nitajaribu kufanya' na badala yake sema 'nitafanya'. Lenga kufanya kwa viwango vya hali ya juu ili hata ukishindwa utakuwa tofauti na anayejaribu kufanya.
👐🏾Nakutakia kila la kheri katika siku hii leo.
🗣🗣 *Mwalimu Augustine Mathias*