👉🏾Habari ya leo mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni matumaini yangu kuwa umeamka salama na upo tayari kuendeleza jitihada za kutimiza malengo ambayo umejiwekea katika kipindi hiki cha mwaka 2020. Kumbuka kuwa lengo letu kubwa ni kuibadilisha Dunia hii kuwa mahala pazuri pa kuishi na lengo hilo ni lazima lianzie katika kubadilisha maisha yako kuelekea kwenye maisha ya ndoto zako.
KUMBUKA UNAWEZA KUPATA MAFUNDISHO HAYA KILA SIKU PAMOJA NA KUJUMUIKA FAMILIA YA FIKRA ZA KITAJIRI KWA BONYEZA HAPA NA KUJIUNGA NA KUNDI LA WHATSAPP.
✍🏾Karibu tena katika neno la tafakari ya leo ambapo tutaangalia kanuni 6 za kuwa tajiri (maisha yenye uhuru wa kifedha) kulingana na ndoto ulizonazo. Neno hili linatushirikisha hatua 6 na kila hatua inahitaji uwe na nidhamu binafsi katika kutimiza malengo unayojiwekea. Kanuni hizo ni kama zilivyoorodheshwa hapa chini:-
✍🏾Kanuni ya kwanza ya utajiri: JILIPE KWANZA. Kanuni hii inakutaka kuhakikisha kwa nidhamu ya hali ya juu kuhakikisha unatunza asilimia flani ya pato lako kabla ya kuanza matumizi. Unaweza kutenga asilimia 10% hadi 20% ya kila shilingi inayoingia mikononi mwako na kuiwekeza sehemu salama. Kumbuka kuwa matajiri wanajilipa kila shilingi inayoingia mikononi mwao na masikini wanatumia kila shilingi inayoingia inayoingia mikononi mwao na madeni juu. Matokeo yake ni kwamba matajiri wanaendelea kuwa matajiri wakati masikini nao wanaoendelea kuwa masikini.
✍🏾Kanuni ya pili ya utajiri: WEKEZA KIASI UNACHOJILIPA KWANZA. Ili utajiri wako uongezeke ni lazima pesa ikufanyie kazi badala ya wewe kufanya kazi ili upate pesa. Maana yake ni kwamba ni lazima uwe na mfumo wa kutengeneza pesa ambao hata kama umelala pesa yako inaendelea kuongezeka thamani. Hivyo, hakikisha kila shilingi unayojilipa inawekezwa sehemu salama ambapo hautashawishika kuitoa hadi pale ambapo utakuwa umetimiza lengo lako la uwekezaji. Mfano, kupitia kujilipa kwanza unaweza kuweka lengo la kukusanya kiasi flani cha pesa kama mtaji wa kuanzisha biashara.
✍🏾Kanuni ya tatu ya utajiri: EPUKA MADENI. Fahamu kuwa Masikini wanalipa riba wakati matajiri wanapokea riba. Siri hii inafanya kazi na tumekuwa tukishuhudia katika jamii tunayoishi jinsi mikopo inavyokandamiza watu wengi. Mikopo sio mibaya bali ubaya uliopo kwenye mikopo husika ni namna mikopo hiyo inavyotumika. Kila unapochukua mkopo unatakiwa kufahamu kuwa umetumia pato lako la siku za baada kabla ya kufikia muda wake. Hivyo, ili kuepukana na matatizo ya kifedha katika siku za baadae unatakiwa kuhakikisha kila mkopo unaochukua utumike kuzalisha faida au kukuza pato lako na si vinginevyo.
✍🏾Kanuni ya nne ya utajiri: EPUKA KUTAFUTA UTAJIRI WA HARAKA. Husitumie pesa yako kwenye michezo ya kamali na bahati na sibu badala yake wekeza kwenye biashara ambazo una ufahamu wa kutosha katika uendeshaji wake. Kumbuka kuwa fedha za haraka haziwezi kukufanya kuwa tajiri kwani hauna misingi halisi ya utengenezaji pesa. Jiwekee lengo la kuanza kidogo huku ukiwa na fikra pana ya kule unakotaka kufika.
✍🏾Kanuni ya tano ya utajiri: WEKEZA NDANI YA NAFSI YAKO. Kanuni hii inakutaka kuwekeza katika elimu inayolenga kukuza maarifa na ujuzi kwa ajili ya kukuza utajiri wako na kukuongezea ufahamu kwenye kila sekta ya maisha yako. Kanuni hii sio kupuuzia maana kama hauna ujuzi sahihi utajikuta unarudia makosa ya mara kwa mara ambayo yataendelea kukuzuia kukuza utajiri wako.
✍🏾Kanuni ya sita ya utajiri: LINDA UTAJIRI WAKO. Baada ya kufanikiwa kuwa tajiri hakikisha unakuwa na mfumo wa kulinda utajiri wako kutumia sheria na kanuni mbalimbali pamoja na kuwa na bima za rasilimali unazomiliki. Pia, unatakiwa kuepuka kuweka mayai yote kwenye kapu moja kwa kuanzisha vitega uchumi vya kutosha.
✍🏾Mwisho, nakumbusha kuwa kanuni hizi endapo utakuwa na nidhamu binafsi zitabadilisha maisha yako kuliko unavyodhania. Kwa maana hii, ni lazima utambue kuwa mafanikio unayotaka katika kila sekta ya maisha yako hasa uhuru wa kifedha ni lazima yaanzie kwenye nidhamu ya fedha ndogo unazopata kwa sasa. Tumia fedha hizo unazopata kwa sasa ili kufikia utajiri wa ndoto zako.
👐🏾Nakutakia kila la heri katika siku hii ya leo.
🗣🗣 Mwalimu Augustine Mathias
Mawasiliano: 763745451/0786881155
Barua pepe: fikrazakitajiri@gmail.com
Tovuti: fikrazakitajiri.blogspot.com