NENO LA LEO (FEBRUARI 15, 2020): ILINDE SANA PESA YAKO KIASI AMBACHO UPO TAYARI UONEKANE MTU WA TOFAUTI KATIKA JAMII

👉🏾Habari ya asubuhi rafiki na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni matumaini yangu kuwa siku ya jana iliisha salama bila kutoka kwenye misingi ya maisha yako na siku hii ya leo upo tayari kuendeleza jitihada zinazolenga kusukuma mbele gurudumu la maisha yako.

👉🏾Ni jambo la kheri kuona kuwa haupotezi dira kuu ya maisha yako kutokana na ukweli kwamba maisha yenye thamani ni lazima yawe na dira ambayo inamuongoza mhusika kila siku. Kwa kutumia dira hiyo mhusika kila iitwapo leo anawajibika kufanya kitu cha thamani ambacho kinamsogeza kutoka hatua moja kwenda hatua kadhaa mbele.

HUSIPOTEZE NAFASI YA KUPATA MAFUNDISHO HAYA KILA SIKU PAMOJA NA KUJUMUIKA NA FAMILIA YA FIKRA ZA KITAJIRI KWA  BONYEZA HAPA NA KUJIUNGA BURE NA KUNDI LA WHATSAPP. Jiunge sasa nafasi ni chache.

✍🏾Karibu katika neno la tafakari ya leo ambapo naendelea kukusisitiza juu ya umuhimu wa kuwa na nidhamu ya pesa bila kuzingatia maneno ya jamii inayokuzunguka. Kupitia neno hili nitakushirikisha sehemu moja ya matumizi ya fedha ambayo unatakiwa kuepukana nayo kwa kadri uwezavyo pale unapoona kuwa siyo lazima kushiriki. Sehemu hii ya matumizi ya pesa imekuwa ni uchochoro wa kutumia pesa zako kila mwaka wakati haikuwa sehemu ya bajeti zako.

✍🏾Katika karne hii ya 21 binadamu ambao tumebahatika kuwa hai tunaendelea kunufaika na ukuaji wa teknolojia. Ni katika karne hii tumeshuhudia mapinduzi makubwa ya Teknolojia ya mawasiliano ambayo imeendelea kutuweka pamoja kuliko kipindi chochote kile katika historia ya maendeleo ya mwanadamu. Ni kupitia teknolojia hii mwanadamu ameweza kuwa na makundi ya kijamii yenye watu wa rika tofauti na kutoka sehemu mbalimbali za Ulimwengu.

✍🏾Makundi haya ya kijamii yana faida na hasara zake, kupitia makala hii nitakushirikisha hasara moja ya makundi haya inayochochea matumizi mabaya ya pesa kwa mtu ambaye hajajitambua. Je ungependa kufahamu ni hasara ipi hiyo ambayo imepelekea uendelee kupoteza pesa zako hovyo?

✍🏾Hasara ya makundi haya au ukuaji wa teknolojia ya mawasiliano ni makundi ya kijamii kuwezeshwa kuombana michango kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kijamii kuliko ilivyokuwa hapo awali. Ni kutokana na teknolojia hii mtu anapohitaji kuoa au kuolewa anaweza kutumia njia hizi kupata michango kutoka kwa watu ambao anafahamiana nao:-
👉🏾Moja, ataangalia kwenye simu yake au kuomba kwa marafiki zake namba za simu za watu aliopotezana nao kwa kipindi kirefu ili awaombe michango ya shughuli yake;
👉🏾Mbili, anaweza kuanzisha kundi maalumu la Whatsapp kwa ajili ya kufanikisha michango ya harusi yake;
👉🏾Tatu, anaweza kutuma ombi lake kupitia kwenye makundi ya mitandao ya kijamii ambayo yeye ni mwanakundi. Kupitia njia hii wanakundi wanalazimishana kila mmoja ndani ya kundi kuchangia michango kwa ajili ya kuwezesha shughuli ya mwenzao.

✍🏾Hii ni hatari kwa maendeleo ya mtu ambaye amedhamiria kufikia uhuru wa kifedha katika maisha yake. Kama unahitaji kuepukana na matumizi yasiyo ya lazima kuanzia sasa anza taratibu kujenga tabia ya kutochangia michango ya shughuli zisizo za lazima. Kama sio mtu wa karibu na wewe husipoteze pesa zako. Ninaposema mtu wa karibu hapa namaanisha ndugu, mfanyakazi mwenzako ambaye mpo ofisi moja au rafiki wa karibu.

✍🏾Mbaya zaidi imefikia hatua ambayo wenye shughuli kupitia kamati za maandalizi wanakusanya michango kiasi ambacho panakuwepo na ziada kubwa ambayo wanakamati baada ya shughuli wanakaa sehemu na kujiburudisha wenyewe. Nyakati nyingine michango ya shughuli hizi imekuwa ikitumika kama sehemu ya kukusanya mitaji au fedha za kununulia vitu muhimu kwa wenye shughuli ambavyo si sehemu ya harusi/shughuli husika.

✍🏾Ndiyo, namaanisha acha kabisa kuchangia michango ya shughuli ambayo siyo ya lazima katika maisha yako. Nasema hivyo kwa kuwa wengi wetu huwa tunachangia kwa lengo la kutopoteza ukaribu na wale tunaowachangia. Hata hivyo, ukweli ni kwamba hata ukimpa mchango kama sio rafiki wa karibu au ndugu ataendelea kuwa mbali na wewe. Kama unataka kugundua ukweli wa hilo changia mchango wa harusi na baada ya muda mtafute yule uliyemchangia kumuomba akusaidie umekwama kupata kiasi cha fedha kwa ajili ya ada ya mwanao. Hakika michango ya muhimu kama hiyo ya kuwezesha maendeleo hakuna ambaye atakuwa upande wako. Sasa kwa nini uendelee kupoteza pesa zako bure?

✍🏾Hata hivyo, kupitia neno la tafakari ya leo simaanishi kuwa hautakiwi kutoa michango yote kwenye jamii. Moja ya kanuni za kuwa tajiri ni kujenga utaratibu wa kurudisha kwenye jamii. Unaweza kurudisha kwenye jamii kupitia kwenye michango ya rambi rambi, michango kwa makundi yasiyojiweza au kuchangia shughuli za maendeleo katika sehemu unayoishi.

✍🏾Mwisho, kupitia neno la tafakari ya leo jenga tabia ya kutochangia michango ya harusi au shughuli yoyote ambayo si ya lazima katika maisha yako. Kumbuka kuwa unavyoanzisha tabia hiyo mpya utapata upinzani wa maneno kutoka kwa watu wako wa karibu ambao watakupa kila aina ya jina. Mara utaitwa mtu ambaye hujichanganyi na wenzako au utaitwa mtu ambaye haupo karibu na jamii (anti-social) na mengine mengi. Maneno hayo yasikuvunje moyo kwa kuwa wewe ndo unafahamu misingi uliyojiwekea kwa ajili ya kufikia uhuru wa kifedha.

👐🏾Nakutakia kila la kheri kwenye siku hii ya leo. Kumbuka husikose kutoa mrejesho wa kile ambacho unajifunza kutokana na uwepo wako kwenye kundi hili.

🗣🗣 Mwalimu Augustine Mathias 
Mawasiliano: 0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua pepe: fikrazakitajiri@gmail.com
Tovuti: fikrazakitajiri.blogspot.com
Kujiunga Kundi la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI, bofya link hii:https://chat.whatsapp.com/JACBxr9kX7K0qt58cQTrrw
onclick='window.open(