Habari ya asubuhi
mwanafamilia ya mtandao wa JILIPE KWANZA. Ni matumaini yangu kuwa umeamka
salama na upo tayari kuendeleza bidii zinazolenga kuboresha maisha yako.
Rafiki naomba
husinichoke maana katika kipindi chote ambacho tutakuwa wote katika kundi hili
salama yangu itaendelea kukumbusha umuhimu wa kutopoteza hamasa na dira kwenye
kuwajibika kila siku kwa ajili ya kufikia maisha ya ndoto zako.
Karibu tena katika
tafakari ya leo ambayo inatukumbusha umuhimu wa kuishi maisha yetu kulingana na
wakati uliopo. Neno hili linalenga kutukumbusha kuwa historia au matukio yaliyopita
hayana nafasi ya kuamua maisha yetu ya sasa kama tunaishi maisha yetu kulingana
na wakati uliopo.
Watu wengi katika
jamii maisha yao yametawaliwa na matukio yaliyopita kiasi ambacho wanaishi
katika huzuni kila mara au wanashindwa kukamilisha mipango yao kwa kuwa
wanahisi mipango haitokamilika kwa kulinganisha na mipango ambayo pengine
haikukamilika katika siku za nyuma.
Bahati mbaya ni
kwamba kama unaishi katika matukio yaliyopita hauwezi kuwa na furaha katika
maisha yako ya sasa kwa kuwa maisha ya mwanadamu yanazungukwa na matukio mengi
ambayo si rafiki. Ukweli ni kwamba maisha ya mwanadamu yana historia ya
kuumizwa, kusalitiwa, kuibiwa, hofu, hasira, kunyapaliwa, kunyimwa haki za
msingi, na mengine mengi. Hivyo, kila mwanadamu ana historia ya matukio mengi yasiyofurahisha
kwenye maisha yake ya wakati uliopo.
Jambo jingine
ambalo unatakiwa kulifahamu kupitia neno la tafakari ya leo ni kutambua kuwa
historia haina nafasi ya kuamua mafanikio yako kwenye kila sekta ya maisha ya
maisha yako. Haijalishi kuwa kama ulizaliwa na kukulia katika familia masikini
na wewe na uwe masikini. Ukweli ni kwamba unatakiwa kutambua kuwa ilikuwa
lazima uzaliwe katika familia masikini ili ujifunze namna ya kukupambana
kuepuka umasikini. Kuzaliwa masikini sio dhambi hila kufa masikini ni dhambi
ambayo unatakiwa kuiepuka.
Jambo jingine
ambalo linashangaza katika jamii tunayoishi ni ile tabia ya watu wengi kuishi
kana kwamba hakuna kesho. Watu wengi hawana mipango ya baadae bali wanaishi
kama ndege waishivyo bila kuandaa maisha ya baadae kwenye kila sekta ya maisha
yao. Kumbuka kuwa mafanikio ya kifedha, kiafya na kimahusiano katika siku
zijazo yanaandaliwa kutoka kwenye maisha ya sasa.
Kubwa ambalo
unatakiwa kulifahamu kupitia neno la leo ni kwamba maisha yako ya kesho
yanaandaliwa katika maisha ya leo. Kile unachokifanya sasa kina nafasi kubwa ya
kuboresha au kubomoa maisha yako kwa siku zijazo. Hivyo, matendo yako ya sasa
unatakiwa kujiuliza yatakuathiri vipi katika siku zijazo kwenye kila sekta ya
maisha yako kuanzia kiuchumi (uhuru wa kifedha), kiafya, kimahusiano na kiroho.
Mwisho,
nakusisitiza kumbuka kuwa maisha yaliyopita yamepita na sasa una nafasi kubwa
ya kubadilisha maisha yako ili yaendane na wakati uliopo kwa ajili ya
maandalizi ya wakati ujao.
👐🏾Nakutakia
kila la kheri katika siku hii leo.
🗣🗣
Mwalimu Augustine Mathias