👉🏾Habari ya asubuhi rafiki na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni matumaini yangu kuwa umeamka salama na upo tayari kuendeleza bidii ya kuboresha maisha yako katika siku hii ya leo.
👉🏾Unavyoendelea na bidii za kila siku zinazolenga kuboresha maisha yako, kumbuka kuwa moja jumlisha moja haijawai kuwa sifuri. Hivyo, hakikisha kila siku unaweka ushindi mdogo mdogo ambao unachangia kwenye ukamilifu wa lengo kuu la maisha yako.
HUSIPOTEZE NAFASI YA KUPATA MAFUNDISHO HAYA KILA SIKU PAMOJA NA KUJUMUIKA NA FAMILIA YA FIKRA ZA KITAJIRI KWA BONYEZA HAPA NA KUJIUNGA BURE NA KUNDI LA WHATSAPP. Jiunge sasa nafasi ni chache.
✍🏾Karibu katika neno la tafakari ya leo ambalo linaendeleza kwenye neno la tafakari ya Jana hasa kwenye kanuni ya kwanza ya kuwa tajiri. Katika neno la jana tuliona kuwa kama una kiu kweli ya kuwa tajiri ni lazima ujilipe kwanza angalau kati ya asilimia 10 hadi 20 kwenye kila shilingi inayoingia mikononi mwako.
✍🏾Neno la tafakari ya leo litaangazia kwenye baadhi ya matumizi ambayo najua kuwa yanagusa asilimia kubwa ya wanakundi hili. Kama eneo ambalo nitagusia halikuhusu haimaanishi kuwa hauwezi kujilipa kwanza bali unachotakiwa ni kujifanyia tathimini kwenye kipato ukilinganisha na matumizi na hatimaye angalia katika matumizi hayo yapi ambayo si ya lazima. Tafakari juu ya matumizi yafuatayo:-
✍🏾 Moja, Tabia ya kununua kwa reja reja. Acha kununua kwa reja reja na badala yake utakuwa umeokoa kiasi kikubwa cha pesa ndani ya mwezi mmoja. Mfano, ukienda kununua kilo 20 za mchele mashineni kwa hapa kwetu ni Tshs. 30,000/= sawa na Tshs. 1,500/= wakati ukienda kununua kwa Mangi kwenye duka la reja reja kilo moja utanununua kwa Tshs. 1,800/=. Hapa utakuwa umeokoa shilingi 300 katika kila kilo unayonunua. Fanya hivyo kwenye mafuta ya kupikia, unga, vitunguu, nyanya n.k.
✍🏾 Mbili, Matumizi ya simu janja. Ni kawaida kwa wamiliki wa simu janja kuwasha data na kila wanapowasha data hupenda kubofya video mbalimbali kwenye Youtube, Facebook au Instangram. Kila unapobofya na kuangalia video katika mitandao hiyo kifurushi chako cha inteneti kinakimbia sio kawaida. Na asilimia kubwa ya watumiaji wa simu janja video wanazofungua hazi athari chanya katika maisha kwani video nyingi ni za udaku kuhusu Diamondi, Zari, Harmonize, Alikiba, Wema kwa kutaja tu baadhi kuwa wamefanya nini. Kama upo kwenye kundi hilo ndugu yangu badilika anza kufuatilia vitu muhimu pekee kwenye simu janja yako.
✍🏾 Tatu, Jiunge kifurushi cha Wiki au Mwezi kwa ajili ya mawasiliano na intaneti. Kanuni ni ile ile, kama ambavyo tumeona katika pointi ya kwanza kuhusu kununua kwa reja reja, ndivyo ilivyo hata kwenye manunuzi ya vocha kwa ajili ya mawasiliano na mtandao wa intaneti. Ili kupunguza bajeti ya mawasiliano unahitaji kuwa na namba ya mtandao wa simu ambao wana vifurushi vizuri za mawasiliano na intaneti na kuanza kujiunga kifurushi cha mwezi. Hata hivyo, unatakiwa kuwa na nidhamu ya kukitumia kifurushi hicho kama ambavyo tumeona katika pointi ya pili. Sio tu kwa sababu una kifurushi unaamua kumpigia kila mtu ambaye hukupanga kumpigia au unaamua kufungua video ambazo hazina tija kwenye ukamilifu wa lengo kuu la maisha yako. Nina hakika kama ulikuwa unajiunga na kifurushi cha siku kwa kujiunga na kifurushi cha mwezi utaweza kuokoa zaidi ya Tshs. 5,000/= kwenye matumizi yako ya vocha.
✍🏾 Nne, Punguza matumizi yasiyo ya lazima. Mfano, kuna watu ambao kila baada ya kula ni lazima anywe soda na baadae maji. Pamoja na kwamba kila mara tunaambiwa soda sio nzuri kwa afya lakini bado watu wameendelea kuwa na uteja(addicted) wa soda. Hapa unaweza kupunguza unywaji wa soda kila siku na kubakiwa na matumizi ya maji tu. Kama kila siku ulikuwa unakunywa soda moja yenye thamani ya Tshs. 500/= kwa kutokunywa soda kila siku utakuwa umeokoa Tshs. 15,000/= ambazo unaweza kujilipa kwanza. Pia, katika kundi hili nitakuwa sijatenda haki kama sitawagusa watumiaji wa bia na sigara. Hakika kama kila wiki unatumia kiwango cha chini cha Tshs. 6,000/ sawa na nia tatu sawa na Tshs. 24,000/ kwa mwezi. Kuanzia sasa amua kutumia bia moja kwa wiki na kiasi kinachobakia amua kujilipa kwanza. Husiogope kupoteza marafiki kwa kutoenda kwenye sehemu wanazouza bia kwani utalazimika hiyo bia yako uanze kunywa ukiwa nyumbani. Vivyo hivyo, kwa wavutaji sigara – uvutaji wa sigara ni hatari kwa afya yako, weka lengo la kuacha kabisa kuhatarisha afya yako na kiasi ulichokuwa unatumia kwenye uvutaji wa sigara kitenge kwa ajili ya kujilipa kwanza.
✍🏾 Tano, Acha kununua vitu ambavyo hukupanga kununua. Ni kawaida watu wengi kununua vitu kwa vile kashawishiwa na Machinga na pengine vitu hivyo havikuwa mpango wa manunuzi yake. Ukifika kwenye nyumba nyingi za watu wa aina hiyo utakuta zimejaa makolokolo ya kila aina ambayo hayana tija kwenye maisha ya kila siku ya mhusika. Watu hawa pia huwa wanadiliki kununua kwa mkopo ambapo kunakuwepo ongezeko la bei ukilinganisha na anayenunua keshi. Hapa napo jifanyie tathimini na uamue kununua vitu ambavyo kweli ulikusudia kununua katika mpango wako wa manunuzi ya kila mwezi.
✍🏾Mwisho, zipo sehemu nyingi ambazo ukikaa na kuruhusu fikra zako zifanye kazi utagundua kuwa unaweza kujilipa kwanza bila kuathirika kiafya na kujikuta unaboresha afya yako na uchumi pia. Kadri nitakavyopata muda kupitia tafakari hizi nitaendelea kukushirikisha sehemu hizo ili ifike sehemu nisikie kutoka kwako kuwa tayari umeanza kujilipa kwanza. Na hilo ndo kusudio langu kubwa kupitia kundi hili.
👐🏾Nakutakia kila la kheri katika siku hii ya leo.
🗣🗣 Mwalimu Augustine Mathias
Mawasiliano: 0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua pepe: fikrazakitajiri@gmail.com
Tovuti: fikrazakitajiri.blogspot.com