NENO LA SIKU_FEBRUARI 8/2022: Muhimu! Fahamu Sehemu Muhimu Ya Mwili Ambayo Unaisahau Kila Mara.
📌Unaendeleaje rafiki na mfuatiliaji wa masomo ya mtandao wa Fikra za Kitajiri! Ni mategemeo yangu kuwa umeianza siku vyema kwa kutimiza majukumu yako ya msingi huku ukizingatia maslahi mapana ya nafsi yako, jamii kwa ujumla wake na mazingira yanayokuzunguka.
📌Karibu tena katika makala ya leo upate chakula cha ubongo ili akili yako ipate kuendelea kuwa hai. Katika makala ya leo nitakushirikisha moja ya kiungo muhimu katika mwili wako ambacho kinahitaji umakini wako sawa unavyoweka malengo na mikakati muhimu kwa ajili ya sehemu nyingine za mwili na kila sekta ya maisha yako.
📌Mwili wa mwanadamu unaundwa na seli mbalimbali ambazo kwa pamoja zinaunda viungo vya mwili kama vile mifupa, nyama, damu na ubongo. Katika mtazamo wa kemia, mwili wako unaundwa na maji na muunganiko wa elementi za kaboni ambazo hujumuisha mafuta, protini, wanga na asidi. Hata hivyo, pamoja na kwamba miili ya wanadamu inaundwa vitu vya aina moja, kinachopelekea wanadamu wawe na maumbo yenye mwonekano tofauti ni taarifa za kijeni (genetic information), mazingira ya nje na tabia ambazo zinaweza kubadilisha mwonekano wa mwili hasa katika kufanya kazi vizuri kwa ajili ya maendeleo ya mhusika.
📌Katika mwonekano wa nje, maumbile ya mwanadamu yanajumuisha sehemu tano za msingi ambazo ni kichwa, shingo, kifua, mikono na miguu. Makala hii itajikita kwenye kuelezea jinsi ambavyo sehemu ya ndani ya kichwa cha mwanadamu ambayo imekuwa si kipaumbele kwa wengi pindi wanapojiwekea malengo muhimu ya maisha. Kwa muonekano, sehemu ya kichwa cha mwanadamu ni ndogo ikilinganishwa na sehemu nyingine za mwili wa mwanadamu japo sehemu hii ndiyo inabeba kiungo muhimu katika suala zima la kuratibu sehemu zote za mwili. Sehemu ya juu ya kichwa hufunika seli laini ambazo muunganiko wake unaunda kiungo cha mwanadamu kijulikanacho kama ubongo.
📌Ubongo wa mwanadamu ni kiini tete au laini chenye mfumo wa nevu za mwanadamu ambapo kwa kuungana na uti wa mgongo hufanikisha kazi zote za mfumo wa fahamu na utambuzi. Kiungo hiki humwezesha mwanadamu kukamilisha kazi zote za mwili kama vile mijongeo, vitendo vya mwili, kuongea (lugha), kuhisi na kuitikia vichocheo sambamba na kutunza kumbukumbu. Kwa kifupi, ubongo ni chanzo na hazina ya akili ya mwanadamu.
📌Pamoja na umuhimu wa ubongo kwa mwanadamu, kiungo hiki kinasahaurika kwa asilimia kubwa ya watu pindi wanapojiwekea malengo muhimu ya maisha. Sawa na ilivyo kwa mwili, ubongo au akili ya mwanadamu inahitaji kutunzwa na kuendelezwa. Mara nyingi watu wanazama kwenye kuweka malengo ya kufanikisha au kudumisha upatikanaji wa chakula, afya bora, kazi au uchumi lakini wanasahau jinsi gani wanatakiwa kulisha ubongo wao.
📌Kama ilivyo muhimu katika kuamua ni nini unapaswa kula kwa ajili ya kuboresha afya ya mwili wako, ni muhimu pia kuilisha akili yako na vitu muhimu ambavyo vinaiwezesha kukua na kuendelea. Kitu cha kwanza ambacho lazima utambue ni kwamba akili yako ndiyo msingi na injini ya kuwezesha maendeleo katika kila sekta ya maisha yako. Hivyo, kuipenda akilli yako ni kujipenda mwenyewe, wengine wanaokuzunguka na mazingira unayoishi. Tunaweza kutafsiri kwa maneno mengine kuwa, jinsi unavyoipenda akili yako angalau kidogo, ndivyo upendo unavyozidi kuenea kwa wale walio karibu nawe.
📌Upendo huu wa ndani utaendelea kukua ikiwa utaendelea kuijali akili yako kwa kuhakikisha inachuja na kufyonza vitu vya msingi kati ya mengi yanayokuzunguka. Hii ni sawa na unavyochagua vyakula sahihi kwa ajili ya mwili wako badala ya kula pasipo kuzingatia mfumo maalumu wa chakula. Unavyolisha akili yako na maarifa sahihi ndivyo akili inakua na kujiendeleza kwa kukuwezesha kupata ufunuo wa uwezo wako halisi katika kila sekta ya maisha. Hata hivyo, kadri ujinga unavyoijaza akili yako, ndivyo inavyozidi kudhoofika. Mfano, ikiwa akili unaijaza na vitu vya giza, hofu, chuki, hasira, choyo, wivu, filamu zisizo na maana, vibweka au vibonzo vya mtandaoni na mambo mengine ya hovyo; ni wazi kuwa akili yako haitakuwa na ubunifu au mawazo chanya yenye manufaa kwako, jamii na mazingira kwa ujumla.
📌Kama huna malengo ya kuendeleza akili yako ni dhahiri kuwa unainyima akili yako kitu cha muhimu sana. Ukweli ni kwamba akili yenye maarifa sahihi ni hazina yenye faida maana unaweza kupoteza kazi yako, unaweza kupoteza watu na vitu vyote, lakini huwezi kupoteza maarifa na ujuzi uliojifunza na kuhifadhiwa akilini mwako. Akili ni sehemu nyingine ya maisha yako ambayo kuanzia sasa unatakiwa kutumia pesa, nguvu na muda kwa ajili ya uwekezaji unaolenga kuikuza na kuiendeleza.
📌Je! Mwaka huu umelenga kusoma vitabu vingapi? Umepanga kusikiliza programu ngapi au semina ngapi zinazolenga kujifunza maarifa mapya? Kitu kimoja ambacho unatakiwa kufahamu ni kwamba "Maarifa ni kama chakula cha ubongo, huwezi kula mara moja na kusema yatosha. Unatakiwa kuulisha ubongo wako na maarifa sahihi mara kwa mara." Fikiria kama kila siku ungekuwa na mpango wa kujifunza jambo moja jipya, katika mwaka mmoja ungejifunza mangapi? James Allen katika kitabu chake cha "As A Man Thinketh" anasema “Mwanadamu ni, na vile anavyofikiri, ndivyo alivyo”. Mtazamo wa maneno haya kuhusu mwanadamu jinsi alivyo na jinsi navyofikiri unatupeleka katika kufikiria umuhimu wa chakula cha akili yenye uwanda mpana husio na ukomo wa kujifunza.
📌Maisha si lolote zaidi ya kuishi, kuchunguza, kupata uzoefu mpya, kujifunza na kushirikisha wengine kama ushauri au masomo kwa walio tayari kupokea. Kushirikisha maarifa muhimu ni moja ya zawadi kuu ambayo mtu anaweza kutoa kwa wengine. Hamu yangu kubwa ni kuishi maisha ya kujifunza kila mara na kuhakikisha nashirikisha wanafunzi ambao kwa hiari yao wapo tayari kujifunza. Hapa ninamaanisha kuwa sio kila mtu anataka kujifunza au kuongeza maarifa. Unaweza kuchagua kupoteza muda wako kutazama televisheni, kufuatilia mambo ya hovyo kwenye mitandao ya kijamii, au kujumuika na marafiki zako, au kutumia muda huo kwa ajili ya kujifunza maarifa sahihi. Unaweza kusoma vitabu kuhusiana na fani yako, biashara, kiroho au vitabu vinavyosaidia katika ukuaji wa jumla wa nafsi yako.
📌Sina lengo la kukuchosha! Hivyo, nihitimishe kwa kusema kuwa katika mwendelezo wa kukushirikisha maarifa sahihi nimekuandalia kitabu cha MAISHA YENYE THAMANI ambacho ni zawadi kwa yeyote mwenye hitaji la kuacha alama ya maisha. Zawadi hii ni kwa ajili ya kuhakikisha unaamsha akili yako ili isije kudhoofu na mwisho wake ikafa. Mtu mwenye akili mfu ni miongoni mwa watu ambao tunasema wanatembea lakini wamekufa! Uzoefu unaoesha watu waliofanikiwa kwenye kila sekta ya maisha ni wale ambao wamewekeza vya kutosha kwa ajili ya kujifunza kuhusu sekta husika. Anza sasa kuilisha akili yako na maarifa sahihi ili upate kutambua uwezo wako halisi. Ikiwa akili inakua kwa kile inachokula, Je mwezi uliopita umeilisha akili yako ni nini? Je! Mwaka huu umepanga kusoma vitabu vingapi na hadi sasa umeshaanza kusoma hata kimoja?
PATA NAKALA YA KITABU CHA MAISHA YENYE THAMANI KUJIFUNZA ZAIDI KUHUSU MISINGI YA MAISHA BORA HAPA DUNIANI
Kitabu hiki bado kinatolewa kwa bei ya OFA kwa kuchangia cha Tshs. 10,000/= tu! Utatumiwa kwa barua pepe au WhatsApp Nakala tete (soft copy) yenye fomati ya Pdf.
Kupata kitabu hiki, lipia kupitia Mpesa kwenye namba +255 (0) 763 745 451 au Airtel Money namba +255 (0) 786 881 155 au Halopesa namba +255 (0) 629 078 410 zote majina ni AUGUSTINE MATHIAS MUGENYI.