NENO LA SIKU_FEBRUARI 11/2022: RAFIKI! Hawa ndiyo marafiki unaotakiwa kujiweka karibu yao.
📌Habari ndugu na mwanafamilia ya mtandao wa Fikra za Kitajiri. Hongera kwa siku hii ya leo! Hongera kwa kuendelea kutimiza majukumu ya siku kama ulivyoainisha kwenye ratiba yako ya siku. Hongera pia kwa kutumia dakika chache za mapumziko kwa ajili ya kujifunza kupitia neno la siku ya leo.
📌Karibu upate kujifunza kupitia makala ya leo ambapo nitakufunulia jinsi ambavyo umeendelea kujirudisha nyuma kupitia aina ya marafiki wanaokuzunguka. Binadamu ni kiumbe mwenye kuishi kwenye makundi ya kijamii yanayolenga kurahisisha upatikanaji wa mahitaji ya msingi. Kupitia makundi ya kijamii wanadamu uanzisha mahusiano ya urafiki yanayolenga kusaidiana katika maisha ya kila siku.
📌Lengo kubwa la urafiki ni wahusika kushiriki katika kutendeana wema na kuchukuliana kulingana na nyakati ambazo kila mmoja anapitia. Tafiti za kisayansi zinapendekeza kuwa watu ambao wana urafiki wa dhati wana nafasi ndogo ya kupatwa na msongo wa mawazo, wana nafasi kubwa ya kuepuka magonjwa ya shinikizo la moyo na wana uwezekano mkubwa wa kuishi muda mrefu zaidi kuliko wale wasio na marafiki. Hivyo, urafiki wa dhati ni sehemu ya kufanikisha furaha na mahitaji ya msingi ya maisha kwa wahusika.
📌Hata hivyo, ukweli ni kwamba sio marafiki wote huchangia katika lengo halisi la urafiki. Marafiki wengi hudanganya, wana wivu, choyo, hila na hung’ata pande mbili kwa maana akiwa na wewe ni rafiki na unapompa kisogo anaanza kukusengenya. Wengine huchukulia urafiki kama sehemu ya kukidhi maslahi yao kuliko kile wanachotoa upande mwingine. Wengine watakupa ushauri unaolenga kukupoteza ili kesho wafurahi kuona umepoteza mwelekeo.
📌Mara nyingi tunapotezwa na marafiki kwa kuwa hatuna misingi na kanuni binafsi zinazoongoza maisha yetu. Ukweli ni kwamba rafiki anatakiwa awe miongoni mwa watu wanaoendana na kanuni au misingi binafsi ya maisha yako. Ikiwa hauna misingi au kanuni hizo ni dhahiri kuwa kila rafiki utaona anafaa kuwa karibu yako. Mwisho wake ni kujikuta unakaribisha marafiki ambao hawana mchango chanya katika maisha yako.
📌Unaweza kupima mchango wa marafiki kwenye ufanisi wa malengo yako kupitia mijadala na matendo yenu ya kila mara. Kama maongezi yenu ni kuongelea mafanikio au maovu ya watu wengine ni dhahiri unapotea! Ikiwa kila mara mnazungumzia na kushiriki kwenye matendo ya uhasama, uovu, maadili mabaya katika jamii au kusaidiana katika kukamilisha mipango hasi, gutuka kuwa hapo hauna marafiki bali una maadui wa maisha yako. Husikubali kuzungukwa na marafiki wenye akili nyepesi ambao mazungumzo yao hujikita katika kujadili maisha ya wengine au matukio katika jamii.
📌Kuanzia sasa hakikisha unazungukwa na marafiki ambao mna mawazo, fikra na matendo yanayoendana na kanuni au misingi binafsi ya maisha yako. Zungukwa na marafiki ambao kiini cha majadiliano yenu ni kuzungumzia fursa mpya au mbinu za kutatua changamoto ambazo kila mmoja anapitia katika majukumu yake au mahusiano. Zungukwa na marafiki ambao kila mara mazungumzo yenu yanalenga kwenye kuinuana na kukua zaidi ya pale mlipo. Zungukwa na marafiki wenye mtazamo chanya katika kila hali mnayopitia. Zungukwa na marafiki ambao malalamiko siyo sehemu ya maisha yao.
📌Nihitimishe kuwa kusema; mara kadhaa tumeruhusu urafiki bila kuchunguza hatima ya urafiki huo kwenye ukamilisho wa kanuni na misingi binafsi ya maisha yetu. Na pengine umekuwa ukikaribisha kila rafiki kwa kuwa hauna kanuni na misingi binafsi ya maisha yako. Athari ya urafiki wa aina hii ni kuendelea kujipoteza kimaisha maana urafiki unakuwa chanzo cha kukurudisha nyuma kimtazamo, kitabia na kimafanikio. Wapo marafiki ambao wanakuja kwako ili kukurudisha nyuma ili uendelee kuwa sawa na wao. Wapo marafiki ambao wanakuja kwa lengo la kukutumia zaidi kuliko wewe unavyonufaika nao. Tumia makala hii kuchunguza aina ya urafiki ulionao kama unachangia kusogea mbele au kurudi nyuma kimaendeleo na fanya maamuzi sahihi.
KIJIFUNZA ZAIDI KUHUSU MISINGI YA MAISHA, JIPATIE NAKALA YA KITABU CHA MAISHA YENYE THAMANI
Kitabu hiki bado kinatolewa kwa bei ya OFA kwa kuchangia cha Tshs. 10,000/= tu! Utatumiwa kwa barua pepe au WhatsApp Nakala tete (soft copy) yenye fomati ya Pdf.
Kupata kitabu hiki, lipia kupitia Mpesa kwenye namba +255 (0) 763 745 451 au Airtel Money namba +255 (0) 786 881 155 au Halopesa namba +255 (0) 629 078 410 zote majina ni AUGUSTINE MATHIAS MUGENYI.
onclick='window.open(