Je! Unaishujudia Pesa Kiasi cha Kushindwa Kuishi Maisha Unayotamani

NENO LA SIKU_FEBRUARI 5/2022: Je! Unaishujudia Pesa Kiasi cha Kushindwa Kuishi Maisha Unayotamani?


Hongera rafiki yangu kwa kuendelea kufuatilia masomo ya mtandao wa Fikra za Kitajiri.

Ni siku nyingine ya kipekee ambayo tumezawadiwa kuongeza idadi ya siku za uhai wetu hapa duniani. Ni siku ambayo huna budi kuitumia kwa ajili ya kutafuta majibu ya maswali muhimu yanayokusumbua katika kila sekta ya maisha yako. Itumie siku hii kuruhusu akili yako ifanye kazi katika kila changamoto inayokusumbua.

Karibu katika makala ya leo ambapo nitaangazia jinsi ambavyo watu wengi wamepoteza uasilia wa misingi ya maisha kwa kuishujudia pesa. Ukweli ni kwamba maisha ya mwanadamu wa karne hii yana uhusiano mkubwa na pesa. Pesa imekuwa ni nyenzo muhimu kwa mwanadamu kujiendeleza kiuchumi, kijamii, kiroho, kiafya na kifamilia.

Kutoka na ukweli huu, haishangazi kuona kila kukicha watu wanazama kwenye majukumu ambayo kwa asilimia kubwa yanalenga kufanikisha upatikanaji wa pesa. Pesa inatafutwa kwa njia halali na hata haramu ili mradi tu mtu afanikishe kukidhi mahitaji yake.

Hata hivyo, ukweli ni kwamba iwe unatafuta pesa kwa njia halali au haramu, kila mara kuna sauti ambayo inalia ndani mwako. Hii ni sauti ambayo inalia kwa kila binadamu mwenye akili timamu. Sauti ambayo kila mara inakuhoji kuhusu hatima ya kile unachofanya dhidi ya matamanio halisi ya maisha yako. Ni sauti ambayo inahoji juu ya uzoefu wa maisha yako dhidi ya mahitaji halisi kwa maisha yanayokungojea. 

Ili kuepuka majuto katika maisha yako ya baadae huna budi kuisikiliza sauti hiyo. Ipo mifano ya watu wengi ambao walidhani pesa ni kila kitu lakini mwishoni waligundua kuwa walikuwa wanapotea njia. Pesa inaweza kununua kila kitu na kukuwezesha kufika kila kona ya dunia hii lakini haiwezi kununua uhai wako pale muda wako unapofikia mwisho. 

Mfano, Steve Jobs ambaye alifanikiwa kuwa tajiri akiwa kijana mdogo tu, ilipofika wakati wa kupambana dhidi ya mauti akiwa na umri wa miaka 56 anasema: "Nilifikia kilele cha mafanikio katika ulimwengu wa biashara. Kwa macho ya wengine maisha yangu ni kielelezo cha mafanikio. Hata hivyo, nikiwa nje ya kazi, sina furaha hata kidogo. Mwishowe, utajiri ni ukweli tu wa maisha ambao nimeuzoea. Kwa wakati huu, nikiwa nimelala kwenye kitanda cha wagonjwa na kukumbuka maisha yangu yote, nagundua kuwa umaarufu wote na mali ambayo nilijivunia sana, imebadilika na kuwa haina maana mbele ya kifo kinachokuja. Unaweza kumwajiri mtu akuendeshee gari, akakutengenezea pesa lakini huwezi kuwa na mtu wa kubeba ugonjwa kwa ajili yako. Vitu vilivyopotea vinaweza kupatikana. Lakini kuna jambo moja ambalo haliwezi kupatikana pale linapopotea - "Maisha".

Tumepewa zawadi ya maisha kupitia uhai tulionao japo kipindi cha maisha haya kinatawaliwa na matamanio mengi ya kufanikisha. Hata hivyo, pesa ni msingi mzuri wa kufanikisha baadhi ya sekta za maisha lakini mbinu zinazotumika kukitafuta zinaweza kusababisha kuangamiza maisha yetu wenyewe. Tunataka kuishi! Kufyonza kila sekunde tunayomiliki katika ulimwengu huu ili kufikia uwezo wetu wa kutosheleza matamanio yetu, na kupata uzoefu wa kila kitu tunachotaka. 

Ni kweli tunataka kuishi maisha yenye kujitosheleza! Lakini bahati mbaya ni kwamba kila hatua tunayopiga inafungua mlango wa kutaka zaidi, tunataka "zaidi", kumiliki zaidi, wingi wa vitu, starehe zaidi, umaarufu zaidi na zaidi na zaidi. 

Ikiwa tunahitaji kuishi kwa ukamilifu! Hatuna budi kufunga breki na kujihoji juu ya uhalali wa njia tunazotumia kutafuta pesa. Maisha yanahitaji utajiri kwenye kila sekta ya maisha zaidi ya utajiri wa pesa. Tunahitaji utajiri wa kiroho, mahusiano ndani ya familia, kijamii na utajiri wa kuokoa nafsi za watu wanaotaabika kwa ajili ya kukosa gahrama za matibabu, chakula na maradhi. Tutumie utajiri wa pesa kuongeza utajiri kwenye kila sekta ya maisha yetu, nje ya hapo ipo siku tutajutia maisha haya.

Nihitimishe kwa kumbusha kuwa, mwanadamu kwa asili haridhiki na kila hatua ya mafanikio anayopata. Wengi wetu jamii imetufanya tuamini kuwa maisha bora yapo kwenye kupata "zaidi". Tunaamini kuwa siku ambayo tutaondoa vikwazo yetu vyote vya kipesa, malengo, au uzoefu ndipo tutakuwa na furaha zaidi ya ilivyo sasa. Hata hivyo, kadri unavyopiga hatua ndivyo unajikuta ukitaka zaidi ili kusogea hatua ya juu. Hali hii hupelekea kutengeneza ombwe kubwa kwenye mafanikio ya sekta nyingine za maisha yetu. Kadiri unavyotafuta pesa ikiwa hauna misingi ya kuishi maisha ya ukamilifu ndivyo utazidi kuwa masikini kwenye sekta nyingine za maisha yako. Cha kusikitisha zaidi, zipo nyakati utaanza kuhisi upweke ndani ya nafsi yako. Kumbe! Tafuta pesa huku ukiendelea kukuza utajiri katika kila sekta ya maisha yako.

PATA NAKALA YA KITABU CHA MAISHA YENYE THAMANI KUJIFUNZA ZAIDI KUHUSU MISINGI YA MAISHA BORA HAPA DUNIANI


Kitabu hiki bado kinatolewa kwa bei ya OFA kwa kuchangia cha Tshs. 10,000/= tu! Utatumiwa kwa barua pepe au WhatsApp Nakala tete (soft copy) yenye fomati ya Pdf.

Kupata kitabu hiki, lipia kupitia Mpesa kwenye namba +255 (0) 763 745 451 au Airtel Money namba +255 (0) 786 881 155 au Halopesa namba +255 (0) 629 078 410 zote majina ni AUGUSTINE MATHIAS MUGENYI.

onclick='window.open(