Je! Umeoa au Kuolewa? Zingatia Ushauri Huu Kudumisha Ndoa Yako.

NENO LA SIKU_FEBRUARI 9/2022: Je! Umeoa au Kuolewa? Zingatia Ushauri Huu Kudumisha Ndoa Yako.
🖊️Habari rafiki yangu ambaye umeendelea kufuatilia masomo ya mtandao wa Fikra za Kitajiri. Hongera kwa kuendelea kutenga muda wako kwa ajili ya kujifunza maarifa mbalimbali kupitia mtandao wa Fikra za Kitajiri.

🖊️Karibu tena katika makala ya leo ambapo nitaangazia jinsi Wanandoa wanavyoweza kudumisha mahusiano ndani ya familia na kudumu katika upendo. Kwa mujibu wa mafundisho ya Kanisa Katoliki, Ndoa ni sakramenti ambayo inahusisha watu wawili wa jinsia ya kiume na kike waliodhamiria na kunuia kuishi pamoja kama mke na mme. Wawili hawa wapo tayari kuacha familia za wazazi wao na kuanzisha familia mpya.

🖊️ Kutokana na Sakramenti ya Ndoa, ulimwengu unaendelea kunufaika na matunda ya ndoa ambayo ni uendelevu wa kizazi baada ya kizazi. Hivyo, ndoa ni chanzo cha upatikanaji wa watoto na wanandoa (wazazi) wana wajibu wa wakuwalea na kuwakuza katika maadili mema. Ndoa imara ni msingi wa maadili mema na huwezesha hupatikanaji wa kizazi chenye ubunifu wa kila aina katika jamii. Ili yote haya yafanikiwe, wanandoa hawana budi kuzingatia ushauri ufutao:-

🖊️Moja, Ndoa ni sehemu ya kudumisha furaha halisi kwa wanandoa. Ndoa siyo sehemu ya kila mmoja kupandisha msongo wa mawazo kwa mwenzake, bali ni sehemu ya kukuza furaha kupitia upendo kwa wanandoa. Na hapa ndipo wanandoa wanatakiwa kutambua kuwa furaha halisi katika maisha ya ndoa haitokani na pesa, akili nyingi au umiliki wa rasilimali za aina yoyote ile. Ndoa nyingi zimevunjika au kuishi bila mwelekeo kutokana na kuendekeza fikra hasi. Mara nyingi wanandoa wengi kwa fikra hizo wanaishi maisha yasiyo na furaha kwa kutegemea kuwa furaha ni zao la umiliki wa fedha nyingi au vitu vya kifahari. Kumbe, furaha halisi katika ndoa si pesa au vitu vya kifahari bali heshima, unyenyekevu, faraja, uvumilivu, maelewano, kusikilizana na msamaha katika maisha ya kila siku kwa wanandoa. KWA undani, yote haya yanajenga hisia hai kwa wenza katika ndoa.

🖊️Mbili, Ndoa ni sehemu ya kuongeza siku za kuishi. Tafiti zinaonyesha kuwa wanandoa ambao wameishi pamoja kwa muda mwingi tena kwao furaha,  wanaishi kati ya miaka minne hadi nane ikilinganishwa na wale ambao wametalikiana au kudumu katika migogoro. Ukweli huu wa kitafiti unatupa angalizo juu ya kutotumia ndoa kama chanzo cha presha kwa wanandoa. Ni dhahiri kuwa ndoa zenye msongo wa mawazo na kila aina ya misukosuko ni chanzo cha miili ya wanandoa kushambuliwa na magonjwa mbalimbali kutokana na upungufu wa kinga za mwili.

🖊️Tatu, Migogoro ni sehemu ya mapito kwa wanandoa. Ndoa inakutanisha mme na mke ambao wamefahamiana ukubwani, kwa maana, kila mmoja amekulia katika misingi tofauti ya makuzi na malezi. Tofauti hizo ni lazima zipelekee nyakati za kutoeelewana ndani ya familia. Hata hivyo, ndoa ni sehemu ya kukosoana na kurekebishana kwa upendo kati ya wanandoa. Mawasiliano kati ya wenza ni nyenzo muhimu ya kutatua migogoro na kurejesha furaha kwa wanandoa. Hiki ni chombo cha kudumisha upendo na penzi la dhati kati ya mke na mme. Wanandoa ambao hawana mawasiliano ya mara kwa mara husababisha migogoro iendelee kati yao kwa muda mrefu. Kupitia mawasiliano wawili katika ndoa wanasikilizana, wanarekebishana na kurejesha uhai wa penzi ndani ya ndoa. 

🖊️Nne, Mme na Mke wanatakiwa kujenga urafiki wa kina na wenye upekee. Ni sahihi kuwa mme au mke wako ni rafiki pekee ambaye mnakaa, mnakula na kulala pamoja kiasi kwamba hakuna rafiki mwingine ambaye mnashirikiana kiasi hiko. Urafiki kati ya wanandoa husaidia kukuza ndoa imara na yenye furaha. Ni muhimu wenza katika ndoa kuishi maisha ya urafiki na katika urafiki huo wenza hawa wanatakiwa kutambua mapungufu ya kila mmoja. Pia, kila mmoja anatakiwa kufahamu vipaumbele vya mwenza wake na kwa pamoja kila mmoja atumie jitihada za kumsaidia mwenza katika ukamilisho wa vipaumbele vyao. Hivyo, ni muhimu wanandoa wakaishi maisha ya urafiki yenye kila aina ya vichocheo vya mapenzi. 

🖊️Tano, Mfahamu Mme au Mke wako kuliko mtu yeyote katika dunia hii. Hili ni sharti la lazima kwako wewe mwanandoa. Unatakiwa kumfahamu mwenza wako kitabia, mapendeleo, uimara na udhaifu wake. Ikiwa unahitaji kudumisha ndoa yako huna budi kumfahamu mwenza wako nje hadi ndani. Fahamu mwenza wako anakabiliwa na tatizo lipi, anapitia kwenye hofu zipi za maisha, fahamu matukio muhimu katika historia yake, chimba zaidi kuhusu changamoto anazopitia iwe za kiafya, kipato, kiroho au kikazi. Baada ya kumfahamu mwenza wako ndani na nje unatakiwa kutumia vitu hivyo kuamsha vichocheo vya mapenzi kwa njia yoyote ile ikiwa ni pamoja na kutenga muda wa utani na kufurahi. Yote hayo yanatakiwa yafanyike kama njia ya kumpunguzia msongo wa mambo ambayo mwenza wako anapitia. Pia, una wajibu wa kumrekebisha au kumuelimisha kwa upendo ikiwa njia anayoelekea siyo salama kwenu na uendelevu wa ndoa yenu.   

🖊️Sita, Watoto ni Baraka na hitaji la kila mwanandoa. Tunda la kwanza la ndoa ni watoto ambao ni zawadi kutoka kwa Muumba. Hata hivyo, wanandoa wengi huwa wanafifisha upendo mara baada ya kujaliwa watoto. Kabla ya kupata mtoto na kipindi chote cha mimba, wanandoa wengi hudumu katika furaha na penzi la dhati. Hata hivyo, wanandoa wengi baada ya kupata watoto huwa wanafifisha upendo kutokana na upendo kuhamia kwa watoto. Mtego huu husababisha ndoa nyingi kufarakana na pengine kuyumba moja kwa moja. Kwa nini hali hii hutokea? Ukweli ni kwamba mara baada ya kupata mtoto wanandoa wanapata majukumu mapya ambayo mara nyingi yanapelekea mapenzi ya wawili hawa yaamie kwa mtoto. Na asilimia kubwa hali hii huanzia kwa akina mama kutokana kuongozeka kwa majukumu mapya ya uangalizi wa mtoto. Ikiwa baba hajaelewa mabadiliko hayo na kuyabeba katika mtazamo chanya ni dhahiri kuwa penzi la wawili hao linaanza kuingiwa na sumu. Pia, mama naye anatakiwa kutambua kuwa watoto huja na majukumu ya ziada lakini hayaondoi nafasi yake kama mama katika kukuza penzi kwa mwenza wake. Hiki ni kipindi cha kuendelea kudumu katika misingi ya awali japo wengi hujikuta wamebadilisha kila kitu kuanzia mpangilio wa nyumba, chumbani hadi mfumo wa kujali miili yao. Hiyo ni sumu ambayo haipaswi kuonjwa kwa wanandoa.

🖊️Saba, Rutubisha na kudumisha hisia hai. Hisia hai dhidi ya mwenza wako ndiyo injini ya kukuza pendo kwa wanandoa. Hisia huzalisha muunganiko kati ya wanandoa kiasi kwamba hata nyakati ambazo hawako karibu wanakuwa pamoja kihisia na kiroho. Hisia hai hudumisha msisimko wa mwili kwa mwanandoa dhidi ya mwenza wake na msisimko huo huzalisha matamanio ndani ya wawili kimwili. Ndoa si lolote zaidi ya msisimko huo, kwa maana, hicho ni kiunganisho cha miili miwili tofauti kuwa mwili mmoja. Wanandoa wenye hisia hai uendelea kuungana kimwili kupitia tendo la ndoa ambalo ndilo asili na kusudi la wawili kuishi pamoja. Hivyo, mara zote hisia zenu na ziwe hai. Mnaweza kukuza hisia zenu kupitia rejea ya kumbukizi ya enzi za uchanga wa penzi au nyakati mnaanzisha mahusiano maana hicho ni kipindi ambacho hisia huwa kwenye kilele. Hata hivyo ni muhimu kila mwanandoa kuhakikisha kila siku anatafuta njia za kumchangamsha mwenza wake kihisia ili muda wote wawili hawa wawe kwenye muunganiko wa kimwili wenye chimbuko la kutoka rohoni.   

🖊️Nane, Nyenyekeaneni nyinyi kwa nyinyi maana katika unyenyekevu mna amani na upendo. Ndoa nyingi zimevunjika au kuanguka kwa kukosa unyenyekevu kati ya wanandoa, yaani, ubabe hutawala kwa kila mmoja. Ikiwa dhumuni la maisha ya ndoa ni wawili (mme na mke) kusaidiana iweje kila mmoja awe mbabe kwa mwenzake? Mme au Mke kuna nyakati ambazo unatakiwa kujishusha kwa mwenza wako kama suluhisho la kutatua changamoto iliyopo mbele yenu. Daima ubabe na ugomvi wa kila mara havijengi familia badala yake ni kubomoa. Pia, ndoa imara ni lazima iepuke malumbano ya mara kwa mara kwa kuwa yote hayo hufukuza upendo na amani ndani ya familia.

🖊️Nihitimishe kwa kukumbusha kuwa, ndoa imara ni faida kwa jamii, taifa la hapa duniani na pia taifa la maisha baada ya maisha haya kulingana na misingi ya imani yako. Kama umejitoa kuishi maisha yako kupitia njia ya ndoa, tambua kuwa hujakosea njia. Hata hivyo, njia hii si tambarare bali ina milima na mabonde ambayo kupitia ushirikiano wa wawili mtaendelea kuyasawazisha na kuifurahia ndoa yenu. Nawatakia kila lenye kheri ili mpate kudumu katika penzi la dhati.
  
PATA NAKALA YA KITABU CHA MAISHA YENYE THAMANI KUJIFUNZA ZAIDI KUHUSU MISINGI YA MAISHA BORA HAPA DUNIANI
Kitabu hiki bado kinatolewa kwa bei ya OFA kwa kuchangia cha Tshs. 10,000/= tu! Utatumiwa kwa barua pepe au WhatsApp Nakala tete (soft copy) yenye fomati ya Pdf.

Kupata kitabu hiki, lipia kupitia Mpesa kwenye namba +255 (0) 763 745 451 au Airtel Money namba +255 (0) 786 881 155 au Halopesa namba +255 (0) 629 078 410 zote majina ni AUGUSTINE MATHIAS MUGENYI.

onclick='window.open(