NENO LA SIKU_FEBRUARI 14/2022: FUNGUKA! Rafiki Unafahamu Nini Kuhusu Siku Ya Wapendanao?
📌Rafiki na mfuatiliaji wa masomo ya mtandao wa Fikra za Kitajiri, hongera kwa kupata muda wa kuendelea kutafakari na kutimiza malengo muhimu ya maisha yako. Ni siku nyingine ambayo kwa utaratibu uliozoeleka, jamii inasherekea SIKU YA WAPENDANAO, yaani Valentine Day. Naamini umekuwa miongoni mwa watu wanaosherekea kwa njia moja au nyingine maana ikiwa tunaishi kwenye jamii wakati mwingine hatuna budi kufanya vitu kwa ajili ya kuwa sehemu ya wanajamii.
📌Katika makala ya leo imenipendaza nikushirikishe machache kuhusu Siku ya Wapendanao ili kuanzia sasa ufikirie utaratibu mpya wa kusherekea siku hii. Kupitia makala hii nitakufunulia baadhi ya maswali kuhusu Februari 14, Siku ya Wapendanao au Valentine Day. Yapo mengi ambayo unatakiwa kufahamu kuhusu siku hii ili kuanzia sasa uisherekee katika mtazamo chanya na pengine iwe sehemu ya kubadilisha maisha yako na wale uwapendao.
📌Kati ya maswali ya tafakari ambayo nataka tujadili ni pamoja na; Kwa nini Februari 14? Kwa nini Valentine Day? Kwa nini Siku ya Wapendanao? Je! Chanzo cha siku hii kuitwa siku ya wapendanao ni kipi?
📌Ukweli ni kwamba Februari 14 imekuwa ikiadhimishwa kama siku ya kuoneshana mapenzi, na ndiyo waswahili wakaipachika jina la Siku ya Wapendanao. Ni ukweli pia kuwa siku kama ya leo ina uhusiano na kumbukizi ya Mtakatifu Valentine. Hata hivyo, kuna walakini kuhusu Mtakatifu Valentine alikuwa nani, na ilikuwaje siku hii ihuisishwe na mapenzi?
📌Kanisa Katoliki linatambua angalau watakatifu tofauti walioitwa Valentine au Valentinus, ambao wote waliuawa kwa nyakati tofauti. Moja ya taarifa kuhusu mmoja wa wawili hawa inasema, Valentine alikuwa Kasisi au Padre aliyehudumu katika karne ya tatu huko Roma kipindi cha utawala wa Claudius wa Pili. Mtawala huyu aliona kuwa wanaume waseja (wasiooa) wana ufanisi mkubwa kwenye majukumu ya kijeshi ikililnganishwa wale waliooa. Kutokana na hilo, aliamua kutunga sheria ya kuharamisha ndoa kwa vijana wa umri wa kati ambao ni hazina jeshini.
📌Valentine ambaye Kasisi aliona sheria hii ni dhalimu kutokana na kunyima vijana wengi haki ya msingi ya kuoa na kuishi na familia zao. Kama mtu ambaye ameapa kutimiza kazi ya Mungu na moja ya majukumu yake ni kufungisha ndoa, Valentine alikaidi amri ya mtawala Claudius wa pili na kuendelea kufungisha ndoa kwa wapenzi vijana huku akifanya hivyo kwa siri. Hata hivyo, Claudius wa pili alifahamishwa matendo ya Valentine na ndipo akatoa amri akamatwe na kuuliwa. Wakati akiwa amefungwa, alimponya binti kipofu wa mtekaji wake, na kupelekea nyumba nzima kugeukia Ukristo na hali hiyo ilihitimisha kazi yake. Hata hiyo, kwa amri ya Mtawala ilibidi ateswe na kukatwa kichwa. Kabla ya kuteswa na kukatwa kichwa mnamo Februari 14, alimtumia barua msichana kipofu aliyemponya ambayo ilisainiwa "Your Valentine."
📌Taarifa nyingine inasema; Mtakatifu Valentine alikuwa ni Askofu wa Termi, huko Roma na huyu ndiye mhusika halisi wa siku hii. Taarifa hii inasema pia kuwa Askofu Valentine alikatwa kichwa na mtawala Claudius wa pili kutokana na kukaidi amri ya kutofungisha ndoa vijana. Hali hii inapelekea kushindwa kujua ni yupi alikuwa Mtakatifu Valentine halisi wa kumbukizi ya siku hii ikizingatiwa kuwa hawa wawili wote wana historia zinazofanana.
📌Pamoja na uwepo wa taarifa zinazotofautiana kuhusu Mt. Valentine hakuna uhusiano wa moja kwa moja wa maisha ya wawili hawa na kuadhimisha siku ya kifo chao kama siku ya matendo ya mapenzi, yaani Siku ya Wapendanao. Je! Ilikuwaje siku hii ikahusishwa na matendo ya mapenzi?
📌Katika kutafuta ilikuwaje siku hii ikahusishwa na mapenzi ndipo nikakutana na neno ‘Lupercalia’. Lupercalia lilikuwa tamasha la kale la kipagani lililofanyika kila mwaka Februari 15 huko Roma. Pamoja na kwamba Siku ya Wapendanao hutumia jina la Valentine, mtakatifu Mkristo aliyeuawa, wanahistoria wengine wanaamini kwamba siku hii imepokea mapandikizi mengi ya Lupercalia. Tofauti ya Siku ya Wapendanao, hata hivyo, Lupercalia lilikuwa tamasha ya umwagaji damu, vurugu na ngono iliyojaa dhabihu za wanyama, na wanaume kuchagua wanawake bila mpangilio maalumu (rondom selection). Hapa bado hatujapata chanzo cha uhusiano wa Februari 14 na matendo ya mapenzi!
📌Bruce Forbes, ambaye alikuwa ni Profesa wa masomo ya dini katika Chuo cha Morningside huko Iowa, anasema “Hadithi mbili ambazo kila mtu huzungumzia, askofu na kasisi, zinafanana sana hivi kwamba zinanitia shaka", anaendelea kusema kuwa Februari 14 ilihusishwa tu na hadithi za Mtakatifu Valentine pamoja na matendo ya mapenzi mwishoni mwa Zama za Kati (middle ages) kupitia mashairi ya Mwingeleza Geoffrey Chaucer.
📌Katika miaka ya 1370 au 1380, Chaucer aliandika shairi lijulikanalo kama "Bunge la Ndege" ambapo ndani lilikuwa na mstari huu: "Kwa maana hii ilikuwa Siku ya Mtakatifu Valentine, wakati kila ndege anakuja huko kuchagua mwenzi wake." Hiki kilikuwa ni kipindi ambacho huko Ulaya mapenzi yalikuwa yanaanza kuteka ajenda za watu. Miaka ya 1400, Watu maarufu wakiongozwa na watu kama Chaucer walikuwa wameanza kuandika mashairi yaliyojulikana kama "valentines" kwa ajili ya kukidhi maslahi ya ajenda mapenzi iliyokuwa inakua kwa kasi. Hizi ndizo nyakati ambapo Februari 14 ilianza kuhusishwa na mapenzi sambamba na Mtakatifu Valentine.
📌Nihitimishe kwa kusema; makala hii ililenga kutafuta ukweli kuhusu uhusiano wa Februari 14, Valentine Day na Matukio ya mapenzi. Kama tulivyoona hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya Mtakatifu Valentine na Februari 14 isipokuwa ile barua kwa Binti Kipofu aliyeponywa na Kasisi au Askofu Valentine ambayo iliandikwa siku ya Februari 14. Uhusiano huu unaweza kujibu maswali juu ya kwa nini Februari 14 ni kumbukizi ya Mtakatifu Valentine. Pia, tumeona kuwa hakuna ukweli wowote kuhusu Februari 14 kutumika kama siku ya watu kuoneshana matendo ya mapenzi. Hii inatoa picha kuwa yawezekana mara kadhaa tumeshiriki kucheza ngoma ambayo hatujui asili yake ni nini. Kumbe, badala ya kuendelea kucheza ngoma hii kama vipofu tunatakiwa kuicheza kivyetu vyetu. Yaani, tuwe na tafsiri inayoendana na misingi na kanuni za maisha yetu badala ya kusherekea katika mapokeo ya zamani.
BOFYA HAPA KUPATA OFA KABABEMBE YA ZAWADI NILIZOKUANDALIA KATIKA SIKU HII YA WAPENDANAO!
BORN TO WIN ~ DREAM BIG
Mwalimu Augustine Mathias
Mawasiliano: 0786 881 155/0629 078 410
Barua pepe: fikrazakitajiri@gmail.com
onclick='window.open(