[Siri] Fahamu Matukio Muhimu Yanayoshikilia Uthamani wa Maisha Yako.

NENO LA SIKU_FEBRUARI 2/2022: [Siri] Fahamu Matukio Muhimu Yanayoshikilia Uthamani wa Maisha Yako. 


📌Ni siku nyingine ambapo naamini unaendelea vyema kutimiza majukumu yako ya siku ya leo. Hongera kwa kufanikiwa kupata kibali cha kuendeleza jitihada za kufanyia kazi malengo muhimu katika kila sekta ya maisha yako.


Kujiunga kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI, TAFADHALI BOFYA HAPA

📌Katika makala ya leo tutaangalia kwa ufupi jinsi gani ambavyo tunaweza kuishi maisha yenye tija kupitia matukio muhimu kwenye maisha yetu. Mara nyingi mwanadamu mwenye kiu ya kuishi maisha yanayoacha alama hutumia muda mwingi katika kutafuta ukweli halisi wa maisha. Mwanadamu wa aina hii mara zote maisha yake hutawaliwa na maswali mengi yasiyo na majibu ya moja kwa moja. Katika hali hii wengi hujikuta katika hali ya kushindwa kujua waamini lipi na kuacha lipi katika maisha yao ya kila siku.


📌Sisi sote ni mashaidi jinsi ambavyo wengi wetu katika kutafuta ukweli wa maisha wanavyoangukia kwenye mashimo marefu na kujikuta katika hali ya kuchanganyikiwa. Hali hutokea kutokana na ukweli kuwa jamii ina asilimia kubwa ya watu ambao hawana misingi na kanuni binafsi za kuongoza maisha yao. Katika hali kama hiyo, ni dhahiri tutegemee kuwa na idadi kubwa ya watu ambao hawajui waegemee upande upi maana kila kukicha upepo unawabadilishia mawimbi. Mfano, fikiria idadi ya watu ambao kila mara wanabadilisha madhehebu na sehemu za kuabudia wakidhani kuwa lipo dhehebu, Mchungaji Mtume au Nabii ambaye atawafunulia Mungu wa Kweli.


📌Pia, wote ni mashahidi jinsi ambavyo kila kukicha dini zinageuzwa kuwa biashara kutokana na idadi kubwa ya watu wanaojiita Mitume, Nabii, Wachungaji na Maaskofu kuongezeka kila kukicha. Tumeshuhudia jinsi ambavyo watu wa aina hiyo wanavyovuna umaarufu kutokana na miujiza wanayotenda na mwisho umaarufu wao hutoweka ghafla. Hata hivyo, pamoja na uwepo wa mifano hai katika jamii zetu bado watu wengi wanaendelea kujazana kwa watu wa aina hiyo. Ni dhahiri kuwa watu wataendelea kujazana kwa kuwa tuna idadi kubwa ya watu ambao wanategemea miujiza itokee maisha mwao kuliko kuiandaa miujiza hiyo kupitia majukumu yao ya kila siku. 


Kupitia makala hii nakushirikisha baadhi ya sehemu ambazo unaweza kujitathimini jinsi gani unaweza kupata  uthamani wa maisha kwa kadri unavyoishi kila siku:-


📌Sehemu Yako Ya Kazi. Ni dhahiri kuwa unapoanza kazi au biashara kwa mara kwanza unakuwa na msisimko na hamasa ya kufanikisha kazi hiyo au biashara husika kwa uwezo wako wote. Jaribu kupata picha siku ya kwanza ulipoanza kazi au kuanzisha biashara yako. Ni dhahiri kuwa kama ni huduma kwa wateja zilitolewa kwa viwango vya hali ya juu. Hata hivyo, kadri siku zinavyosogea msisimko wa kuendelea kutoa huduma kwa shauku na hamasa hufifia. Hali hii hupelekea kudumaza uwezo wako halisi katika kazi husika. Ikiwa unahitaji kuacha alama ya maisha yako, huna budi kuuhisha hamasa, shauku na msisimkoa katika majukumu ya kazi au biashara unayofanya sasa.


📌Uchumba Na Maisha Ya Ndoa. Hebu jaribu kukumbuka enzi zile unaingia kwenye uchumba na mweza wako ambao pengine ulipelekea kuingia maisha ya ndoa. Pata picha jinsi ambavyo ulikuwa unakosa usingizi kutokana na kumuwaza mwenza wako. Fikiria jinsi ambavyo siku hizo maisha yenu yalivyojazwa na furaha kutokana na kutazamana nyuso zenu. Kwa ujumla, uchumba au kuishi maisha ya ndoa uambatana na siku za furaha hila kadri siku zinavyosogea furaha hufifia. Wengine hufikia hatua ya kuiona ndoa kama jehanamu ndogo ya maisha yao kwenye uso wa dunia hii. Hata hivyo, ndoa ni sehemu ya kuboresha uthamani wa maisha yako. Ikumbukwe kuwa ndoa ni sehemu pekee pa kuonesha matunda ya hekima na busara kwa uzao wenu. Kupitia ndoa imara, jamii na taifa kwa ujumla hupata vizazi vilivyoshiba maadili hivyo kuwezesha uwepo wa viongozi bora.


📌Ikiwa Umebarikiwa Kupata Mtoto au Watoto. Watoto huja na baraka za kila aina na hujaza ulimwengu na matumaini kuhusu maisha ya baadae. Ndani ya kila mtoto kuna uwezo wa asili ambao unasubiriwa kuendelezwa kwa ajili ya kukua na kuchanua zaidi kadri mtoto anavyozidi kukua. Yamkini si watoto wote wanaofanikiwa kupata mwongozo sahihi wa kukuza vipaji na kalama walizojaliwa toka enzi ya kuumbwa kwao. Swali muhimu la kujiuliza wewe kama mzazi au mlezi ni; Je unatimiza wajibu wako ipasavyo katika kuongoza watoto ambao Mwenyeji Mungu amekujalia? Tumia wajibu wako kama mzazi kuandaa kizazi bora ambacho kesho na kesho kutwa utajivunia kutimiza wajibu wako kwa ufanisi.


📌Majukumu Ya Kijamii. Ikiwa umefanikiwa kuwa na majukumu kijamii ya ziada nje ya kazi au biashara yako una nafasi nyingine ya kuvuna uthamani wa maisha kupitia majuukumu hayo. Jamii ina asilimia kubwa ya watu ambao wanahitaji msaada wako kupitia majukumu yako ya kijamii. Kadri unavyotenda haki na kuwezesha upatikanaji wa haki kwa wenye uhitaji ndivyo unasaidia kupunguza mateso kwenye jamii. Hata hivyo, wengi wetu tumekuwa chanzo cha kuongeza mateso kwa wanaoteseka kutokana na matendo ya ucheleweshaji au uminywaji wa haki.


📌Matendo Ya Wema Na Kiroho. Hii ni sehemu nyingine ambayo tunaweza kuvuna zaidi uthamani wa maisha. Mara zote matendo yetu yanatakiwa kujikita kwenye kanuni ya dhahabu: Mtendee jirani yako kama ambavyo hungetamani kutendewa. Ikiwa utazingatia kanuni hii katika majukumu yako ya kila siku ni dhahiri kuwa mateso na uonevu katika jamii utapungua. Pia, kupitia matendo ya wema tunakumbushwa kuishi kwa kufikiria maisha ya wenzetu ambao kwa namna moja au nyingine wanapitia changamoto mbalimbali za maisha. Kila mara unaposhiba na kusaza fikiria kuhusu watu ambao kwao kupata mlo mmoja kwa siku ni shida. Vile vile, fikiria ni jinsi gani unaweza kushibisha roho za watu wanaopotea kimaisha kutokana na kukosa miongozo na maarifa sahihi.


📌Mwisho, kupitia makala ya leo nakukumbusha kuwa maisha yenye thamani hayapo nje ya ukamilisho wa majukumu yako ya kila siku kwa ufasaha. Unaweza kuishi kwa ukamilifu ikiwa kila siku utaikamilisha kwa kutenda kadri ipasavyo kwa roho kwako wewe mwenyewe, watu wengine na mazingira kwa ujumla. Hiyo ndiyo siri kuu ya kuishi kwa faida. Nakutakia siku njema.


PATA NAKALA YA KITABU CHA MAISHA YENYE THAMANI KUJIFUNZA ZAIDI KUHUSU MISINGI YA MAISHA BORA HAPA DUNIANI

Kitabu hiki bado kinatolewa kwa bei ya OFA kwa kuchangia cha Tshs. 10,000/= tu! Utatumiwa kwa barua pepe au WhatsApp Nakala tete (soft copy) yenye fomati ya Pdf.


Kupata kitabu hiki, lipia kupitia Mpesa kwenye namba +255 (0) 763 745 451 au Airtel Money namba +255 (0) 786 881 155 au Halopesa namba +255 (0) 629 078 410 zote majina ni AUGUSTINE MATHIAS MUGENYI.




onclick='window.open(