NENO LA SIKU_FEBRUARI 25/2022: UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Fahamu Mambo Ya Kuzingatia Unapoandaa Bajeti Binafsi
๐Rafiki yangu naamini unaendelea vyema katika kutekeleza majukumu yako ya leo. Hongera kwa kuendeleza moto wa mafanikio kupitia yote ambayo umefanikisha katika ratiba yako ya leo. Hata kama umekutana na changamoto, husife moyo endeleza shauku ya kutaka kufikia kilele cha malengo yako.
๐Makala ya leo ni mwendelezo wa kujifunza kuhusu bajeti binafsi kama msingi namba moja wa kuwezesha ukuaji wako kiuchumi. Katika makala zilizopita tulijifunza Kanuni muhimu ya kuzingatia wakati wa kuandaa bajeti binafsi inayoendana na pato lako halisi. Tuliona jinsi unavyotakiwa kugawanya pato lako katika makundi matatu ya matumizi; mahitaji ya lazima (50%), mahitaji ya ziada au yasiyo ya lazima (30%) na Uwekezaji/Akiba.
SOMA: UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Jifunze Zaidi Kanuni Ya 50/30/20
๐Katika makala hii tutajifunza mambo saba ya kuzingatia wakati unapoandaa bajeti yako. Vitu hivi ni maandalizi ya awali ambayo endapo utayazingatia yatakuwezesha uandae bajeti inayotekelezeka. Muhimu! Tukumbuke lengo zima la bajeti binafsi ni kukupatia dira ya jinsi gani unatakiwa kuelekeza pato lako kwenye matumizi mbalimbali. Hivyo, kupitia bajeti unatakiwa kutambua sehemu ambako hela zako huwa zinaelekezwa. Ili ufanikishe lengo hilo huna budi kuzingatia ushauri huu:-
๐Kuwa na sababu zinazokusukuma kuandaa bajeti binafsi, Ili ni jambo la msingi wakati unaandaa bajeti binafsi! Bajeti binafsi haipaswi ionekane kana kwamba ni adhabu kwenye matumizi ya pato lako. Ikiwa hauna sababu za msingi zinazokusukuma kuwa na bajeti binafsi, hutoweza kufurahia bajeti hiyo. Katika kipengele hiki unatakiwa kujibu maswali muhimu kuhusu wewe na bajeti yako. Huna budi kuelezea kwa undani malengo makuu ambayo unahitaji yafanikishwe kupitia utekelezaji wa bajeti yako. Ainisha malengo ya muda mfupi na mrefu katika kila sekta ya maisha yako ambayo unahitaji kuona yanatekelezeka kupitia utekelezaji wa bajeti yako.
๐Hapa unaweza kujiuliza maswali kama vile: Je! Nina deni ambalo napaswa kulipunguza au kulimaliza kabisa kupitia bajeti hii? Je! Kupitia bajeti hii ninataka akiba kwa ajili ya kukamilisha kitu gani cha msingi? Yawezekana unataka kupitia bajeti ufanikiwe kukusanya mtaji, ujenzi, ada n.k?
๐Chagua maneno ambayo yatakupa hamasa na shauku katika kuitekeleza bajeti yako, pengine neno 'bajeti' halikupi hamasa au msukumo. Kama ndivyo, huna budi kuwa na maneno yako ambayo yatakufanya ufurahie utekelezaji wa bajeti yako katika maisha ya kila siku. Wengi wetu linapotajwa neno bajeti hufikiria maisha ya kujibana, ubahili au uhaba wa pesa. Ikiwa na miongoni mwa watu hao, ni vyema ukawa maneno yako ambayo yatakufanya ufurahie bajeti yako. Unaweza kutumia maneno kama vile mpango wangu wa matumizi, kwa mwezi…, au orodha ya vitu ambako nitaelekeza pesa zangu kwa mwezi….
๐Chagua mbinu au Kanuni sahihi ya kukuongoza kwenye sehemu za msingi kuelekeza pato lako, mara zote pesa haijawahi kutosha na itaendelea kuwa hivyo mpaka unakufa. Hata wale unaodhania ni mamilionea huwa wanaelekeza pato lao kwenye vitu vya msingi. Hapa ni lazima utambue vipaumbele muhimu vya maisha yako. Katika makala zilizopita tuliona unaweza kutumia Kanuni ya 50/30/20 kama mwongozo wa matumizi ya pato lako. Pia, unaweza kubadilisha kanuni hii kulingana na mahitaji halisi ya bajeti yako. Muhimu! Kumbuka bajeti unayopanga ni kwa ajili ya kufanikisha nini?
๐Ainisha vipaumbele muhimu vya kutengea bajeti, makala zilizopita nilieleza kwa kina maana ya mahitaji ya lazima (needs), mahitaji ya ziada au yasiyo ya lazima (wants) na Uwekezaji/Akiba (investments/savings). Haya ni makundi muhimu ambayo yanapaswa kubeba vipaumbele vyote vya bajeti yako. Hapa unatakiwa kuainisha vipaumbele ambavyo utafurahia kuona pesa inatumika kwa ajili ya ukamilisho wa vipaumbele hivyo. Husiainishe vipengele vya bajeti ambavyo kesho na kesho kutwa utaanza kujuta mara baada ya pesa kutumika. Ainisha vitu ambavyo roho yako inapenda kulingana na maadili, kanuni binafsi au ndoto za maisha yako.
๐Acha nafasi ya dharura, si mara zote mambo yataenda kulingana na mpango wako wa bajeti. Kuna matukio nje ya uwezo wako ambayo yanaweza kuathiri mpango wako wa matumizi. Kuna nyakati mfumuko wa ghafla (inflation) unaweza kuathiri makadirio ya matumizi ya pesa kwenye makundi makuu matatu ya bajeti yako. Kuna nyakati matukio ya asili yanaweza kuathiri mpango wako wa Uwekezaji na akiba. Yote hayo yanakupa nafasi ya kufikiria matukio ya dharura wakati unaandaa bajeti yako. Ili uwe salama na matukio ya aina hii huna budi kuchukua tahadhari mapema.
๐Tathimini na rekebisha vipengele vya bajeti yako kila mwezi, ni matumizi yatabadilika mara kadhaa kulingana mahitaji ya mwezi husika. Mfano, matumizi katika mwezi Disemba hayawezi kuwa sawa na matumizi ya mwezi Agosti au Januari. Kuna miezi ya kulipia ada za wanafunzi, kodi za nyumba, likizo au siku kuu. Ili bajeti iwe salama kila mwezi unashauriwa kuipitia bajeti yako kila mwezi. Pia, bajeti inatakiwa iendane na mabadiliko kwenye mapato yako katika mwezi husika. Miezi ambayo kipato kimeyumba huna budi kupunguza matumizi ambayo siyo ya lazima na hata kutafuta mbadala kwa mahitaji ya lazima. Kama ulikuwa unakaa kwenye nyumba ya gharama unaweza kutafuta nyumba ya gharama nafuu. Kama ulikuwa unafanya manunuzi 'super markets', unaweza kufanya manunuzi yako kwenye masoko ya kawaida.
๐Epuka kununua kwa mikopo au kuongeza mikopo mibaya, hapa unatakiwa kuelewa kuwa mikopo ni matumizi ya pato la baadae kwa wakati wa sasa. Maana yake ni kwamba unatumia pato lako la baadae kabla ya wakati wake. Pia, epuka manunuzi unayofanya kwa mikopo yakiwa na ongezeko la bei. Watu wengine wanaingia kwenye mikopo midogo midogo kupitia manunuzi ya bidhaa kutokana na kushawishiwa kuwa watalipa kwa awamu kila mwisho wa mwezi. Wengi huwa hawajui kuwa wauzaji wanakuwa wameongeza bei za bidhaa kama gharama ya kufuatilia malipo. Ili uwe salama huna budi kuepuka mitego ya namna hiyo. Ikiwa unahitaji kununua bidhaa au kitu chochote cha thamani hakikisha unaingiza kwenye mpango wako wa bajeti wa muda mfupi au mrefu.
๐Nahitimisha makala hii kwa kusema, uandaaji na utekelezaji wa bajeti binafsi ni vitu viwili tofauti. Wengi wanaandaa bajeti lakini wanashindwa kuitekeleza. Ili hujitenge kwenye kundi la watu hawa huna budi kuzingatia sehemu muhimu za maandalizi ya awali nilizokushirikisha katika makala hii. Nakutakia kila lenye kheri katika kuandaa na kuitekeleza bajeti yako.
NB. Husisite kuwasiliana nami ikiwa unahitaji mwongozo zaidi juu ya jinsi gani unaweza kudhibiti matumizi yako ikilinganishwa na pato lako halisi. Nitumie ujumbe kupitia WhatsApp +255 786 881 155.
WAHI SASA UJIPATIE NAKALA YA KITABU CHA MAISHA YENYE THAMANI
Kitabu hiki bado kinatolewa kwa bei ya OFA kwa kuchangia cha Tshs. 10,000/= tu! Utatumiwa kwa barua pepe au WhatsApp Nakala tete (soft copy) yenye fomati ya Pdf.
Kupata kitabu hiki, lipia kupitia Mpesa kwenye namba +255 (0) 763 745 451 au Airtel Money namba +255 (0) 786 881 155 au Halopesa namba +255 (0) 629 078 410 zote majina ni AUGUSTINE MATHIAS MUGENYI.