[UFUNUO] Fahamu Hekima Ya Juu Tunayopaswa Kuitafuta Katika Maisha!

NENO LA SIKU_FEBRUARI 4/2022: [UFUNUO] Fahamu Hekima Ya Juu Tunayopaswa Kuitafuta Katika Maisha! 


📌Habari ya siku hii ya leo rafiki yangu ambaye umeendelea kuwa mfuatiliaji na msomaji wa makala zangu. Hongera kwa siku hii ya kipekee ambayo inaongeza idadi ya siku za uhai wako hapa duniani. Naamini kuwa unatumia siku hii muhimu kuendelea kuwa bora kupitia utekelezaji wa majukumu yako.  


Kujiunga kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI, TAFADHALI BOFYA HAPA


📌Karibu katika neno la tafakari ya leo ambalo nimeliandaa kupitia kisa cha Biblia Takatifu kuhusu Mfalme Sulemani au Solomoni (1 Wafalme 3: 3-14). Katika sehemu ya maandiko haya tunaona kuwa Mfalme Solomoni katika nyakati za awali za utawala wake baada ya kurithishwa madaraka na baba yake Mfalme Daudi, anatokewa na Mwenyezi Mungu katika ndoto.


📌Akiwa katika ndoto anaambiwa omba ulitakalo nami nitakupata. Solomoni kwa hekima ya hali ya juu anajinyenyekeza na kusema: “Umemfanyia mtumwa wako Daudi, baba yangu fadhili kuu, kadri alivyoenenda mbele zako katika kweli na katika haki, na katika unyofu wa moyo pamoja nawe; nawe umemwekea fadhili hii kubwa, maana umempa mwana wa kuketi kitini pake kama ilivyo leo. Na sasa Ee Bwana, Mungu wangu, umenitawaza niwe mfalme mimi mtumwa wako badala ya Daudi baba yangu; nami ni mtoto mdogo tu; sijui jinsi inipasavyo kutoka wala kuingia. Na mtumwa wako yu katikati ya watu wako uliowachagua, watu wengi wasiyoweza kuhesabiwa, wala kufahamiwa idadi yao, kwa kuwa ni wengi. Kwa hiyo nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuwahukumu watu wako walio wengi?” 


📌Katika kisa hiki kuna mengi ya kujifunza kwa ajili ya kuongoza miendendo ya maisha yetu hasa kwa kadri tunavyoishi na jamii ya watu wanaotunzuguka. Fikiria jinsi ambavyo Mfalme Solomoni katika umri mdogo na kwa madaraka ya juu ambayo alikuwa amekabidhiwa hakutaka kujikweza bali alijinyenyekeza au kujishusha. Tunaona ombi lake kuu ni kuwa na moyo wa adili ili apate kutoa hukumu kwa haki, na kuwa na uwezo wa kupambanua mema na mabaya. 


📌Hapa tunafundishwa umuhimu wa kuhakikisha tunatekeleza majukumu yetu kwa haki, tukihukumu kadri ambavyo tungependa kuhukumiwa. Pia, tunahitaji kuwa na uwezo wa kutambua mema na mabaya ili kujiweka kwenye nafasi ya kuishi maisha yanayompendeza Mungu. Tuna wajibu wa kutambua mema na mabaya dhidi ya nafsi zetu, watu wanaotuzunguka na viumbe wote katika mazingira yetu. Hii ndiyo hekima ya juu ambayo kila mwanadamu mwenye kiu ya kuishi maisha bora anatakiwa kuitafuta kila mara kupitia majukumu yake ya kila siku. Hii ndiyo hekima ambayo yatupasa kuionesha kupitia kila tunalofanya kwenye maisha yetu.


📌Pia katika kisa hiki, tunaona kuwa Mwenyezi Mungu alipendezwa na ombi la Mfalme Solomoni kutokana na jinsi ambavyo ombi lake lililenga zaidi hekima badala ya kuomba kupatiwa maisha marefu, wala akutaka utajiri wa nafsi yake, au kutaka adui zake waangamizwe. Kwa kupendezwa na ombi hilo, Mwenyezi Mungu anampatia Solomoni moyo wa hekima na wa akili kiasi ambacho hakuna mtu kabla au baada yake ambaye atakuwa kama yeye. Zaidi ya yote, Mwenyezi Mungu anamzidishia Solomoni zaidi ya ombi lake kwa kumuongezea mali na fahari kiasi ambacho hapatakuwepo mtu kama yeye na endapo ataendelea kuishi katika haki kama Baba yake atazidishiwa siku za kuishi.


📌Nihitimishe kwa kusema kuwa, makala ya leo inatukumbusha umuhimu wa kutafakari kuhusu mwenendo wa maisha yetu. Tunaweza kujipunguzia siku za kuishi sambamba na kufukuza baraka muhimu maishani mwetu ikiwa tunaendekeza maisha yanayojikita kwenye matakwa ya nafsi zetu, kuridhisha tamaa za mwili, uonevu, dhuruma au kuminya haki za wengine. Tunao wajibu wa kuhakikisha tunatumia maisha ya sasa kwa ajili ya kufungua baraka katika maisha ya kesho kwa faida yetu sisi na vizazi vyetu. Pia, tunakumbushwa kujinyenyekeza dhidi ya watu wanaotuzunguka bila kujali nafsi au cheo chetu katika jamii. Nakutakia kila lenye heri katika majukumu yako ya leo. 


PATA NAKALA YA KITABU CHA MAISHA YENYE THAMANI KUJIFUNZA ZAIDI KUHUSU MISINGI YA MAISHA BORA HAPA DUNIANI

Kitabu hiki bado kinatolewa kwa bei ya OFA kwa kuchangia cha Tshs. 10,000/= tu! Utatumiwa kwa barua pepe au WhatsApp Nakala tete (soft copy) yenye fomati ya Pdf.


Kupata kitabu hiki, lipia kupitia Mpesa kwenye namba +255 (0) 763 745 451 au Airtel Money namba +255 (0) 786 881 155 au Halopesa namba +255 (0) 629 078 410 zote majina ni AUGUSTINE MATHIAS MUGENYI.




onclick='window.open(