BADILIKA! Hivi Na Wewe Ni Miongoni Mwa Wazazi Wanaofanya Kosa Hili?

NENO LA SIKU_FEBRUARI 10/2022: BADILIKA! Hivi Na Wewe Ni Miongoni Mwa Wazazi Wanaofanya Kosa Hili?


📌Hongera rafiki yangu kwa kufanikiwa kuendelea na ratiba ya majukumu yako kwa siku hii ya leo. Ni siku nyingine ya kipekee ambayo inaongeza siku za uhai wetu hapa duniani. Naamini unaendelea kuitumia kutekeleza majukumu muhimu kulingana na vipaumbele vya maisha yako. Jambo la muhimu ambalo ningependa uzingatie kadri unavyoendelea na majukumu yako, ni kutambua kuwa maisha yanajengwa na matendo yako ya kila siku. Kila unachofanya kila siku ya uhai wako huchangia katika kuamua maisha hatima ya maisha yako. 


📌Karibu tena katika makala ya leo ambapo ni mwendelezo wa maarifa kuhusu ndoa, wazazi na watoto. Katika makala ya jana tulijifunza jinsi ambavyo ndoa inatakiwa kulindwa na wanandoa. Tuliona kuwa matunda ya ndoa ni kuwezesha uendelevu wa kizazi cha mwanadamu katika ulimwengu huu. Pia, tuliona ndoa imara huzalisha kizazi chenye maadili bora ambacho ni faida kwa jamii, taifa la hapa duniani na hata taifa la baada ya maisha haya, yaani taifa la Mungu.


KUSOMA MAKALA ILIYOPITA BOFYA MAANDIKA HAYA: Je! Umeoa au Kuolewa? Zingatia Ushauri Huu Kudumisha Ndoa Yako.


📌Katika makala hii ningependa kugusia tabia ya wazazi ambayo imeendelea kuzalisha kizazi lege lege, yaani kizazi dhaifu kisichoweza kujisimamia katika majukumu ya msingi. Tutakubaliana kuwa kwa sasa ni kawaida kwa familia zenye kipato cha wastani hasa katika maeneo ya mjini kuajiri wasaidizi wa kazi. Wasaidizi wa kazi mara nyingi majukumu yao huwa ni kuhakikisha wanakamilisha usafi wa nyumba, mazingira, vyombo, kufua, kupika, uangalizi na usafi wa watoto, kutandika vitanda na shughuli nyinginezo hapo nyumbani.


📌Wazazi wengi wamejikuta kwenye mtego wa kuzalisha kizazi dhaifu kwa kuelekeza majukumu yote ya nyumbani kwa wasaidizi wa kazi. Katika uwepo wa wasaidizi wa kazi, watoto ndani ya familia wanapumzika pasipo kujishughulisha na kazi yoyote katika orodha ya shughuli za nyumbani. Siku hizi, ni jambo la kawaida kukuta mtoto mwenye umri wa miaka zaidi ya  15 ambaye hajui kupika, kufua, kuosha vyombo achilia mbali kufanya usafi kwenye maeneo yanayozunguka nyumba. Jamii ya sasa ina vijana wengi ambao wapo vyuoni lakini hawajui kufua, kupika wala kufanya kazi za usafi wa mazingira katika maeneo wanakoishi.


📌Ni jambo la aibu ambalo limesafishwa lionekane ni utandawazi au maendeleo wazazi kuendelea kulea watoto katika misingi ambayo hawapaswi kujishughulisha na kazi yoyote zaidi ya kukusanya vyombo au nguo na kumsukumia msaidizi wa kazi. Kazi kubwa ambayo watoto wanaweza kujisimamia ni kuwasha TV na kuangalia tamthilia na vipindi mbalimbali au kucheza na kusubiria chakula mezani. Tumefikia hatua ambayo kizazi tunachozalisha hakiwezi hata kujisimamia kutekeleza majukumu ya shuleni kama vile kukamilisha kazi za nyumbani (home work) hadi pale kitakapokumbushwa kufanya hivyo.


📌Tumefikia hatua ambayo mtoto anafikia umri wa kuoa au kuolewa lakini hawezi kujisimamia. Familia za aina hii ni nyingi ambazo zinaendesha maisha ya ndoa kwa kutegemea kila jambo atashauriwa na mzazi, mlezi au ndugu wa karibu. Hii ni aibu ambayo kila mtu mwenye jukumu la kulea anatakiwa kuikimbia kupitia misingi bora ya malezi kwa watoto wake.


📌Tatizo kubwa la wazazi huanzia kwenye kuchukulia shughuli za nyumbani kama mateso kwa watoto. Mtoto anaepushwa na shughuli zote maana mzazi anadhania huo ni upendo kwa mwanae. Katika kufanya hivyo, taratibu mtoto anaendelea kukua pasipo kutambua kuwa kazi siyo mateso bali ni moja ya misingi muhimu katika kufanikisha maisha yake. Tujiulize hivi mtoto au kijana ambaye hajui kutekeleza majukumu ya nyumbani na mazingira yanayomzunguka ataweza vipi kukamilisha kazi ngumu katika maisha yake.


📌Kosa kubwa ambalo wazazi wa kisasa wanafanya ni kulea watoto kana kwamba wana tiketi ya kuishi milele. Wazazi wa aina hii hawajiulizi kesho na kesho kutwa watoto wataishi vipi nje ya uwepo wao. Wazazi hawa hata hawajiulizi ikitokea mabadiliko yoyote katika pato la familia wataweza vipi kuishi na watoto ambao ni mzigo kwa kutoweza kujisimamia katika kukamilisha majukumu ya msingi. Hivi ni ndugu yupi ambaye anaweza kuishi na mwanao uliyemlea kama yai ikiwa kwa bahati mbaya umetangulia mbele za haki? Haya ni maswali ambayo kila mzazi hana budi kujiuliza ikiwa anamtakia mwanae maisha mema ya baadae.


📌Nihitimishe kwa kusema, kuitwa baba au mama ni wajibu, huna budi kutambua kuwa maisha ya mwanao kwa kipindi hiki na siku zijazo yapo mikononi mwako. Mzazi ukilegea kidogo katika kutimiza wajibu huo, unazalisha watoto ambao hawawezi kujisimamia katika jambo lolote la msingi. Familia nyingi zinaendelea kuvunjika kwa vile zimekosa msingi bora wa uwajibikaji katika hatua za ukuaji. Ni dhahiri kuwa mtoto ambaye amelelewa kama yai hawezi kuishi maisha ya ndoa na mtu aliyekuzwa kimaadili. Kwa maana hiyo, mzazi huna budi kutambua kuwa unaijenga familia ya mwanao katika siku za utu uzima wake kupitia makuzi na malezi unayompatia kila siku. 


KIJIFUNZA ZAIDI KUHUSU MISINGI YA MALEZI NA HATUA ZA UKUAJI WA MTOTO JIPATIE NAKALA YA KITABU CHA MAISHA YENYE THAMANI 

Kitabu hiki bado kinatolewa kwa bei ya OFA kwa kuchangia cha Tshs. 10,000/= tu! Utatumiwa kwa barua pepe au WhatsApp Nakala tete (soft copy) yenye fomati ya Pdf.


Kupata kitabu hiki, lipia kupitia Mpesa kwenye namba +255 (0) 763 745 451 au Airtel Money namba +255 (0) 786 881 155 au Halopesa namba +255 (0) 629 078 410 zote majina ni AUGUSTINE MATHIAS MUGENYI.




onclick='window.open(