Makosa 50 Kuhusu Pesa Ambayo Unatakiwa Kuyakwepa Katika Kipindi Hiki cha Mwaka 2021

Uchambuzi wa Kitabu cha 50 COMMON MONEY MISTAKES: Makosa 50 kuhusu pesa ambayo watu wanafanya.

Habari rafiki yangu mpendwa, hongera kwa kuendelea kuwa sehemu ya wanaojifunza kupitia Makala zangu za uchambuzi wa vitabu. Kwa kipindi kirefu nimekuwa nikishirikisha jamii vitabu mbalimbali kupitia uchambuzi wa vitabu kwenye mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI pamoja na kundi la WhatsApp. Karibu katika uchambuzi wa kitabu cha leo ambacho ni miongoni mwa vitabu 15 nilivyosoma katika kipindi cha mwaka huu 2020.

Kama bado hujajiunga na kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya kupata neno la tafakari kila siku pamoja na kujumuika na watu wenye mtazamo sawa, tafadhali JIUNGE SASA.

Kitabu ninachokushirikisha kupitia makala hii ni 50 COMMON MONEY MISTAKES” kutoka kwa mwandishi Olumide Oladapo Emmanuel. Kupitia kitabu hiki mwandishi anatushirikisha makosa hamsini (50) ambayo watu wanafanya kuhusu pesa. Yawezekana makosa hayo yanafanywa na mimi au wewe katika maisha yetu ya kila siku pasipo kutambua kuwa ni makosa. Hivyo, kupitia kitabu hiki tunapewa fursa muhimu kujifunza ili kuepuka makosa kwenye pesa tunayopata. Olumide amekuwa Mjasiliamali, Mhamasishaji na Mshauri wa masuala ya kifedha kwa kipindi kirefu kiasi ambacho amefanikiwa kuwa miongoni mwa matajiri wa karne hii.

Mwandishi anatushirikisha kuwa watu wengi wanaishi kwenye ugumu wa kifedha kutokana na makosa ambayo wanafanya kuhusu pesa. Makosa hayo yamekuwa yakifanyika kwenye maisha ya kila siku kupitia matumizi, mikopo, uwekezaji au biashara ambazo wahusika wanafanya na mwisho wake wanaendelea kuangaika kifedha. Makosa haya kuhusu pesa yanafanyika katika ngazi ya mtu mmoja mmoja, familia au ngazi ya taifa. Kupitia kitabu hiki tutaweza kupiga hatua moja mbele kwenye maarifa muhimu kuhusu pesa.

Karibu ushirikiane nami kujifunza machache kati ya mengi ambayo tunashirikishwa katika kitabu hiki:

Kosa #1: Kushindwa kuweka kipaumbele kwenye elimu ya fedha. Mamilioni ya watu wanaamka asubuhi na kuzama kwenye majukumu ya siku ambayo yanalenga kusaka pesa lakini watu hao hawako tayari kuwekeza muda na pesa kwa ajili ya elimu ya pesa. Kukosekana kwa elimu ya pesa ni chanzo kikubwa watu wengi kuendelea kuishi kwenye dimbwi la umasikini. Wengi wameendelea kwenye mbio za panya ambazo mara nyingi uishia kwenye kingo za kuta kwa maana ni mbio ambazo hazina mshindi. Wengi wamendelea kukimbizana na fursa zenye malisho bora lakini pamoja na kufanikisha fursa hizo wanajikuta bado wanaangaika kifedha. Kwa ujumla, katika maisha muhimu siyo kiwango cha pesa unachotengeneza bali unafanya nini kutokana na pesa unayopata ndilo jambo la muhimu. Hapa ndipo umuhimu wa elimu ya pesa unapoanzia kwa maana elimu ya darasani pekee haitoshi kukukomboa kutoka kwenye umasikini.

Kosa #2: Kutotekeleza yale unayojua yana muhimu. Mwandishi anatushirikisha kuwa baada ya ujinga kuhusu pesa, kikwazo kinachofuatia kuzuia watu wengi kufanikiwa kifedha ni kutochukua hatua za utekelezaji kwa yale ambayo wanadhamiria kufanya. Hakuna maana yoyote ikiwa unajifunza kuhusu elimu ya pesa bila kuchukua hatua za utekelezaji kwenye yale unayojifunza. Tunafahamu kuwa maarifa ni nuru na maarifa ni nguvu japo yanakuwa ni nuru au nguvu pale ambapo maarifa yanatumiwa ipasavyo kumbadilisha mhusika. Unaweza kuwa na maarifa zaidi ya elfu moja lakini ukazidiwa na mtu ambaye ana maarifa kwenye sekta moja na ametumia ufahamu wake kwenye sekta hiyo kubadilisha maisha yake. Wapo watu wengi wenye maarifa kuhusu pesa lakini bado wanaangaika kipesa kwa vile hawabadilishi maarifa waliyonayo kwenye vitendo. Moja ya sababu zinazopelekea wengi kutoishi kwa vitendo ni kuendekeza visingizio vya sababu zinazoelezea kwa nini hawatekelezi yale wanayofahamu kuhusu elimu ya pesa.

Kosa #3: Kupuuza utamaduni wa kuweka akiba. Pesa inaishi katika utatu kwa maana: pesa ina roho, pesa ina mwili na pesa inaishi katika nyakati (wakati uliopita, uliopo na wakati ujao). Kwa ujumla unachotakiwa kufahamu ni kwamba kila shilingi inayoingia mikononi mwako inatakiwa kugawanywa katika matumizi yaliyopo na sehemu kutengwa kwa ajili ya matumizi ya baadae (akiba). Watu wengi ni masikini kwa kuwa wanapuuza utamaduni wa kuwekeza. Kila shilingi inayoingia mikononi mwao wanaitazama katika wakati uliopo na kusahau kuwa kuna matukio yasiyo tabirika kesho yanayohitaji pesa. Ikiwa unahitaji kuwa tajiri unatakiwa kuwekeza angalau asilimia kumi ya kila shilingi inayoingia mikononi mwako. Ana hekima mtu yule anayeishi kwa ajili ya kesho na mpumbavu ni mtu yule anayeishi kama tajiri leo bila kufahamu kesho ataishije.

Kosa #4: Kuwekeza sehemu ambayo hauna uelewa. Watu wengi wanawekeza pesa sehemu ambazo hawana uelewa wa kutosha kwa kuwa wanaongozwa na uchoyo na tamaa. Wengi wanaanzisha biashara au uwekezaji kwa kuwa wameona mtu flani amefanikiwa katika sekta hiyo. Kutokana na tamaa wengi wameshindwa kuruhusu busara na kanuni za maisha kujidhiirisha katika miradi wanayowekeza. Busara inakuta ufanye utafiti wa kutosha kabla ya kuwekeza pesa zako. Bahati nzuri kwa karne hii taarifa zinapatikana kirahisi kwenye mtandao. Unaweza kutumia taarifa hizo kulingana na upande wa sekta au mazingira unayohitaji kuwekeza. Pia, unatakiwa kuwa washauri wa kifedha (financial mentors) kwenye safari yako ya uwekezaji ili kuepuka makosa ambayo wengi wanafanya kwenye uwekezaji.

Kosa #5: Upofu wa kuona fursa. Umasikini unatokana na “Passing Over Opportunities Repeatedly – P.O.O.R”. Tafsiri yake ni kwamba watu wengi wameendelea kuwa masikini kwa kuwa kila mara wanapishana na fursa japo wanaziona kuwa ni fursa lakini hawachukui hatua. Katika safari ya kifedha, fursa ni ufunguo wa milango mipya na fursa ni ngazi ya kuelekea kwenye hatua za juu kwenye uwekezaji. Ni bora kujiandaa na kupitwa na fursa kuliko fursa kukupita kwa kuwa hukujiandaa. Bahati huwa ni pale fursa inakutana na mtu ambaye amejiandaa kuchangamkia fursa husika. Ikiwa unahitaji kuwa na uhuru wa kifedha ni lazima ujifunze kuchangamkia fursa zinazojitokeza kwa kuwa ni fursa pekee zitakazobadilisha maisha yako.

Kosa #6: Kuogopa kuchukua hatari ya uwekezaji (investment risk). Maisha yetu ya kila siku yanahusisha hatari japo inapokuja kwenye suala la uwekezaji au biashara wengi wanaopa hatari. Wapo watu wanafanya maamuzi ya hatari na hovyo kwenye maisha yao lakini kwenye uwekezaji wanaogopa hatari. Badala ya kuogopa hatari unashauriwa kukokotoa kiwango cha hatari iliyopo kwenye uwekezaji na hatimaye kulinganisha na hatari ya kutofanya uwekezaji husika. Kwa kuwa maisha yetu ya kila siku yanahusisha hatari hakuna haja ya kuogopa hatari za uwekezaji au zinazohusiana na biashara. Mfano, unapoamua kuoa au kuolewa unakuwa umeamua kuhatarisha maisha yako kwa kukubali kuishi na mtu ambaye haukuwa kuishi nae toka enzi za ukuaji wako. Kukubali kuoa au kuolewa ni wazi kuwa umekubali kubeba hatari ya maisha yenu ya baadaye kama familia. Kwa ujumla, unatakiwa kutambua kuwa katika uwekezaji sehemu ambazo zina hatari kubwa ndizo zinakimbiwa na watu wengi na sehemu hizo ndizo zina nafasi kubwa ya kutengeneza faida.

Kosa #7: Kuishi maisha ya kujikana. Watu wengi wanaishi maisha ya kujikana ambayo yanajumuisha kupoteza muda, rasilimali, kupoteza fursa, kupoteza fedha na kupoteza kila chenye thamani kwenye maisha yao. Siri moja ya kutengeneza utajiri ni kuishi ndani ya uwezo wako lakini wengi huwa wanaishi maisha ya kuigiza. Ikiwa matumizi yako yanazidi kipato ni wazi kuwa utaendelea kuishi maisha ya kuigiza ambayo yatakulazimu kukopa au kuishi kwa kuunga unga kila wakati. Kila shilingi inayoingia mikononi mwaka unaweza kuipoteza, unaweza kuitumia au unaweza kuiwekeza. Wengi ambao ni masikini huwa wanaishia kuipoteza kwa kufanya manunuzi yasiyo na tija wakati watu wa pato la kati huwa wanaishia kuitumia kwenye matumizi ya maisha ya kuigiza. Wachache ambao wana uhuru wa kifedha huwa pamoja na kutumia wanaiwekeza pesa ili iongezeke zaidi. Watu wengi huwa wanafikiria jinsi ya kutengeneza pesa lakini ni wachache ambao huwa wanafikiria kutafuta mianja inayopoteza hela kwenye maisha yao ya kila siku.

Kosa #8: Kuruhusu Uroho na Uchoyo katika maisha yako. Katika utafutaji wa pesa wengi huwa wanaendekeza uroho na uchoyo wa kuzingatia matakwa binafsi na kusahau kuwa katika mchezo wa kutafuta pesa pande zote zinatakiwa kunufaika (double win victory). Kutokana na tabia hiyo wengi wamejikuta ni wahanga wa michezo ya kamali ambapo wanaishia kupoteza hela nyingi kwa kutegemea kuwa watafanikiwa kipesa. Pia, wengi wamekimbilia kutafuta utajiri wa haraka na mwisho wanaishia kutapeliwa. Kosa kubwa linalopelekea yote hayo kutokea ni kutokana na kuruhusu hisia za kutaka utajiri wa haraka zitawale maisha ya wengi.

Uchambuzi wa kitabu chote unapatikana kwa gharama ya Tshs. 4,999/=. Pia, kupata makala mbalimbali za namna hii kwenye barua pepe yako jiunge na mtandao wa Fikra za Kitajiri kwa  KUBONYEZA HAPA.

 

Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu isiyokuwa na mwisho.


Born to Win ~ Dream Big 


Mwalimu Augustine Mathias

Namba ya Simu:      +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa 
fikrazakitajiri.blogspot.com

Barua pepe:  fikrazatajiri@gmail.com


onclick='window.open(