NENO LA LEO (JANUARI 27, 2021): HUU NDIYO URAHIBU (ADDICTION) UNAOITESA DUNIA YA SASA
Habari
ya asubuhi rafiki yangu mpendwa na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni siku
kipekee ambayo tunaendelea kutumwa katika Dunia hii kukamilisha kusudi kuu la
maisha yetu. Safari bado ni ndefu na katika safari hiyo kila siku tunakumbushwa
kuifanya njia hiyo rahisi kupitia matendo yetu. Hivyo, kila siku ni ukurasa
mpya unaounda kitabu cha siku za uhai wetu hapa Duniani. Kila mmoja wetu ana
wajibu wa kuandika vitu vitakavyovutia watu kusoma kitabu chake katika enzi za
uhai wake na hata baada ya ukomo wa maisha haya.
Katika
neno la tafakari ya leo tutaangalia urahibu unaoitesa Dunia ya sasa. Neno
urahibu au addiction kwa lugha ya kingereza linatumika kumaanisha kilele cha
ukomavu wa tabia kwa mhusika. Urahibu ni zao la mwisho katika hatua za kujenga
tabia mpya. Katika hatua hii mhusika anajikuta anatekeleza au kufanya tukio
pasipo kupitia kwenye mlolongo wa ubongo kufanya maamuzi. Hivyo, mhusika
anajikuta katika hali ambayo hawezi kujizuia kutekeleza tabia husika. Katika
hali kama hiyo, mhusika anapoteza uwezo wa kung'amua mambo, ubunifu na hata
uwezo wa kujitegemea.
Siku za nyuma tulizoea urahibu kama vile matumizi ya bangi, madawa ya kulevya, sigara na matumizi ya vilevi. Urahibu huu tofauti na urahibu wa sasa ulihusisha idadi ndogo ya watu katika jamii na athari zake zilikumba makundi machache ya watu. Mfano, katika jamii tulizoea vijana wanaathirika zaidi na matumizi ya dawa za kulevya au bangi ikilinganishwa na makundi mengi ya watu. Tafsiri yake ni kwamba walioathirika na urahibu katika jamii walikuwa wachache ukilinganishwa na urahibu wa sasa.
Ulimwengu wa sasa unakibiliwa na urahibu wa mitandao ya kijamii (social media addiction) na athari zake ni nyingi ikilinganishwa na athari za urahibu katika historia ya maendeleo ya mwanadamu. Tofauti ya urahibu wa sasa na urahibu uliozoeleka hauchagui kundi la watu. Iwe wasomi au ambayo hawajasomo wote wanaangamia. Iwe vijana, wazee na hata watoto wote wanazama ndani ya kundi hili. Jamii ya sasa inahusudu mitandao ya kijamii (Facebook, Instagram, Twitter na mingineyo) kuliko inavyofanya kwa vitu vya msingi.
Kutokana
na ukomavu wa urahibu huu kwa sasa ni kawaida kukuta katikati ya majadiliano ya
msingi baadhi ya watu wapo bize na kuperuzi simu zao. Tunashuhudia wanafamilia
wanakosa muda wa kuwa karibu na wapendwa wao lakini wanapata muda wa kuperuzi
kwenye mitandao. Tunashuhudia kizazi ambacho ubunifu unapungua kutokana na
athari za kuwaza kuingia kwenye mitandao ya kijamii. Tunashuhudia kizazi
ambacho hakiwezi kusoma kitabu cha maarifa mbalimbali au kushika kitabu cha
maandiko matakatifu lakini ndani ya mitandao ya kijamii kila kitu kinawezekana.
Mwisho, katika neno la tafakari ya leo tumeona kuwa Dunia ya sasa inakabiliwa na urahibu ambao utaendelea kutesa makundi yote ya watu. Watoto, Vijana, Wazee au akina baba na akina mama wanaendelea kuangamia na urahibu huu ikilinganishwa na rahibu zilizozoeleka siku za nyuma. Ni wakati sahihi wa kupima matumizi ya mitandao ya kijamii katika ratiba yako ya siku. Kumbuka, mbegu ikidodoka ardhini ni lazima iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu hii niliyodondosha kupitia neno la tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi katika Maisha yako.
PS: Unaweza kujipatia maarifa kwenye elimu
ya pesa kupitia usomaji wa vitabu. Chagua nakala za uchambuzi wa vitabu
unavyotaka kwa kubofya kiunganisha hapo chini. Kila nakala ya uchambuzi wa
kitabu inapatikana kwa gharama ya Tshs. 3,999. Wahi mapema hii ni OFA ya leo.
BOFYA HAPA KUPATA ORODHA YA UCHAMBUZI WA VITABU
BORN TO WIN ~ DREAM BIG
Mwalimu Augustine Mathias
Mawasiliano:
0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua
pepe: fikrazakitajiri@gmail.com