NENO LA LEO (JANUARI 15, 2021): SIRI YA KUUFANYA MWEZI JANUARI/JULAI UWE SAWA NA MIEZI MINGINE
Habari
ya asubuhi rafiki yangu na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni asubuhi mpya yenye
matumaini na hamasa ya kutosha katika kufikia lengo kuu lililopo mbele yetu. Ni
siku ambayo nakukumbusha kuendelea kufanya vitu vya kipekee ambavyo kila siku
vinakuimarisha katika hatua za ukuaji kuelekea kwenye mafanikio ya ndoto zako.
Pia, nakukumbusha kuwa mwaka 2021 ndo huu tayari unazidi kushika kasi, wakati
ni sasa wa kuishi kwa vitendo malengo uliyojiwekea katika kipindi hiki.
Jiunge na kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI, kwa kujiunga utapata neno la tafakari kila siku pamoja na kujumuika na watu wenye mtazamo sawa, TAFADHALI JIUNGE SASA
Katika neno la tafakari ya leo tutaona jinsi ambavyo kila mmoja wetu anavyoweza kuufanya mwezi Januari au Julai uwe rafiki kwake sawa na ilivyo miezi mingine. Katika jamii tunayoishi kila ikifika mwezi Januari au Julai huwa tunashuhudia malalamiko ya kila aina huku mengi yakihusisha upungufu wa fedha. Katika neno la tafakari ya jana niligusia kuwa miezi hii huwa inahusisha utokaji wa fedha kwa ajili ya kulipia mahitaji ya shule sambamba na kodi za nyumba. Mahitaji hayo ya lazima huwa yanaacha idadi kubwa ya watu katika jamii wakiwa hawana pesa kwa ajili ya kukidhi mahitaji mengine. Hali hii huwa inapelekea watu wengi kuishi kwa msongo mkubwa unaopelekea wengine kuwa na huzuni zinazoambatana na hasira za mara kwa mara bila sababu za msingi.
Ukweli ni kwamba hakuna mtu ambaye anakuwa hajui kuwa mwezi Januari au Julai anatakiwa kulipia ada za wanafunzi au kulipia pango la nyumba. Chanzo kinachopelekea miezi hii iwe na msongo wa pesa kwa watu wengi ni kwa vile watu hawana mfumo wa bajeti ya mahitaji ya mwaka mzima. Njia rahisi ya kuifanya miezi hii iwe rafiki kwako ni kuwa na bajeti ambayo unaitekeleza kutoka mwanzo hadi mwisho wa mwaka. Ninacho maanisha hapa ni kwamba mahitaji ya ada za wanafunzi au malipo ya kodi yanatakiwa kuanza kuandaliwa toka mwezi Januari unapoanza ili itakapofika muda wake liwe ni suala la kukamilisha malipo.
Katika neno la tafakari ya jana tuliona kuwa badala ya kupunguza matumizi unatakiwa kuongeza mifereji ya pesa. Katika mifereji uliyonayo unatakiwa kutenga kila mwezi asilimia flani kwa ajili ya kufanikisha mahitaji ya ada au malipo ya pango la nyumba katika miezi ambayo fedha hizo zinatakiwa. Kama kuna uwezekano unaweza kuanzisha Mfereji maalum kwa ajili ya kukamilisha kila hitaji la pesa au kuhakikisha kila mtoto anakuwa na mfereji wake wa kukamilisha mahitaji ya masomo. Endapo utatumia mbinu hii kwa nidhamu hakika utashangaa kila ikifika mwezi Januari au Julai unakuwa tayari umejiandaa kukamilisha mahitaji ya pesa kulingana na bajeti yako.
Mwisho, katika neno la tafakari ya leo tumejifunza kuwa mwezi Januari au Julai ni miongoni mwa miezi ambayo tunaweza kuishi bila ya kuwa na msongo wa mawazo ikiwa tutakuwa na bajeti na kuhakikisha tunatekeleza bajeti hiyo kila siku. Ukweli ni kwamba hakuna kinachohitaji pesa mwezi Januari au Julai ambacho kilikuwa nje ya ufahamu wako. Hivyo, kuna kila sababu ya kuweka maandalizi kila mwezi kulingana na mahitaji ya pesa yaliyopo kwenye bajeti yako. Kumbuka, mbegu ikidodoka ardhini ni lazima iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu hii niliyodondosha kupitia neno la tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi katika Maisha yako.
PS: Unaweza kujipatia maarifa kwenye elimu ya pesa kupitia usomaji wa vitabu. Chagua nakala za uchambuzi wa vitabu unavyotaka kwa kubofya kiunganisha hapo chini. Kila nakala ya uchambuzi wa kitabu inapatikana kwa gharama ya Tshs. 3,999. Wahi mapema hii ni OFA ya leo.
ππΎππΎππΎππΎππΎ
BOFYA HAPA KUPATA ORODHA YA UCHAMBUZI WA VITABU
BORN TO WIN ~ DREAM BIG
Mwalimu
Augustine Mathias
Mawasiliano:
0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua
pepe: fikrazakitajiri@gmail.com