NENO LA LEO (JANUARI 9, 2021): JE UNAFANYA KAZI YENYE SIFA ZIPI KATIKA KIPINDI HIKI CHA 2021?
Habari
ya asubuhi rafiki yangu na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni siku nyingine
tena ambayo tumepewa kibali cha kuwa hai. Ni katika kipindi hiki wajibu wetu ni
kuendelea kutoa thamani kupitia yale tunayofanya. Maisha yetu hapa yanakuwa na
thamani pale ambapo yale tunayofanya yanasaidia kuboresha Duniani hii kuwa mahala
pazuri pa kuishi kwa viumbe vyote. Hivyo, katika siku ya leo nakukaribisha
kutafakari matendo yako kama yanasaidia kuboresha maisha yako na jamii
inayokuzunguka.
Katika neno la tafakari ya leo
nitakushirikisha makundi matatu kazi ambazo zinajumuisha kazi zetu za kila
siku. Kila kazi inayofanywa na mwanadamu hapa Duniani inaweza kuwa ni: (a) kazi
mbaya – bad work (b) kazi nzuri – good work (c) kazi kubwa – great work. Kundi
la kwanza linajumuisha kazi ambazo zinapoteza muda, nguvu, rasilimali na hata
maisha ya muhusika.
Kundi la pili linajumuisha kazi ambazo mhusika anafanya mara kwa mara na muda mwingi anautumia katika kazi hizo. Mara nyingi kazi za namna hii zinatokana na taaluma au uzoefu wa mhusika hivyo ni kawaida wahusika kufanya kazi hii kwa kiwango cha hali ya juu hata kama tija yake ni ndogo. Kundi la mwisho linahusisha kazi zote ambazo kila mtu anatamani kufanya kwa maana kazi ambazo zinaleta mabadiliko katika maisha ya mhusika. Na kazi hizi zina sifa ya kumfanya mhusika afikirie kwa mapana, aifurahie kazi anayofanya na kila siku atamani kuendelea kufanya kazi pasipo kusukumwa na mtu yeyote.
Ikiwa umedhamiria mwaka 2021 uwe wa tofauti unatakiwa kufikiria kufanya kazi zenye sifa ya kundi la mwisho kwa kuwa kazi hizo zitakufanikishia tija kubwa kwenye malengo yako. Kwa kujitosa kwenye kazi za kundi hilo itakuwezesha kujitofautisha na watu wengine kwa kuwa hautoridhika na matokeo kidogo unayopata. Nasema utajitofautisha na watu wengine kwa kuwa wengi wamezoea kufanya kazi za kundi la pili kwa vile hawataki kujisumbua katika kufikiri, wanaogopa kuchukua maamzi magumu (risk), wanatafuta usalama wa kazi kuliko tija ya kazi na hawako tayari kuangaika mara kwa mara kutafuta maarifa mapya.
Jambo la msingi la kuzingatia ni kwamba kazi za kundi la tatu hazipo nje ya kazi tunazofanya kwa sasa. Muhimu ni kuzingatia viwango vya ubora wa kazi husika na viwango hivyo ndivyo vitakuweka kwenye kundi la pili au kundi la tatu. Unachotakiwa kufanya ni kuhakikisha unatekeleza kazi zako kwa weledi, ubunifu na ukamilifu kufanya hivyo utahamishia kazi zako kwenye kundi la tatu.
IKIWA UNAHITAJI MWAKA 2021 KUJENGA TABIA YA KUJILIPA KWANZA: SOMA MAKA HII
Na mara nyingi siyo lazima kazi kubwa zingatie lengo la kuongeza kipato tu, chochote unachofanya ikiwa ni kwa ajili ya ukamilisho wa kusudi la maisha yako kina sifa ya kuingia kwenye kazi za kundi la tatu ikiwa unatekeleza kazi hiyo kwa viwango vya juu. Kwa mtazamo huu, hatua ya kwanza kabisa ya kufanya kazi kubwa yenye tija ni lazima kufahamu kwanza wewe ni nani na kwa nini uliumbwa jinsi ulivyo. Hapa unaweza kujiuliza mwaswali haya; (i) Ni nini hasa utambulisho wangu katika jamii? (ii) Je ni lipi lengo na mwelekeo wangu? (iii) Watu gani naweza kuambatana nao? Hakuna kazi ambayo utafanya peke yako. (iv) Je ni changamoto zipi ambazo navutiwa kuzitatua? (v) Ni jinsi gani naweza kujenga mtazamo/mazingira chanya juu ya kazi yangu? (vi) Je naitikia vipi kwenye vikwazo vilivyopo mbele yangu? na (vii) Je ni nini furaha yangu?
Mwisho,
katika neno la tafakari ya leo tumejifunza makundi matatu ya kazi. Tumeona kuwa
ikiwa unahitaji mwaka 2021 uwe wa tofauti ni lazima tufanye kazi zilizopo
katika kundi la tatu (great work) kwa kuwa kazi hizo tija yake ni kubwa
ikilinganishwa na kazi katika kundi la kwanza na la pili. Hata hivyo, tumeona
kuwa chochote tunachofanya ni lazima kichangie kwenye ukamilisho wa kusudi la
maisha yetu hapa Duniani. Kumbuka, mbegu ikidodoka ardhini ni lazima
iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu hii niliyodondosha kupitia neno la
tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi katika Maisha yako.
BORN TO WIN ~ DREAM BIG
Mwalimu Augustine Mathias
Mawasiliano: 0763 745 451/0786 881 155/0629
078 410
Barua pepe: fikrazakitajiri@gmail.com