2021 IANZE KWA KUKIAMBIA MAKUNDI YA WATU SUMU

NENO LA LEO (JANUARI 2, 2021): 2021 IANZE KWA KUKIMBIA MAKUNDI YA WATU SUMU.

Habari ya asubuhi rafiki yangu mpendwa na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni matarajio yangu kuwa mwaka mpya na tayari umeshaanza na jukumu ambalo lipo mbele yetu ni kutekeleza malengo ya kipaumbele kwa mwaka huu. Wakati ni sasa na mwaka ndiyo huu hivyo hakuna haja ya kusubiri kwa kutegemea kuwa ni mapema mno.

Mwaka 2020 yawezekana ulishindwa kufikia malengo kutokana na kuendekeza makundi ya watu ambao haukujua athari yao katika kufikia malengo yako. Katika Makala ya leo nitakushirikisha aina ya makundi ya watu sumu ambao unatakiwa kuwakimbia katika kipindi kizima cha mwaka 2021. Yafahamu makundi hayo na athari zake katika kufikia malengo yako:-

JIUNGE NA KUNDI LA WHATSAPP LA FIKRA ZA KITAJIRI KWA KUBONYEZA HAPA NA KUJIUNGA BURE. Jiunge sasa nafasi ni chache.   

Kundi #1: Watu wanaosambaza uhasama na wenye mtazamo hasi. Hawa ni watu ambao katika jamii siku zote wanawaza kuchonganisha na wenzao na mara nyingi wanakuwa na taarifa nyingi kuhusu watu. Watu hawa wanatumia muda mwingi kuongelea maisha ya wengine. Pia, watu hawa linapokuja suala la maisha yao wanakuwa na mtazamo hasi kiasi kwamba kila wanapinga kila wazo ambalo ni geni. Unapokuwa karibu na watu wa aina hii itakuchukua muda kufikia malengo yako kwa kuwa kila mara utakatishwa tamaa. Vilevile, utajikuta ukifuatilia maisha ya watu kuliko kufuatilia majukumu yaliyopo mbele yako.

Kundi #2: Wale ambao wanapinga mawazo yako. Wapo watu katika jamii ambao mara zote wanapinga mawazo ya wengine. Watu hawa unapokuwa karibu nao watapinga kila wazo unalowashirikisha na pengine watatafuta kila sababu kukuonesha kuwa unalowaza halitekelezeki. Mara nyingi watu wa aina hii wanatumia mifano ya watu wengine ambao wamefanya na kutofanikiwa lakini wao hawajawahi kufanya kile ambacho wanakukataza. Ukiwapa nafasi watu wa aina katika maisha yako utajikuta katika hali ya kuua mawazo mengi ambao ulikusudia kuyatekeleza kwa ajili ya kupiga hatua.

Kundi #3: Wale wanaokupotezea muda. Mara mara zote unatakiwa kuatambua kuwa muda ni pesa na ni rasilimali ambayo inayeyuka haraka sana. Watu wote tumepewa muda sawa lakini kupitia matumizi ya muda huo watu wanatofautiana kimafanikio. Tofauti hii ya mafanikio inatokana na jinsi ambavyo watu wanathamini matumizi ya muda wao. Kundi hili linahusisha watu ambao watakupotezea muda kwa kujadili mambo ambayo hayana tija au watu ambao mara zote wanajali utimize majukumu yao wakati ya kwako yamesimama.

 

Kundi #4: Watu wenye wivu. Siri ya mafanikio kupenda mafanikio ya watu wengine. Kadri unavyofurahia mafanikio ya watu wengine ndivyo milango yako inafunguka kupitia watu hao. Hali huwa haiku hivyo katika jamii, watu wengi wanachukia mafanikio ya watu pasipokuwa na sababu. Watu wa aina hii ni sumu kwa mafanikio yako maana wanaweza kufanya lolote kwa ajili ya kukurudisha nyuma. Kutokana na kutokujua dhamira ya watu tuna wajibu wa kufanya siri mipango yetu ili hisijeangukia kwa watu wabaya.

 

Kundi #5: Watu wenye fikra finyu. Hili ni kundi la watu ambao wana uwezo mdogo wa kung’amua mambo ya msingi katika maisha. Unapokuwa karibu na watu hawa kila ambalo utawashirikisha wataliona gumu. Watu hawa wanakuwa na vikwazo vingi kwenye kila wazo ambalo lipo mbele yao ikilinganishwa na njia mbadala za kukwepa vikwazo hivyo. Kaa mbali na watu hao vinginevyo utaona vikwazo kwenye kila lengo ambalo umedhamiria katika kipindi cha mwaka huu.

 

Mwisho, katika Makala hii nimekushirikisha makundi matano ya watu sumu katika kutekeleza malengo yako. Binadamu ni kiumbe ambacho kinatofautiana na viumbe wenzake hasa linapokuja suala la tabia. Kutokana na tofauti hizo, una wajibu wa kuhakikisha wale ambao unashirikiana nao mnakuwa na mtazamo sawa kwa ajili ya kuhamasishana na kupeana fursa mpya. Kumbuka, mbegu ikidodoka ardhini ni lazima iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu hii niliyodondosha kupitia neno la tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi katika Maisha yako.

 

BORN TO WIN ~ DREAM BIG

 

Mwalimu Augustine Mathias

Mawasiliano: 0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410

Barua pepe: fikrazakitajiri@gmail.com

onclick='window.open(