NENO LA LEO (JANUARI 17, 2021): KWA NINI UNAJICHELEWESHA KWA KIGEZO CHA KUTOKUWA TAYARI?
Habari
ya asubuhi rafiki yangu na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni wakati
mwingine tumeamka salama tukiwa na nguvu na hamasa kwa ajili ya kuendeleza pale
tulipoishia jana. Kila siku katika utangulizi wa neno la siku nimekuwa nikikumbusha
umuhimu wa kufanya vitu vyenye muunganiko (Connectivity). Nimekuwa nikifanya
hivyo ili kukuepusha kupoteza nguvu na rasilimali pamoja na muda kwa kufanya mambo
mengi ambayo hayana uhusiano. Watu wengi wameshindwa kufika mwisho wa safari
kutokana na kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja. Katika hali hiyo wanajikuta
hakuna hata jambo ambalo linafikia kwenye viwango walivyokusudia na mwisho wake
ni kukata tamaa.
Katika neno la tafakari ya leo tutaona jinsi gani tumekuwa tunapoteza muda kutokana na kusubiria utayari au ukamilifu wa mahitaji kabla ya kuanza. Watu wengi wamepoteza ndoto zao na wengine kushindwa kupita hatua kutokana na kusubiria utayari au ukamilifu kwa muda mrefu. Katika neno la leo nataka kuanzia sasa uishi kwa kutambua kuwa “wale wote unaowaona kwenye kilele cha mafanikio hakuna hata mmoja ambaye alianzia juu”. Husikubali kudanganywa na mtu yeyote ambaye anasema hakuwahi kuwa kwenye hatua za chini sawa na ilivyo kwako kwa sasa.
Fikiria kwenye kila aina ya mafanikio unayotamani katika maisha yako na jiulize kwa nini unakwama kuanza hadi sasa. Ikiwa ni upande wa mafanikio kwenye siasa – angalia wanasiasa wenye mafanikio makubwa na vuta historia zao. Wengi walianzia kwenye ngazi za chini kabisa kwenye uongozi na utendaji.
Fikiria
kuhusu mafanikio kwenye ngazi za utendaji katika taasisi na Serikali au taasisi
zisizo za Serikali – Watendaji wa ngazi za juu wote walianzia kwenye ngazi
chini. Mfano, Meneja wa Benki alianza kama “Cashier” au Afisa wa kawaida. Wapo
watendaji wengi wa ngazi za chini ambao walianzia kwenya nafasi za chini kabisa
lakini leo hii imebaki kuwa historia.
Yawezekana mwaka huu umepanga kumiliki nyumba yako lakini bado unasita kuanza kwa vile unaona bado haujajikamilisha. Hakuna linaloshindikana kwa kuwa hata huyo mwenye nyumba yako amepitia kwenye maisha unayoyapitia sasa hila ambacho kimemfikisha kwenye viwango alivyonavyo kwa sasa ni uthubutu wa kuanza.
Yawezekana umekuwa unakusudia kuanzisha biashara lakini unachelea kuanza kutokana na kuona hauna mtaji wa kutosha. Ndugu yangu wale wote waliofanikiwa kibiashara wengi wao walianzia kwenye biashara za kawaida kabisa ambazo kwa mtaji huo ulionao unatosha kabisa kuanza. Mfano, “binafsi nilianzisha ufugaji wa nguruwe kwa nguruwe mmoja na Watoto wake sita lakini kupitia nguruwe huyo hadi sasa nina nguruwe 117 na nimeuza nguruwe 85 ndani ya kipindi cha miaka minne tu”. Wakati naanza nilikuwa na banda la banzi lenye milango mitano tu lakini leo hii ni banda za kisasa zenye milango 18.
Mwisho,
katika neno la tafakari ya leo tumejifunza kuwa kusubiria utayari au ukamilisho
ni chanzo cha ndoto nyingi kuchelewa kutekelezwa au kufa kabisa. Wale ambao
tunaona wamefanikiwa katika sekta mbalimbali za maisha kilichowafikisha huko ni
kuwa na uthubutu wa kuanza bila kujali hatua wanazoanzia. Anza kidogo bila
kupoteza picha pana iliyopo kichwani mwako. Kumbuka, mbegu ikidodoka ardhini ni
lazima iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu hii niliyodondosha kupitia
neno la tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi katika Maisha yako.
PS: Unaweza kujipatia maarifa kwenye elimu ya
pesa kupitia usomaji wa vitabu. Chagua nakala za uchambuzi wa vitabu unavyotaka
kwa kubofya kiunganisha hapo chini. Kila nakala ya uchambuzi wa kitabu
inapatikana kwa gharama ya Tshs. 3,999. Wahi mapema hii ni OFA ya leo.
BOFYA HAPA KUPATA ORODHA YA UCHAMBUZI WA VITABU
BORN TO WIN ~ DREAM BIG
Mwalimu
Augustine Mathias
Mawasiliano:
0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua
pepe: fikrazakitajiri@gmail.com