NENO LA LEO (JANUARI 12, 2021): HII NDIYO MIFEREJI YA PESA AMBAYO UNATAKIWA KUIWEKEA MKAZO
Habari
ya asubuhi rafiki yangu na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni matumaini yangu
kuwa kila mmoja wetu anaendelea vyema na majukumu yake bila kujali changamoto
za hapa na pale. Changamoto ni sehemu ya majukumu na changamoto hizo ndizo
zinatuimarisha katika yale tunayofanya. Wajibu wetu mkubwa ni kutoruhusu
changamoto hizo ziturudishe nyuma au kukubali kuacha yale ambayo tumedhamiria
kufanya kwa ajili ya kubadilisha maisha yetu.
Jiunge na kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI, kwa kujiunga utapata neno la tafakari kila siku pamoja na kujumuika na watu wenye mtazamo sawa, TAFADHALI JIUNGE SASA
Uhuru wa kifedha ni kilio cha kila mtu ambaye amedhamiria kuisha maisha yenye tija katika kipindi uhai wake. Hata hivyo, fedha haipatikani ikiwa haijawekewa njia ambazo huwa inapitia. Pesa ina njia zake na wale ambao wameweka njia hizo pesa huwa inakilimbilia kwao wakati wale ambao hawana njia hizo pesa inawakimbia. Huo ndiyo ukweli kuhusu upatikanaji wa pesa. Katika neno la tafakari ya leo tutaangalia baadhi ya njia/mifereji ya pesa ambayo unatakiwa kuwa nayo ili kujihakikishia maisha yenye uhuru wa kifedha. Karibu tupitie mifereji hiyo:-
Mfereji #1: Uwekezaji kwenye masoko ya mitaji. Huu ni aina ya mfereji ambao unawezesha pesa yako ikufanyie kazi
wakati wewe umelala. Zipo aina mbalimbali za uwekezaji wa mitaji lakini katika
mazingira yetu uwekezaji ambao umezoeleka ni:
a) Uwekezaji kwenye masoko ya hisa – Kama mwekezaji
unatakiwa kununua hisa za kampuni ambazo zimeorodheshwa kwenye Soko la Hisa. Kwa
Tanzania uwekezaji wa hisa unaratibiwa na Soko la Hisa la Dar es Salaam (Dar es
Salaam Stock Exchange). Kupitia uwekezaji huu unaweza kunufaika kupitia kupanda
kwa thamani ya hisa ikilinganishwa na kipindi unanunua hisa za kampuni
husika au kupitia gawio (divedend) kwa wanahisa ambalo huwa linategemea faida iliyotengenezwa
na kampuni husika katika kipindi husika.
b) Uwekezaji kwenye Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja (Mutual Fund Investments)
– Huu ni uwekezaji ambao kwa hapa kwetu unafahamika
kama uwekezaji kwenye vipande. Uwekezaji huu unaratibiwa na Serikali kupitia
Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja (UTT) ambayo ipo sita hadi sasa. Kila aina ya Mfuko
una taratibu zake za namna muwekezaji anavyofaidika kutokana na uwekezaji wake.
c) Uwekezaji kwenye Hatifungani/Dhamana za Serikali (Government Bonds) – Huu ni aina ya uwekezaji ambao unahusisha wawekezaji kuikopesha
Serikali kwenye vipindi tofauti vya uwekezaji. Hatifungani za serikali ni fursa
nzuri ya uwekezaji hasa kwa wale wanaohitaji kuwekeza fedha na kupata faida
bila kutumia nguvu nyingi au kuwa na wasiwasi juu ya usalama wa sehemu
wanakowekeza pesa zao. Fursa hii inagawanyika katika sehemu mbili ambazo ni:
Hatifungani/Dhamana za Muda Mfupi (Treasury Bills) na Hatifungani/Dhamana za
Muda Mrefu (Treasury Bonds).
d) Kuwekeza kwenye akaunti maalum za benki za biashara (fixed benki a/c) – Huu ni uwekezaji wa mtaji ambapo mwekezaji anapata faida kulingana na makubaliano au taratibu zilizowekwa kwenye aina ya akaunti au aina ya benki ambayo amewekeza pesa zake.
Mfereji #2: Kazi au biashara. Huu ni mfereji wa fedha ambao unatumiwa na watu wengi Duniani kote. Katika mfereji huu watu wanatengeneza kipato kupitia kazi walizoajiriwa au kupitia biashara. Biashara inaweza kuhusisha uwekezaji kwenye viwanda, kilimo na ufugaji, duka au mazao. Kwa ujumla mfereji huu unatumiwa na watu wengi kutokana na urahisi au usalama wa upatikanaji wa pesa bila kujali wingi au uchache wa pesa inayopatikana. Pia, kwa asili kila mtu ni mfanyabiashara bila kujali kiwango cha mtaji wake katika biashara anayofanya. Vivyo hivyo, wengi wanatumia mfereji wa kazi kama chanzo cha mapato kutokana na mazoea yaliyojengeka katika jamii. Mwanangu nenda shule soma kwa bidii ili upate kazi yenye malipo mazuri – ni kauli ambayo imezalisha watu wengi ambao wanategemea kazi kama mfereji wa mapato.
Mfereji #3: Uwekezaji kwenye ardhi na majengo (Real Estate Invesments). Huu ni uwekezaji mwingine ambao unahusisha utengenezaji wa faida kutoka kwenye kipande cha ardhi au majengo kupitia kodi za matumizi ya rasilimali hizo. Unaweza kuwa na ardhi ambayo ipo eneo zuri la kimkakati lakini hauna pesa za kujenga japo kuna watu wenye pesa ambao wapo tayari kujenga kwa makubaliano maalum ambayo mtaingia. Pia, kupitia uwekezaji wa nyumba za kupangisha unaweza kutengeneza kipato kupitia kodi za wapangaji.
Mfereji #4: Pato kutokana na maarifa au haki miliki (Intelectual property rights) – Hii ni aina nyingine ya mifereji ya kipato ambao unahusisha kuingiza pesa kutokana na maarifa uliyonayo au hatimiliki zilizotokana na matumizi ya akili yako. Mfano, unaweza kuwa unalipwa kutoka na ujuzi ulionao; mwanasheria nje ya pesa anayolipwa kama mshahara wake anaweza kuingiza pato kupitia ushauri wa kisheria. Vivyo hivyo, kwa fani nyingine ambazo zinahusisha utengenezaji wa kipato nje kazi waliyoajiriwa. Tukiachana na pato kutokana na fani yako, mfereji huu unahusisha pia upatikanaji wa pesa kutoka kwenye mauzo ya rasilimali au vifaa ambavyo unavimiliki. Mfano, unaweza kutengeneza kipato kupitia mauzo ya vitabu ulivyoandika au unaweza kutengeneza kipato kupitia mauzo kanuni ya uzalishaji wa bidhaa ambayo unaimiliki wewe. Mfano mwingine, Coca cola au pepsi wanatengeneza pesa nyingi kutoka kila kona ya Dunia kupitia formula ya utengenezaji wa Soda zenye ladha ya Coca au Pepsi.
Mfereji # 5: Uwekezaji kwenye mitandao. Huu ni mfereji mwingine ambao kwa sasa unashika kasi na matajiri wengi ambao wanaongoza kwa kutengeneza pesa nyingi ni wale ambao wanatumia teknolojia ya ukuaji wa mawasiliano. Fikiria kuhusu mmiliki wa Facebook, Instangram, WhatsApp, Twiter, Google. Fikiria kuhusu uuzaji wa bidhaa au maarifa kupitia mitandao. Jeff Bezos (Tajiri namba 2 Duniani) kupitia Amazon na Jack Ma (Tajiri namba moja nchini China) kupitia Alibaba ni miongoni mwa matajiri wakubwa ambao wamenufaika kupitia ukuaji wa teknolojia ya mawasiliano. Ni muda muafaka kila unachofanya kufikiria kitakuingiziaje pato zaidi kutokana na ukuaji wa teknolojia ya mawasiliano. Unaweza kutumia mitandao hii kutoa maarifa, kutangaza bidhaa zako na unaweza kutumia mitandao hii kama Duka sawa na maduka mengine.
Mwisho,
katika neno la tafakari ya leo tumejifunza mifereji mitano ya fedha katika Ulimwengu
wa sasa. Katika kipindi hiki cha mwaka 2021 ni wakati muhafaka wa kuongeza mifereji
ya kipato zaidi ili kujiweka salama kwenye maisha yenye uhuru wa kifedha. Kumbuka, mbegu ikidodoka ardhini ni lazima
iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu hii niliyodondosha kupitia neno la
tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi katika Maisha yako.
BORN TO WIN ~ DREAM BIG
Mwalimu Augustine Mathias
Mawasiliano: 0763 745 451/0786 881 155/0629
078 410
Barua pepe: fikrazakitajiri@gmail.com