JE UNAHITAJI MWAKA 2021 UWE WA TOFAUTI? MAMBO 10 KUZINGATIA.

NENO LA LEO (JANUARI 1, 2021): JE UNAHITAJI MWAKA 2021 UWE WA TOFAUTI? MAMBO 10 KUZINGATIA.

Habari ya asubuhi rafiki yangu mpendwa na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Hongera kwa kumaliza mwaka na kuunza mwaka ukiwa salama, hakika kwa wema wake Mungu tumehitimisha siku 365 na sasa tuna kibarua cha kuendeleza moto katika siku 365 zilizopo mbele yetu. Kila mwaka huwa unakuwa na matukio tofauti na matukio hayo huwa ndiyo yanauwafanya mwaka uonekane ulikuwa bora au mchungu kwa watu binafsi, jamii au taifa kwa ujumla wake. Mwaka 2020 kwa ujumla wake ulikuwa na matukio ya huzuni na majionzi zaidi kwa taifa na Dunia kutokana na kupoteza idadi kubwa ya watu waliopoteza maisha kwa ugonjwa wa virusi vya Corona.

Soma: ONDOKA 2020 LAKINI UMENIACHIA SOMO KUBWA KATIKA MAISHA YANGU.

Kama taifa tumeshuhudia huzuni kubwa ikitawala kutokana na kumpoteza Mhe. Benjamini Willium Mkapa ambaye alikuwa ni nguzo imara katika historia ya uongozi na mapinduzi ya uchumi wa nchi yetu. wakati mwingi Ni mwaka ambao ulitawaliwa na matukio ya majonzi katika kila kona ya Dunia. Hata hivyo, pamoja na yote hayo tuna kila sababu ya kusema ee Mungu umekuwa mwemwa kwangu katika kipindi hiki chote cha mwaka 2020 hivyo naomba wema wako uwe nuru ya kuniongoza katika kipindi chote cha mwaka 2021. Pia, itakumbukwa kuwa mwaka 2020 kama taifa ulikuwa ni mwaka wa uchaguzi ambao kawaida huwa unaambatana na matukio mengi katika kila kona nchi. Matukio yote haya yaliufanya mwaka uonekane kuwa mrefu zaidi ikilinganishwa na miaka mingine ambayo haikuwa na misukosuko mingi kiasi hiki. Pamoja na yote hayo, wewe na mimi na taifa zima la Tanzania tusiposema asante kwa Muumba tutakuwa hatuna fadhira.

Karibu katika Makala maalumu ya siku ya leo ambapo nitakushirikisha mambo kumi ya kuzingatia ili kipindi chote cha mwaka 2021 kiwe na mafanikio ya kila aina kwa kadri ya mahitaji yako kwenye kila sekta ya maisha yako. Naamini na wewe ni miongoni au umewahi katika kundi la watu ambao kila mwanzo wa mwaka huwa wanakuwa na kauli nyingi za kuonesha kuwa mwaka ujao utakuwa wa tofauti lakini mwishowe wanajikuta katika hali ile ile. Leo hii ukizunguka mitaani au kwenye kurasa za mitandao ya kijamii utasikia au kuona kauli nyingi kama vile: “mwaka mpya na mambo mapya, huu ni mwaka mabadiliko, mwaka wa urejesho, mwaka wa upendo,” na kauli nyingine nyingi.

Hata hivyo, kauli hizo huwa zinayeyuka taratibu kadri siku na miezi inavyosogea na mwisho wake watu wanajikuta kwenye sehemu au tabia zile zile ambazo mwanzoni mwa mwaka waliweka mikakati ya kuachana nazo. Huo ndiyo ukweli kwa asilimia kubwa ya watu katika jamii kwa maana wanaishi katika tabia ambazo hawaridhishwi nazo.

Je mwaka 2021 nifanye nini ili mwaka huu uwe wa tofauti katika historia ya maisha yangu?

Ushauri #1: Je umeweka vipaumbele kwa mwaka 2021? Kinachogharimu watu wengi wasifikie malengo kama wanavyodhamiria mwanzoni mwa mwaka ni kutokuwa na vipaumbele. Wengi hawana mpango unaowaongoza n ahata kama wana mpango hawazingatii mpango huo na matokeo yake ni kujihusisha na kila linalokuja mbele yao. Katika hali kama hiyo wanajikuta wameshindwa kufanikiwa katika mambo mengi na mwisho wake ni kukata tamaa. Anza kwa kujiuliza nahitaji nini katika kipindi hiki cha mwaka 2021.

Ushauri #2: Je tayari una bajeti yam waka 2021? Bajeti ni dira ya kukuongoza kwenye vipaumbele vyako. Bajeti ni mwongozo unaokuwezesha vipaumbele vyako viendane na mapato yako. Zaidi ya yote kupitia bajeti unajipima na kugundua sehemu zipi unatakiwa kupambana ili kuongeza kipato zaidi kwa ajili ya kutosheleza mahitaji yako. Vile vile, kupitia bajeti utaweza kudhibiti matumizi ya pesa zako. Hapa ndipo wengi wanaanguka mapema, kwa kutokuwa na bajeti kila pesa wanayopata inaelekezwa katika matumizi ambayo hayakuwa sehemu ya malengo na mwisho wake ni kutofanikisha yale waliyokusudia.

Ushauri #3: Badili mtazamo wako. Maisha ni sasa kwa ajili ya maisha ya kesho. Ikiwa miaka iliyopita umekuwa mtu wa kutofanikiwa kuanzia sasa jisemee kuwa huu ni mwaka wa tofauti na kipekee kwangu kuvunja minyororo ya kutokufanikiwa. Jione ukiwa mtu mpya katika mwaka mpya, historia mpya na uwezo mpya. Unahitaji kuwa mtu wa mtazamo chanya katika kila hali iliyopo mbele yako. Jione wewe ni mtu wa kufanikiwa, jione wewe ni mtu wa kupendwa zaidi, jione wewe ni mtu wa kutoa upendo kwa wengi na zaidi ya yote jione ukikamilisha malengo yote ambayo umejiwekea.

Ushauri #4: Kubali kuanza upya kama kila ulichonacho kipo kinyume na malengo yako. Ili ufanikiwe zipo sehemu ambazo unalazimika kujikana kwa ajili ya kupata hitaji la msingi. Kuna mazingira unapaswa ya kuyakimbia kwa ajili ya kupata changamoto mpya. Kuna kundi la marafiki au ndugu unatakiwa kujiweka mbali nao ili kupata nafasi ya kutafakari upya. Kuna tabia ambazo zinaenda kinyume na mahitaji yako hauna budi kuzitupilia mbali. Na mengine mengi ambayo hayana tija katika mwelekeo mpya wa mwaka huu.

Ushauri #5: Kuwa mtu wa vitendo. Vitendo bila kujali ukubwa (intensinty) wa vitendo hivyo ni njia pekee ambayo itaufanya mwaka huu uwe wa tofauti. Mwanzoni mwa mwaka unakuwa mtu wa matamanio (wishes) na njia pekee ya kubadilisha matamanio hayo ni vitendo. Katika kila lengo ambalo umejiwekea kutokana na matamanio yako una wajibika kuweka mikakati au shughuli ya kutekeleza lengo husika. Hapa ndipo unatakiwa kujikana! hapa ndipo unatakiwa kujiumiza! hapa ndipo unatakiwa kujinyima! hapa ndipo unatakiwa kujitoa sadaka! Hapa ndipo unatakiwa kuongeza maarifa mapya! Hapa ndipo unatakiwa kupunguza masaa ya kuwa kwenye kitanda chako!

Ushauri #6: Kuwa tayari kujiamini na kuamini njia unazotumia. Kelele zitakuwa nyingi katika kipindi hiki ambacho unatamani kuona mwaka 2021 unakuwa wenye mafanikio. Kelele hizo zitatoka kwa watu wako wa karibu ambao wengi wamezoea kukuona katika maisha ya zamani na sasa wanatamani maisha hayo yaendelee. Ni lazima ufahamu mapema kuwa siyo wote wataelewa dhamira yako. Upinzani wa mtazamo wako mpya unaweza kuanzia ndani ya familia yako, marafiki au ndugu kutokana na ukweli kwamba katika maisha mapya kuna mambo mengi waliyozoea awali na sasa hawatayapata tena. Simama imara songa mbele, husikubali kuchanganywa na miruzi mingi njiani.

Ushauri #7: Tafuta washauri katika yale unayofanya. Hakuna jipya chini ya jua, lolote unalofanya tayari kuna watangulizi wako ambao wameshawahi kufanya hayo tena kwa mafanikio. Pale ambao unaona mambo yanakuwa magumu na unahitaji kupata mwongozo mpya hakikisha unatafuta washauri wa kukushika mkono. Na pale inanapobidi kuwa tayari kulipia ushauri au mafunzo hayo kwa ajili ya kupata maarifa mapya katika changamoto iliyopo mbele yako.

Ushauri #8: Weka akiba au jilipe kwanza. Njia pekee ya kufanikiwa kifedha ni kuhakikisha unakuwa na akiba kwa ajili ya dharura na maendeleo ya siku zijazo. Kama ulizoea kila shilingi inayoingia mikononi mwako, wakati ni sasa wa kuanza kutenga asilimia flani pato lako kwa ajili ya siku za baadae. Kuna fursa nyingi ambazo zimekuwa zikikupita kutokana na kutokuwa na akiba. Husidharau kiasi kidogo cha pesa unachowekeza ikiwa kiasi hicho kinawekezwa kwa kufuata misingi ambayo umejiwekea. Mfano, fikiria kama siku unaweka Tshs. 1,000 kwa mwaka ni zaidi ya laki tatu na ikiwa kila siku unaweza Tshs. 5,000 kwa mwaka ni zaidi ya milioni moja na nusu. Maamuzi yapo mkononi mwako kulingana na kipato ulichonacho.

Ushauri #9: Jiongezee maarifa. Kila siku hakikisha unakuwa na muda wa kusoma kitu ambacho kitachochea hali au morali ya kusonga mbele. Kumbuka nimetangulia kukuambia kuwa unatakiwa kuwa na mtazamo chanya katika kila hali. Hauwezi kuwa na mtazamo chanya kama hauna utaratibu wa kujisomea maarifa mapya kupitia Makala mbalimbali, vitabu vya mafanikio au kuwa kwenye makundi yenye mafunzo maalum. Katika mipango unayojiwekea hakikisha unaweza na idida ya vitabu ambavyo unatakiwa kusoma mwaka huu pamoja na idadi ya semina ambazo unatakiwa kushiriki.

Ushauri #10: Husipambane peke yako. Binadamu ni viumbe ambao tunaishi katika makundi ya kijamii. Kama una familia hakikisha wanakuwa washirika wako wa karibu katika yale ambayo unafanya. Hata hivyo, unatakiwa kuhakikisha unajenga mtazamo wao ili wote muwe na fikra zinazofanana. Mshirikishe mwenza wako, washirikishe watoto au mshirikishe rafiki wa karibu sana.

Mwisho, katika Makala hii nimekushirikisha mambo 10 ya kuzingatia kwa ajili ya kuwa na mwaka 2021 wenye mafanikio. Lakini katika yote nakukumbusha umuhimu wa kumtanguliza Mungu ili yote unayofanya yawe na kibali mbele ya macho yake. Namalizia kwa kukutakia kila lenye heri katika mwaka mpya 2021. Kumbuka, mbegu ikidodoka ardhini ni lazima iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu hii niliyodondosha kupitia neno la tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi katika Maisha yako.

 

BORN TO WIN ~ DREAM BIG

Mwalimu Augustine Mathias

Mawasiliano: 0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410

Barua pepe: fikrazakitajiri@gmail.com

 


onclick='window.open(