ONDOKA 2020 LAKINI UMENIACHIA SOMO KUBWA KATIKA MAISHA YANGU.

Habari ya asubuhi rafiki yangu mpendwa na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Hongera kwa kila mmoja wetu kufanikiwa kufikia wakati kama huu ambao tumebakiza masaa machache kuhitimisha mwaka 2020 na kuunza mwaka mpaya 2021. Hakika tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kutokana na jinsi ambavyo mwaka huu ulikuwa na matukio mengi ambayo mengi yalikatisha tamaa kwa mtu mmoja mmoja au jamii kwa ujumla. Ni mwaka ambao ulitawaliwa na matukio ya majonzi katika kila kona ya Dunia. Hata hivyo, pamoja na yote hayo tuna kila sababu ya kusema ee Mungu umekuwa mwemwa kwangu katika kipindi hiki chote cha mwaka 2020 hivyo naomba wema wako uwe nuru ya kuniongoza katika kipindi chote cha mwaka 2021.

Karibu katika Makala maalumu ya siku ya leo ambapo nitakushirikisha namna ambavyo mwaka 2020 umeniachia somo kubwa la kujifunza katika kipindi chote cha maisha yangu. Katika kipindi hiki hasa katika wakati ambao Dunia ilikuwa imetawaliwa na changamoto ya COVID 19 nimejifunza kuwa HOFU ni moja ya hisia ambazo zinatawala maisha ya mwanadamu. Kupitia hisia hii mwanadamu amekuwa akijikadiria chini ya uwezo wake halisi na hivyo yapo mengi ambayo ameshindwa kuyatekeleza kwa kutawaliwa na hisia ya hofu.

Soma: [CHUKUA HATUA] HOFU NI ADUI NAMBA MOJA KATIKA SAFARI YAKO YA MAFANIKIO

Ni katika kipindi cha mwaka 2020 Tanzania imeishangaza Dunia nzima kwa jinsi ambavyo ilikabiliana na ugonjwa wa COVID 19. Mataifa yote yanayozunguka taifa letu yalionesha wazi kuwa Tanzania kama taifa tumeweka mzaa katika kukabiliana na ugonjwa huu hatari. Hata hivyo, pamoja na kusakamwa kila kona lakini Viongozi katika ngazi mbalimbali walisimamia misingi ambayo waliamini ni sahihi katika kupambana na ugonjwa wa COVID. Ni kupitia msimamo huo, taifa limeweza kupambana na ugonjwa wa COVID huku ukiendelea na mfumo wa maisha kama kawaida.

Kama taifa katika kila kona, ushindi dhidi COVID 19 ulipatikana mara baada ya hotuba ya Mhe. Rais John Pombe Magufuli pale alipolihutubia wananchi wa taifa hili na kuwaaminisha kuwa ugonjwa wa Corona ni ugonjwa sawa yalivyo magonjwa mengine. Hapa nanukuu sehemu ya hotuba ambayo aliitoa tarehe 22 Aprili, 2020: “Tuwaondoe hofu wananchi, sio ugonjwa huu pekee unaosababisha vifo kwa wananchi, na sio kila anayepoteza maisha hivi sasa basi amekufa kwa Corona, COVID-19”.  Pia, katika hotuba yake alikataa kata kata kuweka “lock down” kwa nchi nzima au kulifunga jiji la Dar es Salaam kwa kigezo cha ugonjwa wa Corona kwani ilikuwa wazi kuwa kwa kufanya hivyo inafahamika kabisa kuwa jiji hilo ni kitovu cha uchumi wa taifa hili. Huu ulikuwa ni ushindi wa kwanza katika kupambana na ugonjwa huu hatari kutokana na ukweli kwamba hofu dhidi ya ugonjwa huu ilikuwa inasambaa na kuhatarisha maisha ya watu kuliko ugonjwa wenyewe.

Yapo mengi ya kujifunza kutokana na msimamo huu Tanzania katika kukabiliana na ugonjwa wa Corona na hapa nitakushirikisha machache tu:-

Somo #1: Ni muhimu kumtanguliza Mungu katika kila jambo. Wakati Tanzania ilipotangaza siku tatu kwa ajili ya kufunga na kuomba Mungu kuliepusha taifa dhidi ya janga la virusi vya Corona pamoja na kutofunga sehemu za ibada, wengi waliona ni mzaa sawa na kuchezesha shilingi kwenye tundu la choo. Taratibu tulianza kushuhudia hata mataifa mengine yakifuata nyayo hizo hizo kwa ajili ya kujinyenyekeza na kuomba ili kuepushwa na janga hilo hatari. Somo la kujifunza: katika kila hali mtangulize Mungu hata katika nyakati ambazo kila mmoja anashangaa mbinu unazotumia.

Somo #2: Ishinde hofu pale ambapo maisha yako yamezungukwa na giza. Kupitia ugonjwa wa virusi vya Corona nimejifunza kuwa yapo mambo mengi ambayo tumeshindwa kutekeleza katika maisha yetu kutokana na kuendekeza hofu. Binafsi nilikuwa miongoni mwa watu ambao walihofia ugonjwa wa Corona kiasi cha kuanza kuogopa kuwa karibu na watu niliozoeana nao awali. Baada ya hotuba ya Mhe. Rais kuhusiana na umuhimu kuondoa hofu na kuwa tayari kuishi na virusi vya Corona kama ilivyo kwa magonjwa mengine nilijikuta katika hali ya kujiamini. Hali hiyo ilitokana na tumaini jipya dhidi ya ugonjwa huu hatari. Taratibu shughuli zote zilirejea kama kawaida huku majirani zetu katika mataifa mengine yakisubiria maiti za watu kuanza kutapakaa mitaani. Somo la kujifunza: kila mara pambana kuishinda hofu katika kila unalofanya kwenye maisha.  

Somo #3: Kama unahitaji kuwa kiongozi shupavu ni lazima ujifunze kusimamia misimamo yako. Kiongozi unatakiwa kuwa na fikra na maono pana zaidi ikilinganishwa na wafuasi wako. Hata katika nyakati ambazo kila mmoja anapinga njia unazotumia unatakiwa kuziba masikio na kusonga mbele. Wengi wataongea mengi kuhusiana na msimamo wako lakini husipokubali kurudi nyuma utafika wakati ambao wapinzani wako watakuelewa na wote mtaongea lugha moja. Hili lipo wazi kwa jinsi ambavyo Mhe. Rais alipingwa na watu wa kila aina ndani na nje ya nchi lakini mwisho wake wote walielewa msimamo wake na wengine wakaanza kuigiza mbinu zake pamoja na kwamba mwanzoni walizipinga. Somo la kujifunza: ikiwa unahitaji kuwa kiongozi shupavu ni lazima ujifunze kusimamia mawazo ambayo unaamini ni sahihi kwa maslahi mapana ya kundi unaloongoza.

Mwisho, ondoka mwaka 2020 lakini umenifundisha kutoendekeza hisia za hofu katika kila ninalofanya kwenye maisha yangu. Mwaka umeisha na naamini kuwa nitakuwa na mwaka mpya wenye mafanikio zaidi ya niliyofanikisha katika kipindi hiki matukio mengi yalitufanya tuone mwaka umekuwa mchungu. Karibu mwaka 2021 ili kwa pamoja tuendelee kuwa kama familia moja ya FIKRA ZA KITAJIRI. Kumbuka, mbegu ikidodoka ardhini ni lazima iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu hii niliyodondosha kupitia neno la tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi katika Maisha yako.

Nakutakia kila la kheri katika kipindi chote cha mwaka 2021.

 BORN TO WIN ~ DREAM BIG

Mwalimu Augustine Mathias

Mawasiliano: 0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410

Barua pepe: fikrazakitajiri@gmail.com 

onclick='window.open(