Uchambuzi wa Kitabu cha How to Stop Worrying and Start Living: Jinsi ya kuepuka hofu katika maisha.


Habari rafiki yangu ambaye umeendelea kuamini kazi yangu ya uchambuzi wa vitabu kupitia mtandao wa FIKRA ZA KITAJIRI. Karibu katika uchambuzi wa kitabu cha leo ambacho ni 4 kati ya vitabu 30 ambavyo nimejiwekea lengo kuvisoma katika kipindi cha mwaka huu 2020. 

Kama bado hujajiunga na kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya kupata neno la tafakari kila siku pamoja na kujumuika na watu wenye mtazamo sawa, tafadhali fanya hivyo KWA KUBONYEZA HAPA na kujiunga na kundi letu. Nafasi ni chache hivyo fanya maamuzi ya kujiunga sasa.

Kama bado hujajiunga na kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya kupata neno la tafakari kila siku pamoja na kujumuika na watu wenye mtazamo sawa, tafadhali fanya hivyo KWA KUBONYEZA HAPA na kujiunga na kundi letu. Nafasi ni chache hivyo fanya maamuzi ya kujiunga sasa.

Kitabu ninachokushirikisha kupitia makala hii ni How to Stop Worrying and Start Living” kutoka kwa mwandishi Dale Carnegie. Mwandishi huyu ni kati ya wahamasishaji waliowahi kuishi katika kipindi cha maisha yao. Ni kutokana na kazi zake pamoja na kwamba alitangulia mbele za haki kipindi kirefu kilichopita (1955) lakini kazi zake bado zinaishi. Kwa Wenzetu wana msemo wa kuelezea mtu wa aina hii kwa sentensi hii “He is dead alive (amekufa lakini anaishi)”. Katika enzi za uhai wake Dale Carnegie alikuwa ni mkufunzi binafsi kwenye masuala ya maendeleo ya nafsi (self improvement), mauzo katika biashara, mafanikio ya kampuni na mbinu za kuongea mbele ya umaa (public speking skills). Amefanikiwa kuandika vitabu mbalimbali kama vile How to Win Friends and Influence People (1936) na Lincoln the Unknown (1932) na vingine vingi.

Kupitia kitabu hiki mwandishi anatushirikisha namna alivyokuwa akiishi maisha ya hofu zilizotokana na mahitaji makubwa ya pesa ikilinganishwa na kipato cha kazi yake. Pamoja na kwamba enzi za masomo yake alikuwa na ndoto kubwa sana ya kufanikiwa kimaisha alijikuta kwenye wakati mgumu wa kutimiza ndoto hiyo kutokana na ugumu wa maisha mwanzoni mwa ajira yake ya kwanza.

Hali hiyo ilipelekea kuanza kutafuta ajira nyingine ambayo alihisi kuwa itamuodolea dhiki ya maisha aliyokuwa nayo kwa wakati huo. Kama kawaida katika kipindi kama hicho huwa kinaambatana na kukataliwa sambamba na kukatishwa tamaa, lakini kwake ilikuwa tofauti. Kukataliwa kwake katika Vyuo vingi ambavyo alikusudia kupata ajira ili afundishe kozi za jioni ilimfanya aanzinshe taasisi yake ya Y.M.C.A ambayo ilimwezesha kuanza kuishi kusudi la maisha yake.

Karibu ushirikiane nami kujifunza machache kati ya mengi ambayo tunashirikishwa katika kitabu hiki:

SEHEMU YA KWANZA: UKWELI HALISI UNAOPASWA KUHUSU HOFU

1. Chanzo cha hofu ni kushindwa kutambua umuhimu wa kuishi kulingana na hali ya wakati husika. Kinachosababisha maisha ya hofu kwa watu wengi ni kuendelea kuishi kwenye athari ya yaliyopita pamoja na uoga wa maisha yajayo. Mwandishi anatushirikisha kuwa Jana amekufa hivyo hana nafasi katika maisha yako ya sasa na Kesho hajazaliwa hivyo hakuna maana ya kuwa na hofu juu yake. Maisha ni sasa, akili yako yote inatakiwa kujikita kwenye matukio ya wakati husika. Hata hivyo, tafsiri sahihi ya maneno hayo siyo kwamba mtu hatakiwi kujiandaa kwa ajili ya maisha ya baadae la hasha. Maisha ya kesho yanaandaliwa kutokana na kutimiza majukumu yako ya leo kwa ukamilifu. Hivyo, badala ya kuhofia kuhusu maisha yajayo unatakiwa kujiuliza ni majukumu yapi ambayo ni lazima yatimizwe kwa wakati husika na kwa ukamilifu wa hali ya juu.

2. Kesho iliyo bora inaandaliwa kutokana na matendo ya leo. Kumbe, badala ya kuhofia kuhusu kesho unachotakiwa ni kuweka maandalizi bora kupitia majukumu yako ya sasa kwa ajili ya kesho. Mwandishi anatushirikisha kuwa matokeo bora katika kesho ni zao la mpangilio wa majukumu yako ya kila siku. Unatakiwa kuwa na ratiba inayokuongoza juu ya kipi kifanyike kwanza na kipi kifuatie. Hapa ndipo watu wengi huwa tunashindwa kwa vile tunachanganya majukumu ya siku bila kuwa na mpangilio, matokeo yake siku inaisha bila kupata matokeo tarajiwa. Hali hii inapelekea kuianza siku mpya kwa presha ya majukumu ambayo hayakukamilishwa siku iliyoisha Jana. Hapa unatakiwa kutambua kuwa kila siku ni siku mpya kwa mtu mwenye hekima. Hivyo, timiza wajibu wako sasa bila kujali yaliyopita wala kuogopeshwa na yajayo. Pia, kila mara furahia maisha kupitia yale ambayo yapo ndani ya uwezo wako badala ya kuhairisha furaha kwa kusubiria kupata vitu/hali ambayo kwa sasa ipo nje ya uwezo wako. “Hii ndio siku aliyoifanya Bwana tufurahi na kushangalia ndani yake….”

3. Hofu inapofusha uwezo akili katika kutafuta mbadala wa hali au tukio unalohofia. Mwandishi anatushirikisha kuwa kadri unavyoishi kwenye hofu ndivyo akili yako inashindwa kutafuta mbadala ambao ungewezesha kuepukana na hofu husika. Tunapoishi kwa wasiwasi akili yetu inashindwa kutulia kwani inakuwa inaruka ruka kwenye jambo moja hadi jingine bila kukamilisha hata moja. Njia rahisi ya kukabiliana na hofu ni kupitia kanuni ya Dr. Willis H. Carrier ambayo inahusisha hatua tatu zifuatazo:-
ü  Hatua ya kwanza Fanya tathimini inayolenga kugundua matokeo mabaya yanayoweza kupatikana katika maisha yako kama athari ya hali/tukio unalohofia. Mfano, kama umetenda jambo ambalo ni kinyume na misingi ya kazi zako – athari iliyopo mbele inaweza kuwa kufukuzwa kazi ambako kunaweza ambatana na kufungwa endapo umeajiriwa. Vivyo hivyo, kama ni mfanyabiashara kosa moja katika misingi yako ya biashara linaweza kupelekea kufilisika au kupoteza sehemu ya mtaji wako.
ü  Hatua ya pili – Kuwa tayari kukabiliana na matokeo ya aina yoyote katika tukio/hali unayohofia kulingana na tathimini uliyofanya katika hatua ya kwanza. Kama ni kufukuzwa kazi au kupoteza mtaji jione katika maisha hayo mapya. Kuwa na hali chanya kuhusiana na maisha hayo mapya. Mfano, endapo nitafukuzwa kazi bado nina uwezo wa kupata kazi nyingine na maisha yakaendelea. Kama ni kufungwa bado nitakuwa na maisha na huko gerezani yapo mengi ambayo nitafanya kwa ajili ya kuongeza thamani ya maisha yangu.
ü  Hatua ya tatu – Kila mara tafuta njia mbadala za kukuwezesha kuishi kwa mafanikio katika ile hali ambayo tayari umekubaliana nayo katika mfumo wa akili yako. Mfano, kama ni hasara katika biashara fikiria mbinu mbadala za kukuwezesha kupunguza hasara husika. Hatua hizi tatu kwa pamoja zitakufanya uwe na tumaini jipya na hivyo kuondokana hofu.

4. Moja ya athari hasi inayotokana na hofu ni kufa kabla ya muda wako. Hofu inasababisha kuongezeka kwa magonjwa ndani ya mhusika hivyo kusababisha uwezekano wa kufa kabla ya muda wake. Hali hii inatokana na uoga ambao husababisha kiwango cha hofu kuongezeka hali inayopelekea kuongezeka kwa magonjwa yanayosababishwa na msongo wa hofu au wasiwasi. Mfano, tafiti zinaonesha kuwa magonjwa ya vidonda vya tumbo yanasababishwa kwa kiwango kikubwa na msongo wa hofu za upatikanaji wa mahitaji muhimu katika maisha. Tafiti hizo pia zinaonesha kuwa hofu, wasiwasi, chuki, ubinafsi uliopitiliza na kushindwa kudhibiti hisia za matamanio ya mwili kulingana na uhalisia/uwezo katika maisha ni chanzo kikuu cha magonjwa ya aina mbalimbali kwa watu wengi.

5. Kutokana na msongo wa hofu watu wengi wanaumwa ugonjwa wa akili japo hawajatambua kuwa ni waathirika. Mwanafalsafa Plato aliwahi kusema “tatizo kubwa linalofanywa na Wanafizikia (Wataalamu wa Tiba) ni kujaribu kutibu mwili bila kuweka jitihada za kutibu akili”. Tafsiri yake ni kwamba magonjwa mengi ya mwili yanasababishwa na msongo wa akili hila hakuna tiba inayotolewa kwa ajili ya kutibu chanzo hicho cha magonjwa. Tatizo hili la ugonjwa wa akili chanzo chake ni hofu na wasiwasi katika maisha ya watu walio wengi katika jamii.

SEHEMU YA PILI: MBINU ZA MSINGI ZA KUITATHIMINI HOFU YAKO

6. Zoezi la kutathimini hofu iliyopo mbele yako linahusisha hatua tatu muhimu ambazo zilifundishwa na kutumiwa na mwanafalsafa nguli Aristotle katika maisha yake. Kupitia kitabu hiki mwandishi anatushirikisha kuwa kanuni hiyo ya Aristotle inaweza kutumiwa na mtu yeyote kwa ajili ya kupata tiba ya hofu iliyopo mbele yake. Kanuni hii inahusisha:-
ü  Kupata ukweli/taarifa kuhusiana na hofu husika – Hatua hii inalenga kupata taarifa au maarifa sahihi kuhusiana hofu inayokukabili. Bila kuwa na taarifa/maarifa sahihi siyo rahisi kuepukana na hofu na badala yake utajikuta umechanganyikiwa zaidi. Ushauri ni kwamba pindi unapotafuta ukweli/taarifa kuhusiana na tatizo lililopo mbele yako unatakiwa kuweka mbali hisia na mtazamo wako ili taarifa utakazopata ziwe haziegemei upande wako.
ü  Chambua ukweli/taarifa husika Baada ya kupata taarifa/maarifa kuhusiana na hofu iliyopo mbele sasa unatakiwa kuandika taarifa hizo kwenye kipande cha karatasi au kwenye kompyuta. Hatua ya kwanza ni kuelezea vizuri hofu inayokukabili hatimaye kuhusianisha hofu hiyo na taarifa/maarifa ambayo umepata. Hapa unatakiwa kujiuliza maswali mawili na kuorodhesha majibu yake pamoja na athari zitakazojitokeza kwa kila hatua ambayo utachukua. Swali la kwanza, jiulize kwa nini unahisi hofu? Ainisha sababu inayopelekea kuwa na hofu kwa wakati huo. Swali la pili, jiulize je naweza kufanya nini kwa ajili ya kuepukana hofu hii?. Ainisha njia mbadala zote zilizopo pamoja na athari zake.
ü  Fanya maamuzi na kuchukua hatua stahiki juu ya maamuzi yako – Baada ya kujiridhisha juu ya mbadala ambao una faida nyingi ukilinganisha na njia zote ulizoainisha sasa unatakiwa kutekeleza kwa vitendo. Katika hatua hii unatakiwa kuchukua hatua mara moja bila kusita au kuhairisha kwa kuhofia matokeo ya matendo yako.

7. Unaweza kupunguza asilimia 50 ya hofu zinazohusiana na biashara au kazi kwa kutumia muujiza uliopo katika kujibu maswali haya manne. Swali la kwanza – Jiulize je tatizo ni lipi? Eleza tatizo linalopelekea uwe na hofu/wasiwasi kuhusiana na mwenendo wa biashara/kazi yako; Swali la pili – Jiulize je ni kipi chanzo cha tatizo? Ainisha sababu zinazopelekea mwenendo wa biashara/kazi ambao umepelekea uwe na hofu; Swali la tatu – Jiulize njia zipi zilizopo ambazo ni suluhisho la tatizo husika. Ainisha njia zote mbadala ambazo zinaweza kutumika kutibu tatizo linalopelekea uwe na hofu; na Swali la nne – Jiulize ni njia ipi ambayo ni bora kati ya njia mbadala zilizoainishwa. Mbinu hii inaweza kutumika kwa ajili ya kutatua changamoto yoyote inayopelekea uwe na hofu katika maisha yako ya kila siku.

SEHEMU YA TATU: JINSI YA KUEPUKANA NA HOFU KABLA HAIJAWA NA MADHARA KWAKO.

8. Hakikisha una ratiba inayokubana kila siku kwa ajili ya kukamilisha majukumu ya siku husika. Wanasaikolojia wanakubaliana kwenye Sheria inayosema kuwa “akili ya mwanadamu haiwezi kuwaza zaidi ya suala moja ndani ya muda huo huo”. Tafsiri yake ni kwamba kadri unayokuwa bize na majukumu ya siku, akili yako inakosa muda wa kuwaza hisia mbaya katika Maisha. Majukumu ni tiba tosha zidi ya hofu inayokusumbua katika Maisha, iwe hofu au huzuni ukitumia muda wako vizuri katika kukamilisha kazi zinazokubana utajikuta umesahau hisia hizo. Tumezoea msemo kuwa “kukaa bila kazi ni dhambi” – tafsiri halisi ni kwamba katika muda ambao hauna kazi ndipo shetani nae anapata muda wa kukujaribu.

9. Hofu ya vitu vidogo vidogo inasababisha madhara makubwa katika maisha. Mwandishi anatushirikisha kuwa hofu ya vitu vidodo katika Maisha inapelekea matatizo makubwa kwa wahusika katika jamii. Mfano, familia nyingi zinavunjika kutokana na hofu katika ya wanafamilia. Kuna hisia ambazo tunazipa nafasi ndani ya akili yetu kiasi kwamba zinapelekea matatizo yaongezeke kuliko ambavyo tungejifunza kupotezea baadhi ya hisia ambazo hazina umuhimu. Maisha ni mafupi hivyo hakuna sababu ya kubeba hisia ambazo hatupotezi chochote pale tunapoamua kuzipotezea na kuendelea na Maisha kama kawaida.

10. Tumia sheria ya wastani kwa ajili ya kukabiliana na hofu inayokukabili: Sheria ya wastani inasema kuwa “uwezekano wa tukio au hali flani kutokea ni kupitia takwimu za utokeaji wa tukio au hali husika katika kipindi kilichopita”. Mara zote jiulize kuna uwezekano kiasi wa yale unayohofia kwenye Maisha yetu yana nafasi kiasi gani ya kujidhihirisha katika uhalisia wake. Ukweli ni kwamba Maisha yetu yanatawaliwa na hofu juu ya matukio au hali ambazo kiukweli huwa ni nadra sana kujitokeza. Matukio au hali ambazo tunahofia katika Maisha yetu hata pengine hazijawahi kututokea katika Maisha yetu. Mfano, katika kipindi cha ukame tunahofia kukosa chakula na hivyo kufa njaa; ukweli ni kwamba huwa nyakati hizo zinapita na tunaendelea na Maisha kama kawaida. Mtu anahofia kukosa mahitaji muhimu kutokana na kufukuzwa kazi au biashara kuyumba lakini pamoja na matatizo yote hayo nyakati kama hizo huwa zinapita na Maisha yanaendelea kama kawaida.

11. Kubaliana na hali au tukio ambalo lipo nje ya uwezo wako. Kuna matukio au hali ambazo pengine zinapelekea tunakuwa walemavu baada ya kupoteza baadhi ya viungo vya mwili; pengine magonjwa yanaweza kukufanya husiwe na mwonekano wako wa awali; kuna matukio au hali zinazotusababishia hasara labda kutokana na majanga ya kimazingira au kuna kipindi tunapoteza wapendwa wetu kutokana na kifo au kuwa katika hali ambayo watu wa muhimu katika Maisha yetu wametukimbia kutokana na tamaa au sababu mbalimbali. Uchaguzi wa maamuzi sahihi katika nyakati kama hizo ni kukubaliana na hali au matukio hayo tayari yametokea na hatuna nafasi ya kuyazuia au kurudi katika hali ya awali. Hakuna sababu ya kuendelea kuishi Maisha ya hofu, hasira, kilio, huzuni, uchungu au chuki kutokana na matukio au hali ambazo zipo nje ya uwezo wetu wa kuzuia au kurudi katika hali ya zamani. Ufalme wa mbinguni upo ndani mwetu na ndivyo ilivyo uovu pia upo ndani mwetu. Upande upi unaamua kujikita ndiyo utaimarisha au kuharibu Maisha yako. Kumbe tunatakiwa kufurahi katika kila hali au tukio linalotokea katika Maisha yetu. Kwa ujumla, mara zote tunatakiwa kuwa upande chanya kwenye changamoto zinazojitokeza katika Maisha yetu ya kila siku.

12. Jiwekee kiwango cha ukomo kwenye kila hisia hatarishi katika Maisha yako. Hisia za hasira, huzuni, majuto, kilio au chuki unatakiwa kujiwekea kiwango cha ukomo wa uvumilivu (level of torelance). Hali hii itakuwezesha kukabiliana na hofu za Maisha bila kukuathiri sana. Jiulize je hali au tukio linalohofia lina faida gani katika Maisha yangu? Jiulize je ni kiwango nipo tayari kuvumilia hofu hii kabla ya kuipotezea ili Maisha yaendelee. Mwisho, jiulize ni gharama kiasi gani upo tayari kuzibeba kutokana na hofu inayokukabili?

13. Husipoteze muda kubadilisha matukio yaliyopita maana kufanya hivyo ni sawa na kupanda mbegu ya mchango huku ukitegemea itastawi na kuzaa matunda. Pengine katika Maisha ya sasa tunajutia makosa tuliyofanya siku za nyuma na pengine tunatumia gharama kubwa kwa ajili ya kufunika makosa hayo. Mwandishi anatushirikisha kuwa jambo muhimu katika Maisha ni kufanya tathimini ya makosa uliyayofanya na kujifunza kosa lililopelekea uingie kwenye makosa hayo. Tumia fundisho unalopata kutokana na makosa katika kuhakikisha makosa hayo hayajirudii katika kipindi kilichobakia kwenye uhai wako. Jifunze kukubali yaliyofanyika yamefanyika kwa namna yalivyofanyika na sasa hauna nafasi ya kurekebisha. Nafasi pekee uliyonayo ni kuhakikisha unaboresha yaliyopo mbele yako. Kauli kama vile “ningejua” haziwezi kukusaidia tena maana hukujua ndiyo maana haikutokea jinsi unavyotaka kwa sasa.

SEHEMU YA NNE: NJIA 7 ZA ZITAKAZOKUZA MTAZAMO WA AKILI YAKO KWA AJILI YA KUWA NA AMANI NA FURAHA KATIKA MAISHA

14. Kila binadamu jinsi alivyo katika Maisha yake ya kila siku ni zao la yale anayotumia muda mwingi kufikiria. Sisi ni zao la fikra zetu. Tafsiri yake ni kwamba tatizo kubwa tunalotakiwa kutatua katika Maisha yetu ni namna gani tunaweza kuchagua fikra/mawazo yenye tija. Tukijikita kwenye fikra/mawazo ya furaha hakika tutakuwa na furaha na tukijikita kwenye mawazo/fikra za hofu na huzuni hakika Maisha yetu yatawaliwa na matukio ya hofu na huzuni kila mara. Tukiwaza magonjwa muda mwingi hakika tutapatwa magonjwa hayo au tukiwaza kukataliwa na jamii hakika tutakataliwa kila mara. Kumbe badala ya kujikita kwenye fikra hasi tunatakiwa kujikita kwenye fikra chanya. Tafsiri yake ni kwamba badala ya kuhofia changamoto zilizopo mbele yetu tunatakiwa kufikiria njia bora na kuweka mikakati ya kukabiliana nazo.

15. Jifunze kuwapenda adui zako kama njia ya kumaliza uhasama wenu. Kadri tunavyochukia adui zetu ndivyo tunawapa nafasi ya kuvuruga Maisha yetu. Tunakosa furaha halisi, usingizi, hamu ya kula, tunavuruga mfumo wa afya yetu na kusababisha magonjwa ya moyo kama vile presha na kisukari kadri tunavyoendelea kubeba chuki na malipizo ya kila aina dhidi ya maadui zetu. Kumbe kutokana na kubeba hisia hasi dhidi ya maadui zetu hatuwaumizi wao badala yake tunajiumiza wenyewe. Hivyo kumpenda adui yako ni tiba tosha kwa mtu anayependa nafsi yake. Hata Yesu alisema mpenda adui na samehe mara sabini. Unaposamehe siyo kwamba ni faida kwa anayesamehewa bali ni faida na kwako pia kutokana na tulizo la maumivu ya moyo unayopata kabla ya kusamehe. Hii ni kutokana na ukweli kwamba hasira au jazba inaweza kupelekea moyo kushindwa kufanya kazi na matoke yake kupelekea kifo cha ghafla.

16. Husitegemee shukrani kutoka kwa wanadamu kutokana na matendo yako. Kwa asili binadamu ni kiumbe hasiye na shukrani. Anaweza kukushukuru leo kutokana na wema uliomfanyia hila kesho akakuna kuwa hujawahi kumsaidia. Hivyo, ili uishi Maisha ya amani na furaha unatakiwa kutopoteza muda kwa ajili ya kusubilia kupata shukrani kutoka kwa jamii inayokuzunguka. Kwa asili katika kila kundi la jamii kuna watu ambao wana tabia ya kuongea sana kulalamikia wengine kana kwamba wao ni malaika. Pale unapokubaliana na ukweli huu hakika hautopoteza muda kusubiria shukrani za wanadamu. Kumbe, katika Maisha hautakiwa kulazimisha kupendwa au kupewa shukrani badala yake unatakiwa kugawa matendo ya upendo bila kutegemea kulipwa. Tenda wema na uondoke zako huku ukifurahia wema wako. Hii ni sawa na Aristotle alivyomuelezea mwanaume halisi kuwa: “Ni yule ambaye anafarijika na kufurahi kutokana na matendo mema kwa wengine; lakini anajisikia aibu pale anapopokea matendo mema kutoka kwa wengine – kwa kuwa ni alama ya ukamilifu kutoa wema kwa wengine na udhaifu kupokea kutoka kwa wengine”. Tafsiri yake ni kwamba ni heri kutoa kuliko kutegemea kupokea.

17. Husijione mnyonge au dhaifu kutokana na maumbile au hali ya Maisha yako. Unaweza kujiona dhaifu kutokana na kukosa uwezo wa kumudu viatu vizuri wakati kuna mtu ni mlemavu wa miguu na anafurahia jinsi alivyo. Unaweza kujiona mdhaifu kutokana na kukosa kiungo kimoja katika mwili wakati kuna mtu hana viungo zaidi ya kimoja. Kubwa ni kwamba tunatakiwa kuwa na furaha na amani kutokana na maumbile au hali yetu ya kimaisha. Maumbile au hali ya Maisha yetu ni afadhari kuliko watu wengine. Kile ambacho tunaona ni kidogo wapo ambao wanakesha wakitamani kufikia hatua ulizofikia. Kumbe tunatakiwa kusherekea baraka tulizopewa kuliko kutumia muda mwingi kujutia mapungufu tuliyonayo.

18. Jitambue wewe ni nani na hakikisha unaishi Maisha yako – husiishi Maisha ya kujaribu kuwa kama flani maana yeye ni yeye na wewe ni wa kipekee. Kitu pekee ambacho unatakiwa kufahamu ni kwamba kila mtu ameumbwa na kupewa kalama au vipaji tofauti. Hata hivyo, mazingira tuliyokulia pamoja na malezi tuliyopata yana nafasi kubwa ya kuamua jinsi tulivyo kwa sasa. Hakuna sababu ya kuishi katika huzuni kubwa au kujutia namna tulivyo na badala yake jambo tunalotakiwa kufanya ni kuweka jitihada za kujitambua kwa nini tupo jinsi tulivyo. Unapojitambua ni rahisi kujifunza wapi panatakiwa kuboreshwa ili uendane na kasi ya Maisha. Watu wengi wanateseka na kuishi Maisha ya utumwa kutokana na tabia ya kuiga Maisha ya wenzao. Hali hii ipo katika jamii tunayoishi na mfano, mzuri unaweza kuangalia wasanii wengi jinsi wanavyoharibikiwa kimaisha kutokana na tabia ya kuigiza Maisha ya wasanii wenzao ndani au nje ya nchi.

19. Jenga tabia ya kujifunza kutokana changamoto au hali ya mazingira inayokuzunguka. Watu wengi wanakata tamaa kimaisha kutokana na changamoto za Maisha – changamoto ya kawaida mtu anajisemea kuwa sina budi ya kuangaika kwa kuwa haya ndiyo maisha yangu. Wengi hajisumbui kujiuliza ni namna gani naweza kubadilisha changamoto iliyopo mbele yao kuwa fursa ya kubadilisha Maisha yao. Kati ya nguvu alizopewa mwanadamu ni uwezo wa kubadilisha hali hasi kuwa chanya. Hata hivyo, ni watu wachache sana wanaojua kutumia uwezo huo ipasavyo katika Maisha yao ya kila siku. Jifunze kuyafundisha macho yako yaone fursa katika kila changamoto iliyopo mbele yako.  Mfano, wanaume wawili wakiwa kifungo waliangalia nje ya nondo za madirisha ya sero zao, mmoja aliona matope na mwingine aliona nyota. Tafsiri yake ni kwamba kadri unavyoona “nyota” kwenye changamoto iliyopo mbele yako ndivyo una nafasi ya kubadilisha changamoto hiyo huku ukifanikiwa kuwa na maisha yenye furaha na amani.

20. Kama unataka kukubalika katika jamii ambayo inakubeza hakikisha unakuwa mtu wa msaada kwa jamii husika. Wapo watu wengi ambao wamekulia katika mazingira ambayo yanapelekea kutokukubarika katika jamii wanayoishi, hali hii inapelekea watu hao kuishi maisha ya huzuni na uchungu kutokana na matendo au mtazamo wa jamii inayozunguka. Mfano, mtoto kutoka familia masikini anapata wakati mgumu sana pale anapojikuta yupo katikati ya Watoto wa familia za kitajiri. Kama ni shuleni mtoto huyu hatokubalika katika kila anachofanya endapo hakina faida kwa Watoto wenzake. Mtoto huyu atakubalika kwa Watoto wengine pale ambao atakuwa na msaada dhidi yao. Mfano, kama atakuwa na akili nyingi moja kwa moja ataanza kuwasaidia Watoto wenzake kujibu maswali wanayopewa. Ndivyo ilivyo katika maisha, kadri unavyotengeneza sababu za kutegemewa na jamii ndivyo utasahau hofu zinazotokana na kutokukubaliwa na jamii.

Hakika yapo mengi ambayo mwandishi wa kitabu anatushirikisha katika kitabu hiki kwa ajili ya kukabiliana na hofu inayotukabiri katika maisha. Tukutane wiki ijayo kwa ajili ya kumalizia sehemu ya kitabu hiki iliyobakia. Ili uendelee kufaidika na mafundisho kama haya hakikisha unajiunga na mtandao wa Fikra za Kitajiri kwa  KUBONYEZA HAPA.

Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate elimu isiyokuwa na mwisho.

Born to Win ~ Dream Big 

Mwalimu Augustine Mathias

Namba ya Simu:      +255 786 881 155
Mwanzilishi wa Mtandao wa 
fikrazakitajiri.blogspot.com
Barua pepe:  fikrazatajiri@gmail.com

onclick='window.open(