NENO LA LEO (APRILI 14, 2020): [USHAURI] JE PESA ZAKO HUWA ZINAPITILIZA NA HAUJUI ZINAKOENDA? TUMIA MBINU HII.

👉🏾Habari ya asubuhi rafiki yangu mpendwa na mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni matumaini yangu kuwa umemaliza vyema siku za pasaka na sasa una uhuisho mpya kwa ajili ya kuendeleza kile unachofanya. Kumbuka nimekuwa nakusisitiza kuhakikisha kila siku unatengeneza ushindi mdogo mdogo maana ni kupitia ushindi huo ipo siku watu watashangaa mafanikio makubwa uliyonayo bila kujua kuwa wanachokiona kimeandaliwa kwa muda mrefu.

JIUNGE NA KUNDI LA WHATSAPP LA FIKRA ZA KITAJIRI KWA  KUBONYEZA HAPA NA KUJIUNGA BURE. Jiunge sasa nafasi ni chache.

✍🏾Karibu katika neno la tafakari ya leo ambapo nitakushirikisha mbinu moja ambayo unatakiwa kuitumia kwa ajili ya kujua sehemu ambazo huwa zinavujisha pesa zako. Katika jamii tunayoishi ni kawaida kusikia watu wakilalamika kuwa kila wakishika pesa zinapitiliza na hawajui zinakoelekea. Wengi ni rahisi kukumbuka kiasi cha pesa ambacho walikuwa nacho lakini hawawezi kukumbuka pesa hiyo imeshaje kwa maana namna ilivyotumika.

✍🏾Kama na wewe ni mmoja wa hao ambao huwa hawajui pesa zao zinaenda wapi, kupitia neno la tafakari ya leo nakushirikisha mbinu ambayo itakuwezesha kujua sehemu ambazo pesa yako huwa inaelekea. Mbinu hii si nyingine bali kuanzia sasa tafuta kijinotibuku kidogo na yake hakikisha unaandika kila pesa unayopata na kila aina ya matumizi unayofanya. Andika kila kiasi cha pesa kinachotumika bila kujali ni kidogo au kikubwa.

✍🏾Ndiyo namaanisha kila aina ya matumizi yanayohusisha pesa yako hakikisha yamerekodiwa kwenye kijitabu chako. Kama umekunywa chai hotelini rekodi chai hiyo umelipia shilingi ngapi. Kama umekunywa maji na soda rekodi gharama hiyo ya vinjwaji kwa kuainisha gharama ya kila aina ya kinywaji ulichotumia. Kama umenunua vocha au kujiunga kifurushi kwa mpesa au tigo pesa hakikisha unaandika kiwango ulichotumia kwenye muamala huo. Vivyo hivyo, kama kuna pesa umeitenga kama akiba au kuiwekeza hakikisha na yenyewe inarekodiwa.

✍🏾Fanya zoezi hila ndani ya mwezi wa kwanza na mwisho wa mwezi jumlisha matumizi yako ili kujua kama kiasi ulichoandika kinaleta jumla ya kiasi cha pesa ulichopata katika mwezi husika. Baada ya mwezi wa kwanza endelea na utaratibu huu kwa kipindi cha miezi kadhaa hadi pale ambapo utakuwa umejua sehemu ambako pesa yako huwa inaelekea.

✍🏾Kwa nini zoezi hili? Zoezi hili pamoja na kukusaidia kujua sehemu ambako pesa yako huwa inaelekea litakusaidia kugundua baadhi ya matumizi ya pesa ambayo siyo ya lazima. Baada ya kugundua sehemu zisizo za lazima ambazo zinavujisha pesa yako sasa unatakiwa kuandaa bajeti inayoendana na pato lako. Pia, kupitia zoezi hili utaweza kugundua sehemu zipi unaweza kuokoa pesa ambayo umekuwa ukiipoteza kwenye matumizi yasiyo ya lazima na sasa pesa hiyo unaweza kuiwekeza sehemu yenye tija.

✍🏾Mwisho, neno la tafakari ya leo limetufunulia kuwa tumekuwa tukipata pesa na mwisho wake hatujui inakoelekea kwa vile hatuna utaratibu wa kuorodhesha matumizi ya pesa yetu. Kuanzia sasa tumeshauriwa kuhakikisha tunakuwa na kijitabu kidogo ambacho ndani yake tutaorodhesha matumizi ya pesa yote na hatimaye kujua kiasi tunachotumia ndani ya muda wa mwezi mmoja. Naendelea kukumbusha kuhakikisha unapata nakala yako ya uchambuzi wa kitabu cha Rules of Money ambacho ndani yake utajifunza kanuni 107 kuhusu pesa.

👐🏾Nakutakia kila la kheri kwenye siku hii ya leo. Kumbuka husikose kutoa mrejesho wa kile ambacho unajifunza kutokana na uwepo wako kwenye kundi hili.

 BORN TO WIN ~ DREAM BIG

🗣🗣 Mwalimu Augustine Mathias
Mawasiliano: 0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua pepe: fikrazakitajiri@gmail.com
Tovuti: fikrazakitajiri.blogspot.com

Kujiunga Kundi la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI, bofya link hii: https://chat.whatsapp.com/JACBxr9kX7K0qt58cQTrrw
onclick='window.open(