Habari rafiki yangu
ambaye umeendelea kuamini kazi yangu ya uchambuzi wa vitabu kupitia mtandao wa FIKRA
ZA KITAJIRI. Karibu katika uchambuzi wa kitabu cha leo ambacho ni 4 kati ya
vitabu 30 ambavyo nimejiwekea lengo kuvisoma katika kipindi cha mwaka huu 2020.
Kama bado hujajiunga
na kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI kwa ajili ya kupata neno la
tafakari kila siku pamoja na kujumuika na watu wenye mtazamo sawa, tafadhali
fanya hivyo KWA KUBONYEZA HAPA na
kujiunga na kundi letu. Nafasi ni chache hivyo fanya maamuzi ya kujiunga sasa.
Kupitia makala hii nakushirikisha sehemu iliyobakia ya uchambuzi wa kitabu “How
to Stop Worrying and Start Living” kutoka kwa mwandishi Dale Carnegie.
Unaweza kusoma sehemu ya kwanza ya uchambuzi wa kitabu hiki kwa kubofya kiunganisho hiki hapa chini.
Soma: Uchambuzi wa Kitabu cha How to Stop Worrying and Start Living: Jinsi ya kuepuka hofu katika maisha.
SEHEMU YA TANO: KANUNI YA KIPEKEE
KATIKA KUISHINDA HOFU
21.
Kuishi maandiko
matakatifu ni moja ya njia rahisi ya kuepukana hofu. Maisha ya wanadamu walio
wengi yanatawaliwa na hofu inayotokana na gharama za mahitaji ya kila siku. Mtu
mzima yoyote kila anapoamka anawaza atapata vipi hela kwa ajili ya chakula cha
familia, ada za Watoto wa shule, mahitaji ya maradhi, afya, bili za maji na
umeme na mengine mengi. Ni kutokana na mahitaji hayo wapo watu wengi ambao
wanakata tamaa kiasi cha kutaka kujinyonga ili kuepuka ghadhabu/kalaa ya
Maisha. Hata hivyo, kupitia maandiko matakatifu kila mmoja kwa Imani yake ni
sehemu ambapo mtu anapata faraja, uvumilivu na tumaini la Maisha. Maisha
ya mwanadamu yanazungukwa na mafumbo mbalimbali ambayo yanamfanya kila mara
ahofie Maisha yake ya baadaye. Hata hivyo, kupitia misingi ya dini kila
mwanadamu anaweza kuishi Maisha yenye thamani.
22.
Maisha bila misingi
ya Imani hayana maana. Imani imeweka misingi
muhimu katika Maisha ya mwanadamu. Misingi hii inamfundisha mwanadamu namna
anavyotakuwa kuishi katika mazingira yake. Ni kutokana na misingi ya Dini, Maisha
ya mwenye Imani yanakamilika pale ambapo anayatoa Maisha yake kwa ajili ya watu
wengine au viumbe vingine kwa ujumla wake. Hebu fikiria kama kusingekuwa na
jinsi ambavyo maovu yanayoambatana na mauaji, wizi, ugomvi, fitina na mengine
mengi ambavyo yangeshamiri katika ulimwengu huu. Dini imekuwepo kwa ajili ya
mwanadamu kuishi Maisha yenye upendo na amani, ni kupitia dini hiyo mwanadamu
kila mara anatakiwa kuishi kwa ukamilifu badala ya kuishi Maisha ya hofu.
Ieleweke kuwa kinachomfanya mtu kuwa mtu wa Dini siyo tu kwenda Kanisani au
Msikitini bali ni ile hali ya kuwa na Roho sambamba na kushiriki matendo mema kwenye
Maisha ya kila siku. Kwa ujumla Imani ni moja nguvu za ulimwengu huu ambazo
zinamwezesha mwanadamu aishi Maisha yenye amani, furaha na tumaini.
23.
Kuna nguvu kubwa
katika muunganiko wa mwanadamu na Mungu. Muunganiko
huu unakamilika kupitia sara ambapo mwanadamu anamlilia Muumba wake dhidi ya
matatizo yanayomkabili pamoja na kushukuru baraka anazojaliwa. Mwandishi
anatushirikisha kuwa tatizo lililopo kwa wanadamu wengi ni kusubiria nyakati za
tabu na shida ndipo wamkumbuke Muumba wao. Hakika kwa mwanadamu ambaye anaishi
katika sara kila siku hana cha kuhofia katika Maisha kwa kuwa matatizo na
furaha yake yote kila mara anajua kuna Mungu mwenye nguvu dhidi ya matatizo
aliyonayo. Ni kupitia muunganiko huu nguvu na hamasa mpya inajitokeza kwa mtu
anayeishi Maisha ya sara. Hivyo, kila mara anauhuishwa kupitia sara. Kumbe
katika Maisha yetu ya kila tunatakiwa kukumbuka maandiko matakatifu yanatuambia
kuwa: “Omba na utapewa; tafuta na utapata; na bisha hodi na utafunguliwa”.
SEHEMU YA SITA: JINSI YA
KUEPUKANA NA HOFU YA KUKOSOLEWA
24. Watu wengi wana hofu inayotokana na kutojiamini
kutokana na majukumu waliyonayo. Wengi kutokana na kiwango cha elimu au uzoefu
walionao wanajikuta kwenye hali ya kudhania kuwa kazi walizonazo ni viatu ambavyo
vinawapwaya. Hauwezi kuzuia watu wakubeze katika kila
unachofanya hila unaweza kuhakikisha katika kila wanalobeza unawajibu kwa
matokeo chanya. Kanuni kubwa unayotakiwa kuiishi ni: Mti wenye matunda ndiyo
unapigwa mawe. Kadri utakavyoendelea kutoa matokeo chanya katika kazi unayoifanya
ndivyo maadui wasiyokutakia mema watazidi kuongezeka. Ndivyo mwanadamu alivyo
maana wivu ni moja ya tabia za asili walizonazo wanadamu. Wajibu ulionao siyo
kupambana nao bali ni kuendelea kuishi misingi ya kanuni ulizojiwekea kuhusu Maisha
yako na kazi unayoifanya.
25.
Kanuni ya kuepuka
hofu inayotokana na kukataliwa ni: kutambua kuwa hakuna mtu anayejali Maisha yako
maana kila mtu yuko bize na Maisha yake. Kwa
kutambua kanuni hiyo unatakiwa kuwa bize na majukumu yako ya kila siku katika Maisha
na kuacha kuumizwa au kutumia muda mwingi kufikiria maneno ya watu wanaokubeza
au kukukosoa. Fanya yale unayoamini ni sahihi kutoka ndani ya roho yako kwani
hata ukifanya kulingana na mapenzi yao bado utakosolewa tu. Kumbuka hauwezi kuridhisha
watu wote na ndiyo maana hata Yesu mwenyewe alisalitiwa na mmoja wa Mitume
wake. Hivyo kwa kutambua ukweli huu kuhusu mwanadamu, hautakiwi kuishi kwa
ajili ya kufurahisha wanaokuzunguka bali ishi kutimiza yale unayoamini ni
sahihi na kujifanya kana kwamba hausikii maneno ya wakosoaji wasiyo na dhamira
njema juu ya matendo yako. Hata hivyo, unatakiwa kutambua kuwa unaweza
kujifunza kutokana na kukosolewa pale unapokosolewa kwa haki.
26.
Njia nyingine
ya kukabiliana na hofu ya kukosolewa ni kutenga muda wa kujifanyia tathimini dhidi
ya matendo yako ya kila siku. Kila siku au kila mwisho wa wiki tenga muda kwa
ajili ya kujiuliza ni makosa yapi umefanya katika kipindi cha wiki nzima
ikilinganishwa na yale uliyotenda kwa usahihi. Jiulize makosa hayo yalisababishwa
na nini na unaweza kufanya nini ili uhepukane na makosa hayo katika Maisha ya
sasa na baadaye. Jiulize katika makosa hayo kuna uzofu upi ambao ni muhimu katika
Maisha yako. Tafsiri yake ni kwamba katika yale unayokosolewa kwa haki kuna
somo kubwa ambalo unatakiwa kujifunza kwa ajili ya kusonga mbele kwa mafanikio
zaidi. Kumbe, kabla kusubiria maadui zetu kutukosoa tunaweza kujikosoa wenyewe
kutokana na kufanya tathimini ya mara kwa mara kuhusiana na matendo tunayofanya
katika majukumu ya kila siku.
27.
Wakati mwingine ni
muhimu kukaribisha wanaokukosoa kwa ajili ya kujifunza somo muhimu katika Maisha.
Unapokuwa katika ngazi ya kufanya maamuzi ambayo yana athari kwa kundi kubwa la
watu ni lazima uwe tayari kupokea wakosoaji na kupokea ushauri kutoka kwa watu
wa karibu na wewe. Hakuna anayependa kukosolewa kutokana
na ukweli kwamba mwanadamu anatawaliwa na hisia (feelings) kuliko mantiki
(logic). Kumbe, kama unahitaji kujifunza kutoka kwa wakosoaji wako unatakiwa maamuzi
yako fanyike kwa kutumia mantiki kuliko kuongozwa na hisia binafsi. Kama nguli
wa sayansi Albert Einsten aliwahi kunukuliwa kuwa “wakati mwingine hayuko
sahihi kwa asilimia 99” ndivyo na wewe unatakiwa kutambua pengine maamuzi
unayoona ni sahihi ni kutokana na hisia zako binafsi.
SEHEMU YA SABA: NJIA 6
ZITAKAZOKUWEZESHA KUEPUKANA NA UCHOVU NA KUKUFANYA UWE NA NGUVU YA MWILI NA
ROHO
28.
Uchovu ni moja ya sababu
zinazopelekea hofu katika Maisha. Ni kutokana na ukweli huo
mwandishi kupitia sehemu anatushirikisha mbinu muhimu za kukabilianana na
uchovu. Kutokana na tafiti za kitabibu, uchovu unapunguza uwezo wa mwili kukabiliana
na homa ya kawaida pamoja na magonjwa mbalimbali. Pia, kulingana na tafiti za
matibabu ya akili, uchovu hupunguza uwezo wa kukabiliana na hisia za hofu na
wasiwasi. Hivyo, kutokana na tafiti hizo kuna kila sababu ya kufahamu namna ya
kukabiliana na uchovu kama sehemu ya kukabiliana na hofu katika Maisha ya kila
siku. Hivyo, kupata muda wa kupumzika ni moja ya njia ya kuepukana na wasiwasi
au hofu; kanuni ni kwamba ili upunguze hofu hakikisha: unapata muda wa kupumzika
mara kwa mara na pumzika kabla ya kuchoka. Tenga muda wa dakika kadhaa katika
siku yako kwa ajili ya kutuliza kichwa kutoka majukumu yote ya siku. Muda wa
kupumzika ni muhimu kwa ajili ya kuhuisha nguvu mpya kabla ya kuendelea na
majukumu yaliyopo mbele yako. Muda unaotumia kupumzika siyo kwamba unaupoteza
bali ni muda muhimu kwa ajili ya afya ya roho na mwili.
29.
Je uchovu unasababishwa
na nini? Mwandishi anatushirikisha kuwa tafiti zinaonesha kuwa kuwa kazi inayohusisha
ubongo/akili haiwezi kusababisha uchovu kwa mhusika. Kinachosababisha
uchovu ni mtazamo au mazoea ya akili pamoja na hisia. Kwa tafsiri ya haraka ni
kwamba kinachosababisha uchovu ni sababu za kisaikolojia ambazo mhusika
anapambana nazo kwenye Maisha yake ya kila siku. Tafiti zinaendelea kuonesha
kuwa hisia zinazopelekea uchovu ni zile hasi ambazo zinaambatana na mhusika
kuwa na: chuki, kuhisi kutothaminiwa katika kazi yake, wasiwasi wa
kutokamilisha kazi kwa wakati, na hofu kutofanya kazi kwa haraka. Matokeo yake
ni kupelekea mhusika kupunguza uzalishaji kwenye kazi yake na hatimaye kurudi
nyumbani na maumivu ya kichwa akidhani kuwa ni uchovu kumbe uchovu ameuzalisha
mwenyewe bila kujua. Kumbe, njia rahisi ya kuepukana na uchovu ni kuwa na
utulivu wa akili kwenye jukumu lililopo mbele yetu. Utulivu huu unapelekea neva
za mwili (nerveous) kujihisi vyema na hivyo kutoa ushirikiano kwa akili katika
kazi inayofanyika.
30.
Hofu au
wasiwasi kuhusu masuala ya familia ni moja ya chanzo kikuu cha magonjwa mengi
kwa wanawake walioolewa au wenye familia kwa ujumla katika karne ya sasa. Magonjwa
mengi kama vile magonjwa ya moyo, kansa ya uzazi, kansa ya ziwa, tumbo na
magonjwa ya figo ni matokeo ya wasiwasi na hofu kubwa waliyonayo wanawake wengi
juu masuala ya familia. Hali hii inatokana na uchovu ambao unasababishwa na majukumu
ya familia kwa akina mama. Ndiyo maana ukienda kwenye mikusanyiko ya kidini
wanaojazana ni akina mama ikilinganishwa na wababa kwa vile wanategemea kupitia
mikusanyiko hiyo wapata suluhisho la matatizo yao. Mwandishi anatushirikisha
kuwa matatizo mengi yanayowakabili akina mama huwa yanatibika pale wanapopata ushauri
wa wataalamu wa magonjwa ya saikolojia. Pia, mwandishi anatushirikisha kuwa
akina mama wengi wanateseka na masuala ya familia kwani kwa asili wana tabia ya
kutokutoa vitu ndani. Ni kutokana na tatizo hilo, tafiti zinaonesha kuwa wapo
wengi ambao wamepona matatizo yao kutokana na tiba ya maneno tu. Hivyo, ni
muhimu kujenga tabia ya kutoa vitu ndani, pale unajihisi kusongwa na mambo
tafuta mtu ambaye unamwamini kwa ajili ya kukupa ushauri juu ya kile ambacho
kinakutatiza.
31.
Kila mwanamke
anaweza kupunguza hofu au wasiwasi juu ya masuala ya kifamilia kwa kutumia
mbinu zifuatazo:-
ü
Kuwa na kijinotibuku ambacho unatembea
nacho kila sehemu – Ndani ya kijinotibuku hicho
hakikisha unaweka vitu vya muhimu ambavyo vinakufanya ujihisi tulizo la moyo. Mfano,
unaweza kuweka nukuu kutoka kwenye misitari muhimu ya maandiko matakatifu,
unaweza kuweka vesi za nyimbo au mashairi ambayo huwa ukiimba unajisikia faraja
ndani ya nafsi yako.
ü
Husitumie muda mwingi kwenye
mapungufu ya wengine – Tambua kuwa mme wako ni binadamu
na ana mapungufu mengi maana kama angekuwa malaika msingeweza kuoana. Mara zote
jaribu kutafuta mazuri ya watu unaoishi nao na ujikite kwenye mazuri yao kuliko
maovu waliyonayo. Hii itakusaidia kupunguza msongo wa mawazo unaotokana na
maovu ya watu wa karibu na wewe.
ü
Jenga urafiki na majirani
zako – Jivunie kuzungumza na majirani wanaokuzunguka
na hakikisha unakuwa mtu wa msaada au kimbilio la mawazo. Wafanye wengi wavutie
na ushauri wako ambayo unalenga kwenye suluhisho la matatizo badala ya kutoa
ushauri wa kubomoa.
ü
Andaa ratiba ya siku inayofuata
kabla ya kwenda kulala – Bila kuwa na mpangilio wa
majukumu hakika kutokana na wingi wa majukumu ya mama, atajikuta kila siku inaisha
bila kumaliza kazi zake za msingi. Hali hii itamfanya muda wote awe na uchovu
hali itakayopelekea wasiwasi na hofu.
ü
Kuwa na muda wa kupumzika
katika ratiba ya siku yako – Kila mara unapojisikia
kupumzika hakikisha unaitendea haki nafsi yako kwa kupata muda kidogo wa
kupumzika. Kwa kupumzika ni rahisi kuondo msongo wa matatizo yanayokukabiri na kujikuta
kwenye uhuisho mpya wa nafsi (self rejuvenation).
32.
Tumia
mbinu nne zifuatazo kwa ajili ya kuepuka uchovu husiyo wa lazima katika majukumu
yako ya kazi:-
- Mbinu ya kwanza, safisha meza yako ya kazi kwa kuondoa karatasi zote ambazo hazitumiki kwa wakati husika. Hakikisha meza yako ina vitu kulingana na mpangilio wa kazi kwenye ratiba yako. Mpangilio ni sheria muhimu ya kupunguza uchovu katika kazi au biashara unayofanya. Vitu vyote vinavyojitokeza nje ya ratiba yako hakikisha unavikamilisha muda huo huo kabla ya kuendelea na yale yaliyopo kwenye ratiba. Mfano, unapofungua barua pepe yako na kukuta ujumbe unaotakiwa kujibiwa haraka hakikisha unaufanyia kazi badala ya kusema nitajibu baadaye.
- Mbinu ya pili, tekeleza majukumu yako kwa mpangilio ya umuhimu wa kila kazi. Fanyia kazi kwanza majukumu ya muhimu kabla ya kujihusisha na yale ambayo siyo ya muhimu. Ili ufanikiwe katika mbinu hii unatakiwa kukuza uwezo wako wa kufikiri sambamba na uwezo wa kupangilia vitu kwa umuhimu wake. Hapa ndipo kuna umuhimu wa kupanga majukumu ya siku kabla ya kulala au kuamka asubuhi na mapema katika hali tulivu na kupangalia majukumu ya siku kutokana umuhimu wake.
- Mbinu ya tatu, unapokutana na tatizo litatue kwanza na kama una ukweli kuhusiana na tatizo husika utumie kufanya maamuzi. Mara nyingi watu wanajikuta kwenye mrundikano wa matatizo yanayotakiwa kutafutiwa suluhisho kutokana na tabia ya kutofanya maamuzi kwa haraka. Ni kawaida kukuta vikao vingi vinajadiri matatizo kibao ambayo mwisho wa kikao hakuna hata moja ambalo limepatiwa suluhisho la kudumu. Hivyo, badala ya kuorodhesha matatizo mengi ni bora kushughulikia tatizo moja na baada ya kulifanyia maamuzi ndipo ugeukie tatizo jingine.
- Mbinu ya nne, jifunze kupanga, kugatua majukumu na kusimamia. Watu wengi wanajichimbia kaburi kutokana na uchovu wa kila siku kwa kuwa wanashindwa kugatua majukumu kwa watu wengine. Zipo kazi za kawaida ambazo zingefanywa na wasaidizi wao kwa usimamizi wa karibu na hatimaye kupunguza majukumu kwenye ratiba yako. Mbinu hii pia ni muhimu kwa wafanyabiashara maana biashara nyingi zinasimamiwa na mtu mmoja hasa baba au mama jambo linalopelekea kutopata muda wa kupumzika.
33.
Uchovu wakati
mwingine unatokana na mtu kuboreka (bored) na kile anachofanya. Mwandishi anatushirikisha
kuwa mtu anapoboreka kiwango cha mzunguko wa hewa oxyjeni mwilini huwa kinapungua
na kupelekea mmengenyo wa chakula kushuka. Hali hii inamfanya mhusika ajihisi
hali ya uchovu kutokana kushuka na kwa nishati ya kufanyia kazi. Tafiti zinaonesha
kuwa mtu akirudi kwenye mudi ya kazi presha ya damu inaongezeka hali
inayopelekea mzunguko wa hewa ya oxyjeni kuongezeka mwilini. Ni kutokana na
ukweli huu wote tunashuhudia kuwa ni nadra sana kujihisi uchovu kama tunafanya
kazi tunayoipenda. Unaweza kujikuta unafanya kazi zaidi ya masaa sita kwa kazi unayoipenda
wakati kazi ambayo inakuboa utajikuta kila baada ya nusu saa unataka kupumzika.
Kumbe somo kubwa la kujifunza ni kwamba uchovu hautokani na kazi tunazofanya bali
ni matokeo ya wasiwasi/hofu, chuki na mafadhahiko. Mwisho, kuepukana na uchovu
hakikisha unapenda kazi unayofanya kwa wakati husika.
34.
Pia mara nyingine
uchovu unasababishwa na hofu ya kukosa muda wa usingizi. Kila binadamu anataka
kupata muda wa kutoshereza kwa ajili ya usingizi japo hakuna mwenye kujua kwa
undani usingizi ni nini. Wengi wanakosa usingizi kutokana na hofu
zinazowakabili katika Maisha hali ambayo inapelekea kulala usiku mzima bila
kupata usingizi. Hali hii inapelekea kuianza siku mpya wakiwa na uchovu na
matokeo yake ni kukosa ufanisi katika kazi. Hata hivyo, mwandishi
anatushirikisha kuwa kinachopelekea kukosa usingizi ni ile hofu ya kutopata
usingizi na tafiti zinaonesha kuwa wengi wanaosema hawapati usingizi huwa wanasinzia
bila ya ufahamu wao. Kumbe, tunapolala tunatakiwa kujihisi tupo kwenye mikono ya
amani na hivyo kuachia Maisha yetu kwenye mikono ya mamlaka yenye nguvu kuliko
sisi. Tafsiri ya haraka haraka ni kwamba utapata usingizi pale utakapojihisi Maisha
yako yapo kwenye mikono salama.
SEHEMU
YA NANE: JINSI YA KUPATA KAZI YENYE FURAHA NA MAFANIKIO
35.
Ukiwa bado haujapata
kazi na upo chini ya umri wa miaka 18 hakikisha unafanya maamuzi mawili sahihi katika
Maisha ambayo yataamua hatima ya furaha, uchumi na afya yako. Moja, amua aina ya kazi ambayo unataka kuifanya katika Maisha
yako. Je unahitaji kuwa mkulima? Je unataka kuwa mfugaji? Je unataka kuwa mfanyabiashara?
Je unataka kuajiriwa? Kama unataka kuajiriwa chagua fani/sekta ambayo unataka
kuifanyia kazi, mfano, udaktari, sheria, misitu/wanyamapori, uhandisi, uhasibu
na fani nyinginezo. Mbili, amua aina ya mtu ambaye unahitaji awe baba au mama
wa Watoto wako. Maamuzi yote haya ni sawa na kucheza kamali katika Maisha hivyo
ni muhimu kuhakikisha unakuwa makini maana hatima ya ndoto zote za Maisha yako itategemea
na maamuzi hayo. Utaifurahia kazi kama unaipenda kutoka rohoni, ni kutokana na
furaha hiyo kila mara utahitaji kuendelea na kazi. Vivyo hivyo, utaipenda ndoa
kama mnapendana na kuelewana na mwenza wako.
36.
Tatizo kubwa ni
kwamba watu wengi kazi wanazofanya siyo kazi za ndoto zao. Wengi wanafanya kazi
hizo kwa vile ndipo nafasi ya ajira ilipojitokeza hila kile walichotamani toka utotoni
pengine hawakubahatika kupata ajira au ufahalu haukuwawezesha kusomea fani
hiyo. Hali hii ndiyo inapelekea watu wengi hawafurahishwi na kazi wanazofanya
na kwa vile hawana namna inabidi tu waendelee na kazi kwa ajili ya kupata ridhiki
ya Maisha. Ana heri mtu yule anayepata kazi ya ndoto yake na tafiti zinaonesha
kuwa mtu anayependa kazi anayofanya ana nafasi ya kuishi miaka mingi. Kama mzazi
wajibu wako ni kuhakikisha unawaongoza wanao kuchagua kufikia kazi ya ndoto yao.
Hapa ndipo wazazi wengi wanakosea kwa kulazimamisha Watoto wao kufanya kazi
ambazo wao wanaona ndiyo kazi bora. Katika kuchagua kazi ya kufanya katika Maisha
yako zingatia ushauri huu:-
- Husichague kazi ambayo kila mtu anakimbilia – tafuta fani ambazo zinakimbiwa na watu wengi.
- Chagua kazi ambayo itakuwezesha kukidhi mahitaji ya Maisha yako - Fanya maamuzi ya kuachana na kazi ambayo unatumia nguvu na akili nyingi lakini bado haiwezi kukidhi mahitaji ya muhimu ya Maisha yako.
- Fanya utafiti wa kutosha kwenye kazi unayofikiria kuifanya kabla ya kujitosa moja kwa moja kwenye kazi hiyo. Uliza watu ambao tayari wapo kwenye kazi hiyo kwa kipindi kirefu ili kupata uzoefu walionao kwenye kazi husika. Swali muhimu, waliuze kama wangepata nafasi ya kuchagua kazi ya kufanya upya je wangekuwa tayari kuchagua kazi wanayofanya kwa sasa?
- Epuka Imani kuwa kila mtu anaweza kufanya kazi moja katika kipindi cha Maisha yake. Ukweli ni kwamba mtu mwenye akili timamu anaweza kufanikiwa katika kazi nyingi sawa na ilivyo mtu huyo huyo anaweza kushindwa kufanikiwa katika kazi nyingi pia. Hivyo, kushindwa kufanikiwa katika kazi moja hisikufanye ukate tamaa ya kutafuta kazi nyingine ambayo unaiona kuwa bora ikilinganishwa na kazi ya sasa.
37.
Tafiti zinaonesha
kuwa takribani asilimia 70 ya hofu au wasiwasi wa wanadamu katika Maisha yake
ya kila siku zina uhusiano na mahitaji ya pesa. Tafiti hizi zinaonesha kuwa watu
waliohojiwa walikiri kama kipato chao kingeongezeka angalau kwa asilimia 10
hakika wangeweza kumaliza hofu zinazotokana na mahitaji ya pesa. Hata hivyo
hali hii siyo sahihi maana ongezeko la kipato huwa linaambatana na ongezeko la
matumizi. Hivyo, tatizo siyo kwamba hawana pesa ya kutosha badala yake wanakosa
elimu ya namna ya kubajeti vyema pesa wanazopata. Kumbe, kinachosababisha
asilimia sabini ya wasiwasi/hofu ni kutokana na watu kukosa elimu sahihi kuhusu
pesa. Hizi hapa baadhi ya kanuni ambazo mwandishi anatushirikisha kuhusu namna
bora ya kuondokana na hofu zinazotokana na mahitaji ya pesa:-
ü Watu wengi wanajiuliza sehemu ambako pesa zao huwa
zinaenda bila kupata majibu. Kanuni
ya kwanza, hakikisha unaandika
kila unachofanya na gharama yake. Ainisha kila aina ya matumizi ya siku kwenye
kijinotibuku chako na hatimaye mwisho wa mwezi utagundua sehemu ambazo huwa
zinapoteza pesa zako.
ü Kanuni ya pili, andaa bajeti kulingana na mahitaji yanayoendana na pato
lako. Mwandishi anatushirikisha kuwa familia mbili ambazo zinaishi kwenye
nyumba mbili zinazofanana, katika eneo moja, zikiwa na idadi sawa ya wanafamilia
na zote zikiwa na pato linalofanana lakini cha hajabu utakuta bajeti
zinatofautiana. Unaweza kushangaa kati ya familia hizo moja pato linatosheleza
na nyingine inaangaika kipesa.
ü Kanuni ya tatu, jifunze kutumia
kwa busara. Siyo kila pesa
uliyonayo ni lazima itumike tu bila mpangilio bali hakikisha pesa inatumika
kulingana na mpango wako wa matumizi.
ü Kanuni ya nne, husiongeze
matumizi yasiyo ya lazima kwenye pato lako. Angalia upya vitu unavyonunua kama vinaendelea kuchukua
hela kutoka kwenye pato lako huna budi ya kuachana navyo. Nunua vitu
vinavyosaidia kukuza pato lako.
ü Kanuni ya tano, boresha uaminifu
wako sehemu ambazo unaweza kuomba kukopeshwa. Kuna nyakati ambazo dharura zinajitokeza kama hauna
uaminifu itakuwa vigumu kupata msaada. Pia hakikisha kabla kukopa jiridhishe kama
kuna ulazima wa kukopa – kopa mkopo ambao utatumika kuzalisha faida.
ü Kanuni ya sita, kata bima ya
afya na bima ya kulinda mali zako dhidi ya majanga/ajali. Bima ni kwa ajili ya kukulinda katika matukio ambayo
hujui yatatokea lini hivyo ni tahadhari ya kukuhepusha na upotevu wa mali zako
pale majanga yanapotokea.
ü Kanuni ya saba, badala ya
kuwekeza kwenye bima ya Maisha kwa ajili ya wategemezi wako baada ya uhai wako
wekeza kwenye vitega uchumi ambavyo vitawapa uhakika wa kipato kila mwezi. Mwandishi anatushirikisha kuwa uzoefu unaonesha kuwa
wajane wengi baada ya kulipwa pesa za bima ya Maisha baada ya kuondokewa na
waume zao pesa hizo huwa hazidumu.
ü Kanuni ya nane, wafundishe wanao
misingi ya elimu ya pesa. Mtoto
anatakiwa kufundishwa kuhusu umuhimu wa kutumia fedha kwa nidhamu sambamba
kuhakikisha matumizi hayazidi pato lake. Jambo jingine ambalo mtoto anatakiwa
kufundishwa ni kuhusu umuhimu wa uwekezaji toka akiwa mdogo.
ü Kanuni ya tisa, kama kuna
ulazima tengeneza pesa za ziada nje ya pato lako. Kuna miradi midogo ambayo unaweza kuifanya katika
muda wako wa ziada na kukuwezesha kupata pato la ziada nje ya mshahara wako. Pato
hilo ndilo litatumika kujazilizia kwenye upungufu kulingana na bajeti yako.
ü Kanuni ya kumi, kamwe
husicheze kamali. Mwandishi
anatushirikisha kuwa Kampuni za Kamali na “Betting” ni wezi ambao wanakubalika
kisheria. Kampuni hizi zinatengeneza pesa nyingi kutokana wengi kukimbilia huko
wakidhania watafanikisha Maisha yao kupitia bahati.
ü Kanuni ya kumi na moja, kama
hauwezi kuboresha zaidi pato lako ridhika na ulichonacho na siyo kuendelea
kulalamika na kuishi kwa huzuni. Ifanye akili yako ikubaliane na hali ya kifedha uliyonayo na hakikisha
unaishi kulingana na pato lako.
Hakika tunaweza kuishi Maisha yasiyo na
hofu au wasiwasi kufuata misingi ambayo mwandishi ametushirikisha katika kitabu
hiki. Utamu wa Maisha upo pale ambapo tunafanikiwa kuweka mbali hofu tulizonazo
katika kila sekta ya Maisha yetu. Jiunge na mtandao wa Fikra za Kitajiri
kwa KUBONYEZA HAPA.
Karibuni kwenye fikra za kitajiri ili upate
elimu isiyokuwa na mwisho.
Born to Win ~ Dream Big
Mwalimu Augustine Mathias
Namba ya Simu: +255 763 745 451 au +255 786 881 155 au +255 629 078 410
Barua pepe: fikrazatajiri@gmail.com