NENO LA LEO (OKTOBA 31, 2020): UKANDA WA FARAJA: KANDA TATU AMBAZO UNATAKIWA KUPITIA BAADA YA KUUKIMBIA UKANDA WA FARAJA.
Habari ya asubuhi rafiki yangu mpendwa na
mwanafamilia ya FIKRA ZA KITAJIRI. Ni asubuhi mpya ambapo tunaendelea kuwa
kwenye changamoto ya kufungwa kwa mitandao ya kijamii. Naamini kila mmoja wetu
ameamka salama na yupo tayari kuendelea na majukumu yake ya siku ya leo. Basi tuianze
siku kwa kusema “hii ndiyo siku bora aliyoifanya Bwana, nitafurahi,
nitamshukuru na kuitumia vyema siku hii kwa ajili ya kuongeza thamani ya maisha
yangu hapa Duniani”.
Karibu katika neno la tafakari ya leo ambapo tutajifunza kuhusu ukanda wa faraja (comfort zone) na kanda tatu ambazo unatakiwa kuzipitia baada ya kuukimbia ukanda wa faraja. Kwa asili tumeumbwa katika hali ambayo miili yetu haitaki kuumia hivyo inaridhika inapokuwa kwenye mazingira salama au tulivu (comfort). Mwili wa binadamu unaogopa mabadiliko kiasi kwamba inapotokea mabadiliko ya namna yoyote ile mwili unakuwa katika hali ya mshutuko. Ni kutokana na sababu hiyo, watu wengi wanaridhika kuwa kwenye mazingira ambayo yamezoeleka (comfort zone) kuliko kujaribu mazingira mapya.
Athari ya kuridhika na mazingira yaliyozoeleka ni kukosa ubunifu ni uthubutu wa mawazo mapya katika ukuaji wa mhusika kwenye kipindi cha uhai wake. Watu wanaofanikiwa kimaisha ni lazima wawe tayari kuukimbia ukanda wa faraja kwa ukanda huo unawafanya wengi kubweteka na hali inayowazunguka. Katika mzunguko wa ukuaji mhusika ni lazima apitie kwenye ukanda wa faraja (comfort zone), ukanda wa hofu (fear zone), ukanda wa kujifunza (learning zone) na ukanda wa ukuaji (growth zone). Karibu tuangalie sifa za kila ukanda.
Pia Soma: JE NI MARA NGAPI UNAJILAZIMISHA KUTOKA KWENYE UKANDA WA FARAJA?
Ukanda wa hofu – Huu ni ukanda unaofuatia baada ya ukanda wa faraja. Katika ukanda wa faraja mhusika anaridhika na kila hali inayomzunguka hila katika ukanda huu mhusika anakuwa hajiamini kwenye kila hatua anayokusudia kuchukua katika maisha yake. Katika ukanda huu mhusika anajiona mnyonge dhidi ya mawazo ya wengine (mawazo ya wengine ni bora kuliko yake); kila mara anatafuta visingizio vya kujifariji kulingana na hali yake; na hofu inamzuia kuchukua hatua zinazolenga kutekeleza kwa vitendo mawazo aliyonayo katika kuboresha maisha yake.
Ukanda wa kujifunza – Huu ni ukanda muhimu kwa
mwanadamu yeyote anayelenga kuishi maisha ya thamani. Katika ukanda huu hakuna
changamoto ambayo inamzuia mhusika kusonga mbele kwa kuwa katika kila changamoto
mhusika anatafuta suluhisho. Pia, katika ukanda huu mhusika anajifunza mbinu na
maarifa mapya yanayomuwezesha kuongeza uzoefu dhidi ya mazingira
yanayomzunguka. Hata hivyo, kwenye ukanda huu mhusika anaweza kujikuta ameingia
kwenye ukanda mpya wa faraja hali ambayo itapelekea hasiweze kukua zaidi katika
yale anayofanya.
Ukanda wa ukuaji – Huu ni ukanda ambao mhusika anaishi kusudi la maisha yake kwa ukamilifu. Kwa kuliishi kusudi la maisha yake mhusika anaishi ndoto alizonazo kuhusu maisha kwa kuhakikisha kila mara anaweka malengo mapya mara baada ya kutekeleza malengo ya awali. Ilifanikiwe katika ukanda huu ni lazima ujifunze kuishi kwa hali ya uchanya (positive oriented) kwenye kila hali iliyopo mbele yako. Makwazo, madhaifu na changamoto siyo sababu ya kukuzuia kusonga mbele.
Mwisho, kupitia neno la tafakari ya leo tumejifunza kanda nne za ukuaji katika kuelekea kwenye mafanikio unayotamani. Watu wengi huwa wanajikuta wameishia kwenye ukanda wa faraja hali inayopelekea wasiweze kukua zaidi au kufanikisha ndoto walizonazo. Ikiwa unahitaji mafanikio ni lazima kila mara ukimbie ukanda wa faraja katika kila hatua unayopiga. Jiulize je hatua uliyonayo sasa siyo sehemu ya ukanda wa faraja? Kumbuka, mbegu ikidodoka ardhini ni lazima iote na kuzaa matunda, nami naiombea mbegu hii niliyodondosha kupitia neno la tafakari ya leo ipate kuzaa matunda mengi katika Maisha yako.
PS: Unaweza kujipatia maarifa kwenye elimu ya pesa kupitia usomaji wa vitabu. Chagua nakala za uchambuzi wa vitabu unavyotaka kwa kubofya kiunganisha hapo chini. Kila nakala ya uchambuzi wa kitabu inapatikana kwa gharama ya Tshs. 3,999. Wahi mapema hii ni OFA ya leo.
👇🏾👇🏾👇🏾👇🏾👇🏾
BOFYA HAPA KUPATA ORODHA YA UCHAMBUZI WA VITABU
Nakutakia kila la kheri kwenye siku hii ya
leo. Kumbuka husikose kutoa mrejesho wa kile ambacho unajifunza kutokana na
uwepo wako kwenye kundi hili.
BORN TO WIN ~ DREAM BIG
Mwalimu Augustine Mathias
Mawasiliano: 0763 745 451/0786 881 155/0629 078 410
Barua pepe: fikrazakitajiri@gmail.com