NENO LA SIKU_MACHI 23/2022: UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Nifanye Biashara Gani Ili Kukuza Pato Langu? Sehemu ya tano.
Rafiki na mfuatiliaji wa masomo ya mtandao wa Fikra za Kitajiri, hongera kwa kuwa na siku bora katika maisha yako. Siku ya leo naamini imekuwa siku muhimu ya kukusogeza kwenye kilele cha mafanikio unayotamani katika kipindi cha uhai wako.
Kujiunga kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI, TAFADHALI BOFYA HAPA
Karibu katika mwendelezo wa makala zinazokufunulia mbinu za jinsi gani unaweza kuwa tajiri kuanzia ngazi ya chini kabisa. Makala ya leo ni mwendelezo wa makundi ya biashara ambayo unaweza kuchagua kundi moja wapo na kuanzisha biashara ambayo itakuwezesha kukuza pato lako.
Ikiwa ni mara yako ya kwanza kufuatilia masomo haya nashauri usome makala zilizotangulia kupitia wavuti yetu ya FIKRA ZA KITAJIRI.
SOMA: UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Nifanye Biashara Gani Ili Kukuza Pato Langu? Sehemu ya Nne
Tuhitimishe kujifunza makundi ya biashara kwa kuangazia kundi la mwisho la Biashara mtandaoni (online or electronic business).
Hili ni kundi la mwisho kuelezewa siyo kwa umuhimu wake bali kutokana na makundi yote tuliyojifunza yanaweza kuhusisha biashara mtandao kama njia ya kufungua masoko mapya au kuongeza mauzo.
Biashara ya “Kielektroniki” au “Mtandaoni" ni aina yoyote ya shughuli za kibiashara inayohusisha ubadilishaji wa taarifa za biashara kwa njia ya mtandao.
Hivyo, shughuli yoyote inayohusisha ubadilishaji wa bidhaa au huduma kwa malipo kati ya mtu binafsi, kundi la watu au taasisi kupitia mtandao inafaa kutafsiliwa kama biashara mtandao.
Biashara ya kielektroniki inazingatia matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano ili kuwezesha shughuli za biashara nje ya uhusiano wa ana kwa ana kutokana na kuunganishwa na mtandao.
Biashara ya kielektroniki inatofautiana na makundi mengine ya biashara kutokana na shughuli za kuuza na kununua kukamilishwa kupitia mtandao.
Pia, e-business huwezesha kufanywa michakato yote ya biashara (usafirishaji wa ndani/nje, utengenezaji na uendeshaji, uuzaji na kununua, huduma kwa wateja) ndani ya mnyororo wa thamani kupitia mitandao ya ndani au nje.
Biashara mtandao ni fursa hai kwa kila mtu katika karne hii ya mapinduzi ya teknolojia ya mawasiliano. Kundi hili la biashara limezalisha na litaendelea kuzalisha mabilionea wengi kutokana na kukua kwa kasi ya watumiaji wa mtandao.
Mfano, mtandao wa First Site Guide unatoa takwimu zinaonesha kuwa kwa mwaka 2021 takribani “watu bilioni 1.79 walinunua vitu kupitia mtandao.” Katika kipindi hicho 70% ya biashara ndogo hadi za kati ziliwekeza zaidi katika matumizi ya mfumo wa biashara za kidijitali.
Mifano ya baadhi ya mabilionea ambao wamekuza utajiri wao kupitia matumizi ya biashara mtandao ni: Jeff Bezos, mmiliki wa Kampuni ya Amazon ambayo inajihusisha na kuuza na kununu bidhaa kwa njia ya mtandao; Jack Ma, mmiliki wa Kampuni ya Alibaba inayowezesha kuuuza na kununua kupitia mtandao; Bill Gates, mmiliki wa Kampuni ya Microsoft ambayo inajihusisha na uuzaji wa mifumo ya kompyuta; Mark Zuckerberg, mmiliki wa mitandao ya kijamii ya Facebook, Instagram na WhatsApp; Larry Page, mmiliki wa mtandao wa Google; Pierre Omidyar, mmiliki wa eBay; Garrett Camp, mmiliki wa mtandao wa Uber unaowezesha kuunganisha wateja na vyombo vya usafiri mjini.
Kwa hapa Tanzania, mitandao maarufu inayowezesha biashara mtandao ni pamoja na: KiKuu (uagizaji wa bidhaa kutoka China); Kupatana (mauzo mtandao ya bidhaa mbalimbali); Zoom Tanzania (mauzo ya bidhaa mtandaoni); na Bolt (kuunganisha wateja na usafiri mjini).
FAIDA ZA BIASHARA MTANDAONI. Kama ambavyo tuliona faida na changamoto za kila kundi la biashara, biashara mtandaoni ina faida zifuatazo:-
Huondoa vikwazo vya eneo na mipaka: Unapofanya biashara kwa njia ya mtandao ni rahisi kuuza kwa wateja nje ya eneo lako maana mtandao unakuunganisha watu kote ulimwenguni.
Pia, mtandao unakuwezesha kueneza taarifa za biashara yako kwa kasi na hupatikanaji wa taarifa hizo muda wote (masaa 24).
Hii ni tofauti na kuuza bidhaa au huduma kwa kuweka biashara yako kwenye pango la biashara.
Kwa mfumo wa kufanya biashara nje ya mtandao, unategemea kupata wateja wanaoweza kulifikia duka au huduma yako katika muda wako wa kazi.
Hupunguza muda na pesa zinazotumika: Kufanya biashara mtandao kunaondolea kodi za pango la eneo la biashara, umeme, maji na gharama gharama nyingi za uendeshaji.
Mfano, kwa teknolojia ya mtandao mtu mmoja aweza kuhudumia wateja zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja kwa kuunganishwa na teknolojia.
Pia, gharama za mawasiliano na matangazo zinapungua kutokana na teknolojia kuwezesha ujumbe maalumu wa biashara yako kusambazwa kwa watu wengi.
Huharakisha huduma kwa wateja: Huduma kwa Wateja kupitia mtandao ni rahisi ikilinganishwa na makundi mengine ya biashara.
Zaidi ya hayo, aina hizi za huduma kwa wateja zinazonyumbulika kwa kuwa zinaweza kufanyika zaidi ya saa za kazi za ikilinganishwa na makundi mengine ya biashara.
Pia, ni rahisi kutunza kumbukumbu za malalamiko au maoni ya wateja kuhusu bidhaa au huduma unazouza.
Urahisi wa kuanzisha: Biashara ya mtandao ni rahisi kuanzishwa maana haitaji uwe na mtaji mkubwa. Unaweza kuanzisha biashara hii hata ukiwa nyumbani kwako maana hitaji la msingi ni kifaa kilichounganishwa na mtandao na chenye programu maalumu za kuunganisha na wateja wako.
Ni rahisi kufanya tathimini: Kupitia ‘software’ maalumu za kuwezesha biashara mtandao ni rahisi kuwa na kumbukumbu muhimu za uendeshaji wa biashara yako. Hii nyenzo muhimu ya kufanya tathimini ya mwenendo wa biashara yako.
Mfano, ni rahisi kujua jinsi bidhaa au huduma yako imekuwa na manufaa katika nyakati tofauti kulingana na matukio muhimu katika kipindi cha mwaka mmoja. Kupitia taarifa hizo ni rahisi kujua matakwa ya wateja wa muda mrefu au kugundua ikiwa kuna wateja wapya.
Njia ya kuepuka usumbufu wa gharama za kodi na tozo: Unapofanya biashara yenye pango au eneo maalumu la biashara kuna kodi na tozo nyingi kulingana na kanuni za nchi husika.
Unapofanya biashara mtandao kuna baadhi ya kodi au tozo ambazo utafanikiwa kuzipunguza. Mfano, kupitia biashara mtandao hautoulizwa leseni ya Halmashauri au tozo za usafi n.k.
CHANGAMOTO. Kila kundi la biashara lina changamoto zake, biashara mtandaoni inakabiliwa na changamoto zifuatazo:-
Ukosefu wa muunganiko wa ana kwa ana: Unapofanya biashara mtandao unamnyima mteja fursa ya kukutana na muuzaji, kuchunguza au kuhojiana ana kwa ana kuhusu bidhaa au huduma zako.
Hii ni tofauti na utaratibu wa biashara uliozoeleka ambao humwezesha mteja kuchunguza au kuhoji kuhusu bidhaa au huduma kabla kufanya malipo.
Muda wa kusubiria: Unaponunua bidhaa mtandaoni ni lazima uwe tayari kusubiria kipindi cha muda wa siku kadhaa kabla ya kupokea bidhaa husika.
Hii ni tofauti na makundi mengine ya biashara ambapo mteja hupokea bidhaa yake pale anapokamilisha malipo.
Usalama na Uaminifu: Mtandaoni kuna wafanyabiashara waaminifu na baadhi wanafanya ulaghai unaopelekea watu kuogopa kufanya biashara kwa mtandao.
Pia, kukua kwa teknolojia kunaweza kupelekea udukuzi wa taarifa binafsi za mteja hali ambayo inatia doa uaminifu wa biashara za mtandaoni.
Baadhi ya wateja bado hawaamini biashara za mtandaoni kwa kutokana na uwepo wa ulaghai wa kila aina kwenye mitandao.
HITIMISHO. Kwa karne hii ambayo tunashuhudia ukuaji wa teknolojia ya mawasiliano, biashara mtandao ni fursa ambayo kila mfanyabiashara anatakiwa kuifahamu.
Dunia inahama kutoka kwenye mifumo ya kuuza na kununua kwa kutumia pesa taslimu na kuelekea kwenye malipo kwa njia mtandao.
Ni rahisi kufanya biashara mtandaoni maana wakati mwingine siyo lazima uwe na mtaji, siku hizi kuna watu wanaingiza pesa nyingi kwa kutangaza bidhaa za watu wengine (wamiliki wa maduka) na kisha kuuza mtandaoni na kurejesha halali ya mmiliki wa duka.
Pia, ni rahisi kuuza ujuzi au maarifa uliyonayo kupitia njia ya mtandao. Mfano, unaweza kuendesha semina au programu za mafunzo na kuziuza kwa njia ya makundi ya WhatsApp au majukwaa mengine.
NB. Wasiliana nami kwa ajili ya kupata mwongozo kwenye masuala ya udhibiti, bajeti na uwekezaji wa pesa zako kupitia WhatsApp +255 786 881 155.
JIPATIE NAKALA YA KITABU CHA MAISHA YENYE THAMANI
Kitabu hiki bado kinatolewa kwa bei ya OFA kwa kuchangia cha Tshs. 10,000/= tu! Utatumiwa kwa barua pepe au WhatsApp Nakala tete (soft copy) yenye fomati ya Pdf.
Kupata kitabu hiki, lipia kupitia Mpesa kwenye namba +255 (0) 763 745 451 au Airtel Money namba +255 (0) 786 881 155 au Halopesa namba +255 (0) 629 078 410 zote majina ni AUGUSTINE MATHIAS MUGENYI.
onclick='window.open(