UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Fahamu Mambo Ya Kuzingatia Unapoamua Kuwa Mjasiliamali

NENO LA SIKU_MACHI 15/2022: UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Fahamu Mambo Ya Kuzingatia Unapoamua Kuwa Mjasiliamali

Habari rafiki yangu na mfuatiliaji wa masomo ya mtandao wa Fikra za Kitajiri. Hongera kwa kuwa na siku bora ambayo naamini umeitumia kutekeleza majukumu muhimu yanayoongeza ushindi mdogo mdogo kwa ajili ya kuelekea kwenye kilele mafanikio katika maisha yako. 

Kujiunga kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI, TAFADHALI BOFYA HAPA

Karibu katika makala ya leo ambayo ni mwendelezo wa mafundisho juu ya jinsi gani unaweza kutengeneza utajiri kuanzia ngazi za chini kabisa. Makala hizi ni ufunguo kwa kila mtu mwenye kiu ya kuwa tajiri lakini mara kadhaa ameshindwa kufikia hadhima yake kutokana na kukosa miongozo sahihi. Hakikisha unafuatilia makala zilizopita kwa kutembelea wavuti yetu ya FIKRA ZA KITAJIRI.

SOMA: UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Anzisha Au Miliki Biashara Kama Njia Ya Kukuza Utajiri Wako

Katika makala iliyopita tulijifunza umuhimu wa kuanzisha biashara kama njia ya kukuza pato lako wakati unaendelea kutengeneza utajiri wa ndoto yako. Tuliona kuwa ni muhimu kuwa na ubunifu wa ziada katika kuzalisha na kuongeza thamani bidhaa au huduma na kisha kuziuza kwa faida.

Pia, tulijifunza sifa za mjasiriamali ambao ni msamiati unaotumika kujumuisha wafanyabiashara wengi katika jamii. Makala ya leo tutajifunza mambo muhimu ya kuzingatia unapochagua safari ya ujasiriamali kama njia yako ya kukuza kipato.

Karibu ujifunze mambo ya kuzingatia unapoinza safari yako ya ujasiriamali:-

Ubunifu: Sifa kuu ya mjasiriamali au mfanyabiashara yeyote ni kuwa mbunifu. Safari ya ujasiriamali haipo tambarare kama ambavyo wengi tumezoea, safari hii inahitaji vitendo zaidi kuliko nadharia.

Ni safari ambayo haina mara nyingi hubadilika kulingana na eneo, jamii au tamaduni. Katika mazingira kama hayo ni kawaida biashara ambayo uliiona sehemu au kuambiwa inalipa ikashindwa kufanya vizuri kwako.

Fursa moja inaweza kuwa fursa hai kwa mtu mmoja lakini fursa hiyo hiyo ikashindwa kuwa hai kwa mtu mwingine. Hapa ndipo mjasiriamali unatakiwa kuwa mbunifu katika kila fursa ya biashara unayoianzisha.

Ubunifu husaidia kuzalisha fursa mpya za utatuzi wa changamoto katika jamii na humwezesha mjasiriamali kuingiza bidhaa au mbinu mpya za uzalishaji na usambazaji katika soko. Unapochagua kufanya biashara huna budi kujiuliza utatumia mbinu zipi ambazo zitakuwa tofauti na mbinu za wafanyabiashara wengine katika soko unalolilenga.

Dhibiti hesabu za mtaji wako: Uhai wa biashara yoyote upo kwenye udhibiti wa fedha zinazoingia na kutoka. Mtiririko wa pesa (financial flow) kwenye biashara ni sawa na mzunguko wa damu ulivyo kwenye uhai wa mnyama.

Ikiwa hauwezi kudhibiti pesa inayoingia na kutoka ni dhahiri kuwa safari yako ya ujasiriamali ni fupi sana. Wajasiriamali waliofanikiwa ni wale ambao wanaelewa na kulinda mzunguko wa pesa kwenye biashara wanazofanya.

Pia, kuna mifano ya wajasiriamali wengi katika jamii zetu ambao biashara zao zimedumaa au zimefungwa kutokana na kushindwa kudhibiti pesa inayoingia na kutoka.

Mfano, tunashuhudia wajasiriamali ambao wanachukua mikopo lakini wanashindwa kusimamia mikopo hiyo na mwisho wake ni kufilisika. Tunashuhudia wajasiriamali ambao wameshindwa kupiga hatua kutokana na kushindwa kutofautisha hela ya mtaji na faida inayotengenezwa.

Hivyo, kabla ya kuchukua maamuzi yoyote kuhusu pesa kutoka kwenye biashara yako unatakiwa kujiridhisha kama maamuzi yako hayana athari kwenye uendelevu wa biashara yako.

Jiwekeze kwenye kukuza ujuzi na ustadi mbalimbali: Kuwa mjasiriamali ni kuwa mtu asiye na ubobevu kwenye fani moja. Ufanisi wa biashara na ukuaji kifedha unakuta uwe ujuzi na ustadi katika kila sekta ya biashara yako.

Unatakiwa kujifunza kuhusu pesa, uwekezaji, usimamizi, utawala, masoko, mauzo, uzalishaji, malighafi, usambazaji, huduma kwa wateja, na teknolojia mpya.

Mara nyingi mjasiriamali hujifunza zaidi ujuzi na ustadi mpya wa biashara yake pale anaposhiriki kwa vitendo kupitia shughuli za kila siku za biashara husika.

Unapokuwa na ujuzi na ustadi wa kutosha kuhusu biashara yako unakuwa kwenye nafasi nzuri kufanya maamuzi sahihi katika kila sekta ya biashara yako.

Hivyo, kama umechagua ujasiriamali kama njia ya kukuza kipato chako ni lazima uwe tayari kujifunza (learning) maarifa mapya na kuondoa maarifa (unlearn) yaliyopitwa na wakati. 

Uwezo wa kubeba hatari. Ikiwa hauna utayari wa kusafiri njia ambayo haijulikani, ni dhahiri kuwa katika safari ya ujasiriamali huwezi kugundua au kufanya kitu cha pekee.

Ikumbukwe kuwa tumeona ujasiriamali unakutaka uwe mbunifu wa mbinu au bidhaa mpya kwenye soko. Unapobuni mbinu ya kuingiza huduma au bidhaa mpya katika soko unakuwa umebeba hatari ya kusafiri katika mawazo ambayo ni wewe pekee ambae unaamini mawazo hayo.

Hakuna mtu mwingine anayeamini katika wazo, bidhaa au huduma yako isipokuwa wewe pekee. Hivyo, kama mjasiriamali ni lazima uwe tayari kubeba hatari hizo pale unapowekeza katika fursa mpya au wakati unachagua masoko mapya.

Mpango wa biashara. Pengine, hili ndilo jambo la muhimu zaidi kati ya mengine yote. Bila kuwa na mpango wa biashara yako ni njia ya kuelekea kwenye anguko la biashara husika.

Huwa kuna msemo kuwa; “kushindwa kupanga, unapanga kushindwa (failure to plan is plan to fail)." Mjasiriamali unatakiwa uwe na ramani ya ukuaji wa biashara yako katika hatua mbalimbali za ukuaji.

Unatakiwa uwe na mpango unaokuwezesha kuiona biashara yako katika kipindi cha mwaka mmoja, miaka mitano, miaka kumi na kuendelea.

Kupitia mpango huo, unatakiwa kuainisha rasilimali unazomiliki kwa sasa sambamba na jinsi zitakavyotumika kukuza mtaji wako. Fikiria jinsi gani unatavyofanikiwa kuepuka vikwazo sokoni au jinsi ya kukabiliana na washindani wako kibiashara.

Kujitangaza. Pamoja na umuhimu wa kuwa na ujuzi na ustadi mbalimbali, unatakiwa kujitangaza kwa kutumia mifumo na teknolojia zilizopo.

Unatakiwa kusambaza maudhui kuhusu wewe na bidhaa au huduma zako kwa kutumia kila fursa ya matangazo iliyopo. Unaweza kutumia podikasti, kuandaa vitabu, makala au mitandao ya kijamii.

Hapa ndipo unatakiwa kujiweka sawa kitaarifa kulingana na ulimwengu unaokuzunguka. Tumia faida ya ukuaji wa teknolojia kukuza mtaji na biashara yako kwa gharama nafuu.

Hitimisho. Njia ya kukuza utajiri kupitia biashara au ujasiriama ipo wazi kwako ikiwa umedhamiria kuishi tabia za wajasiriamali.

Kila mtu anaweza kuwa mjasiriamali bila kujali cheo au kazi anayofanya kwa sasa. Mwajiriwa unaweza kuwa mjasiriamali na ukaendelea na ajira yako ikitegemeana na fursa ya ujasiriamali utakayochagua.

Jambo la msingi kwa yeyote anayetaka kuwa mjasiriamali ni kujenga nidhamu ya kudhibiti mapato yake. Wengi wameshindwa kuanzisha biashara kwa kigezo cha mitaji lakini wengi wao wakiulizwa ni biashara gani wanataka kuanzisha unakuta hawana hata wazo la biashara.

Ikiwa hauna wazo la biashara hauwezi kutambua mtaji unaotakiwa na hatima yake ni kwamba utaendelea kulalamikia kuhusu ukosefu wa mtaji.

Pia, wengi wanajikwamisha kwa kusubiria mitaji mikubwa na kusahau kuwa kuna fursa ambazo zinahitaji mtaji mdogo ambao upo ndani ya uwezo wao. Maamuzi ya kuianzisha safari ya ujasiriamali yapo mikononi mwako sasa!


NB. Wasiliana nami kwa ajili ya kupata mwongozo kwenye masuala ya udhibiti, bajeti na uwekezaji wa pesa zako kupitia WhatsApp +255 786 881 155.


WAHI SASA UJIPATIE NAKALA YA KITABU CHA MAISHA YENYE THAMANI 

Kitabu hiki bado kinatolewa kwa bei ya OFA kwa kuchangia cha Tshs. 10,000/= tu! Utatumiwa kwa barua pepe au WhatsApp Nakala tete (soft copy) yenye fomati ya Pdf.


Kupata kitabu hiki, lipia kupitia Mpesa kwenye namba +255 (0) 763 745 451 au Airtel Money namba +255 (0) 786 881 155 au Halopesa namba +255 (0) 629 078 410 zote majina ni AUGUSTINE MATHIAS MUGENYI.




onclick='window.open(