NENO LA SIKU_MACHI 22/2022: UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Nifanye Biashara Gani Ili Kukuza Pato Langu? Sehemu ya Nne.
Hongera mpendwa rafiki yangu kwa kuendelea kufuatilia masomo ya Mtandao wa Fikra za Kitajiri. Naamini umekuwa na siku bora kwa ajili ya kuendelea kuboresha maisha yako.
Kujiunga kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI, TAFADHALI BOFYA HAPA
Karibu katika makala ya leo ambapo tutajifunza kundi la tatu la biashara ambayo unaweza kuanzisha kama njia mbadala ya kukuza pato lako.
Katika makala zilizopita tuliangalia makundi mawili yanayobeba biashara za aina mbalimbali ambazo unaweza kuchagua kundi mojawapo na kuanzisha biashara ya ndoto zako.
Kama hukufanikiwa kusoma makala hizo unaweza kufuatilia mfululizo wa makala zote kupitia wavuti yetu ya FIKRA ZA KITAJIRI.
Karibu katika makala ya leo ambapo tutajifunza kundi la biashara zinazohusiana na uzalishaji/utengenezaji wa bidhaa (product manufacturing).
Hili ni kundi la biashara ambalo linahusisha kubadilisha malighafi kwenda kwenye bidhaa au vitu ambavyo vinahitajiwa na watumiaji wa mwisho.
Ni biashara ambazo huongeza thamani ya vitu kupitia mabadiliko ya kiufundi, kimwonekano au kemikali, umbo, na ubora na kuzalisha bidhaa mpya kulingana na mahitaji ya watumiaji wa mwisho.
Tofauti kubwa ya biashara katika kundi hili na biashara za kundi la kuuza bidhaa ni; biashara ya utengenezaji wa bidhaa inahusika na kuzalisha bidhaa ambazo wachuuzi (merchants) huziingiza sokoni kwa watumiaji wa mwisho.
Mfano wa biashara hizi ni kama vile: utengenezaji wa vito vya thamani kutoka kwenye madini ghafi; utengenezaji wa vifaa vya samani kutoka kwenye mazao ya misitu; utengenezaji wa vinjwaji kutoka kwenye matunda au malighafi yoyote; utengenezaji wa nyuzi za vitambaa au kuzalisha nguo; uzalishaji wa vifaa vya ujenzi.
Pia, ifahamike kuwa siyo kila biashara huzalisha au kutengeneza bidhaa ambazo zipo tayari kuingizwa sokoni, kuna biashara ambazo unaweza kuzalisha bidhaa zitakazotumiwa kama malighafi na kampuni nyingine za ulizashaji au utengenezaji wa bidhaa.
FAIDA ZA BIASHARA YA KUZALISHA AU KUTENGENEZA BIDHAA. Kama ambavyo tuliona katika makundi ya biashara yaliyotangulia, biashara ya kuzalisha au kutengeneza bidhaa zako mwenyewe ina faida na changamoto zake. Baadhi ya faida za biashara katika kundi hili ni pamoja na:-
Gharama ndogo za uagizaji wa bidhaa: Unapozalisha bidhaa zako mwenyewe unapunguza gharama za usafirishaji wa bidhaa kwa kuwa wachuuzi hubeba gharama hizo kutoka eneo la uzalishaji hadi kwenye soko (kwa watumiaji wa mwisho).
Kupitia uzalishaji wa bidhaa unaokoa gharama za kusafirisha bidhaa ndani na nje ya nchi. Fikiria ni gharama kiasi gani ambazo wafanyabiashara (wachuuzi) wanaingia kwa kuagiza bidhaa nje nchi kama vile Uchina, Uturuki au Marekani.
Gharama ndogo za kuajiri: Wafanyakazi wengi wa viwandani ni wale wenye elimu au ujuzi wa kawaida ikilinganishwa na waajiriwa wengine kwenye kampuni za usambazaji na mauzo ya bidhaa.
Pia, kwa kuzalisha au kutengeneza bidhaa zako mwenyewe unazalisha ajira kwa vijana katika eneo lako la kiwanda. Hali hii itakuwezesha kupunguza ukosefu wa ajira kwa jamii inayokuzunguka ikiwa ni pamoja na ndugu au jamaa zako wa karibu.
Kuepuka gharama zinazotokana na gharama za kubadilisha fedha: Unapoagiza bidhaa nje nchi kuna ongezeko la gharama zinazotokana na kupanda na kushuka kwa viwango vya fedha za kigeni ikilinganishwa fedha za nchi yako.
Kutengeneza bidhaa zako katika nchi unayoishi kutakuondolea gharama za kila mara gharama zisizotabirika kutokana na viwango vya kubadilisha pesa.
Ni rahisi kuzalisha bidhaa zinazoendana na mahitaji ya wateja wako. Wafanya biashara wengi wanaingia hasara inayotokana na kuagiza mzingo wa bidhaa ambazo hazikidhi mahitaji ya watumiaji wa mwisho.
Kuna bidhaa ambazo unaweza kununua kwa matarajio ya kutengeneza faida lakini ukajikuta umelaza mtaji kutokana na bidhaa hizo kutokukidhi ubora wa viwango au mahitaji ya bei ya wateja wako.
Unapozalisha bidhaa zako mwenyewe ni rahisi kuhakikisha unalinda ubora sambamba na kuzalisha bidhaa kulingana na mahitaji ya watumiaji wa mwisho.
CHANGAMOTO. Biashara katika kundi hili kama ilivyo kwa makundi mengine zinakabiliwa na changamoto kama vile:-
Mtaji mkubwa. Ili uzalishe bidhaa zako mwenyewe unatakiwa uwe na mtaji wa kutosha kwa ajili ya kununua mashine za kutengeneza bidhaa sambamba na ujenzi wa kiwanda.
Kulinda viwango vya ubora. Kila bidhaa zinazozalishwa zinatakiwa kukidhi matakwa ya viwango vya ubora kulingana na kanuni za uzalishaji wa bidhaa husika.
Kwa hapa, Tanzania kabla ya kuzalisha bidhaa unatakiwa kuzingatia matakwa ya TBS ili bidhaa yako iruhusiwe kuuzwa ndani na nje ya nchi.
Upinzani wa kibiashara. Unapozalisha bidhaa zako mwenyewe una hatari ya kuhakikisha unamaliza changamoto za wazalishaji wengine katika sekta yako.
Ikumbukwe kuwa unapozalisha bidhaa mpya unakabiliwa na changamoto ya kushawishi wateja waamini bidhaa zako ikilinganishwa na bidhaa nyingine za aina hiyo katika soko.
Ugumu wa kupanua biashara yako. Kadiri biashara inavyokua, ndivyo matatizo yanaanza kutokea hasa kutokana changamoto za mashine kadri zinavyotumika zaidi (tering and wear).
Kuna gharama ambazo unatumia kurekebisha mitambo ambazo zingetumia kukuza biashara. Kuhakikisha kuwa vifaa vyako vinafanya kazi na pasipo kuchelewesha uzalishaji wa bidhaa ni mojawapo ya changamoto muhimu za ambazo unatakiwa kuzishinda.
Hitimisho. Ikiwa umeamua kufanya biashara fikiria kundi la biashara zinazohusiana na uzalishaji au utengenezaji wa bidhaa. Kila kundi la biashara ambalo tumejifunza hadi sasa lina changamoto na faida zake.
Hata hivyo, changamoto zipo kila sehemu na ndiyo maana hutakiwa kuogopa changamoto hizo ikiwa umejiridhisha kwenye uendelevu wa biashara ambayo umeichagua.
Hatua ya kwanza kabisa kama ambavyo tuliona katika makala zilizopita, ni kuhakikisha una tafiti za kutosha kuhusiana na biashara ambayo unataka kuingiza mtaji wako.
Kundi la biashara za kuzalisha au kutengeneza bidhaa zako mwenyewe ni kundi ambalo lipo hai kuwekeza bila kuogopa changamoto ambazo tumeainisha katika makala hii.
Pia, haupaswi kuogopeshwa na neno kiwanda maana unaweza kuanza na kiwanda kidogo na ukaendelea kukipanua taratibu hadi kufikia kiwanda kikubwa.
Mwisho, nakushauri kabla ya kuanzisha uzalishaji wa bidhaa huna budi kufanya tafiti za kutosha kabla ya kuzama kwenye biashara unayohisi ni fursa hai.
NB. Wasiliana nami kwa ajili ya kupata mwongozo kwenye masuala ya udhibiti, bajeti na uwekezaji wa pesa zako kupitia WhatsApp +255 786 881 155.
JIPATIE NAKALA YA KITABU CHA MAISHA YENYE THAMANI
Kitabu hiki bado kinatolewa kwa bei ya OFA kwa kuchangia cha Tshs. 10,000/= tu! Utatumiwa kwa barua pepe au WhatsApp Nakala tete (soft copy) yenye fomati ya Pdf.
Kupata kitabu hiki, lipia kupitia Mpesa kwenye namba +255 (0) 763 745 451 au Airtel Money namba +255 (0) 786 881 155 au Halopesa namba +255 (0) 629 078 410 zote majina ni AUGUSTINE MATHIAS MUGENYI.
onclick='window.open(