Hongera rafiki yangu kwa siku hii ambayo naamini imekuwa miongoni mwa siku bora kwako. Hapana shaka kuwa imekuwa siku bora ikiwa umeitumia kukamilisha mambo ya msingi hasa yale yanayochangia kwenye ukamilisho wa ndoto za maisha yako.
Kujiunga kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI, TAFADHALI BOFYA HAPA
Karibu katika makala ya siku ya ambayo ni mwendelezo wa maarifa muhimu kuhusu uwekezaji kwa ajili ya utajiri wa uhuru kipato ambao ni hitaji la watu wengi katika jamii.
Kama ndio umeanza kusoma makala hizi, nashauri ufuatilie makala zote ili kuwa na uelewa wa pamoja.
Kupitia makala ya leo, nitakushirikisha maarifa muhimu kuhusu uwekezaji katika hisa.
Unapofikiria kuwekeza kwenye hisa huna budi kujua yafuatayo:-
Nini maana ya hisa? Neno hisa katika uwekezaji hutumika kumaanisha sehemu ya umiliki wa mali (asset).
Ni mfumo wa uwekezaji ambao unawezesha watu kadhaa kumiliki mali kwa pamoja na kila mmiliki hutambuliwa kwa idadi ya hisa anazomiliki.
Mwenye hisa nyingi anakuwa na sauti ya kufanya maamuzi muhimu yanayohusu uendelevu wa kampuni ikilinganishwa na yule mwenye hisa chache.
Mfumo huu, unawezesha kampuni kukuza mtaji kutokana na kuuza hisa zake kwa wawekezaji mbalimbali (Wakubwa kwa wadogo).
Hivyo, kwa maneno rahisi hisa ni utambulisho wa maslahi ya kila mmiliki kwenye umiliki wa kampuni husika.
Hisa moja ni asilimia ndogo sana ya umiliki wa kampuni, unavyomiliki hisa kadhaa za kampuni unakuwa ni miongoni mwa wamiliki wa kampuni na una haki ya kushiriki katika maamuzi ya kampuni kupitia Mkutano Mkuu wa Wanahisa.
Biashara ya uwekezaji kwenye hisa inaratibwa vipi kwa hapa Tanzania?
Kwa Tanzania uwekezaji kwenye hisa unaratibiwa na kusimamiwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) kupitia Soko la Hisa la Dar es Salaam (Dar es Salaam Stock Exchange - DSE).
Mamlaka ya Masoko na Mitaji ni taasisi ya Serikali ambayo ipo chini ya Wizara ya Fedha na Uchumi.
Mamlaka hii ilianzishwa chini ya Sheria Na. 5 ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ya mwaka 1994 kwa lengo la kuanzisha, kusimamia na kuendeleza masoko ya mitaji na dhamana nchini.
Hivyo, Soko la Hisa la Dar es Salaam ni moja ya matunda ya mamlaka hii, na lilianzishwa kwa lengo la kuendesha biashara ya mitaji na dhamana (hisa, vipande, hatifungani na dhamana nyinginezo) kwa kampuni zote ambazo zimeoorodheshwa katika Soko hilo kwa ajili ya kuuza na kununua dhamana au kwa lugha ya kigeni 'securities'.
Soko hili hadi sasa lina jumla ya kampuni 29 ambazo zimeoorodheshwa kwa wawekezaji mbalimbali kununua hisa zake.
Nitafaidika vipi kutokana na kuwekeza kwenye hisa? Uwekezaji kwenye hisa una faida ya aina mbili.
Moja, faida kutokana na ongezeko la thamani ya hisa. Hii ni faida inayotokana na kupanda kwa thamani hisa ikilinganishwa na thamani ya hisa wakati unanua.
Mfano, kama nilinunua hisa za CRDB mwaka 2017 na thamani ya hisa moja ikiwa ni Tshs. 200 na mwaka 2022 nahitaji kuuza hisa zangu na thamani ya hisa moja ni Tshs. 350. Basi faida yangu kwa kila hisa niliyonunua ni Tshs. 150.
Hivyo, faida ya ongezeko la thamani ya hisa hupatikana pale unapounza hisa zako ikilinganishwa na bei uliyonunulia.
Hii ni faida ambayo watu utengeneza utajiri wa kutosha katika nchi zilizoendelea ambapo wawekezaji wenye ufahamu wa kutosha katika kutabiri mienendo ya hisa za kampuni katika masoko wananunua na kuuza hisa pale zinapopanda.
Mbili, faida kutokana na gawio (dividend). Hii ni faida kwa Mwekezaji ambayo hutokana na kiasi ambacho hutolewa kwa Wanahisa kwa muda fulani kulingana na faida iliyotengenezwa na kampuni husika katika kipindi hicho.
Kiasi cha gawio hukokotolewa na kugawanywa kwa Wanahisa kulingana na idadi ya hisa wanazomiliki. Mwenye hisa nyingi anapata gawio kubwa ikilinganishwa na mwenye hisa chache.
Nawezaje kununua hisa za kampuni? Hapa unatakiwa kujua hisa za Soko la awali (Initial Public Offer - IPO) na Hisa za Soko la pili.
Hisa za Soko la awali (IPO) ni mauzo ya hisa ya awali wakati kampuni inaroodheshwa kwenye soko la hisa.
Mauzo ya soko la pili, ni ununuzi wa hisa kutoka wamiliki ambao walinunua hisa hizo iwe kwenye soko la awali au Soko la pili.
Ikiwa unahitaji kununua hisa ambazo zinauzwa kwenye soko la awali kuna mawakala maalum ambao huwa wamepewa wajibu wa kuuza hisa za kampuni kwa wawekezaji wenye uhitaji.
Kama ni mwekezaji mwenye uhitaji unatakiwa kujaza fomu ya maombi na kukabidhi pesa kwa wakala kulingana na idadi ya hisa unazotaka kununua na utapewa stakabadhi pamoja na kikaratasi cha mwisho kwenye fomu yako kama uthibitisho wako na idadi ya hisa ulizonunua.
Ieleweke kuwa; mauzo ya hisa ya awali hutokea pale tu ikiwa kuna kampuni mpya ambayo inaingiza hisa zake kwa mara ya kwenye Soko la Hisa.
Ikiwa ni mwekezaji ambaye unahitaji kununua hisa kutoka katika soko la pili (DSE), inabidi uwaone madalali au mawakala wa soko la hisa (Brokers and Dealers).
Inashauriwa kabla ya kununua kama hauna taarifa za kutosha za kampuni zilizopo sokoni, ni vyema kuomba ushauri kwa mawakala au madalali wanaotambuliwa na CMSA, yaani madalali waliosajiliwa rasmi kwa kazi hiyo.
Dalali anatakiwa kukushauri na kisha ufanye maamuzi mwenyewe.
Ufuatao ni utaratibu wa kuuza na kununua hisa katika soko la pili (DSE):-
Ununuzi wa hisa; Mwekezaji anayetaka kununua hisa anatakiwa kufuata taratibu zifuatazo:-
- Wasiliana na dalali wa soko la hisa na kumweleza kusudio lako la kununua hisa
- Jaza fomu maalum za kununua hisa na kulipia hisa unazotaka kununua
- Dalali ataweka fedha kwenye akaunti maalum ya benki kwa ajili ya kununua na kuuza hisa za wateja
- Dalali ataweka oda yako ya kununua hisa kwenye mfumo wa kompyuta wa soko la hisa akitumia namba maalum ya mteja
- Iwapo bei unayotaka kununulia hisa itafanana na bei ya mwekezaji mwingine anayetaka kuuza, basi atakuwa amekununulia hisa hizo
- Kisha baada ya ununuzi kukamilisha utapokea cheti cha kuthibitisha kuwa ni mwekezaji kwenye kampuni husika
Kuuza hisa; Ikiwa unahitaji kuuza hisa unazomiliki kwenye kampuni fulani unatakiwa kufuata utaratibu ufuatao:-
- Wasiliana na dalali wa soko la hisa na kumweleza kusudio lako la kuuza hisa
- Kabidhi hati yako ya umiliki wa hisa kwa dalali
- Dalali atahakiki umiliki wa hisa hizo kabla ya kuuza.
- Dalali ataweka oda yako ya kuuza hisa kwenye mfumo wa kompyuta wa soko la hisa akitumia namba maalum ya mteja
- Iwapo bei unayotaka kuuzia hisa itafanana na bei ya mwekezaji mwingine anayetaka kununua, basi atakuwa amekuuzia hisa hizo na utalipwa pesa zako
Pia, kulingana na ukuaji wa teknolojia mwekezaji anaweza kununua au kuuza hisa kupitia mfumo wa simu ya mkononi kwa kupiga *150*36# na kisha kufuata maelekezo.
Hitimisho
Uwekezaji kwenye hisa inafahamika kwa watu wachache sana. Pia, vijana wengi hawavutiwi na uwekezaji wa hisa kwa vile walio wengi wanataka utajiri wa haraka. Uwekezaji wa hisa unabadirika kila wakati na hivyo ni uwekezaji ambao kabla ya kuwekeza unahitaji kufahamu mabadiliko ya namna hiyo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba soko la hisa linaendeshwa na hisia za wanunuaji pamoja na wauzaji wa hisa. Kutokana na biashara hii kuendeshwa kwa hisia, tukio la ghafla linaweza kushusha au kupandisha thamani hisa na kupelekea kufilisika au kutajirika kwa kampuni husika na Wanahisa wake. Unapoamua kununua au kuuza hisa fanya hivyo kwa dhana ya kuwa bei ya wakati huo ni halisi kwa maana ya kwamba hisa husika haiuzwi kwa bei ya juu/chini kuliko thamani yake. Hata hivyo, unahitaji kukumbuka kuwa hata kama bei ni halisi bado bei hiyo si ya uhakika kwani inaweza kubadilika ndani ya masaa au siku.
NB. Husisite kuwasiliana nami ikiwa unahitaji mwongozo zaidi juu ya jinsi gani unaweza kujiunga na Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja. Nitumie ujumbe kupitia WhatsApp +255 786 881 155.
WAHI SASA UJIPATIE NAKALA YA KITABU CHA MAISHA YENYE THAMANI
Kitabu hiki bado kinatolewa kwa bei ya OFA kwa kuchangia cha Tshs. 10,000/= tu! Utatumiwa kwa barua pepe au WhatsApp Nakala tete (soft copy) yenye fomati ya Pdf.
Kupata kitabu hiki, lipia kupitia Mpesa kwenye namba +255 (0) 763 745 451 au Airtel Money namba +255 (0) 786 881 155 au Halopesa namba +255 (0) 629 078 410 zote majina ni AUGUSTINE MATHIAS MUGENYI.