UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Fahamu Kuhusu Mifuko Ya Uwekezaji Wa Pamoja

NENO LA SIKU_MACHI 02/2022: UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Fahamu Kuhusu Mifuko Ya Uwekezaji Wa Pamoja.


Rafiki yangu na mfuatuliaji wa mtandao wa Fikra za Kitajiri hongera kwa siku hii muhimu katika historia ya maisha yako. Siku ya leo ni miongoni mwa siku ambazo kila siku nakukumbusha kuzitumia kwa ajili ya kujenga mnara wa mafanikio unayotamani. 

Tumia dakika kadhaa kujiuliza imeitumia vipi siku ya leo ikilinganishwa na ndoto za maisha yako. Ikiwa yale uliyofanya hayana uhusiano na ndoto za maisha yako tambua kuwa unatakiwa kubadilika kuanzia sasa.

Kujiunga kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI, TAFADHALI BOFYA HAPA

Karibu katika makala ya leo yenye lengo la kupanua uelewa wako kuhusu Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja (Mutual/Collective Investment Fund). Makala hii ni mwendelezo wa makala zinazokuletea mafundisho kuhusu siri za utajiri na jinsi gani unaweza kutumia siri hizo kubadilisha hali ya pato lako. 


Kabla ya kujua Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja inafanyaje kazi, kwanza tuelewe maana yake. Mifuko ya Uwekezaji wa pamoja ni aina ya Uwekezaji ambapo kuna kampuni inayokusanya pesa (mitaji) kutoka kwa wawekezaji mbalimbali na kuwekeza pesa hizo katika dhamana kama vile hisa, dhamana na hatifungani za muda mfupi. 

Mara nyingi Uwekezaji huu unakusanya mitaji ya Wawekezaji wadogo ambao hununua vipande (unit) kwenye aina ya mifuko waliyowekeza na kampuni hutumia mitaji yao kuwekeza kwa niaba yao. 

Kila mwekezaji kiasi anachowekeza hugawanywa kwenye vipande (units) kulingana na thamani ya kipande (unit) cha Mfuko husika wakati anaanza kuwekeza. 

Hivyo, kadiri thamani ya mfuko inavyoongezeka au kupungua ndivyo thamani ya kipande huongezeka au kupungua. 

Thamani ya kipande inavyoongezeka ndivyo thamani ya Uwekezaji kwa kila mwekezaji huongezeka kulingana na idadi ya vipande anavyomiliki. Yaani, idadi ya vipande inategemea bei ya ununuzi wa kipande, wakati wa uwekezaji na kiwango cha pesa kilichowekezwa.  

Uwekezaji katika Mifuko hii ni rahisi na salama kwa mwekezaji yeyote ambaye ana malengo ya Uwekezaji wa muda mfupi, kati au muda mrefu. 

Ni Uwekezaji ambao unafaa kwa watu ambao wanakusanya mtaji kwa njia ya kudunduliza (kukusanya kidogo kidogo) au kukusanya pesa kwa malengo ya kukidhi mahitaji maalumu ya maisha.

Kuna njia mbili za kufaidika na Uwekezaji katika Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja; njia ya kwanza ni ongezeko la thamani ya kipande na njia nyingine ni gawio la mapato ambalo hutokana na kukua kwa thamani ya Mfuko kutokana na uwekezaji wa pamoja. 

Muhimu! Siyo Mifuko yote ambayo hutoa gawio, baadhi ya Mifuko faida hutegemea upande mmoja tu wa ongezeko la thamani ya kipande. 

Faida kutokana na ongezeko la thamani ya kipande hukokotolewa kwa kuhakikisha kila kipande kinapata mapato sawa, yaliyotokana na kiwango kilichowekezwa kama mtaji katika kipindi husika. 

Mfano, kama Mfuko X thamani ya kipande chake kwa mwaka 2019 ilikuwa Tshs. 100 na kwa mwaka 2022 thamani ya kipande katika Mfuko huo ni Tshs. 112. 

Tafsiri yake ni kwamba thamani ya Mfuko X imeongezeka kwa Tshs. 12 na kila mwekezaji ambaye aliwekeza pesa zake kwa kipindi hicho kila kipande anachomiliki kimeongezeka thamani kwa Tshs. 12.

Kwa hapa Tanzania, Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja huendeshwa na UTT - AMIS ambao ndiyo Wasimamizi wa Mfuko hii. 

Kampuni ya UTT AMIS inasimamia Mifuko sita ya uwekezaji wa pamoja ambayo ni Mfuko wa Umoja, Mfuko wa Wekeza Maisha, Mfuko wa Watoto, Mfuko wa Kujikimu, Mfuko wa Ukwasi na Mfuko wa Hati Fungani. 

UTT AMIS ilianzishwa na Serikali mwaka 2003 na awali ilijulikana kama Dhamana ya uwekezaji Tanzania (UTT) ambayo ilianzishwa chini ya Sheria ya Udhamini (Sheria ya Dhamana Na. 318) na kupewa majukumu kadhaa muhimu ikiwa ni pamoja na Kuanzisha na kuendesha mifuko ya uwekezaji wa pamoja katika njia ambayo itaongeza thamani ya mifuko hiyo, kuhamasisha watu kujenga utamaduni wa kuweka akiba kupitia ushiriki mpana katika umiliki wa vipande. 

Kampuni hii inaendeshwa na Bodi ya Wakurugenzi inayoundwa na wataalamu wenye taaluma mbalimbali na uzoefu kwenye soko la fedha na mitaji. 

Kuna faida gani za kuwekeza kwenye Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja? Zipo faida nyingi za Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja na baadhi yake ni:-

Kuruhusu Uwekezaji Mseto (Diversification). Wasimamizi wa Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja hugawanywa mitaji ya wawekezaji kwenye uwekezaji wa aina mbalimbali. 

Mgawanyiko wa mitaji hupunguza hatari ya kuwekeza kwenye aina moja ya uwekezaji na kuongeza nafasi ya kukuza thamani ya Mifuko. 

Pia, kwa kuruhusu umiliki wa wawekezaji wengi kunatoa nafasi ya kukuza mtaji wa Mfuko ambao huwekezwa sehemu tofauti. 

Kwa njia hii, siyo rahisi kupoteza thamani yote ya uwekezaji wa Mfuko pale ambapo sehemu moja ya uwekezaji inaenda tofauti au kupitia misukosuko kwenye soko la uwekezaji wa mitaji. 

Usalama wa mitaji. Mifuko ya uwekezaji wa pamoja inaratibiwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na inadhibitiwa na sheria ya mifuko ya uwekezaji wa pamoja yenye lengo la kumlinda mwekezaji. 

Kanuni hizi zinahusiana na shughuli za kampuni za Usimamizi/Uwendeshaji wa mifuko ya uwekezaji wa pamoja. Hivyo, kila mwekezaji dhamana zake zinatambuliwa na kulindwa kwa mujibu wa Sheria na taratibu za nchi.

Usimamizi wa Kitaalamu. Wawekezaji wengi hawana muda, rasilimali au maarifa ya kutosha kuhusu masoko ya mitaji ambayo ni fursa ya Uwekezaji kwa kila mtu. Hapa ndipo usimamizi wa kitaalamu unaofanywa na Wasimamizi wa Mifuko (UTT - AMIS) unakuwa wa muhimu sana. 

Wasimamizi hawa husaidia kusimamia, kuchagua sehemu za kuwekeza na kufuatilia uwekezaji kila wakati na kurekebisha kwa kadri ipasavyo ili kufikia malengo ya wawekezaji. 

Hii ni faida kubwa kwa mwekezaji kwa kuwa husaidia kuongeza kipato cha mwekezaji.

Unafuu wa kuwekeza na kujiondoa. Ni rahisi kujiunga na kujiondoa kwenye Uwekezaji huu kulingana na malengo ya mwekezaji. 

Unaweza kufungua akaunti siku moja na siku hiyo hiyo ukanunua vipande kwa kadri ya mpango wako wa Uwekezaji. 

Pia, unaweza kuuza vipande vyako vyote au sehemu ya vipande vyako kulingana na masharti ya Mfuko ambao umechagua kuwekeza. 

Pia, Mifuko ya uwekezaji wa pamoja inakupa unafuu wa kununua hisa za makampuni yanayofanya vizuri. 

Mwekezaji ana uwezo wa kupata hisa zote ambazo mfuko umewekeza kwa ununuzi mmoja.

Ukwasi (liquidity). Mwekezaji anaweza kuwekeza kwa muda mrefu au mfupi kulingana na sifa za mfuko. 

Mwekezaji ana uwezo wa kuamua wakati anaotaka kuuza vipande pia kupata pesa za mauzo ya vipande kwa muda mfupi. 

Kwa kuwa uwekezaji ni zoezi la muda mrefu, wawekezaji wanashauriwa kuwa na mtazamo wa muda mrefu ili kunufaika zaidi na uwekezaji.

Nihitimishe kwa kusema; ikiwa umeamua kujilipa kwanza, Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja ni sehemu sahihi ya kuwekeza pesa unazojilipa. Mifuko hii ni mizuri kwa kuwa inapokea wawekezaji wa kila aina (Wakubwa na wadogo). Mifuko hii kibubu kwa wawekezaji wadogo ambao wana kiu ya kukuza mitaji yao. 

NB. Husisite kuwasiliana nami ikiwa unahitaji mwongozo zaidi juu ya jinsi gani unaweza kujiunga na Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja. Nitumie ujumbe kupitia WhatsApp +255 786 881 155.

WAHI SASA UJIPATIE NAKALA YA KITABU CHA MAISHA YENYE THAMANI 
Kitabu hiki bado kinatolewa kwa bei ya OFA kwa kuchangia cha Tshs. 10,000/= tu! Utatumiwa kwa barua pepe au WhatsApp Nakala tete (soft copy) yenye fomati ya Pdf.

Kupata kitabu hiki, lipia kupitia Mpesa kwenye namba +255 (0) 763 745 451 au Airtel Money namba +255 (0) 786 881 155 au Halopesa namba +255 (0) 629 078 410 zote majina ni AUGUSTINE MATHIAS MUGENYI.
onclick='window.open(