UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Fahamu Jinsi Ya Kukuza Pato Lako

NENO LA SIKU_MACHI 11/2022: UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Fahamu Jinsi Ya Kukuza Pato Lako

Ni siku nyingine ambayo naamini imekuwa bora kwako kwa kuwa umeweza kutekeleza majukumu ya msingi. Hongera rafiki yangu na mfuatuliaji wa masomo ya mtandao wa Fikra za Kitajiri kwa kuendelea kujenga mnara wa mafanikio unayotamani kupitia matendo yako ya kila siku. 

Kujiunga kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI, TAFADHALI BOFYA HAPA

Karibu katika makala ya leo ambayo ni mwendelezo wa mafundisho kuhusu safari ya kutengeneza utajiri kuanzia ngazi ya chini kabisa. Makala hizi ni kwa ajili ya kila mtu mwenye kiu ya kuwa na uhuru wa kifedha katika maisha yake.

Zaidi ni kwamba mfululizo wa makala hizi ni kwa ajili ya watu wote ambao wanatamani utajiri lakini hawana mwongozo sahihi juu ya jinsi gani wanaweza kuanza safari ya kujenga mnara wa utajiri wa ndoto zao.

Katika makala ya jana, tulijifunza aina kuu tatu za mapato ambazo kila mtu anaweza kuzitumia kukuza utajiri wake. Kupitia makala ya leo tutajifunza mbinu ambazo za wazi kwa ajili ya kukuza pato lako.

SOMA: UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Tumia Aina 3 Za Kipato Kukuza Utajiri Wako

Ieleweke kuwa naendelea kuweka msisitizo kwenye kukuza pato lako maana huu ni ugonjwa ambao unaendelea kuwakwamisha watu wengi kupiga hatua kuelekea kwenye uhuru wa kifedha.

Ni wazi kuwa ukiuliza watu wengi kwa nini hawana bajeti kwa ajili ya akiba na uwekezaji ni dhahiri jibu la moja kwa moja utaambiwa kipato hakitoshi. Hivyo, njia pekee ambayo itakuwezesha kuianza safari ya utajiri wa ndoto yako ni kufikiria mbinu na njia mbadala za kukuza pato lako.

Njia moja ya kujiimarisha kwenye bajeti ya akiba na uwekezaji ni kupata pesa zaidi au kuziba maeneo ambako pesa yako imekuwa ikivuja (kuondoa matumizi yasiyo ya lazima). Mara nyingi katika hatua za awali za kuanza safari ya utajiri huwa ni ngumu kukuza pato lako kwa kuongeza njia mpya za mapato (mifereji mipya ya kipato).

Kumbe, jambo la kwanza unatakiwa uanze na kudhibiti kile ambacho una uhakika nacho kwa maana ya pato lako halisi ambalo tayari una uhakika nalo. Pamoja na hayo, pale inapowezekana unaweza kutumia mbinu zifuatazo kukuza pato lako:- 

Kuongeza muda zaidi wa kufanya kazi. Kupitia mbinu hii tunatakiwa kufahamu maana halisi ya maneno: ‘muda ni mali’. Muda ni mali endapo unatumika kwa ajili ya kuzalisha pesa.

Ikiwa pato lako kwa sasa linapatikana kupitia muda wa masaa nane na nusu kwa siku (kama ilivyo kwa waajiriwa wengi), ili ukuze pato lako huna budi kujiuliza ni jinsi gani utatumia masaa yanayobakia katika siku kwa ajili ya kuzalisha kipato cha ziada.

Unapaswa kuongeza muda wa kufanya kazi (extra duty) nje ya muda uliozoleka ili upate kuzalisha pato la ziada. Mbinu hii pia inaweza kutumiwa na Mfanya biashara kwa kuongeza masaa kadhaa ya kuwahi kufungua biashara au kuchelewa kufunga kulingana na aina ya biashara.

Muhimu! Iwe mfanya biashara, mwajiriwa, fundi au mkulima; jambo la msingi kunufaika na mbinu hii ni kufikiria jinsi gani utaongeza muda wa kufanya kazi ili uongeze uzalishaji wa ziada ikilinganishwa na mazoea yako ya awali.

Tumia vipaji na karama ulizojaliwa kuzalisha pesa nje ya utaratibu uliozoeleka. Kipaji au karama ni pesa ambayo imelala inasubiriwa itumike katika muda na nyakati sahihi.

Watu wengi wanashindwa kufaidika na vipaji walivyojaliwa kutokana na mazoea ya kutumia mbinu ambazo zinatumiwa na kila mtu katika kuzalisha pesa.

Hakuna anayekuzuia wewe kama mfanya biashara au mwajiriwa au mtu yoyote yule kutumia kipaji cha ziada nje ya kazi inayokuzalishia pesa.

Kuna watu wana vipaji vya utangazaji (MCs), kuimba, vichekezo, utunzi au uandishi wa vitabu na makala lakini wameacha vipaji hivyo viendelee kusinzia ndani mwao.

Kuna watu wana fani nzuri za ususi, mapishi ya kila aina, uwezo wa kufundisha (iwe kwenye mitandao), ubunifu wa mitandao au ujuzi wa kupamba kumbi lakini wanashindwa kutumia fani hizo kuzalisha pesa za ziada.

Kwa ujumla kupitia mbinu hii, unatakiwa kujiuliza una kipaji kipi ambacho hadi sasa hakitumiki kuzalisha pesa japo ni kipaji ambacho hakihitaji gharama kubwa kukiendeleza.

Ongeza elimu. Makazini kuna watu wanashindwa kupanda madaraja au kupandishwa vyeo kutokana na kukosa sifa za kiwango cha elimu.

Ikiwa ni mmoja wa watu kama hao na uhakika kuwa endapo utaongeza kiwango cha elimu utapandishwa cheo au kupandishwa daraja huna budi kufikiria kurudi darasani kama njia ya kukuza pato lako.

Hata hivyo, bila kujali wewe ni mwajiriwa ambaye unahitaji kupandishwa cheo, elimu kama mbinu ya kukuza pato inaweza kutumiwa na kila mtu.

Kila mtu anaweza kuongeza kipato chake kwa kuongeza ujuzi zaidi katika sehemu yake ya kazi. Teknolojia inakua na husipo badilika kulingana na mabadiliko ya teknolojia ni dhahiri kuwa utaendelea kuachwa nyuma kila siku.

Hivyo, kila mtu anaweza kuongeza ujuzi kwenye sehemu yake ya kazi au biashara kupitia mbinu mbalimbali za kujifunza. Unaweza kushiriki mafunzo ya muda mfupi, semina au kununua kitabu kwa ajili ya kujifunza ujuzi mpya ambao utaongeza kitu cha ziada kwenye pato lako.

Ongeza idadi ya wazalishaji. Ikiwa unaweza kuongeza uzalishaji zaidi kwa kuongeza idadi ya wafanyakazi kwa gharama nafuu, basi tumia mbinu hii kukuza pato lako. Hata hivyo, kabla ya kuongeza uzalishaji ni lazima uwe na uhakika wa soko la bidhaa utakazozalisha zaidi.

Pia, mbinu hii inaweza kutumiwa na familia ambazo zina watu wengi lakini wanao husika kwenye uzalishaji wa pato la familia ni wachache.

Mfano, kuna familia nyingi ambazo uzalishaji wa pato la familia upo mikononi mwa baba au mama pekee. Kwa familia za aina hii unaweza kuongeza chanzo kipya cha mapato ambacho kitasimamiwa na mmoja wa wanafamilia (baba, mama au mtoto) kwa usimamizi wako wa karibu.

Ongeza aina mpya ya kipato. Katika makala ya jana tulijifunza aina tatu za kipato. Ili kuongeza zaidi pato lako huna budi kujiuliza kwa sasa unategemea aina zipi za kipato na kuangalia uwezekano wa kuongeza njia mpya ya kipato ambayo itakuwa ni mfereji mpya wa kuingiza pesa.

Kama unategemea pato hai (active income) fikiria kuhusu pato tulivu (portfolio income) au pato endelevu (passive income). 

Hitimisho. Unapoamua kuchukua hatua za ziada kwa ajili ya kukuza kipato chako, hakikisha kuwa umedhamiria na una nia sahihi. Ushindi katika kila kitu unaanzia kwenye dhamira ya kweli na kisha nia sahihi.

Dhamira pamoja na nia vitakusukuma kuendelea na safari ya kukuza pato lako bila kushawishika kurudi nyuma.

Njia ya utajiri ipo mikononi mwako, utafanikiwa kuwa tajiri ikiwa utajielewa unataka nini na upo tayari kufanya nini kwa ajili ya kubadilisha mazoea ya maisha ya sasa.

NB. Wasiliana nami kwa ajili ya kupata mwongozo kwenye masuala ya udhibiti, bajeti na uwekezaji wa pesa zako kupitia WhatsApp +255 786 881 155.


WAHI SASA UJIPATIE NAKALA YA KITABU CHA MAISHA YENYE THAMANI 


Kitabu hiki bado kinatolewa kwa bei ya OFA kwa kuchangia cha Tshs. 10,000/= tu! Utatumiwa kwa barua pepe au WhatsApp Nakala tete (soft copy) yenye fomati ya Pdf.


Kupata kitabu hiki, lipia kupitia Mpesa kwenye namba +255 (0) 763 745 451 au Airtel Money namba +255 (0) 786 881 155 au Halopesa namba +255 (0) 629 078 410 zote majina ni AUGUSTINE MATHIAS MUGENYI.


onclick='window.open(