UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Nifanye Biashara Gani Ili Kukuza Pato Langu? Sehemu ya Pili

NENO LA SIKU_MACHI 17/2022: UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Nifanye Biashara Gani Ili Kukuza Pato Langu? Sehemu ya Pili.

Habari rafiki yangu na mfuatiliaji wa masomo ya Mtandao wa Fikra za Kitajiri. Ni fahari kwangu kuona unaendelea kujifunza masomo mahsusi yanayolenga kubadilisha maisha yako.

Mtandao wa Fikra za Kitajiri umedhamiria kukuletea masomo yatakayo badilisha maisha yako kwa ujumla ikiwa hata hivyo utaamua kuweka masomo haya katika vitendo kupitia maisha yako ya kila siku. 

Kujiunga kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI, TAFADHALI BOFYA HAPA

Karibu katika makala ya leo ambayo ni mwendelezo wa masomo kuhusu jinsi unavyoweza kukuza kipato chako na hatimaye kutengeneza utajiri wa ndoto zako.

Katika makala ya jana tulijifunza kuhusu umuhimu wa kufanya tathimini kuhusu soko unalolilenga kabla ya kuingiza bidhaa au huduma kwenye soko husika.

Tuliona umuhimu wa kuchagua sehemu sahihi sambamba na kuhakikisha unaingiza sokoni bidhaa au huduma inayokidhi mahitaji ya nyakati au teknolojia katika soko husika. Kusoma mfululizo wa makala zilizotangulia  tembelea wavuti yetu ya FIKRA ZA KITAJIRI.

SOMA: UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Nifanye Biashara Gani Ili Kukuza Pato Langu? Sehemu ya Kwanza.

Katika makala ya leo inafungua mfululizo wa makala zinazoelezea makundi ya biashara ambayo unaweza kuchagua kama njia mbadala ya kukuza pato lako.

Ieleweke kuwa kabla ya kufanya biashara yoyote ni vyema uhakikishe unawekeza zaidi kwenye kujifunza kuhusu biashara husika.

Zipo biashara ambazo zinahitaji ujuzi au ustadi maalumu; zipo biashara ambazo unalazimika kufahamu muundo wa jinsi gani zinafanya kazi; kuna biashara ambazo unalazimika kufahamu mzunguko wa uzalishaji na usambazaji wa bidhaa/huduma; kuna biashara ambazo unatakiwa kujiridisha kwenye uhakika wa upatikanaji wa malighafi au bidhaa; zipo biashara ambazo unatakiwa kufahamu kanuni na sheria na sheria maalumu zinazoongoza utaratibu wa kuendesha biashara husika kisheria; na zipo biashara ambazo unatakiwa kujua mtazamo, mila na tamaduni za wateja unaowalenga (targeted customer). 

Baada ya kujifunza kwa mapana kuhusu biashara yako na soko lake, hapa chini nakushirikisha la kwanza la biashara ambapo miongoni mwa biashara katika kundi hilo unaweza kuchagua mojawapo ya biashara inayokufaa:-

Biashara zinazo husiana na utoaji huduma (Service related business). Hili ni kundi la biashara ambalo linahusisha utoaji huduma katika soko ambalo umechagua.

Kila mtu ana ujuzi au kipaji ambacho ni cha thamani kubwa kwa wengine pale ambapo ujuzi au kipaji hicho hutumika kutatua changamoto za watu katika eneo linalokuzunguka.

Kwa ujumla, kundi hili linahusisha biashara zote ambazo zinauza rasilimali au vitu ambavyo havishikiki (non-tangible property).

Mfano, biashara ya ‘saloon’ za kike au kiume; huduma za masaji ya mwili; huduma za mazoezi ya viungo; ushauri wa kitaalamu ambao unaweza kutolewa ana kwa ana au kwa njia ya simu au mtandao; huduma ya ufundi magari, TV/Radio au ushonaji; huduma za usafi majumbani au kwenye taasisi; huduma za utunzaji wa watoto au wazee (child or elder care); huduma za elimu ya awali, msingi, sekondari au vyuo; na huduma za kwenye matukio (kupamba kumbi za sherehe, upigaji picha au video, kusherehesha, kuimba, kukodisha kumbi, magari au vifaa vya matukio ya kijamii); au huduma za usafirishaji. 

Faida. Zipo faida nyingi za biashara zinazo husiana na utoaji huduma na miongoni mwa faida hizo ni pamoja na;  

Mtaji mdogo. Baadhi ya biashara za utoaji huduma hazihitaji mtaji mkubwa wa kuanzisha biashara. Baadhi ya biashara hizi siyo lazima uwe na pango au kujenga jengo kama ilivyo kwenye biashara nyingine za viwanda.

Mtaji mkubwa wa biashara hizi ni kipaji, ustadi, ujuzi au maarifa na wakati mwingine gharama za kujitangaza. Hata hivyo, zipo biashara za utoaji huduma ambazo utalazimika kuwa sehemu maalumu ya biashara kulingana na aina ya huduma unayotoa. 

Gharama ndogo za uzalishaji. Sio lazima kutengeneza bidhaa hivyo hakuna gharama zinazotokana na mabadiliko ya bei za kununua malighafi.

Pia, baadhi ya biashara siyo lazima ukaguliwe na mamlaka za serikali kama sehemu ya kudhibiti viwango vya huduma zako.

Mara nyingi ili kulinda ubora wako katika soko mdhibiti mkubwa wa viwango vya huduma unazotoa ni wewe mwenyewe.

Urahisi wa kutoa huduma kulingana na mahitaji ya mteja. Tofauti na biashara nyingine, biashara ya utoaji huduma inaweza kubadilishwa kwa urahisi kulingana na  matakwa ya mteja.

Kwa mfano, biashara ya saloon ya kike inaweza kubadilisha mitindo ya kusuka kulingana na mahitaji ya wateja wake kwa wakati husika. Vivyo hivyo, upambaji wa kumbi utabadilika kulingana na aina ya tukio au mahitaji ya mteja.

Urahisi wa kuongeza mauzo kutokana na hisia za wateja. Moja ya sifa bora kuhusu biashara za huduma ni kwamba zinaweza kuanzishwa katika sekta yoyote au eneo lolote.

Tafsiri yake ni kwamba ni rahisi kupata fursa zinazoendana na hisia za wateja katika soko lako. Kadri unavyotoa huduma bora kwa wateja ndivyo unateka hisia za wateja wako na kufanikiwa kueneza sifa zako kwenye soko lako. 

Ni njia ya kutumia kipaji au ujuzi wako kukuza kipato chako. Kwa kuwa ujasiriamali wa utoaji huduma mara nyingi unahusu kuuza ujuzi, ustadi, maarifa au kipaji chako badala ya bidhaa halisi au vitu, ni njia ya kukuza kipato kutokana karama ulizojaliwa.

Katika makundi mengine ya biashara mara nyingi unalazimika kuanza na mtaji wa pesa hila kwenye utoaji huduma unaweza kuanza kukuza mtaji kwa kutumia kipaji chako.

Mfano, kuna vijana wengi ambao nawafahamu wamefanikiwa kukuza mitaji yao na kuwekeza kwenye biashara nyingine kupitia huduma ya kusafisha na kuweka urembo wa kucha za akina mama. Hivyo, katika utoaji huduma mtaji wa kwanza ni kipaji, ujuzi, ustadi au maarifa yako.

Biashara katika kundi hili haziathiriwi sana na mfumuko wa bei. Faida nyingine muhimu ya biashara za huduma ni kwamba haziathiriwi sana na kushuka kwa uchumi ikilinganishwa na biashara za bidhaa.

Wafanyabiashara wanaotoa huduma pia wana uwezekano mkubwa wa kulinda bei za huduma zao au kupandisha bei wenyewe maana biashara nyingi katika kundi hili zinahusisha maelewano ya mtoa huduma na mteja wake.

Changamoto za kufanya biashara za utoaji huduma. Zipo changamoto kadhaa ambazo zinakabiri biashara za utoaji huduma na miongoni mwa changamoto hizo ni:

  • Huduma hazionekani au kushikika - hali hii husababisha ugumu wa kuingia sokoni kwa wafanyabiashara wapya; 
  • Huduma haziwezi kutenganishwa na watoa huduma - hali hii husababisha ugumu wa usambazaji huduma kwa wateja (Mfano, msusi ni lazima afanye kazi ya ususi ili aingize kipato); 
  • Ujuzi, ustadi, maarifa au kipaji - Mbali na hayo, wajasiriamali wanatakiwa kuhakikisha kuwa wana ujuzi na mafunzo sahihi au kipaji cha kutoa huduma bora kwa wateja katika soko lao; 
  • Huduma kwa wateja - Ili uendeleze biashara ya utoaji huduma ni lazima ulinde viwango, ubora, ubunifu na kauli kwa wateja wako. Mara zote unatakiwa kujikita kwenye kutatua changamoto za wateja wako kwa viwango vya juu, hii ni tofauti na biashara ya bidhaa maana kuna bidhaa ambazo zinajiuza zenyewe kutokana na ubora wake kwenye soko. 
Hitimisho. Biashara ya utoaji huduma ni fursa hai kwa kila mtu kutokana na urahisi wa kuanzisha biashara hii kuanzia kwenye hatua za chini.

Ili kufaidika na biashara katika kundi hili unachotakiwa kufanya ni kujiuliza una ujuzi, ustadi, kipaji au maarifa yapi ambayo yanaweza kutumika kutatua changamoto za watu katika jamii inayokuzunguka.

Baada ya kugundua uwezo uliopo ndani mwako, hatua inayofuata ni kuanza kutoa huduma kwa jamii inayokuzunguka.

Wakati mwingine unaweza kuanza kutoka huduma bila malipo kama njia ya kutangaza uwezo ulioko ndani wako. Anza sasa na kumbuka kunishukuru baada ya kuona matokeo!

NB. Wasiliana nami kwa ajili ya kupata mwongozo kwenye masuala ya udhibiti, bajeti na uwekezaji wa pesa zako kupitia WhatsApp +255 786 881 155.


WAHI SASA UJIPATIE NAKALA YA KITABU CHA MAISHA YENYE THAMANI 

Kitabu hiki bado kinatolewa kwa bei ya OFA kwa kuchangia cha Tshs. 10,000/= tu! Utatumiwa kwa barua pepe au WhatsApp Nakala tete (soft copy) yenye fomati ya Pdf.


Kupata kitabu hiki, lipia kupitia Mpesa kwenye namba +255 (0) 763 745 451 au Airtel Money namba +255 (0) 786 881 155 au Halopesa namba +255 (0) 629 078 410 zote majina ni AUGUSTINE MATHIAS MUGENYI.




onclick='window.open(