UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Hizi Ndizo Sehemu Ambazo Unaweza Kuokoa Za Kujilipa Kwanza

NENO LA SIKU_MACHI 09/2022: UNAHITAJI KUWA TAJIRI? Hizi Ndizo Sehemu Ambazo Unaweza Kuokoa Za Kujilipa Kwanza

Hongera rafiki yangu kwa kuendelea kufuatulia masomo ya mtandao wa Fikra za Kitajiri. Nafarijika kuona unaendelea kujifunza maarifa mbalimbali kupitia mtandao huu. 

Nitafurahi sana kupata mrejesho wako ukielezea jinsi gani ambavyo masomo haya yamekubadilisha kimtazamo, vitendo na mafanikio uliyoyapata mpaka sasa.

Kujiunga kundi letu la WhatsApp la FIKRA ZA KITAJIRI, TAFADHALI BOFYA HAPA

Karibu katika makala ya leo ambapo nitakushirikisha baadhi ya matumizi ambayo yameendelea kutumia pato lako japo siyo matumizi ya lazima katika maisha ya kila siku. 

Katika makala zilizopita nilikushirikusha umuhimu wa kugawa matumizi yako katika makundi mawili; matumizi ya lazima (Needs) na yale siyo ya lazima (Wants). 


Pia, tuliona kuwa unaweza kufanikiwa kuongeza pesa unayojilipa kwa ajili ya Uwekezaji na Akiba kwa kupunguza orodha ya matumizi yasiyo la lazima. 

Makala ya leo itakufunulia baadhi ya matumizi yasiyo ya lazima ambayo unaweza kuachana nayo kabisa au kupunguza na ukajikuta umefanikiwa kuokoa kiasi kikubwa cha pesa kwa ajili ya kujilipa kwanza. 

Makala hii ni maalumu kwa wewe ambaye hadi sasa unasema huwezi kujilipa kwanza kwa kuwa pato lako halikuruhusu kufanya hivyo. 

Hata hivyo, kila mtu ana pato la kutosha kujilipa kwanza hila wengi hawajui pato hilo limejificha kwenye matumizi ambayo yamekuwa sehemu ya mfumo wa maisha. 

Karibu upitie matumizi yafuatayo kisha ujifanyie tathimini kwenye maisha yako halisi:-

Huduma ya ving'amuzi na idadi ya visimbuzi unavyomiliki. Je, unamiliki visimbuzi vingapi? Je, kila mwezi unatumia shilingi ngapi kama bajeti ya huduma ya ving'amuzi katika kila kisimbuzi unachomiliki? 

Hivi kuna ulazima wa kulipia king'amuzi zaidi ya kimoja wakati huo huo hauna muda wa kuangalia TV? 

Hivi katika king'amuzi hicho unacholipia hauwezi kulipia gharama ya chini (kifurushi cha chini) na maisha yakasonga? 

Pointi ya msingi katika kundi hili la matumizi inatokana na tabia ya baadhi ya watu kumiliki kisimbuzi zaidi ya kimoja (Azam na DSTV au Startimes na DSTV) na kuendelea kupoteza pesa nyingi kila mwezi kupitia malipo ya king'amuzi wakati huo huo wanaendelea kukosa bajeti ya kujilipa kwa ajili Uwekezaji na Akiba.

Mikopo midogo midogo. Je, huwa una utaratibu wa kununua kwa mkopo kwa kuwa umeahidiwa kulipa kidogo kidogo japo kwa ongezeko la bei? 

Siri ya mikopo ni kutambua kuwa kila unapokopa leo unatumia pato la siku za baada kabla ya wakati wake. 

Mwenendo huo wa kutumia pesa kabla ya kuipata hupelekea kila mara pato lisiongezeke maana linatumika kabla ya muda wake. 

Unapokopa laki moja leo kwa mategemeo ya kulipa mwisho wa mwezi, tafsiri yake ni kwamba mwisho wa mwezi pato lako limepungua kwa laki moja. 

Hali hii hupelekea kuongeza msongo wa matumizi kwenye pato lako la kila mwezi na hatimaye kujiona pato lako halitoshelezi mahitaji yako. 

Hivyo, ili uondokane na mikopo huna budi kuishi kulingana na hali ya pato lako. Nunua kile ambacho kipo ndani ya uwezo wako au ishi kulingana na hali ya pato lako.

Gharama za pango la nyumba. Hili ni kundi jingine ambalo watu wengi wanajiingiza kwenye mtego wa matumizi makubwa tena yenye msongo mkubwa. 

Watu wengi wanataka waonekane matawi ya juu kupitia nyumba za kupanga wakati hawajafikia ngazi ya maisha hayo. 

Ni kawaida kukuta mtu anaishi kwenye nyumba ya gharama ya juu wakati pato lake haliendani na hadhi ya nyumba anayoishi. 

Unapochagua nyumba ya kupanga ni vyema utafute nyumba ya hadhi ya kawaida ili kiasi unachookoa kwenye pango kiwekezwe kwa ajili ya ujenzi wa nyumba yako. 

Pitia upya huduma ambazo umejiunga nazo kupitia mitandao. Watu wengi wamejiunga na mitandao mbalimbali pasipo kutazama upande wa gharama za matumizi zinazotokana na kujiunga na mitandao hiyo. 

Hivi ni wangapi ambao wanatambua kwa mwezi wanatumia kiasi gani cha pesa kutokana na kujiunga na mitandao ya kijamii kama vile Tiktok, Facebook, WhatsApp, Instagram au Linkedin. 

Wengi wetu hudhania kuwa hakuna gharama za ziada zinazotokana na matumizi ya mitandao ya kijamii kwa kuwa hatulipi gharama hizo moja kwa moja. 

Hivi, ulishawahi kujiuliza mitandao ya kijamii ambako umejiunga inaongeza gharama kiasi gani kwenye matumizi ya vocha au vifurushi kwa mwezi? 

Unapogundua ni gharama kiasi gani kila unapofungua video kwenye Tiktok, WhatsApp au Instagram inaongezeka kwenye bajeti ya matumizi ya vocha au vifurushi ndipo utaona umuhimu wa kujiunga na mitandao ya kijamii ambayo ni ya muhimu kwako. 

Punguza bajeti inayotokana na matumizi ya nishati. Hapa tunazungumzia bajeti zinazotokana na matumizi ya nishati kama vile umeme, mkaa au gesi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za nyumbani. 

Hivi kuna ulazima gani wa kupikia au kuchemsha maji kwa vifaa vya umeme wakati unaweza kufanya hivyo kupitia jiko la gesi? 

Je, ni kipi chenye gharama nafuu kati ya kutumia jiko la gesi jiko la mkaa kulingana na sehemu unayoishi? 

Mfano, inashangaza kuona mtu anaisha Dar es Salaam ambako kwa wastani gunia moja la mkaa ni kati ya shilingi 45,000 hadi 70,000 wakati gunia hilo haliwezi kutumika zaidi ya wiki tatu.  

Kwa nini husitimie gesi ambayo mtungi mmoja wa shilingi 55,000 unakaa zaidi ya mwezi mmoja? 

Au ni kwa vile tumekaririshwa kuwa gesi ni gharama au kwa vile tumezoea kununua mkaa wa reja reja?

Jenga utamaduni wa kula nyumbani badala ya kula hotelini. Kutayarisha na kula chakula nyumbani kunaweza kuokoa pesa nyingi kwenye bajeti yako ya chakula kwa mwezi. 

Hapa unapaswa kutambua mahitaji chakula kwa kila wiki na kisha kubadilisha utaratibu wako wa chakula. 

Tabia ya kula nyumbani itakusaidia kupunguza gharama za chakula cha hotelini sambamba na kukuwezesha kula kulingana na mahitaji ya mapishi unayotaka. 

Pia, unaweza kununua bidhaa kama ngano, sukari n.k kwa ajili ya kuandaa vitafunwa nyumbani ikiwa una ujuzi wa kuandaa vitafunwa kama maandazi, chapati n.k. 

Mfano, gharama ya samaki mmoja kwenye hoteli za wastani ni kati ya shilingi 7,500 hadi 10,000. Hila wastani wa bei ya kilo moja ya samaki kwa maeneo mengi Tanzania ni kati ya elfu 8,000 hadi 12,000. 

Kwa nini ule hotelini samaki wa bei hiyo wakati ukinunua kilo moja ya samaki inatosha kula zaidi ya mlo mmoja pamoja na familia yako?

Husifanye manunuzi bila kuongozwa na orodha ya manunuzi (shopping list). Akina mama wengi huwa wanaangukia kwenye mtego huu kwa kujikuta wananunua bidhaa nyingi nje ya mahitaji ya lazima. 

Kununua kwa kuongozwa na orodha ya manunuzi ni tabia rahisi ambayo itakuwezesha kupunguza gharama za manunuzi yasiyo ya lazima. 

Pia, tabia hii itakusaidia kuondokana na kununua kwa kusukumwa na hisia, yaani kununua kila kinachopita kwenye upeo wa macho yako ili mradi tu una hela mfukoni. Unaweza kuandaa orodha ya manunuzi kwa siku au wiki. 

Hitimisho, Nimalizie kwa kuuliza; Pesa yako huwa inaenda wapi? Ikiwa hauna bajeti ya matumizi kamwe hauwezi kujibu swali hili! 

Kuna sehemu mbili ambako pesa huwa inaelekezwa zaidi; Moja, matumizi yanayoongeza thamani ya utajiri wako (asset column) - Ni kundi ambalo ikiwa unataka kuwa tajiri huna budi kuwekeza pesa nyingi katika kundi hili. 

Mbili, matumizi ambayo yanapunguza utajiri wako (liability column) - Ni kundi ambalo pesa inapotoka haiongezi thamani kwenye mali unazomiliki. Hili kundi ambalo unatakiwa kupunguza matumizi kwa kadri uwezavyo ikiwa una nia ya kuwa na uhuru wa kifedha.

WAHI SASA UJIPATIE NAKALA YA KITABU CHA MAISHA YENYE THAMANI 

Kitabu hiki bado kinatolewa kwa bei ya OFA kwa kuchangia cha Tshs. 10,000/= tu! Utatumiwa kwa barua pepe au WhatsApp Nakala tete (soft copy) yenye fomati ya Pdf.


Kupata kitabu hiki, lipia kupitia Mpesa kwenye namba +255 (0) 763 745 451 au Airtel Money namba +255 (0) 786 881 155 au Halopesa namba +255 (0) 629 078 410 zote majina ni AUGUSTINE MATHIAS MUGENYI.

onclick='window.open(